Tujikumbushe.

Mtoto wa Mkulima

JF-Expert Member
Apr 12, 2007
681
126
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais ametoa ahadi nyingi tu nzuri ambazo Wabunge na Madiwani pia wanazizungumzia na ahadi hizo ambazo zimo ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Ni vyema basi ikazitengea mafungu maalum ya fedha ili zitekelezwe ili wananchi waone kuwa Serikali yao ya Chama cha Mapinduzi inatimiza ahadi yake ili kila Mtanzania awe na maisha bora.

Serikali Tunafahamu kwamba hali ya hewa imeathiri uchumi wetu kwa kiasi fulani, ambayo hivi sasa Serikali inajitahidi kwa uwezo wake kujaribu kuyaweka mambo yaende vizuri na mimi nina matumaini makubwa tutafika mahali mambo yote yata–stabilize na hali ya maisha itakuwa kama ilivyokuwa awali, ili tuweze kuendelea kuchangia yale mambo muhimu ambayo wananchi wanayahitaji katika maisha ya kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninachosema ni kwamba, ili Serikali iendeshe shughuli zake vizuri, ni lazima iwe inapata mapato mazuri kwa kukusanya kodi mbalimbali katika nchi yetu. Yapo maeneo mengi ambayo yanahitaji kupewa kipaumbele na kuweka mikakati madhubuti ili makusanyo ya kodi yawe mazuri na hatimaye bajeti iwe nzuri na hali kadhalika tunaweza tukashughulikia kero za wananchi mbalimbali bila ya kuwa na matatizo makubwa na hatimaye tufike mahali tunaachana na kutegemea wafadhili katika Bajeti zetu. Hilo ni la msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni sekta nyingi ambazo zinaweza zikachangia Pato la Taifa, mimi nianze kuzungumzia migodi yetu ya dhahabu. Migodi ya dhahabu tumeianzisha siyo muda mrefu sana na tuna matumaini tutafika mahali migodi hii iweze kuchangia pato kubwa la Taifa kama ilivyo katika nchi mbalimbali zinazozalisha dhahabu. Lakini, kuna mapungufu mengi ambayo tunahitaji tuyatizame upya na Serikali izingatie kwamba hoja hapa katika migodi ya dhahabu ni jinsi gani tutapata share ya kutosha ili kukidhi Bajeti yetu ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafikiri kuna jambo la kwanza ambalo linarudisha nyuma, ni ile team ambayo inafanya negociation ya mikataba kati ya Serikali na makampuni yanayokuja kuwekeza katika uchimbaji wa dhahabu. Aidha, skills za negotiation siyo nzuri. Vile vile, pengine kuna baadhi ya watu wanakuwa wanakosa uzalendo, wanashindwa kutambua kwamba hili ni jambo la msingi na hii ni rasilimali ya wananchi wetu na hatimaye kukubali kwa urahisi kuwapa nafasi kubwa wawekezaji bila kujitazama sisi wenyewe tunafika sehemu gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Kamati ya Uchumi na Fedha imesema: "Nafikiri Serikali sasa hivi imekwishajifunza vya kutosha kwamba sasa tunaweza tukajua tumekosea wapi, turekebishe wapi." Hatimaye sasa tunapopata wawekezaji wengine, basi tutizame vizuri. Tunazungumza nao kwa kiasi fulani na kuhakikisha kwamba Serikali inapata mapato ya kutosha katika migodi yetu.

Nami naungana na Mheshimiwa Rais kwa kusema kwamba, Mikataba ya Madini itazamwe upya ili kukidhi haja ambayo naizungumzia hivi sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitoe mfano, Kahama Gold Mine ilikuwa inamilikiwa na Sutone Resources, wao wakauza share zao kwa Barrics. Naye Barrics sasa hivi ameingia mkataba na Placerdom. Leo asubuhi kulikuwa na swali kuhusu madini na mikataba na mimi niliuliza swali, hivi hii mikataba kunapofanyika tansaction za kuuza share kati ya Kampuni na Kampuni, hivi Serikali inapata kodi?

Mheshimiwa Waziri alijaribu kufafanua, lakini, inaonyesha wazi kwamba mikataba yetu iko dhaifu, haikuweza kueleza specifically maeneo kama haya. Migodi ipo kwetu Tanzania, lakini, yale makampuni yanapouza share, sisi tunabaki kutizama macho wanafanya tansaction zao, wanapeana pesa, lakini Serikali haipati hata senti tano. It's not fair. Sasa, huo ni upande mmoja , tutizame vizuri mikataba yetu. Hii inatokana kwa sababu Serikali haina share katika hii migodi. Nafahamu kwa sababu gani labda Serikali haina share, labda ni kwa sababu haina uwezo. Lakini tuweze kufika pahala basi, Serikali kwa jinsi yoyote, ni lazima iwe na share japo ya asilimia tano katika migodi yote ya dhahabu iliyopo hapa nchini

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo linaweza likatusaidia na maeneo mengine mbali mbali ambayo yanaonekena yana udhaifu katika kupata mapato katika migodi ya dhahabu pamoja na migodi mingine ya Almasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze kwenye Benki ya Tanzania, BoT. Sarafu yetu inashuka na haya ni mambo ya kitaalam unapozungumzia katika Bunge au Serikali inaposema uchumi unakua. Lakini Sarafu yetu inaanguka, wao wanaona chakula kinapanda bei, mafuta yanapanda bei, haelewi, uchumi unakua, sarafu inaanguka, chakula kiko juu. Sasa hili suala la biashara huria, mimi naiomba sana Bank of Tanzania ifike pahala iweze ku – stabilize hii currency yetu. Hatuwezi tukaiachia currency ijisawazishe yenyewe katika soko. Hatuna uchumi ambao ni mkubwa na mzuri sana kuweza tukafikia pahala kama huko.

Watu wengi watatumia loopholes hizi na sisi tutazidi kupoteza nguvu ya sarafu yetu. Sasa, naiomba sana BoT na sheria ambayo tumekwishaipitisha. Tumewapa nafasi kubwa sana wahakikishe kwamba wanafanya kila jitihada kwamba sarafu yetu inakuwa imara, maana yake nina wasiwasi sasa tutafika kama ile sarafu ya Zambia ilivyo. Ilikuwa ni Dola moja – Kwacha 2400, sasa hivi imeishafika 4000. Sasa tusifike huko. Inatuumiza sana. Inatuumiza katika bei za mafuta, inatuumiza katika kuagiza bidhaa kutoka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, vitu vingi vinaagiziwa kutoka nje kwa ajili ya matumizi ya wananchi hapa ndani, bei zao zinakuwa kubwa, wanaona ni gharama kubwa kununua na inafika mahala inatuumiza, lakini hii ni kazi ya Bank of Tanzania na hivi sasa tumewapa meno waweze kuitumia sheria vizuri na Wizara ya Fedha ijitahidi kuisimamia Bank of Tanzania kuhakikisha kwamba ina-stabilize uchumi wetu na hatimaye ili twende vizuri pamoja na haya matatizo ya ukame yakishamalizika, lakini tuone basi hali inakuwa ni nzuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie vile vile katika mpango mzima wa kuweza kuinua uchumi wa wananchi kwa maana ya kufanya biashara kwa kukopa pesa katika Mabenki. Yamezungumzwa hapa ni kwamba wewe ukienda kukopa pesa Benki, riba ni kubwa sana. Huwezi ukafanya biashara kwa riba kama hivyo. Nawe unaweka pesa yako Benki, mwananchi anaweka pesa Benki, anapewa riba ya asilimia 2.5, 3, haizidi. Hivi nani atafika mahali aseme mimi naweka pesa yangu Benki? Ndiyo maana wengi wanaamua kuweka fedha zao nje, kwa sababu vivutio vya Benki zetu, havivutii kwa wananchi wenyewe kuweka pesa Benki na hatimaye waweze kupata faida katia fedha zao. Wanashindwa kukopa kwa sababu wanajua riba ni kubwa, biashara ni ngumu, sarafu iko chini. Siyo rahisi kwa yule mwenye kipato cha chini kuweza kukopa na hatimaye akafanya biashara vizuri.

Sasa hivi Serikali nashukuru wameweka utaratibu wa kuwakopesha wafanyabiashara wadogo wadogo katika maeneo yetu. Lakini, pia itazame kwamba kuna mtu mmoja tu katika kila Benki ya NMB ambaye anasimamia masuala ya mikopo. Afisa yule, aende Vijijini, Afisa yule akae Ofisini, aratibu shughuli za mikopo, haiwezekani. Naiomba Wizara ya fedha ijaribu kuzungumza na NMB angalau kila Benki ya NMB katika Wilaya zetu, wawe na Maofisa angalau wawili, watatu kuweza kuratibu shughuli za mikopo ili kila mwananchi aweze kunufaika na mikopo ambayo tumeilenga kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika kero nyingine ambayo inaturudisha nyuma katika kupata mapato na watu kuwa na uzito wa kuleta bidhaa hapa kwa sababu ya kero za Bandarini na hasa katika suala la ushuru. Mimi nitoe mfano wa uagizaji wa magari.

Unapompa mtu nafasi ya kuamua yeye akisie gari hii ilipiwe ushuru wa kiasi gani, wengine watafaidika, wengine wataumia, kwa sababu umemuachia mtu binafsi amue kama yeye. Ni vyema sasa Serikali ikaweka utaratibu mzuri, kwa sababu inaeleweka kabisa kwamba gari za Kijapani zinajulikana kwa CC zake na mwaka ambao zimetengenezwa (Manufacturing Year). Sasa, kutokana na vipengele hivi au vigezo hivi, iamuliwe kwa makusudi na katika Bajeti Waziri amesema kwamba sasa magari ambayo toka yametengenezwa mpaka miaka kumi, baada ya miaka kumi, usilete gari nchini.

Mimi ninaipongeza, kwa sababu inatugharimu pesa nyingi ya kununua spare kwa sababu ya magari mabovu yaliyopo nchini. Lakini, ndio uwezo wa wananchi kununua hayo magari ambayo wameona kule ni bei nafuu, lakini yakija huku nako, kigongo cha ushuru ni kikubwa sana. Basi, Serikali iweke utaratibu mzuri kwamba, gari ya mwaka fulani, yenye CC namba fulani au CC ya kiwango fulani, ushuru wake ni kiasi kadhaa, ili yule anayenunua gari anajua kwamba hii gari nikiipeleka nyumbani, ushuru wake ni kiasi fulani kwa sababu ya CC na mwaka uliotengeneza ile gari. Utaondoa matatizo ya mtu mmoja kukaa Ofisini na kuamua kwamba wewe ulipe kiasi gani. Hii kwa kweli inaleta mianya ya rushwa ambayo haki wakati mwingine haitendeki katika maamuzi ya kumuamulia mwananchi alipe kiasi gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nizungumzie T-Scan. T-Scan imeletwa hapa nchini kwa nia njema. Lakini inapofanya kazi zake mpaka watoe taarifa yule mteja au yule aliyeleta bidhaa alipe kiasi gani, inaweza ikamchukua hata wiki tatu. Kwa hiyo, unamlazimisha yule mteja alipe port charges bila ya sababu. Haiwezekani document imekwishakaguliwa kontena au bidhaa aliyoleta itoke Mkoani kwa mfano Tanga iende Dar es salaam na hatimaye sasa Dar es salaam ndio waamue alipe kiasi gani, inachukua wiki tatu au wiki mbili wakati storage charge zikifika, Bandari wataendelea kutoza storage charge.

Kwa kweli tutakuwa hatumtendei haki huyu mwananchi ambaye anaagiza bidhaa. Haya yote ndiyo yanayo rudisha nyuma, kukosekana kwa mapato mengi na kwa urahisi wa watu kufanya biashara kwa furaha zaidi. Anafikiria akileta mzigo wake atapatikana na misukosuko kama hii. Kwa kweli inaipunguzia sifa nchi yetu kwa wawekezaji ambao wanataka kuja kuwekeza maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, muda uliobaki naona hautoshi, lakini nilikuwa na haya machache ya kuchangia. Naiomba sana Serikali itizame maeneo mengi ambayo bado ni kero katika mapato yetu ambayo ndiyo msingi wa Bajeti nzuri katika miaka ijayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwa kupunguza gharama za gesi. Lakini, vile vile watazame na majiko ya gesi, yaingie bila ya ushuru ili kila mwananchi Kijijini sasa awe na utamaduni wa kutumia gesi na hatimaye tuweze kuhifadhi misitu yetu ili tuweze kuwa na angalau na hali nzuri ya mazingira, tuondokane na masuala ya ukame na ukataji wa miti hovyo ambao unatuletea athari.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, nakushukuru kwa kunipa nafasi na niseme naunga mkono hoja. Ahsante sana.


Source:www.bunge.go.tz/bunge/ContrLst.asp&...e=11+Tscan+Tanzania&hl=en&ct=clnk&cd=10&gl=jp
 
Back
Top Bottom