TUCTA yapasa kufikiria maslahi ya Taifa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

TUCTA yapasa kufikiria maslahi ya Taifa

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by jamadari, Apr 28, 2010.

 1. jamadari

  jamadari JF-Expert Member

  #1
  Apr 28, 2010
  Joined: Feb 13, 2010
  Messages: 295
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 0
  [​IMG]
  Maoni ya katuni  Kwenye ukurasa wa kwanza wa gazeti hili toleo la leo, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC), Emanuel Ole Naiko, amekaririwa akitahadharisha kuhusu mgomo wa wafanyakazi, unaokusudiwa kuitishwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta).
  Tucta imepanga kuitisha mgomo usio na kikomo wa wafanyakazi nchi nzima kuanzia Mei 5, mwaka huu.
  Hata hivyo, Ole Naiko ambaye anatambua umuhimu wa maslahi mapana ya wafanyakazi, anasema mgomo huo, una madhara kwa uchumi na ustawi wa wananchi, hivyo haustahili kuwepo.
  Hoja ya Ole Naiko inapata nguvu zaidi kutokana na ukweli kwamba muda uliopangwa wa kuanza kwa mgomo huo, kutakuwa na mkutano wa kujadili hali ya uchumi duniani, maarufu kama World Economic Forum (WEF) utakaofanyika kati ya Mei 5 hadi 7 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
  Mkutano huu ambao utazishirikisha nchi mbalimbali duniani, ni muhimu na nchi yetu ya Tanzania imepata fursa hii ya kipekee kuwa mwenyeji wake.
  Kimsingi, tunaungana na TIC kupitia kwa Ole Naiko, kwamba mkutano huo ni fursa nzuri kwa Tanzania kupanua wigo wa uwekezaji na ajira nchini.
  Kama ilivyo kwa TIC, sisi tunatambua na kuheshimu maslahi ya wafanyakazi, lakini zaidi tukiwa chombo cha habari, tunatambua umuhimu wa kulinda maslahi ya umma na Taifa kwa ujumla.
  Kushamirisha kasi ya ukuaji ajira na uwekezaji kupitia WEF, ni miongoni mwa mambo yanayopaswa kuungwa mkono, hivyo rai ya Ole Naiko kutaka mgomo huo usipewe nafasi, inapaswa kuungwa mkono kwa kila namna.
  Hakuna sababu ya kuwafanya wawekezaji watakaowasili nchini kwa ajili ya mkutano huu wa WEF, wajenge hofu itakayokwamisha jitihada, nia na dhamira ya kuwekeza hapa nchini kwetu penye sifa kemkem za mazingira mazuri, utulivu na amani.
  Iwapo hoja hiyo itapuuzwa, ni dhahiri kwamba Taifa litakuwa limeingia katika dimbwi la ukosefu wa ajira na kushindwa kukuza uchumi wake na hapana shaka nchi nyingine zilizonyimwa fursa ya kuuandaa, zitatushangaa na kutuona wa aina yake.
  Kwa hali hiyo, tunaamini kwamba kwa namna iwayo yote, faida zitakazotokana na kutofanyika kwa mgomo huo, zitakuwa kubwa kuliko ukifanyika, na kushuhudiwa na wageni wakiwemo wawekezaji watakaohudhuria WEF jijini Dar es Salaam.
  Ni wakati mwafaka kwa Tucta kuzielewa kwa makini hoja za Ole Naiko na kutambua ukubwa wa tatizo la ukosefu wa ajira linalowakabili raia hasa vijana wa mijini na vijijini, na ambalo litapungua ama kuondoka ikiwa Taifa litakuza uwekezaji ukiwemo wa washiriki wa WEF.
  Bado tunaamini kwamba, viongozi wa Tucta ni wasikivu na waelewa ambao bila shaka wataangalia kwanza maslahi ya taifa kabla ya kufikia uamuzi huu mzito.
  Ni wakati pia mwafaka kwa viongozi wa pande zote mbili yaani Tucta kwa upande mmoja na serikali kwa upande mwingine, kutumia muda huu mfupi uliobaki kuhakikisha kwamba mgomo huu unamalizwa kwa njia za amani kupitia mazungumzo.  CHANZO: NIPASHE
   
Loading...