Kuna utani mbaya unaoendelea kushika hatamu kuhusu Mwanaume wa Dar. Utani huo usiofaa, unamdhalilisha na kupotosha sifa muhimu za mwanaume anayeishi na kutafuta maisha katika Jiji kubwa la kibiashara la Dar es Salaam.
Sisi kama Great Thinkers tukiendelea kukaa kimya, in the long run utani huu unaweza kupunguza ari ya vijana wengi kupambana na maisha, kuathiri baadhi ya biashara hivyo kupunguza mapato katika jiji hili tegemezi la taifa.
Mathalani, soko la viazi ni kubwa sana katika jiji hili kutokana na zao hilo kutumika katika kuandaa chakula cha haraka (fast food) kwa ajili ya wale wasiopata muda wa kukaa jikoni na kujiandalia chakula cha mchana/jioni kutokana na mishe mishe zao.
Viazi (chips) ni biashara kubwa na imeajiri wengi, hivyo kutania kwamba chakula hiki hakifai kuliwa na wanaume, kunaweza kusababisha athari kubwa ya kiuchumi kwa wakulima na wachuuzi kule Mbeya kwa rafiki yangu Ipyana, japo kwa sasa tunaweza kuchukulia kama mzaha. Isitoshe, sijaona maelezo yoyote ya kitaalamu yanayoonesha kuwa chakula hiki hakifai kwa matumizi ya binadamu, achilia mbali mwanaume.
Mifano ipo mingi na inafahamika. Kwa mfano baadhi ya vipindi vya televisheni, radio, mavazi, na kazi kadha wa kadha zinadharauliwa kwamba zinafanywa na Wanaume wa Dar - yaani eti kuna biashara/kazi hazifai kufanywa na Mwanaume. Dunia hii ya sasa?!
Nakumbuka miaka ya nyuma kidogo kulikuwa na utani wenye maslahi. Sifa kubwa ya Mwanaume wa Dar ilikuwa ni mtu mwenye matumizi makubwa ya akili (bongo) ambayo ilichochea kwa kiasi kikubwa vijana kuwa active kwenye mishe zao. Misemo kama kuzaliwa mjini pekee ni form 6 iliongeza motisha ya uchakakarikaji. Na hiyo ni miongoni mwa sababu kubwa iliyolikuza Jiji hili na kustawi kibiashara.
Nihitimishe kwa kukumbushia sifa za kweli za Mwanaume wa Dar:
1. Ni mzaliwa au mkazi wa kudumu wa Jiji la Dar es Salaam.
2. Msomi, mwerevu na mchangamfu kwa kila mtu.
3. Mwenye ndoto, mipango na malengo ya kufanikiwa kimaisha.
4. Ana hulka ya uchakarikaji, uthubutu na mtumiaji mzuri wa fursa za kiuchumi.
5. Mwenye maarifa na ujuzi wa mambo yanayoendelea duniani. Ni mtu mjanja na anayeendana na kasi ya sayansi na teknolojia.
Kimsingi, hii picha inayotengenezwa sasa kuhusu mwanaume wa Dar haina uhalali wowote. Ni matokeo ya kiwango cha ujinga uliokithiri katika jamii zetu na wanaouendekeza utani huo ni watu duni kifikra.
Tuukatae utani huu usio na manufaa yoyote zaidi ya kudhalilisha. Tuukatae kwa sababu unaturudisha nyuma.