TRA yazua sokomoko kikao cha Muungano | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

TRA yazua sokomoko kikao cha Muungano

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Oct 13, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Oct 13, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,461
  Likes Received: 81,711
  Trophy Points: 280
  Date::10/13/2008
  TRA yazua sokomoko kikao cha Muungano
  Na Salma Said, Zanzibar
  Mwananchi

  VIONGOZI wakuu wa pande mbili za Muungano waliokutana juzi visiwani Zanzibar kwa lengo la kuzungumzia kero za Muungano, wameshindwa kukubaliana na ripoti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), iliyowasilishwa katika kikao hicho.


  Kikao hicho, kilichofanyika chini ya uenyekiti wa Makamu wa Rais Dk Ali Mohammed Shein, kilitawaliwa na mijadala mikali huku baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar wakionekana kushindwa kuikubali ripoti ya TRA kutokana na utata uliojitokeza.

  Utata huo ulijitokeza katika suala la ushuru wa magari yenye namba za Zanzibar kutozwa ushuru wakati yaingiapo Tanzania Bara.

  Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Mohammed Seif Khatib, kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Bwawani Mjini hapa, alisema viongozi wa Zanzibar walieleza ukweli halisi juu ya kero hiyo.

  Alisema wajumbe hao walidai hawaoni sababu ya Mamlaka hiyo kutoza ushuru huo pale bidhaa na magari hayo kutoka Zanzibar yanapoingizwa Tanzania Bara, wakati bidhaa hizo zilishatozwa ushuru Zanzibar na mamlaka hiyo.

  Wajumbe wengi kutoka Zanzibar walishindwa kukubaliana na wenzao wa Tanzania Bara katika suala zima la ushuru, wakidai kuwepo kwa utata na kwamba hawawezi kukubaliana na ripoti hiyo ya TRA.

  Suala la ripoti hiyo lilizua mjadala mkali kutokana na ripoti ya mamlaka hiyo kudai kuwa mivutano iliyokuwepo juu ya suala la ushuru imemalizika, jambo ambalo wajumbe hao hawakukubaliana nalo.

  “Kutokana na mvutano huo kikao kimeamua kuundwa kwa kamati ya pande mbili ambayo itazihusisha Wizara za Biashara, Fedha, TRA na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali kwa ajili ya kutafuta namna ya kuondoa kero hiyo ya Muungano,” alisema Khatib.

  Suala jingine ambalo wamekubaliana liundiwe kamati ni la uwiano wa nafasi za ajira za Muungano katika ngazi za juu, ambazo alisema Wizara za Elimu, Utumishi, Menejimenti ya Umma na Ofisi ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar zitakaa pamoja kujadili namna ya Zanzibar itakavyoshirikishwa katika utoaji wa ajira hizo.

  Kwa mujibu wa Khatib suala lililovuta hisia za wajumbe wengi hasa kutoka Zanzibar ni hatima ya mafuta yanayodaiwa kuwepo visiwani humo, suala ambalo liliwekwa kiporo kutokana na kusubiri ripoti ya mshauri elekezi inayotarajiwa kutoka Desemba mwaka huu.

  Waziri Khatib alieleza pia kuwa uamuzi huo umekuja baada ya mawaziri wawili wanaohusika na nishati, Mansoor Yussuf wa Zanzibar na William Ngeleja Bara, kukubali ili kuepuka kupata hasara kutokana na kazi hiyo kuwepo kwa mwelekezi huyo na kwamba ripoti yake ndiyo itakayokuwa mwongozo wa nini kifanyike hapo baadaye.

  Alisema baada ya kukamilika, ripoti hiyo itawasilishwa kwa serikali zote mbili ili kuangalia kama matakwa ya Zanzibar yamezingatiwa kwa kiasi gani.

  Kuhusu suala la gesi ambalo tayari Tanzania Bara inafaidika nalo kwa miaka minne sasa, Khatib alisema wamekubaliana kuwa litabakia kama lilivyo kwa hivi sasa na kusubiriwa ripoti ya mwelekezi ili kuona ni namna gani Zanzibar itaingizwa katika suala hilo.

  Katika hatua nyingine, Waziri Khatib alisema viongozi wa Serikali ya Muungano wamekiri kuwepo kwa kasoro kutokana na suala la ushiriki wa Zanzibar katika mikutano ya kimataifa. Inadaiwa Zanzibar huingizwa katika dakika za majeruhi za maandalizi yake na kuahidi kwamba suala hilo litashughulikiwa.

  Alifafanua kwamba imeonekana kuwa maandalizi yanayofanywa Tanzania Bara yamekuwa hayatoi nafasi kwa Zanzibar kushiriki katika hatua za awali na hivyo kikao hicho kimetaka kuona visiwa hivyo vinashirikishwa tangu hatua za awali.

  Kwa upande wa suala la mgawo wa 4.5 asilimia za Zanzibar katika Muungano, nalo limekwama kutokana na ripoti iliyotolewa na kamati iliyoundwa na rais, upande wa Tanzania Bara kuwa haijamaliza kuyapitia, huku Zanzibar ikiwa tayari imeshapiga hatua kubwa katika kuipitia ripoti hiyo.

  Waziri Khatib alieleza kwamba kutokana na kuwepo kwa hali hiyo, kikao hicho kimeutaka upande wa Bara kuhakikisha kuwa inaifanyia kazi haraka ripoti hiyo ili iweze kuanza kufanya kazi.

  Rais Kikwete pia aliombwa na kikao hicho kuunda tume mpya kutokana na tume iliyopo kuwa imeshamaliza muda wake.

  Pia Waziri Khatib alieleza kuwepo kwa suala kubwa la mapendekezo ya Zanzibar yatayopelekwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ili iweze kupatiwa mikopo na misaada.

  Alisema wataalamu wa kuifanya kazi hiyo hivi sasa wapo nchini Rwanda na wanatarajiwa kuwasili Zanzibar kuanza kufanya kazi hiyo.

  Alisema miradi ambayo imependekezwa na Zanzibar ni pamoja mradi wa ujenzi wa jengo la uwanja wa ndege ambalo litagharimu dola 78 milioni za Kimarekani.

  Mradi mwingine ni uzalishaji umeme kwa upepo ambao utagharimu dola 70 za Kimarekani.

  Aliitaja miradi mingine kuwa ni ule wa bandari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Maruhubi itakayotumia kiasi cha dola 400 milioni za Kimarekani, mradi wa utafiti wa uendelezaji na ukuzaji wa zao la mwani dola 60 milioni za Kimarekani na mradi wa kuratibu magonjwa ya mifugo katika ukanda wa Zanzibar ambao utatumia dola 22 milioni za Kimarekani.

  Aliitaja miradi mingine kuwa ni wa kuimarisha mazao ya kilimo na usindikaji na kuongeza kuwa ubora wa mazao kwa kutumia teknolojia ya kisasa, mradi wa miundo mbinu ya ukanda wa bahari Kuu na ujenzi wa Bandari kavu, mradi wa ukuzaji wa zao la Taifa na karantini ya wanyama.

  Kuhusu suala la uvuvi wa bahari kuu, Waziri Khatib alisema kikao hicho kilifahamishwa kuwa tayari limeamuliwa kuwa katika kijiji cha Fumba Fumba ndio kutajengwa kituo hicho.

  “Hivi sasa mchakato wa ujenzi wa jengo linalokusudiwa kujengwa upo, Benki ya Dunia na wao wataangalia namna ya kupata mzabuni atakayeshughulikia ujenzi huo,” alithibitisha Khatib.

  Alisema wakati hayo yakiwa katika mchakato wa utekelezaji, taasisi husika zinatarajia kufanya uteuzi wa mkurugenzi atakayesimamia kituo hicho wakati kitakapokutana Oktoba 20 na kwa sasa watafanyia kazi zao katika jengo la Uwekezaji la ZSTC, Gulioni mjini hapa.

  Kutokana na mapendekezo hayo Khatibu alisema suala la vikao hivyo kuchelewa linatakiwa kuondolewa na kuwekewa ratiba maalumu.

  Alisema kuanzia sasa vikao hivyo vitafanyika kila Oktoba, Desemba, Machi, Aprili na Juni ya kila mwaka na vitafanyika katika ngazi tofauti kwa vikao vya viongozi wakuu wa pande hizo, mawaziri, makatibu wakuu na wakurugenzi.
   
Loading...