[ This is wrong y'all! ]: alianza Mkapa, na sasa ni Kikwete na Serikali yake | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

[ This is wrong y'all! ]: alianza Mkapa, na sasa ni Kikwete na Serikali yake

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BongoTz, Oct 11, 2010.

 1. BongoTz

  BongoTz JF-Expert Member

  #1
  Oct 11, 2010
  Joined: Nov 3, 2006
  Messages: 272
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Hivi kwanini serikali ya chama cha mapinduzi inadhani kuwa wao pekee ndio wenye monopoly ya vyombo vya habari hapa nchini? Nalisema hilo kwasababu chini ya utawala wa rais Mkapa, mara nyingi kama sio zote, serikali ya awamu ya tatu ikiongozwa na waziri mkuu wa ovyo aliyewahi kuliongoza taifa letu la Tanzania, Fredrick Sumaye, ilikuwa inatumia vitisho vikali dhidi ya mwaandishi wa habari yeyote yule aliyeonekana kupingana na muelekeo wa serikali hiyo hata kupelekea kutishia kuwavua urai baadhi ya waandishi wakongwe wa habari. Nasikitika kuandika kuwa Kikwete na serikali yake wameanza kutumia the same tactics katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu ili kuwatisha waandishi wa habari wanaoandika postive news kuhusu Dr. Slaa/negative news kuhusu CCM. It's wrong and we should all be outraged.

  I mean, ibara ya kumi na nane (18) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaeleza waziwazi kwamba: [1] Kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati. [2] Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbali mbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii (zikiwemo habari za kampeni ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani).

  Ingawa kumekuwepo na ongezeko la Vyombo vya habari nchini (Redio, Televisheni, Magazeti, Majarida, nternet [Tovuti], tangu sera ya habari na utangazaji ilipotolewa kwa mara ya kwanza mwaka 1993; ukweli ni kwamba ongezeko hilo halina maana yoyote ikiwa Idara kuu za serikali kama vile Utendaji (executive), Bunge (legislative) na Mahakama (Judicial) hazioni umuhimu wowote ule wa kufuata sheria mama zilizomo ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano (hususani sheria ya uhuru wa habari).

  Nakubaliana kabisa na Mkurugenzi wa mradi wa Excellence in Journalism, Bw. Tom Rosenstiel kuwa vyombo vya habari ni sawa na Idara ya nne ya Serikali ambayo kando na kutoa habari, kuelimisha na kuburudisha jamii; dhima nyingine kubwa ni kuziangalia hizo Idara nyingine tatu za serikali na kuhakikisha kuwa hazifanyi mambo ambayo hazitakiwi kufanya.

  Hii ni kwa waandishi-wachunguzi kuwaanika wazi wale wanaotumia madaraka yao vibaya kwa kuvunja sheria zilizopo kwa maslahi yao wenyewe, ama kujichukulia njia za mkato kwa lengo la kujineemesha kupitia migongo ya raia wanyonge.

  Kwa muda mrefu, vyombo vya habari Duniani kote vimekuwa ndio chanzo kikubwa cha kufichua watenda makosa wa Idara nyingine za serikali. Hili tumelishudia sana katika nchi zilizoendelea. Kadhia ya miaka ya sabini (70s) ya Watergate iliyomlazimisha Rais Richard Nixon kujiuzuru ni mfano mzuri kabisa wa kutizamwa.

  Japo Serikali ya Tanzania imeridhia matamko rasmi ya Umoja wa Mataifa, na Umoja wa Afrika kuhusu uhuru wa kutoa na kupokea habari; na pia kutambua kuwa utoaji na upokeaji wa habari ni moja ya haki za msingi za binadamu, inasikitisha kusema kuwa serikali ya Tanzania, inayojitangaza duniani kama "Serikali ya Kidemokrasia" imeshindwa kabisa kuheshimu maridhio hayo na badala yake inatumia sera za vitisho kuwagadamiza wale wote wanaoripoti na kuandika habari zinazopingana na mtizamo wa serikali.

  Nadhani sote tunakumbuka kilichotokea February 12, 2002: Serikali ya awamu wa tatu iliamua kuushangaza umma wa watanzania pale ilipotangaza kuwa Jenerali Ulimwengu sio raia tena wa nchi ya Tanzania! Kwanini?--Kwasababu tu za kijinga zilizojengwa katika uzindiki wa kisiasa na culture ya kipuuzi ya kulipa visasi. Maana akiwa kama Mkurugenzi wa Habari Corporation, Ulimwengu hakusita kuwasha taa iliyomulika na kuanika hadharani maovu yaliyokuwa yanaendeshwa ndani ya serikali na kuwapasha habari wananchi ili wao wenyewe waamue kama kuna kosa lolote limetendeka au la...

  Na ni katika kuibua kadhia mbalimbali zikiwemo zile za rushwa ndani ya serikali, ndipo alipoonekana kuwa si Mtanzania halisi. Lakini wakati akipewa vyeo mbalimbali ndani ya chama na serikali kama vile; ukuu wa wilaya (1989-1993), mjumbe wa NEC (1992-1997) na ubuge (1990-1995) suala la uraia halikuwa na tatizo.

  Kadhalika mwandishi-muchunguzi Bw. Richard Mgamba ambaye alikamatwa na hata kutishiwa kuvuliwa uraia wake wa Tanzania eti kwasababu tu alihojiwa katika mshito wa Jinamizi la Darwin, ni mfano mwingine mzuri wa kutizamwa. I mean, hivi kumbe ni kosa kubwa kiasi hicho kwa waandishi wa habari kueleza mawazo binafsi ikitokea mawazo yao yakatofautiana na mawazo ya viongozi fulani wa serikali?

  Ikiwa ndivyo basi, hakuna umuhimu kabisa wa kuwa na katiba kama sheria zilizopo ndani ya katiba hazifuatwi.

  Kinachokera zaidi ni sheria mbaya za magazeti na utangazaji [zilizopo] ambazo zinampa Waziri mwenye dhamana ya habari na utangazaji mamlaka ya kuadhibu vyombo vya habari ambavyo vinachapisha au kutangaza taarifa ambazo, kwa tafsiri yake Waziri, zinamvuto/onekana kutishia maslahi ya umma.

  Huwezi kudai kuwa "serikali yetu ni serikali ya kidemokrasia" wakati sheria za uhuru wa habari zilizopo, zipo kwenye maadishi tu na kwamba, kwa tafsiri yake, Idara ya utendaji ina haki ya kugandamiza na kuadhibu yeyote yule anayetangaza ama kuripoti habari ambazo zinahitilafiana na serikali hata kama habari hizo ni za kweli.

  Kuna msemo maarufu usemao kuwa, vyombo vya habari ni kama nuru imulikayo sehemu zenye kiza. Na madhali serikali yetu bado haijaruhusu waziwazi waandishi-wachunguzi kuwasha taa zao na kumulika maovu, kadhia, pamoja na vitendo vya rushwa vilivyojificha ndani ya Idara mbalimbali za serikali, madai kwamba "serikali yetu ni serikali ya kidemokrasia" ni kejeli tu za kisiasa zisizo na mizizi ya kifikra.

  kwa wale waandishi wenzangu wanaotumia Internet [tovuti] ambayo haitawaliwi na sheria yoyote nchini, iweni hodari basi wala msikubali kamwe kupandisha bendera ya kushidwa! Andikeni habari zote bila kusikiliza vitisho vya Idara ya utendaji. Daima kumbukeni maneno ya aliyekuwa Rais wa Tatu wa Marekani, Thomas Jefferson, aliyewahi kusema, nami namnukuu: "kama inanilazimu niamue kati ya serikali ya kidemokrasia bila ya uhuru wa habari, au uhuru wa habari peke yake, nitachagua habari."
  Mungu ibariki Tanzania!​
   
Loading...