The must read story!

Song of Solomon

JF-Expert Member
Aug 5, 2021
2,733
5,490
Nikiwa sina hili wala lile mtoto wa Mjasiriamali napita vitongoji kadhaa ndani ya Wilaya ya Njombe Kata ya Yakobi. Nakutana na mzee mmoja akiwa amejichokea taabani kweli kweli. Mzee ameshikilia mkwaju wake! Bila ajizi nampatia mzee heshma yake! Mzee anaipokea heshma yake na ninamwambia nikusogeze kidogo kwa lift! Nilikuwa naendesha Boda yangu aina ya Kinglion niliyokodisha kwa Jamaa yangu Mwinuka pale stendi ya Zamani! Mzee ananishukuru na kukalia boda na safari inaendelea!

Mzee ananiambia " Nashukuru sana kijana wangu maana hili jua la siku hizi linachoma kweli kweli,utadhani hii sio Njombe,enzi hizo wakati kama huu ilikuwa baridi kweli kweli,yaani unavaa makoti usiku na mchana,huwezi hata kusikia joto hadi usogee kwenye moto,miaka hiyo ya 1980"s ukilaza ndoo ya maji nje ukiamka asubuhi unakuta maji yana chembechembe za barafu" Story kadhaa zinaendelea nikiwa mwendo wa taratibu nafika kijijini na mzee ananielekeza wapi nimshushe.

Nilipomshusha mzee,ananikaribisha ndani na anasisitiza japo nipate kikombe cha maji ya kunywa,naingia kwenye nyumba moja kuu kuu ambayo inaonekana enzi zake ilikuwa nyumba hasa. Ninapokaa kwenye kochi moja la kizamani namuona mzee anaingia ndani analeta chupa ya chai mezani! Mzee ananimiminia kikombe cha chai na mazungumzo yanaendelea! Mzee anaingia ndani na kuniletea picha mbili akiwa amezishika mkononi! Napokea na kuziangalia ni picha za rangi ambazo zimefifia kiasi. Mzee ananiambia "huyu ni mimi tena enzi hizo nikiwa mtu kweli kweli.

Nilikuwa mwanajeshi kwenye jeshi la wananchi wa Tanzania, nilistaaf miaka ya 2006 nikiwa na cheo cha Saa Meja! Kijana wangu usinione hivi leo nilivyo mimi enzi zangu nilikuwa mtu sana,nimeshiriki vita ya kumuondosha Dikteta Idd Amin kule Kagera,nimeshiriki kwenye kuleta Aman Kongo,nimeenda Msumbiji,nimeenda Africa ya Kati. Kijana wangu enzi hizo tunavaa gwanda tulikuwa tunaheshimiwa kwelikweli"

Mzee anaongea maneno kadhaa ya kilugha ambayo hata sikuyaelewa! Mzee ananiambia "kijana wangu kila enzi na enzi zake,sasa nimekongoloka, wezangu wengi wametangulia,wakati ule nilikuwa naishi kwenye kambi za jeshi maeneo ya lughalo, nilipostaafu niliamua kurudi nyumbani kijijini kwetu na hapa ndio nilipozaliwa na kukuwa. Nilianzia shule hapa na wazazi wangu pia waliishi hapa. Nilitamani nifanye ufugaji wa ng'ombe za kisasa ila shughuli ilinishinda kadri miaka inavyosogea nguvu zinapungua sana. Niliporudi hapa nilikuwa na fedha kiasi za kiinua mgongo na ndipo nilipojenga hii nyumba unayoiona!

Nilinunua na mashamba kadhaa ambayo hadi sasa nalima japo nguvu zimeisha kijana wangu,naokoteza chakula cha kula. Mke wangu ameenda kuishi na watoto huko mjini na alikataa kuishi hapa kijijini baada ya kuona sio maisha aliyozoea, kijana wangu huwezi amin hapa naishi peke yangu kabisa sina hata mtu wa kukaa naye"

Ninapoendelea kumsikiliza huyu mzee akilini vinapita vitu vingi sana,Nilikuwa naenda kuangalia shamba la viazi ila hiki ninachokutana nacho ni zaidi ya viazi mbatata. Naanza kuwaza huyu alikuwa mwanajeshi tena hodari kweli kweli na anazo beji kadhaa alizowahi kushiriki vita na mapambano kadhaa kama askari wa jeshi la wananchi lakini sasa yupo hoi bin taabani huku kijijini tena anaishi bila hata matumaini. Sasa mimi mtoto wa Mjasiriamali uzee wangu utakuaje? Daaah naendelea kukata kikombe cha chai niliyopewa na mzee nikiwa sijui hata sukari ameipata wapi kwa wakati huu.

Mzee ananiambia "ukienda mjini wakumbushe vijana wangu na wanangu kuwa kuna kesho na inahitaji maandalizi,waambie kuna uzee. Waambie wale askari wanaovaa magwanda ipo siku watayavua! Waambie heshma wanayopata leo sababu ya kofia wanazovaa ipo siku haitakuwepo maana watavua tu wakati wa kustaafu utakapofika.

Kawaambie vijana wangu maana utakuwa umewasaidia. Kawaambie kuwa sasa wanaukimbia ujasiriamali sababu wana mishahara na posho nyingi. Achilia mbali vyeo na misheni nyingine zinazowapatia pesa ila wakumbushe kuwa baada ya kustaafu watapaswa kurudi kwenye ujasiriamali kwa lazima,watastaafu kazi ila tumbo halina kustaafu.

Mzee anasema wakumbushe kuwa heshma wanayopata barabarani sababu ya nguo nyeupe wanazovaa na nembo ya Taifa iliyopo kwenye kofia ipo siku haitakuwepo kabisa. Leo wanasimamisha magari na yanasimama ipo siku hata toroli au mkokoteni hautasimama baada ya kuvua hayo magwanda.

Kawaambie vijana wangu wale wenye mamlaka na wanaofanya kazi za serikali wafanye kazi kwa weledi mkubwa na wapende kazi na watu wanaowahudumia. Kawakumbushe kuwa wao sio bora sana sababu wana vyeo na elimu maana wapo wenye akili na ufahamu mkubwa ni vile tu hawakupata fursa au hawakuwa na mfumo wa kuwaingiza kwenye hizo ajira. Waambie wasifanye watu wakae kwenye mabenchi ya foleni kwa muda mrefu bila sababu wao wakiwa wanachezea simu zao.

Nenda kawaambie vijana wangu hasa wale wanaofanya kazi kwenye mahakama za Tanzania kuwa wana wajibu wa kutoa haki kama walivyojifunza kwenye sheria. Leo wapo kwenye mamlaka ya kuamua vema ila ipo siku watatoka kwenye hayo mamlaka na kurudi kwenye maisha ya kawaida kabisa na hawatakuwa na uwezo hata wa kutoa maamuzi kwenye kesi za kuku maana wakati wao utakuwa ushapita hivyo wajiwekee akiba kwa kutenda kwa haki.

Nenda kawakumbushe vijana wangu wanaokusanya kodi za serikali. Waambie hayo ni mapito tu wafanye kwa haki maana.wakumbushe kuwa mwalimu anaona vizuri akiwa anasahihisha makosa ila hata yeye akisahihishiwa makosa yake yataonekana.Waambie wapange kodi kwa watu kama wanavyostahili na kuwapa elimu kiusahihi namna ya kulipa kodi. Wasiwaonee wajasiriamali wadogo ambao hata elimu ya kodi hawana. Wasiowaonee wamama wenye vibiashara vidogovidogo. Wasimnyanyase yeyote sababu ya vyeo vyao, watende kwa haki na kesho yao ipo mikononi mwao, Wanawenza kuibomoa kesho yao kwa kujifanya hawaoni leo yao.

Kijana wangu Nenda kawaambie matabibu na wauguzi kule kwenye Vituo vya afya,zahanati na Hospitalini kuwa wawatibu watu kwa upendo maana huo ni wito. Rushwa ndogo na kubwa wanazopokea leo ipo siku zitakoma kabisa na watapaswa kuanza maisha mapya na wenyewe watarudi kutibiwa kama watu wengine. Japo wao wanasema ujuzi wao hauzeeki ila waambie kuwa wakati ni ukuta watende wema tu na ndio akiba yao ya baadae.

Kijana wangu nenda kawaambie wafanyakazi wa benki na taasisi zote za fedha wajitahidi kutenda haki na watoe huduma kwa upendo, huwa tukifika benki wanatuangalia kwa dharau na kuna saa wanadhani wao hawatazeeka. Kijana wangu, tunaenda benki mara moja kwa mwezi kuchukua kiinua mgongo tena fedha yenyewe hata laki 2 haifiki ila tunapofika huwa wanatuangalia kwa dharau sana na wanahisi sababu ya uzee hatuelewi. Waambie zile ni ofisi tu na sisi tulipita huko. Ipo siku watastaafu.

Kijana wangu, waambie wanasiasa na watunga sera, wasipotengeneza sera bora za kuwasaidia wazee leo kesho na wao watakuwa wazee hivyo zitawahusu tu na wataziishi kwa lazima. Waambie wasitumie wazee kwa maslahi yao pekee wanapohitaji nafasi za uongozi ila wawasaidie wazee kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa.

Kijana wangu nisikuchoshe sana ila naomba usisahau kuwaambia waalimu kuwa wafanye kazi hiyo kwa juhudi sana maana wanaandaa Taifa la kesho. Waambie wasisitize uzalendo kwa wajukuu zetu. Waambie walimu kuwa wao wanaishi sana na wanafunzi au watoto wetu. Kwenye siku 7 wao wanaishi na watoto wetu siku 5. Kwenye miezi 12 wao wanaishi na wajukuu zetu miezi 10. Walimu wana sehemu kubwa ya kuathiri Utaifa na Uzalendo kwa watoto wetu. Tafadhali waambie Walimu wasivunjike mioyo na wafanye kazi yao kwa uadilifu japo wanayo mahitaji mengi ila hata wasipoyapata Mungu atawalipa"

Mzee anasema "Waambie wajasiriamali waendelee kupambana na ujasiriamali huku wakiweka akiba kidogo kwa ajili ya uzee wao maana uzeeni nguvu zinapungua na hawataweza kufanya kazi kama vijana"

Mzee anatoa lesso yake,anafuta machozi,ananipokea picha kadhaa alizonipa niangalie. Mzee ananiambia "ipo kesho kijana wangu,mimi nilichezea jana yangu na leo yangu ndio hii,hapa naweza kufa huku ndani na maiti yangu ije igundulike baada ya wiki au mwezi. Nina vijana wangu watatu ila hii simu inaweza ikakaa hata mwezi hawajaipiga. Wao wapo na mama yao tu sasa wamenisahau kabisa ila hilo pia uwaambie vijana wangu kuwa wasiwasahau wazazi wao, hatuna mahitaji makubwa sana maana bado tunapambana kwa nguvu zetu ila tunatamani upendo wao" Machozi yalianza kunitoka. Mtoto wa Mjasiriamali huzuni inanishika na ninashika simu yangu ya mkononi kuzima sehemu ya kuzimia.
 
Wafanyakazi wengi wa serikalini walikuwa wanajiona zaidi ya wafalme, ila muda wao ukisha huwa wanyonge sana na wenye hekima kweli.

Huwa najiuliza hii hekima ya uzeeni kwanini hawakuwa nayo ujanani, tena pale wakuwapo makazini?.
 
Back
Top Bottom