TFF ya Malinzi inaongozwa kwa mbwembwe

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,020
367_malinzi.jpg



KUNA ule usemi wa Kiswahili usemao, ‘Matendo hukidhi haja maridhawa, kuliko maneno'. Lakini pia kuna ule mwingine wa, ‘Maneno matupu hayavunji mfupa'.

Hii ni misemo miwili ambayo inaelekea kuwa na maana moja ya kwamba, hakuna haja ya kuwa na maneno mengi bali matendo ndiyo jambo la msingi pale mtu anapopania kufanya kitu chochote.

Napiga picha jinsi ilivyokuwa mwaka jana mwishoni, wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi wa Shirikisho la soka nchini, (TFF). Yaani kwa jinsi wagombea walivyokuwa wakihaha kutangaza sera zao iwapo wataingia madarakani.

Rais wa sasa wa TFF, Jamal Malinzi ndiye aliyeshinda uchaguzi huo, baada ya kuhangaika sana, hadi huko FIFA. Ni vizuri kwa sababu alikuwa akitetea haki yake na hatimaye ilitendeka akaingia madarakani.

Wazaramo wana usemi wao ambao wanapenda kuutumia sana: ‘Zilongwa mbali zitendwa mbali'. Usemi huu una maana kwamba kinachoongelewa sio kinachofanyika.

Kwa wale wanaofuatilia masuala ya soka watakubali kuwa moja ya vitu vinavyomuweka mgombea madarakani ni pamoja na kuwa na sera nzuri ambazo wapiga kura wake wanakuwa na imani kuwa anaweza kuzitimiza akishakuwa madarakani.

Kwa hakika, Malinzi alifanikiwa kuzinadi vizuri sana sera zake, hali kadhalika historia yake ya kuwa katika mchezo wa soka ikampa sifa zaidi akaingia madarakani kuwa Rais wa TFF.

Kwa sasa, Malinzi na timu yake wana muda wa takribani miezi tisa tangu waingie madarakani. Kitu alichofanya kwanza alipoingia madarakani ‘akawapiga chini' baadhi ya watendaji wa ngazi za juu waliokuwepo katika uongozi uliopita. Akapanga safu yake.

Baadhi ya wadau wakakosoa hilo, lakini pia kuna waliomtetea wakasema kuwa rais yoyote au kiongozi yoyote akiingia madarakani huwa anapanga safu yake. Haikuwa mbaya sana, akazisuka upya kamati 18 za TFF.

Hilo likapita, kwani alisema kuwa hiyo ni njia mojawapo kwake kujipanga kwa ajili ya kuleta maendeleo katika soka la nchi hii ambalo miaka nenda rudi, hadithi ni ile ile ya kuboronga na kutong'ara kimataifa.

TFF wakaanza na mpango maalumu wa kuboresha timu ya soka ya taifa, Taifa Stars. Wakawakusanya vijana kutoka mikoa yote wakawekwa kambini Lushoto. Baada ya hapo walipatikana vijana wachache ambao walikwenda Mbeya na hatimaye wakapatikana wengine wachache wakajiunga na timu ya taifa.

Wakati hayo yanafanyika, kulikuwa na mchakato mwingine wa kumpata kocha wa Stars kwa sababu, moja ya mabadiliko yaliyofanywa na Malinzi alipoingia madarakani ni pamoja na kumtimua kocha wa timu hiyo, Kim Poulsen na kuahidi kumtafuta kocha mwingine mwenye uzoefu na timu za Afrika.

Hilo nalo liliwakera baadhi ya wadau kwa sababu Poulsen ni kocha ambaye alikuwa amekaa muda mrefu, awali kabla ya kuwa kocha wa Stars alikuwa kocha wa timu ya vijana. TFF hawakujali hoja hizo, hatimaye wakampata kocha mpya wa sasa kutoka Uholanzi, Mart Nooij.

Alichofanya kocha huyu mpaka sasa ni kuwaondoa kimtindo wale wachezaji waliopandishwa kutoka katika mpango wa maboresho, akitaka kuwa na wale wenye uzoefu. Sasa hivi timu ya Taifa inatawaliwa na wachezaji wakongwe tu.

Kuna wadau wa soka ambao wameenda mbali zaidi na kusema kuwa TFF walikosea kufanya mchakato wa kuboresha Stars, kabla hawajapata kocha, bali wangemsubiri kocha ili afanye mwenyewe kazi hiyo ya kuangalia vipaji vipya ambavyo vingeboresha timu ya taifa.

Kuna wakati, TFF walifikiria kubadilisha jina la Taifa Stars na jezi, vitu ambavyo ni muhimu, lakini sina uhakika kama huo ulikuwa wakati wake.
Katika msukosuko wa uchaguzi mkuu wa Klabu ya Simba uliofanyika hivi karibuni, TFF walijichanganya pale walipozuia uchaguzi huo usifanyike lakini wakairuhusu Kamati ya Rufaa ya TFF kupitia rufaa ya aliyekuwa mgombea wa nafasi ya urais, Michael Wambura.

Lakini pia TFF walisimamisha uchaguzi huo kinyume na katiba ya Simba, ambapo kamati ya uchaguzi ya klabu hiyo inaelekeza kwamba kamati ya uchaguzi ndiyo yenye maamuzi ya mwisho na haipaswi kuingiliwa na mtu yeyote isipokuwa kuishauri. Walichotakiwa kufanya TFF ni kutoa ushauri na si kutoa uamuzi.

Funga kazi sasa, wakati sarakasi hizo zote zikiendelea, TFF walihamisha ofisi kutoka Uwanja wa Karume, Ilala, hadi katikati ya jiji la Dar es Salaam jengo la PPF Tower. Sababu kubwa iliyotolewa ni kutaka kufanya ujenzi wa jengo kubwa la kibiashara pale Karume.

Hakuna ujenzi uliofanyika hadi sasa, na taarifa nilizozipata ni kwamba katika jengo hilo gharama ya pango si chini ya Sh milioni 10 kwa mwezi.
Juzi, ujumbe wa Shirikisho la soka Duniani (FIFA) ulikuwa nchini kwa ajili ya mazungumzo kuhusu maboresho mbalimbali ikiwemo utawala, fedha, masoko, ufundi, mashindano na timu za taifa.

FIFA wamewaambia TFF kurudi Karume, wakidai kuwa huo ni ubadhilifu wa fedha. TFF hawana kipingamizi kwa hili la kurudi Karume. Lakini, je, wakati wanafanya uamuzi kama huo waliwashirikisha wadau wangapi ambao waliona kuwa ni sahihi wao kuhama Karume?

Kwa tafsiri ya haraka haraka, kuna aina fulani ya ukurupukaji ndani ya TFF katika utendaji wake katika mambo mengi. Tukianza na la kumfukuza kocha Kim Poulsen, Maboresho ya Stars, Uchaguzi wa Simba na hili la kuhamisha ofisi, hakuna lolote lililoleta mafanikio ya kusifiwa.

TFF sasa imekuwa ya mbwembwe tu, maneno mengi na mipango ambayo inaonekana kuwa uzaaji wake wa matunda ni mgumu sana kutokana na mipangilio mibovu tokea awali.

Kasoro kubwa ambayo imekuwepo, hata kwa uongozi uliopita wa TFF, ni kuangalia vikombe na si kuangalia jinsi ya kujipanga kwa ajili ya kufanya vizuri baada ya miaka minne au zaidi kwa wakati ujao.

Kuna haja ya kupunguza maneno na kufanya kazi ya kukuza soka. Bado Malinzi na wenzake wana muda mrefu katika uongozi wao. Kwa maana ya kwamba wanatakiwa kujirekebisha na pale wapoona kuna ugumu basi wawatumie wataalamu.

Chanzo: RaiaMwema

 
Back
Top Bottom