Teknolojia ya Alama za QR inavyoweza kubadilisha biashara yako

Status
Not open for further replies.

JamiiTalks

JF Advocacy Team
Aug 7, 2018
625
938
qr_Instagram copy_Twitter.jpg


Moja ya changamoto ya kutoa huduma yenye ushindani ni kutumia njia ya haraka na salama ya kutoa taarifa kuhusu bidhaa au huduma yako. Kama njia ya kurahisisha upatikanaji wa taarifa, teknolojia inawezesha uwezo wa kuhifadhi taarifa kuhusu bidhaa au huduma katika mfumo utakaowezesha taarifa hiyo kupatikana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kwa mfumo wa QR Code, au Msimbo wa QR.

QR Code (Quick Responce) Code ni mfumo wa kuhifadhi taarifa kielektroniki ambao unaweza kutambuliwa na vifaa vya kielektroniki kama simu ya mkononi na hutumika katika magazeti, tovuti na matangazo, au hata kulipia bidhaa na huduma mtandaoni. Mfumo huu umeleta mapinduzi ya utoaji wa huduma kwa kupunguza muda wa utoaji huduma na kuongeza usalama wa usafirishaji wa taarifa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.

Mfumo wa kutumia Alama za QR ni mwendelezo wa mfumo wa bar code ambao ulianza kutumika zaidi ya miaka 60 iliyopita. Bar code hufanya kazi kwa kuhifadhi taarifa katika mfumo wa mistari na namba ambayo huweza kutafsiriwa na vifaa vya kielektroniki kuonesha aina ya bidhaa, thamani au ubora wake. Mfumo huu wa bar code hutumika katika kutambua bei ya bidhaa katika baadhi ya maduka, hasa maduka makubwa (super markets).

Tofauti na bar code, QR Code inaweza kuhifadhi taarifa nyingi zaidi, kama vile namba ya simu, kuunganisha wi-fi, kuandika barua pepe au ujumbe mfupi wa maandishi (text message). Mfumo huu sasa ndio mfumo unaotumika zaidi wa kuhifadhi taarifa, ukitumiwa na zaidi ya watu bilioni 2.7 wanaotumia simu janja (smartphones) mwaka 2019, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kufikia mwishoni mwa mwaka 2020.

Unawezaje kutumia Alama za QR katika matumizi yako ya kila siku?
Upatikanaji wa mtandao wa intaneti duniani unatarajiwa kuongezeka kufikia asilimia 90 ya watu wote duniani kufikia mwishoni mwa mwaka 2020, na hii inaongeza umuhimu wa kuwa na mfumo utakaowezesha upatikanaji wa taarifa kwa njia rahisi.

QR Code ni huduma ya wazi inayoweza kutumiwa na mtu yeyote; unaweza kutengeneza Alama za QR kwa ajili ya matumizi ya biashara yako mwenyewe au kutumia Alama za QR zilizotengenezwa kwa ajili ya kupata huduma kwa njia rahisi. Baadhi ya tovuti unazoweza kutumia kutengeneza Alama za QR kwa matumizi yako binafsi ni pamoja na
ForQRCode, QRZebra, Beaconstac's QR Code Generator na Unitag.
Kupitia tovuti zote hizi, unaweza kutengeneza QR Code kwa ajili ya huduma na bidhaa zako bure, ingawa unaweza kulipia ikiwa utahitaji kutumia QR Code yako kufanya vitu vingi zaidi.

Baadhi ya mambo unayoweza kufanya kwa kutumia Alama za QR ni pamoja na:
1. Kuwaelekeza wateja wako katika tovuti yako
Badala ya kutumia njia ya anwani ya tovuti, wateja wako wanaweza utumia Alama za QR kutembelea tovuti yako, kwa kuwa QR Code inaweza kuhifadhi taarifa za anwani ya tovuti yako hivyo kupunguza muda anaoweza kutumia mtu kuandika anwani ya tovuti.
Angalia Alama za QR ya tovuti ya JamiiForums.

JamiiForums.png


2. Kupiga simu au kuhifadhi taarifa za namba ya simu
Alama za QR inaweza kutumika kuhifadhi taarifa zako binafsi ikiwemo namba yako ya simu, na huokoa muda wa kubadilishana taarifa kwa kuandika namba ya simu kisha kuihifadhi kwenye simu yako. WhatsApp, kwa mfano, ilianzisha huduma ya kutumia QR Code kupata taarifa zako au za mtu mwingine kwenye simu yako. Kufahamu zaidi kuhusu jinsi ya kutumia huduma ya QR Code ya WhatsApp bonyeza hapa.

3. Kutuma ujumbe mfupi wa maandishi au barua pepe
Mfumo wa matumizi ya Alama za QR ni njia nzuri na rahisi zaidi ya kuleta ukaribu baina yako na wateja wako kwa kutengeneza taarifa ya ujumbe mfupi ambao utahifadhiwa ndani ya Code hiyo. Mtumiaji wa Alama za QR anaweza kutuma au kupokea ujumbe baada tu ya kutambaza (scan) Alama za QR hiyo kwa kutumia simu yake. Njia hii huweza kusaidia kuongeza mauzo ya bidhaa, kutoa msaada pale unapohitajika, au kuwaunganisha wateja wako na huduma binafsi kuhusu bidhaa yako.

4. Kupakua programu nukushi (Apps)
Hii ni njia rahisi ya kuwaelekeza wateja wako kupakua programu nukushi kutoka Playstore au Appstore kwa kuwatengenezea QR Code ambayo itawapeleka moja kwa moja kupakua programu yako. Baadhi ya makampuni ya kibiashara kama vile Angry Birds yamekuwa yakitumia mbinu hii kuongeza idadi ya watu wanaopakua programu zao. Zaidi, baadhi ya makampuni kama Spotify yametumia QR Code kama njia ya kuweza kupendekeza wimbo kwa mtu mwingine, ambapo baada ya ku-scan QR Code, mtu mwingine anaweza kutumiwa anuani ya tovuti itakayompeleka moja kwa moja kusikiliza au kupakua wimbo huo.

Alama ya QR ya Angry Bird


5. Kuwaelekeza wateja wako kufika ofisini kwako
Alama za QR zinaweza kutumika kuwaelekeza wateja wako kukufikia ulipo kwa urahisi. Unaweza kutengeneza Alama za QR zenye taarifa kuhusu biashara yako ilipo na kumpunguzia mteja usumbufu wa kutafuta biashara yako ilipo mtandaoni.

6. Kuwaunganisha wateja wako na kurasa zako za mitandao ya kijamii
Hii ni njia ya kuongeza ukaribu wako na wateja wako. Unaweza kuweka taarifa za mitandao ya kijamii za biashara yako katika Alama za QR na kumfanya mteja kufuatilia kinachojiri kuhusu bidhaa au huduma yako. Zaidi, unaweza kuweka njia ya kutoa punguzo la bidhaa au huduma ikiwa mteja atafuata mitandao ya kijamii ya bidhaa au huduma yako kupitia Alama za QR.

7. Kuuza na kununua bidhaa mtandaoni
Kutumia Alama za QR ni njia rahisi ya kufanya biashara mtandaoni (E-Commerce). Alama hizi zinaweza kutumika kutafuta bidhaa unayoitaka mtandaoni, na mara nyingi huwekewa punguzo. Njia rahisi inayoweza kumfanya mteja kununua bidhaa mtandaoni kwa njia kutumia Alama za QR ni kwa kumwekea maelezo anayohitakiwa kufanya kwa kutumia Alama hizo, mfano, "Nunua Sasa" "Lipa Hapa" nk., ikiwa ni sehemu ya kumshawishi mteja kuchukua hatua ya kununua bidhaa au huduma yako.

Alama za QR ni njia bora zaidi kuendesha biashara yako mtandaoni kwa kukusaidia kufuatilia mwenendo wa biashara yako mtandaoni. Kwa kutumia Alama za QR, unaweza kubaini soko lako na kuliwekea msisitizo kwa kupata taarifa za wateja wanaotumia Alama za QR na kuongeza uwezo wako wa kuwafikia wateja kwa urahisi.

Kama hiyo haitoshi, baadhi ya huduma, kama vile huduma za afya hospitali, zinaanza kutumia Alama za QR kuhifadhi taarifa za wateja wake. Katika baadhi ya hospitali, mgonjwa anaweza kubandikwa karatasi yenye Alama ya QR mkononi inayoonesha taarifa zote muhimu za mgonjwa kwa ajili ya kuwasaidia manesi au madaktari, ikiwamo taarifa zake binafsi, ugonjwa unaomsumbua, dawa anayotumia, muda wa kupewa dawa, tarehe anayotarajiwa kutoka nk.

Kama wewe ni mbunifu unayependa kuendana na wakati, ni wakati wako kujiongeza na kuanza kutumia teknolojia inayoweza kukurahisishia utendaji wako wa kazi na kukufungulia milango ya kukutana na wateja wapya na kukuza biashara yako.​
 
Status
Not open for further replies.
Back
Top Bottom