Tasnifu za njano5: Uhusiano kati ya dini na siasa za tanzania

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Nov 22, 2012
1,985
1,282
Naomba kujua hivi siasa na dini hapa Tanzania vinahusiana vipi naomba majibu hasi na chanya.[ Hilo ni swali aliloniuliza Devis Shirima]

Kwanza sitaki kuamini kuwa muulizaji aliposema majibu hasi na chanya alidhamiria kupatiwa majibu yenye kuridhisha na yasiyoridhisha, kwa hivyo nataka kuamini kuwa muulizaji alitaka nioneshe pasina shaka yoyote uhusiano chanya na hasi kati ya siasa na dini. Hivyo naomba nijikite katika kujadili huo uhusiano wa mambo hayo. Kwa kuanzia nafikiri kuna haja ya kujua maana ya Dini, Udini na Siasa. Nitajaribu kufafanua kwa kutumia ufahamu wangu na ninapenda kujifunza toka kwenu.

DINI:
DINI ni mfumo wa maisha wenye lengo la kuleta upatano kati ya mja na Mungu wake. Mungu ni nini? Mungu ni uwezo unaoweza na usiwezwa na kitu chochote. Kuna miungu mingi sana na tena iso na idadi, hata Mungu wa kwenye Biblia na Qur-an wanakubali kuwa kuna miungu mingi. Nimelazimika kutumia vitabu hivyo katika kuthibitisha kuwa miungu iko mingi kwasababu asilimia kubwa ya watanzania ni waumini wa vitabu hivyo.


"Yaangalieni hayo yote niliyowaambia; wala msitaje kabisa majina ya miungu mingine, wala yasisikizwe kutoka kinywani mwako"
Kutoka 23:13

"Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake, Azar: Unayafanya masanamu kuwa ni miungu? Hakika mimi nakuona wewe na watu wako mmo katika opotofu ulio wazi."
Qur-an 6:74

Mfano ya miungu maarufu ni Yesu, Yehova, Allah[s.w], Budha, Jua, na mizimu. Kwakuwa miungu iko mingi basi pia dini ziko nyingi pia. Hapa petu Tanzania ziko dini nyingi pia, ila dini kubwa na maarufu ni mbili ambazo ni Ukristo na Uislamu, zote hizi ni za kigeni.

UDINI:
Udini kwa fikra zangu ni kile kitendo cha kuwabagua, kuwatenga, kuwanyanyasa na hata kuwatesa watu wa dini fulani tu huku watu wengine wakiendelea kuneemeka. Pamoja na hayo siwezi kusema kuwa nchi ya Uingereza ina udini kisa tu serikali ya nchi hiyo inafuata na kutii mambo kadhaa ya kanisa la kianglikani, siwezi kusema kuwa nchi ya Italy ina udini kisa tu inatii na kufuata mambo kadhaa ya kanisa la Roma, pia siwezi kusema kuwa Saudi Arabia ina udini kisa tu inafuata na kutii mambo kadhaa kiislamu.

Katika nchi ambazo idadi ya wakristo ni kubwa, mfano izidi % 90, ni sawa kwa nchi hizo kuingiza mambo kikristo katika taratibu zao za kuendesha nchi ili mradi tu hizo taratibu hazitaondoa uhuru wa kuabudu kwa watu wa dini zingine. Katika nchi hizo si vibaya kwa serikali kutumia fedha za umma kujenga makanisa au kusaidia miradi ya kanisa. Pia katika nchi ambazo idadi ya waislamu kubwa, mfano iwe ni zaidi ya % 90 ni sawa kwa serikali za nchi hizo kuingiza mambo ya kiislamu katika uendeshaji wa nchi. Katu huu huwezi kuuita ni udini.

Katika nchi ambazo idadi ya waislamu na wakristo inalingana au inazidiana kidogo haitakiwi hata kidogo, naam, japo kwa kudhaniwa kuwa serikali inatumia fedha za umma katika kufadhili au kusaidia miradi ya dini fulani, au inajihusisha katika taratibu za kiibada za dini fulani. Mambo yanayofanywa Italy au Saudia hapa kwetu yanatafsirika kuwa ni udini. Mfano wa mambo hayo.

Baadhi ya viongozi wa serikali kutoa matamko yenye kuwapa uhalali waislamu kuchinja na kuzitia hila nyama zilizochinjwa na wakristo.
Serikali kushughulikia suala la mahakama ya kadhi,
Serikali kuvunja EAMWS na kujihusisha katika uundwaji wa BAKWATA,
Mkataba wa MOU,
Ofisi za umma kupambwa wakati wa X-MASS kwa kutumia fedha za umma.

SIASA:
Siasa ni njia ya kufanya maamuzi ya umma katika mji, au nchi au duniani haijalishi kwa maslahi ya umma huo au kwa maslahi ya watu wachache. Kwakuwa masuala mengi yanayohusu umma kama vile ya afya, ajira, elimu, na mengi ya kufananayo yanahitaji maamuzi ya umma, na kwakuwa siasa ndio njia ya kufanya hayo maamuzi ya umma, hivyo basi mambo yote yanahouhusu umma hutawaliwa na siasa. Kwa hivyo napata uhalali wa kusema kuwa siasa ndio kila kitu kwa mustakabali wa umma na katu mwanadamu hawezi kujitenga na siasa midhali yungali ni sehemu ya umma.

Kila umma huwa na utamaduni wake, aghalabu njia ya kufanya maamuzi ya umma katika taifa lolote huathiriwa na utamaduni wa taifa hilo. Ndani ya utamaduni wa umma fulani kuna mambo kadhaa yanayofanya jamii zinazounda huo umma husika kuungana na kutafautiana. Dini moja ya mambo yanayopatikana ndani ya utamaduni. Katika utamaduni wa taifa la Italy ndani yake kuna dini ya kikristo, dini hiyo ndio kitu kikubwa kinacho waunganisha waitaly na ni sehemu ya utamaduni wao.

Kama nilivyosema hapo juu kuwa njia ya kufanya maamuzi ya umma katika taifa lolote huathiriwa na utamaduni wa taifa husika, hivyo si ajabu na wala si mwiko katika kidogo kwa siasa za Ujerumani, Italy, na Uingereza kutawaliwa na mambo ya kikristo, pia si vibaya kwa Saudia na Iran siasa zake kutawaliwa na Uislamu. Kwanini dini katika mataifa haya zikajikuta zinaingia katika siasa nzima nzima[fully]?

Pamoja na mambo mengine, sababu kuwepo kwa dini katika jamii ni kuhakikisha hiyo jamii inakuwa na maisha bora. Kwa vyovyote vile suala la maisha bora kwa jamii linahitaji maamuzi ya umma juu ya mambo kadhaa ambayo kwayo umma utaona kuwa yataleta maisha bora endapo yakifanywa. Kwakuwa dini inataka jamii iwe na maisha bora, na kwakuwa suala la maisha bora linahitaji maamuzi ya umma, hivyo basi dini hulazimika kuikiingia kwenye siasa aidha ikiwa nzima au kidogo.[fully or partially] Bw Shirima kabla sijaitupia jicho Tanzania, naomba ujue kuwa siasa na dini zinahusiana katika muktadha huu.

SIASA ZA TANZANIA NA DINI.
Tanzania tuko na dini kubwa mbili ukristo na uislamu. Kwakuwa siasa za taifa lolote huathiriwa na utamaduni wake, na kwakuwa dini kimaumbile ina tabia ya kujiingiza kwenye siasa, hivyo basi hata hapa nchini siasa zake huathiriwa na dini zenye idadi kubwa ya watu katika namna ya kuyakumbatia yale yanayoziunganisha hizo dini na kuheshimu yale yanayozitofautisha hizo dini. Kwakuwa asilimia kubwa ya watu katika umma wana dini, hivyo ni lazima maamuzi ya umma yaathiriwe na dini hata kiukweli hizo dini zinatafautiana.

Mfano sikukuu ya Iddi ni ya waislamu, iweje serikali isiyokuwa na dini ikaweka siku ya sikuu hii iwe mapumziko? Pia sikukuu ya X-MASS ni ya kikristo, pia iweje siku hii serikali ikaifanya ni ya mpumziko? Maamuzi ya serikali kufanya siku hizi kuwa za mapumziko yameshinikizwa na dini hizo. Kwakuwa kwa mujibu wa ukristo sikukuu ya iddi si halali, kwakuwa kwa mujibu wa uislamu sikuu ya X-MASS si halali, na kwakuwa siasa imezifanya siku za kusheherekea sikukuu hizi ni mapumziko, hivyo basi naweza kusema kuwa dini zimeingilia siasa za Tanzania katika namna ya kuvumiliana.

Niseme jambo moja kuwa dini ya kikristo na kiislamu hapa Tanzania zimejiingiza kidogo katika siasa, kama nilivyosema hapo awali kuwa, pamoja na mambo mengine, lengo la kuanzishwa dini ni kuleta maisha bora kwa jamii, na kwakuwa maisha bora ya jamii huhitaji maamuzi ya umma juu ya mambo kadhaa ambayo kwayo umma unaona pindi yakifanywa maisha yatakuwa bora, hivyo basi dini zetu nazo hujiingiza katika siasa kwa minajili ya kuharakisha harakati za kuleta maisha bora.

Matamko ya maaskofu, mashekhe, wachungaji, maimamu na viongozi wa kidini juu ya ufisadi na uvunjaji wa sheria unaofanywa na serikali ni kishiria cha dini hizi kutaka kuathiri njia ya maamuzi ya umma[siasa]. Hivyo tunaweza kusema kuwa dini inaingilia siasa kwa kiasi fulani kwa lengo kutaka umma upate maisha bora. Si vibaya hata kidogo kwa dini kuathiri siasa za nchi katika muktadha huu.

UDINI NA SIASA ZA TANZANIA.
Kama nilivyosema awali kuwa udini kitendo cha kuwabagua, kuwatenga, kuwanyanyasa na hata kuwatesa watu wa dini fulani tu huku watu wengine wakiendelea kuneemeka. Kitendo hichi chawezwa kufanywa na mtu au serikali au taasisi yoyote hususani zile ambazo si za kidini. Kwa kuzingatia tasfiri hiyo, udini unaweza usiwepo katika dola za kikristo au za kiislamu lakini ukawepo katika dola ambazo zinatangaza kuwa hazina dini. Pamoja na kwamba Uingereza ni dola ya kianglikani lakini huwezi kusema uingereza kuna udini kwasababu watu wa dini zingine hawabaguliwi bali wanaheshimiwa kama wanavyoheshimiwa waanglikani.

Kwa Tanzania kuna viashiria vingi vinavyoonesha kuwa serikali ya Tanzania ina udini. Kitendo cha serikali kuingia mkataba wa MOU na kujihusisha katika migogoro ya waislamu katika namna ya kuianzisha na hatimaye kuichochea ni kiashiria cha serikali ya Tanzania kuwa na udini.

Nilisema huko juu kuwa pamoja na kwamba lengo kuanzishwa dini ni kuleta upatano kati ya mja na mungu wake, lakini pia lengo lingine kuu la kuanzishwa dini kuleta maisha bora ya mwanadamu hapa duniani. Ikumbukwe kuwa wakati wa ukoloni serikali ya kikoloni ilikuwa inatoa huduma zake za jamii hususani elimu kwa kuupendelea ukristo. Kwa muislamu ili upate kusoma sharti ubatizwe na kuwa mkristo, waliobahatika kusoma bila kubatizwa ni watoto wa machifu.

Waislamu wa Tanganyika huku wakijua kuwa lengo la uislamu ni kuleta maisha bora, na kwa kuzingatia ukweli kuwa maisha bora hayapatikani endapo watu wakiwa hawana elimu, hivyo kwa unyonge wao wakaanzisha harakati za kupambana na ubaguzi wa kikoloni katika namna ya kudai uhuru, walifanya hivyo huku wakitarajia kuja kupata usawa ndani ya Tanganyika huru

Hapa tunaona dini tena ya kiislamu ilijiingiza katika siasa si kwa lengo la kupata upendeleo wa kidini, bali ni kwa lengo la kuleta maisha bora kwa umma. Siasa zile za ukombozi na za kudai uhuru zilitawaliwa na dini ya kiislamu, hata Nyerere mwenyewe mara kadhaa amenukuliwa akisema kuwa wazee wa Kiislamu walikuwa wanamwambia afunge, nyerere na waislamu walikuwa wanafunga na kusali kwa lengo la kupata uhuru kwa amani.

Baada ya uhuru mambo yakaanza kwenda tafauti, ikajengeka dhana kuwa SERIKALI inaupendelea UKRISTO. Dhana hii ikawafanya Waislamu kwa kupitia EAMWS kuendelea na harakati za kutaka usawa na ndugu zao wa kikristo. Serikali kwa makusudi ikauvunja EAMWS na kisha ikashiriki kwa namna fulani katika mchakato wa kuanzishwa kwa BAKWATA. Kama tujuavyo BAKWATA imekuwa ni kibaraka wa CCM na kubwa zaidi chini ya baraza hili mambo mengi ya waislamu yameharibika.

Hii ni kwa kuthibitisha tu, mara baada ya kutokea uchomaji wa makanisa jijini Dar es salaam, CHADEMA kwa kupitia wajumbe wake wa kamati kuu walitoa tamko. Katika tamko lao wote wiwili kwa pamoja Prof Safari na Wakili Mabere Malando walisema kuwa jamii ya kiislamu ilipambana katika kudai uhuru kwa lengo kupata serikali itakayoondoa ubaguzi, kinyume chake mara baada ya uhuru jamii ya kiislamu ikaendelea kubaguliwa. Chama hichi kupitia wajumbe wake walionesha udini uliopo kwenye serikali ya CCM.

Mwalimu Nyerere wakati akitetea msimamo wake wa serikali mbili, pamoja na mambo mengine alisema kuwa hatutaki serikali moja kwasababu Tanganyika ni nchi kubwa sana ukilinganisha na Zanzibar, kwakuwa tulikuwa tunapambana na ukaburu wa Afrika Kusini hatukutaka hata kwa bahati mbaya watu wadhani kuwa Tanganyika inaanzisha ukaburu mwingine kwa kuimeza Zanzibar, kwa hivyo tukaonelea Zanzibar iwe na serikali yake ndani ya Muungano.[Hapa naomba msomaji rejea kitabu cha "UONGOZI WETU NA HATIMA TANZANIA" cha Mwl Nyerere]

Sasa ikiwa Mwl Nyerere alitaka tuwe na serikali mbili kwa kuogopa kudhaniwa kuwa tunaimeza Zanzibar, iweje Nyerere alinyamaza kimya kwa kuona serikali ikingia mkataba na makanisa? Je, aliona ni sahihi kwa serikali kudhaniwa ni ya kikristo? Hivi ni jambo lipi baya zaidi, Tanganyika kudhaniwa inaimeza Zanzibar au serikali kudhaniwa ina udini? Hivi Mwl Nyerere hakuona kuwa upambaji wa ofisi za umma siku za X-MASS na mwaka mpya inajenga dhana ya udini? Pamoja na uzuri wa mkataba wa MOU kwa taifa, hivi Mwl Nyerere na viongozi wetu hawakujua kuwa mkataba huu unawafanya watu tudhani serikali inapendelea ukristo?

Katika nchi iso dini kama yetu ni heri na ni vema kwa kiwango kikubwa kwa dini kujiingiza katika siasa kwa lengo na dhumuni la kuleta maisha bora kwa umma, lakini ni hatari kwa siasa kuacha kutazama maslahi ya umma badala yake ikajikita katika kutii na kutimiza matakwa ya dini moja tu katika namna ya kubagua dini nyingine. Kama tulivyoona katika nchi za kiislamu au kikristo ni sawa kwa siasa kutii matakwa ya dini moja ambayo kimsingi asilimia kubwa ya watu katika nchi hiyo ni waumini wa dini hiyo.

Je, ni wakati gani kwa siasa za nchi zisizokuwa na dini hujiingiza katika udini? Siasa katika nchi hizi hukumbatia udini wakati ule viongozi wa kisiasa wanapoanza kuweka mbele maslahi ya dini zao kuliko maslahi ya umma, lakini pia panaweza kutokea taasisi ya kidini kuwarubuni viongozi wa kisiasa kwa rushwa kwa lengo la kuwafanya viongozi hao kutoa upendeleo kwa taasisi hiyo, hii ni kwa mfano, katika muktadha huu ni rahisi kukuta hata kiongozi wa kisiasa ambaye ni muislamu akashiriki katika dhambi ya udini kwa kutoa upendeleo kwa ukristo kinyume chake ni kweli pia. Waislamu wanadhani kuwa upenzi wa Nyerere kwa kanisa katoliki ndio msingi wa udini wa serikali unaondelea sasa. Wanadhani kuwa upenzi wake huo ukamfanya hata asaahu kuwa Tanzania ni nchi isiyokuwa na dini.

Pamojana kwamba kuna viashiria vingi vya udini kwa serikali yetu, lakini Tanzania yetu hakuna chuki ya kidini kati ya waislamu na wakristo. Wakristo na waislamu wanaishi pamoja kwa upendo mkubwa hata kufika hatua za mkristo kumuoa muislamu au muislamu kumuoa mkristo. Haya matatizo ya kupigana yaliyotokea huko Geita ni matokeo ya wanasiasa kutumia hila chafu katika kuthibitisha uwepo wa chuki za kidini au niseme udini kama anavyouita wenyewe.

Wakati hadi sasa SERIKALI ikiwa imeshindwa kujivua joho la dhana ya kuwa ni SERIKALI ya KIKRISTO, ndio kwanza imeamua kujitwika dhana nyingine kuwa ni SERIKALI ya KIISLAMU, hii ni pale CCM ilipotia suala la mahakama ya kadhi kwenye ilani yake ya mwaka 2005 na pale SERIKALI ilipoamua kulifanyia kazi suala hilo la kadhi kwa lengo la kutekeleza ilani yake. Hivi CCM na SERIKALI hawajui kuwa nchi yetu haina dini? Kadhi ni kitanzi kingine, kwani wakristo washapata midomo huku wakisaahu suala la MOU.

DINI NA MWANASIASA WA KITANZANIA:
Kwa kuanzia naomba ninukuu vifungu vya katiba yetu ya mwaka 77 venye kuonesha uhuru wa mtu kuabudu na kuamini dini anayotaka na kutangaza dini hiyo. Vifungu hivyo vya katiba vinatoa uhuru wa kila mtanzania kuamua kuwa na dini anayoitaka. Pia vinatoa uhuru kwa kila mtanzania kutangaza dini na imani yake juu ya mungu.
Kifungu cha 19.(1) Kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake. (2) Kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi, na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.

Mwanasiasa wa kitanzania ni sehemu ya jamii ya kitanzania, hivyo naye ana uhuru wa kuwa na dini na kuamini katika mungu. Karibu wanasiasa wote wa Tanzania wana dini zao, wengi wao ni wakristo na waislamu isipokuwa Kingunge Ngombare Mwiru ambaye yeye anaamini dini za kiasili. Kuwa mwanasiasa hakumaanishi kuwa ule uhuru wako wa kikatiba wa kuwa na dini na kuamini juu ya mungu basi ndio unaporwa na kazi za kisiasa.

Dr.Kikwete ni rais na mwenyekiti wa CCM dini yake muislamu.
Freeman Mbowe ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni na ni mwewnyekiti wa CHADEMA mkristo.

Aghalabu kila kiongozi wa kisiasa au mwanasiasa anakuwa na dini yake, lakini pia hutokea kiongozi wa kidini anakuwa mwanasiasa. Hii ina maanisha kuwa wapo viongozi wa kidini ambao ni wanasiasa au viongozi wa kisiasa.
Mfano:
Getrude Lwakatare ni mchungaji na mbunge wa kuteuliwa na rais.
Msigwa Peter ni mchungaji na mbunge wa jimbo la Iringa Mjini.
Dr.Wilbroad Slaa ni katibu mkuu wa CHADEMA na Padri.
Christopher Mtikila ni mwenyekiti wa chama cha DP na ni mchungaji.

Hawa wanasiasa na viongozi wa kisiasa wana uhuru kutangaza dini na imani zao, uhuru ambao unatolewa na katiba yetu. Kwa upande wa katiba ya nchi yetu hawa wanasiasa hawalazimishwi kutangaza dini na imani zao, ila kwa upande wa dini zao suala la kutangaza dini na imani ni wajibu kwa kila muumini. Wajibu huu ndio huwafanya viongozi wa kisiasa wakati mwingine kujikita katika utangazaji wa dini na imani zao hata kama hawapendi kufanya hivyo.

"Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa."
Marko 16:15-16

"Na kumbusha, kwani ukumbusho huwafaa Waumini."
Qur-an 51:55

Aya hiyo katika kitabu cha Marko 16:15-16 kinamtaka kila mkristo kutangaza Injili, jambo hili si la hiari, bali ni wajibu kwa mkristo kufanya hivyo, kinyume chake huu ukristo usingefika Tanzania na Afrika kwa ujumla. Katika aya hiyo ya Qur-an 51:55 inaonesha kuwa kila muislamu ana wajibu wa kuutangaza uislamu. Kwa hivyo, ni hiari kwa wanasiasa kujiingiza katika kutangaza dini kwa mujibu wa katiba ya nchi lakini ni wajibu kwa wanasiasa kutangaza dini kwa mujibu wa vitabu vyao vya dini.

Kwakuwa kila mwanasiasa anaweza kuwa na dini yake, kwakuwa kila mtu yuko huru kutangaza dini yake, na kwakuwa ni wajibu kwa muumini kutangaza dini yake, hivyo basi hatuwezi kumuuita "mdini" mwanasiasa anayetangaza dini yake na tutapingana na katiba ya nchi endapo tukimkataza mwanasiasa kutangaza dini yake. Kutokana na ukweli huu, ndio maana siku za jumapili Mch Lwakatare yupo kanisani akihubiri injili na siku za kazi yupo katika ofisi yake ya ubunge.

Kama nilivyosema huko juu kuwa mwanasiasa ataitwa "mdini" endapo tu akitumia siasa katika kuipendelea na kuinufaisha dini yake au atatumia siasa katika kuwabagua na kuwanyanyasa watu wa dini fulani. Kwa maana hii katu hatuwezi kumuita Dr.Slaa ni mdini hata kama leo hii akisimama kwenye jukwaa la kidini akihubiri injili, kwani yuko huru kuendelea na kazi zake za kisiasa sanjari na kumtangaza mungu anayemuamini na kumtegemea.

KASHFA ZA KIDINI NA UHURU WA KUTANGAZA DINI TANZANIA.
Pamoja na kwamba labda nitakuwa nimetoka nje swali nililoulizwa na Bw Device Shirima, lakini nafikiri niko na haja ya kuelezea kashfa za kidini na uhuru wa kutangaza dini. Kama nilivyosema huko juu kuwa, kwa mujibu wa katiba yetu kila mtu yuko huru kutangaza dini na imani yake, lakini ni wajibu kwa kila muumini kutangaza dini yake; hii ni kwa mujibu wa Qur-an na Biblia na ndio vitabu vya dini kubwa hapa nchini, hata Kingunge atakuwa na wajibu huo ingawa kitabu chake sikijui.

Dini ya ukristo na uislamu ni dini zenye asili moja, dini hizi mbili pamoja na uyaudi ni dini za asili ya Ibrahim. Kutokana na dini hizi kuwa na asili moja ndio maana kuna baadhi ya mambo zinatautiana na baadhi ya mambo zinapatana.
Kwanza zote zinakubali Mungu ni mmoja. Waislamu wanaamini kuwa huyo mungu mmoja hafanani na kitu chochote na ya kwamba hakuzaa wala hakuzaliwa. Mungu huyo ndio aliyemfanya Yesu kuwa nabii na mtume kwa wana waisraeli, ndiye aliyempaisha Yesu mbinguni na pia atamrudisha tena duniani. Hivyo ni wajibu kwa waislamu kuitangaza imani hii.
Wakristo pia wanaamini kuwa mungu ni mmoja. Isipokuwa Mungu huyo mmoja amegawanyika katika nafsi tatu, yaani, Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu; hawa watatu wote ni umoja na si watatu. Kuhusu hii imani ya utatu naomba kutoa ufafanuzi kidogo.

Kwa mfano, kuna mtu anaitwa Bw Njano5.

Huyu Bw Njano5 anafundisha Facebook Nussary School, pia analima mpunga huko Kilombero Morogoro, pamoja na kulima na kufundisha Bw Njano5 ana mke lakini hawakubahatika kupata watoto.

Hivyo basi huyu Bw Njano5 atakuwa anatambulika kama ifuatavyo.
Wanafunzi watamwita Bw Njao5 kwa jina la mwalimu.
Watu wa Kilombero watamwita Bw Njano5 kwa jina la Mkulima.
Mkewe atamwita Bw Njano5 kwa jina la "Mume wangu" au "Baba Kijacho"

Huyo Mwalimu, Mkulima na Baba Kijacho wote ni mtu mmoja ambaye ni Bw Njano5 na si watu watatu tafauti. Lojiki hii ukiileta kwa wakristo ndipo utakapojua ni kwanini watu hawa huamini kuwa 1+1+1= 1. Wakristo wana haki na uhuru wa kutangaza imani hii na zile zote wanazoziamini.

Kwakuwa imani hizi za kiislamu na kikiristo kuna baadhi ya mambo ambayo ndio nguzo za imani hizo hupingana, hivyo basi mtu yoyote wa imani hizi hujikuta moja kwa moja tena bila hata kudhamiria akipingana na imani ya mwenzake wakati akifanya shughuli zake za kutangaza dini aidha ndani ya nyumba yake ya ibada au kwenye mikutano ya hadhara.
Mkristo akihubiri YESU ni mungu, moja kwa moja atakuwa anapinga na uislamu, na muislamu akisema YESU si mungu pia atakuwa anapingana na ukristo. Hivyo watu wa imani hizi hujikuta kila mmoja akimtuhumu mwenzake kuwa anakosea na ya kwamba yeye ndio yuko sahihi. Haijawa kashfa kwa waislamu kwa kitendo cha wakristo kutangaza YESU ni mungu na ya kwamba kafa msalabani kwa dhambi za ulimwengu, naam, haijawa kashfa hata kama kiukweli uislamu unapinga uungu wa Yesu na kifo chake cha msalabani.

Pia haijawa kashfa kwa wakristo kwa kitendo cha waislamu kutangaza YESU si mungu na wala hakufa msalabani ingawa kiukweli ukristo unaamini kuwa YESU ni mungu na ya kwamba kafa msalabani kwaajili ya dhambi zetu. Nasema tena haijawa kashfa ingawa wachochezi wa chuki za kidini wanataka watuaminishe kuwa ni kashfa kwa wakristo endapo muislamu akitangaza kuwa YESU si mungu. Wachochezi wa chuki za kidini ndio waliosababisha waislamu kupigwa mabomu na kuuliwa pale MwembeChai mwaka 1998.

Jambo litakuwa ni kashfa endapo tu jambo hilo ni urongo na linasemwa au kutangazwa kwa lengo la kumchafua mtu mbele ya jamii. Mkristo kusema muislamu anakosea kusema YESU si mungu katu haiwi kashfa kwa muislamu endapo ni kweli muislamu anasema hivyo, kinachotakiwa kwa huyo muislamu ni kujenga hoja za kuonesha kuwa YESU si mungu badala ya kuchukia na kufura kwa hasira.

Kwakuwa kutangaza uislamu au ukristo si kashfa, ndio maana kuna midahalo mingi sana ya kidini inayofanyika nchini, katika midahalo hiyo wakristo na waislamu wanakutana na kujadili yale mambo wanayotafautiana katika dini zao. Kikubwa kinachotakiwa ni kuvumiliana na kuheshimiana, mdahalo ukikushinda au ukipatwa na hasira ni vema kuacha kujadiliana kwani hakuna anayelazimishwa kushiriki mdahalo na katu huwezi kumzuia mtu kutangaza imani yake hata kama kiukweli kutangazwa kwa imani hiyo ndio kupingwa kwa imani ya mtu mwingine.

HITIMISHO.
Katu hatuwezi kutenganisha dini na siasa. Pamoja na kwamba hatuwezi kutenganisha dini na siasa, lakini kiukweli yapo mahusiano chanya na hasi ya dini na siasa katika nchi yetu.

MAHUSIANO CHANYA:
Mosi, Viongozi wa kidini kuingilia siasa kwa lengo la kutaka siasa ilete au iharakishe maisha bora kwa umma. Maaskofu, Mashekhe na viongozi wengine wa kidini huwa wanatoa matamko yenye lengo la kuitaka serikali itekeleze wajibu wake kwa umma.

Pili, Viongozi wa kidini kuingilia siasa kwa lengo la kutaka umma uchague viongozi bora na kubwa zaidi kuwaimiza waumini wajiandikishe kupiga kura, wahudhurie mikutano ya kampeni ya vyama vyote, kisha wajitokeze bila kukosa siku ya kupiga kura na mwisho wajiepushe uvunjaji wa sheria na taratibu za uchaguzi.

Tatu, Viongozi wa kisiasa kushiriki katika shughuli za kidini haijalishi hizo dini zao au la. Mara kadhaa viongozi wa kidini huwa wanawaalika viongozi wa kisiasa katika shughuli za kidini kama vile Baraza la Iddi, Kusimikwa kwa maaskofu, Misa na Ibada za X-Mass na Pasaka, mazishi ya viongozi wa kidini.

Nne, Viongozi wa kidini kushiriki katika kumuapisha rais mteule wa nchi.

Tano, Viongozi wa kisiasa kutumia Biblia au Qur-an wakati wakila kiapo cha uaminifu.

Sita, Dua inayosomwa na spika wa bunge kabla ya vikao vya bunge.

Saba, Wimbo wetu wataifa pamoja na mambo mengine unatuombea baraka toka kwa Mungu.

Nane, katiba ni matokeo ya mchakato wa kisiasa, lakini katiba hiyo inatambua uwepo wa dini na mungu.

Tisa uwepo wa dodoso la dini katika fomu za kuomba kuchaguliwa katika nyadhifa ya kisiasa.

MAHUSIANO HASI:
Mosi, viongozi wa kisiasa kutumia siasa kupendelea dini zao.

Pili, viongozi wa kisiasa kutumia siasa kuwanyanyasa, kuwabagua na kuwatenga watu wa dini fulani.

Tatu, Viongozi wa kisiasa kuwaadaa au kuwatumia watu wa dini fulani kwa lengo kutaka kukubalika kisiasa au kushinda uchaguzi. Mfano CCM iliwaadaa waislamu katika uchaguzi wa mwaka 2005 kwa lengo la kupata kura za waislamu. CCM katika ilani yake ilisema kuwa itawapatia mahakama ya kadhi waislamu pindi ikishinda uchaguzi, CCM ilishinda suala la kazi likawa ni longo longo.

Nne, Viongozi wa kidini kutaka waumini wao wachague kiongozi anayetokana na dini yao. Miongozo ya kanisa katoliki na ya BAKWATA katika uchaguzi wa mwaka 2010 ililenga kuwataka waumini wa dini hizo kuchagua viongozi wenye kuamini dini hizo.

Tano, Vyama vya siasa kushutumiana kuwa vina udini, ili hali sheria za vyama vya siasa hairuhusu kuanzishwa chama cha siasa kwa misingi ya kidini. Cha kushangaza viongozi vyama vya siasa wanashutumiana badala ya kufuata mkondo sheria kwa kupeleka ushahidi kwa msajili wavyama vya siasa ili havifute vyama vyenye udini. Vyama vya siasa kutumia karata hii katika kudhoofishana kuna jenga mahusiano hasi kati ya dini na siasa.

Asanteni.

Njano5.
0784845394
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom