figganigga
JF-Expert Member
- Oct 17, 2010
- 25,717
- 55,819
Bhoke Matiko akiugulia mkono
MARA: Jamani Mara; ukatili huu hadi lini? Hayo ni baadhi ya maneno yaliyotamkwa na watu baada ya mwanamke aitwaye Bhoke Matiko, 45, (pichani), mkazi wa Mtaa wa Nyamiobho Mogabiri, wilayani Tarime mkoani Mara, kufanyiwa ukatili wa kutisha wa kucharangwa mapanga na vijana waliodaiwa ni sungusungu katika ‘grosari’ yake eneo la Mogabiri Senta na kupoteza fahamu.
Tukio hilo lililothibitishwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum Tarime na Rorya, liliripotiwa na mama huyo Alhamisi iliyopita katika Kituo cha Polisi Bomani mjini hapa na kufunguliwa jalada namba TAR/IR/2421/2016 – KUJERUHI.
Baada ya mama huyo kucharangwa mapanga saa 2.46 usiku na vijana aliodai wanafahamika kwa majina na makazi yao, walipasua chupa zilizokuwa na bia na kupasua balbu katika grosari yake hiyo kisha kutoweka bila kukamatwa.
Akisimulia mkasa huo mama huyo alisema:
“Nilishitukia vijana ninaowafahamu ambao ni sungusungu wakimtaka kijana aliyekuwa mteja wangu akiwa anakunya kinywaji, wamchukue kwenda naye ofisini kufuatia makosa waliyokuwa wanamtuhumu.
“Kabla ya kumchukua niliwaomba wamuache kwanza alipe fedha za vinywaji alivyokunywa likawa kosa, walinigeuzia kibao na kunicharanga mapanga huku wakinilazimisha niwapatie fedha ya mauzo ya siku hiyo, nikakataa.
“Walianza kunikata mapanga, nilipiga mayowe lakini baada ya muda nilianguka na kupoteza fahamu, kumbe wasamaria wema walifika lakini hawakufanikiwa kuwakamata vijana hao.
“Nilichukuliwa na kupelekwa Kituo cha Afya cha Tarime Goodwil na kulazwa wodi namba tatu baada ya kupitishwa kituo cha polisi na kupewa PF3,” alisema.
Muuguzi wa zamu wa kituo hicho, Tatu Manyama alisema kuwa mama huyo alifikishwa kituoni hapo akiwa na hali mbaya baada ya kutokwa damu nyingi.
Afisa mmoja wa polisi aliyeomba jina lake kutoandikwa gazetini kwa kuwa siyo msemaji, alisema jeshi la polisi linawasaka vijana hao ili liwafikishe mahakamani kwa makosa ya kumjeruhi mama huyo.
“Vijana hao wanaendesha ulinzi wa jamii maarufu kama sungusungu lakini baadhi yao wanatumia nafasi hiyo kufanya uhalifu kwa baadhi ya watu,” alisema afisa huyo.
Licha ya kuanzishwa kwa kanda maalum ya kipolisi, Mkoa wa Mara umekithiri kwa wananchi kukatana mapanga na gazeti hili limekuwa likiripoti matukio ya aina hiyo mara kwa mara kwa miaka mingi, jambo ambalo linatia doa eneo hilo la nchi.
Chanzo: Uwazi