Tanzania tusipobadilika tutaendeleaje?

Shishye

JF-Expert Member
Feb 26, 2009
269
1
Jana nilikuwa na safari ya kwenda airport nikitokea nyumbani maeneo ya mikocheni. Nilitoka nyumbani saa 8 mchana, nikapitia Ali Hassan-Bibi titi-Nyerere road. Kuanzia mjini niliona askari wa traffic kila mahali kwa idadi isiyo ya kawaida. Nikahisi ni matatizo ya umeme kwenye taa za kuongozea magari hivyo wanakuja barabarani kutoa msaada. Cha kushangaza ni kwamba baada tu ya kufika maeneo ya kiwanda cha sigara karibu na TAZARA, foleni ikawa kubwa magari yote yamesimama.

Tumesimama kama masaa mawili hivi, kisha nikaona ving'ora na magari yakitoka mbio upande ninakoelekea. Kumbe ni mheshimiwa rais alikuwa anapita. Ndio akili ikanijia! Ala! Kumbe ndio sababu ya yote haya. Kutoka pale mpaka nijinasue na msongamano ule, nilifika airport saa 11 jioni. Safari ya nusu saa ikawa imenichukua masaa 3.

Nikaanza tena safari ya kurudi nyumbani, hali ikawa ni ile ile. Kutokana na ule msongamano uliosababishwa na rais, ule msongamano wa kawaida wa siku zote ukawa mara mbili zaidi. Nilifika nyumbani saa mbili usiku. Safari ya nusu saa ikawa tena imenichukua masaa 3.

Ninasikitishwa sana na hali hii. Dar es salaam ina msongamano wa magari kwa sababu ya ufinyu wa miundo mbinu yake. Halafu mtu maarufu kwa jina 'mheshimiwa' anadiriki kuuongeza bila aibu ili yeye awahi baada ya starehe yake ya kubembea. Hawa anaowanatisha barabarani ndio wale wanaomzalishia kodi ya kufanya asiyotakiwa kufanya ikiwemo kubembea (kama vile hakupitia utoto) na kwenda hospitali kupima akili wakati hili ni wazi linadhihirisha hali ya akili yake.

Kama tusipobadilisha jinsi ya kufanya shughuli zetu tutaendeleaje? Barabara tulizo nazo hivi sasa licha ya kuongezeka magari kwa maelfu, sio tofauti sana na tulizokuwa nazo miaka 20 iliyopita. Namaanisha hakuna uwiano wa ukuaji. Swali langu la kwanza ni kwanini tuendelee na tabia ileile ya kuzuia magari yote jiji zima wakati 'mheshimiwa' anapopita kama tulivyokuwa tunafanya miaka hiyo tukiwa na magari kumi?

Miaka ya sitini na sabini rais alikuwa anapita na kingo'ra ili jiji lote lijue(wakati huo watu na magari ni machache na mfumo ulikuwa wa kibabe). Je ni lazima hadi leo tuendelee kufanya hivyo hata kama tunajua shughuli za uzalishaji mali zinasimama?

Barabara zinaanzaga kufungwa pindi tu ndege inapokaribia kutua, au rais akiwa anajiandaa lisaa limoja kabla ya safari. Je kuna umuhimu wa kuendelea kufanya hivyo hata kama tunajua shughuli za maendeleo zimesimama kwa kuwa 'mheshimiwa' hajajenga barabara za kutosha?

Ni kwa nini askari polisi wanajaa barabarani kuzuia magari ya wananchi walipa kodi na wazalishaji mpaka 'mheshimiwa' apite halafu na wenyewe wanatokomea kusikojulikana na kuwaacha watu barabarani wanateseka kwa msongamano waliousababisha? Hii nchi inamtumikia mtu mmoja? Ni kwa nini basi tulipe kodi? Kuwalipa polisi kumtumikia 'mheshimiwa' tu?

Kama 'mheshimiwa' anatumia barabara ya uelekeo moja, ni kwa nini watumiaji wa uelekeo mwingine wasiruhusiwe kuendelea? Hata barabara kama ya Nyerere, lane za kushoto ziko mbali kabisa na lane za kulia. Ni kwa nini zote zizuiwe wakati mheshimiwa anahitaji kutumia moja tu at a time? Kuna siri gani ya ajabu hapa? Mnaohusika mmeliona hilo?

Mbona nchi nyingine zilizoendelea viongozi wao hawana misafara? Wanakaa kwenye foleni na wananchi wa kawaida hivyo wanapata changamoto ya kuleta mabadiliko? Kama hatuwaigi walioendelea tutaendeleaje?

Mimi nakerwa sana na muda unaopotea barabarani pasipo na sababu ya msingi. Mengi ya tunayoyafanya ni mapokeo ya tangu enzi za mkoloni, hakuna anayetaka kuumiza kichwa kufanya mabadiliko. Ni wakati sasa wa kuyatizama. Nawasilisha.
 
Back
Top Bottom