Mimi nadhani Tanzania bado hatujawa na uchumi wenye sura inayoonekana. Wakati wa ukoloni tulikuwa na mfumo wa uchumi wa kibepari japo wananchi wa chini walifanya kazi katika mfumo wa ubepari na wakapata chakula chao katika mfumo wa ujima wa kati. Baada ya Uhuru tuliazimia kuingia katika Ujamaa na Kujitegemea. Tukaanzisha mashirika chungu nzima ya umma. Tukaanzisha vijiji vya ujamaa na kuwahamisha wananchi kwa nguvu toka kwenye mahame kwenda kwenye vijiji vya ujamaa nk. Wakati tunafanya mabadiliko makubwa kama hayo, sheria zetu nyingi zikabaki zile zile za mkoloni. Tukaendelea kuwatumia nchi za kibepari kuinua uchumi wetu na wakati huo huo tukizitumia nchi za kikoministi. Ili kujiweka katika nafasi ya kupata kote, na kwakuwa wakati huo dunia iligawanyika katika matapo makuu mawili kutokana na vita baridi, tukaamua kuchukua sera za kutofungamana na upande wowote. Maana yake Marekani tupo na Urusi tupo.
Kutokana na kutokuwa na maandalizi mazuri ya kisera na kisheria, mashirika yetu ya umma yakaonekana kama mashimo ya kumeza fedha za umma. Mashirika ya umma yakawa yanaendeshwa kwa ruzuku. Shirika moja lenye mashine moja likaweza kuajiri mamia ya wafanyakazi ili mradi kila mtu ana ajira. Matokeo yake ni kwamba kiwanda kinachozalisha shilingi 10,000,000/= kwa mwezi kiliweza kutumia 100,000,000 kwa mwezi kwaajili ya mishahara. Kwa upande mwingine, sekta ya kilimo ikabaki namna ile ile ilivyoachwa na mkoloni na pengine duni zaidi. Kilimo kikabaki cha jembe la mkono kikitegemea vyua. Miundo mbinu ikabaki duni sana kiasi kwamba mahindi yangeweza kuoza Sumbawanga wakati Shinyanga watu wanakufa na njaa na fedha wanayo. Safari ya kutoka Morogoro hadi Dodoma ikawa ya siku mbili wakati Mwanza Dar Es Salaam safari ya wiki nzima. Kwa mazingira kama haya pamoja na matatizo mengine mengi yaliyoendana nayo yakatulazimisha kujaribu ubepari.
Tukarudia matatizo yale yale katika kwenda ubepari. Sera ikawa ya kibepari lakini sheria za kijamaa. Tukabinafsisha mashirika ya umma bila kuweka mazingira mazuri ya kisheria na liuchumi. Matokeo yake mashirika ya umma yakauzwa kwa "bei poa" kama anavyosema Prof Lipumba. Rasilimali kama dhahabu na almasi zikauzwa kwa bei za kugawa. Japo pamekuwepo na mabadiliko makubwa katika miundo mbinu bado maandalizi ya kuingia free market economy bado sio mazuri. Tutumie mtaji wa katiba mpya kuweka mufaka mpya.