Tanganyika, Z`bar na gundi ya miaka 45 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tanganyika, Z`bar na gundi ya miaka 45

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by X-PASTER, Aug 17, 2010.

 1. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #1
  Aug 17, 2010
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Tanganyika, Z`bar na gundi ya miaka 45

  Na Conges Mramba

  AGOSTI mwaka jana, waliojitambulisha kuwa ni Wazanzibari waishio Uingereza, walinishambulia kwa maneno makali, kuandika gazetini kwamba Zanzibar si nchi, bali ni ncha.

  Nilikuwa nikimuunga mkono Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa kauli yake bungeni kwamba Zanzibar si dola, kwa sababu dola ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Muungano ambao Zanzibar ni ni ncha; ni kipande chake.

  Naam, Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa sababu hiyo, Wazanzibari na Watanzania wa Bara ni wote ni Watanzania.

  Jumapili iliyopita (Aprili 26) tulipoadhimisha miaka 45 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, nikakumbuka hilo sakata la ‘Zanzibar ni nchi’.

  Yaani, akina ‘Zanzibar ni nchi’ ndani Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waishio Ulaya, waliniandikia ujumbe kwa barua pepe kusema, hata Pinda aseme mpaka machozi yamkauke, wao hawajawahi kuwa Watanzania, bali ni Wazanzibari waishio na kufanya shughuli zao Ulaya. Kwa mtazamo mwepesi, huo ni uhaini wa dhahiri.

  Paspo shaka, hawa ni watoto wa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waishio huko Visiwani. Wanapenda wajulikane kama Wazanzibari, lakini walisomeshwa kwa kodi za Watanzania, zikiwamo za Wanyamwezi na Wajitta wa Bara.

  Kwa yakini, Mraba hauna tashtiti watoto wa Visiwani kusomeshwa kwa kodi za Watanzania. Kwa sababu ni dhahiri Zanzibar ni sehemu (ncha) ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

  Wazanzibari, kama wanavyopenda waitwe, hawajakanusha kusomeshwa kwa kodi za Wahaya, Waha, Wameru na Waarusha waishio kwenye kwato za Mlima Meru.

  Isipokuwa, wanachokazania sana ni kwamba siku hizi wao ni Wazanzibari, ingawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewateua kushika nyadhifa nyeti anuwai katika Serikari ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyoungwa kwa gundi na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, Aprili 26, 1964 – kwa pamoja wawili hao waliuasisi Muungano wa Tanzania.

  Miongoni mwa raia wa Visiwani wanaoshika nyadhifa katika Dola ya Jamhuri ya Muungano ni Balozi Ali Karume, mtoto wa Mwasisi wa Muungano. Ali, aliyepata kuwa Balozi wa Tanzania Umoja wa Ulaya (EU) mjini Brussels katika Ubelgiji, ambako pia akina ‘Zanzibar ni nchi’ wamekolea, wapo wanaishi na kufanya kazi kwa baraka za Tanzania.

  Hili, la akina Ali Karume kushika nyadhifa za ubalozi wa Tanzania Ulaya, haliupi Mraba huu tatizo lolote. Kwa sababu, raia wote wa Zanzibar na wale wa Bara, wanashiriki bega kwa bega kula (na kulilia?) matunda ya uhuru, kwa kuwa wanaishi nchi moja – Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

  Kwamba, Watanzania wa Bara na Visiwani wanaishi na kuhudumiwa chini ya mbawa za dola moja (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) ingawa ingalipo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ambayo kimsingi haiwapi wao hati za kusafiria zinazowapa baraka kuishi na kuendesha mambo yao huko waliko.

  Hawa, akina ‘Zanzibar ni nchi’ ati hawapendi kusikia wanaitwa Watanzania! Nikasema kwamba, hawa akina ‘Zanzibar ni nchi’ watakapojitenga, lazima tuwafungulie kesi nzito ya madai.

  Kwa sababu wametuvurugia Muungano wetu, umoja wetu, udugu na mipango yetu ya muda mrefu na mengine mengi kabila hiyo.

  Hawa, wamesomeshwa kwa kodi zetu, yaani fedha za sangara, kahawa, korosho, pamba, chai na furu wa Ziwa Victoria. Basi, wajiandae kutulipa fidia na riba.

  Kwa sababu wamefaidi mno Muungano, kisha wakaanza kupanga njama huko waliko ughaibuni, ili wawashawishi Wazanzibari waanzishe chokochoko na kutaka kuvunja mkataba ili kujitoa kienyeji katika Muungano, pasipo masharti ya mkataba.

  Naam, akina ‘Zanzibar ni nchi’ watulipe fidia yenye riba, kutokana na kutumia Utanzania wakati wao ni Wazanzibari.

  Wana hati za kusafiria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wanasema wao si Watanzania, bali Wazanzibari. Je, wana uraia gani na hati za kusafiria za nchi gani; Zanzibar? Nani kawadanganya ile ni nchi yenye hadhi ya utawala kamili na dola? Hawakuisikia hukumu ya mahakama ya juu kuliko zote hapa nchini?

  Hawa, wanaitaka Zanzibar yao iliyopandwa mithili ya mbegu sambamba na Tanganyika, ili kuotesha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tanganyika ilipopandwa na Zanzibar ili kuotesha Tanzania, bila shaka mbegu mbili zilikufa kabla ya kuotesha mmea mpya uitwao Tanzania. Wanachokifanya sasa ni kama wale wanaotaka ‘vuna vuna’ kule kwa wachungaji wakati mavuno hayaruhusiwi tena. Zimefia ndani kwa ndani.

  Wanaoungana kwa misingi ya waasisi wetu tuliyoirithi na sasa tunaiendeleza, hukubali kuweka pamoja rasilimali zao, yaani madini, rasilimali watu, wanyama, fursa, ardhi, bahari, mafuta, vipaji na hata changamoto na matatizo yao – lengo ni kujenga familia moja na kuishi pamoja katika tabu na raha, magonjwa na afya, vita (Jalali apishe mbali) na amani.

  Sasa, tumeanza kuona akina ‘Zanzibar ni nchi’ wakidai walikuja ndani ya Muungano wakiwa na kiti na meza na mafuta; na kwamba chochote chao ni mali yao. Ebo!

  Ni kwa sababu hii, Mraba unakuwa na tashtiti, kama upo Muungano wenye nia au kusudi moja. Au kama kuna Muungano (Unity) wenye malengo ya kuunda umoja uitwao ‘Oneness’. Nazungumzia ‘Oneness’ katika ‘Unity’.

  Kwa sababu, kuna dalili kwamba, ‘Zanzibar ni nchi’ wanatuona sisi Watanzania wenzao mabwege!

  Tukaondoa vizuizi kwetu kwa ajili yao wakati wao wakiendekeza ubinafsi na ubaguzi dhidi yetu ili kufanya ‘chetu kiwe chao; lakini chao si chetu’.

  Leo, msomaji wa Mraba, anasikia sakata la mafuta ya Zanzibar, kwamba si mali ya Jamhuri ya Muungano ili kudumisha tu ile falsafa ya chetu chao, chao si chetu.

  Akina ‘Zanzibar ni nchi’ wameambukizwa Virusi vya Ukosefu wa Umoja na Uzalendo (VUUU), hadi wakaugua maradhi ya ukosefu wa uzalendo moyoni – malpatriotism.

  Hawa si wa CUF tu, bali pia wale wa Chama tawala, CCM. Ni tangu wananchi wa kawaida sana hadi ‘waheshimiwa sana’ wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaolipwa posho nono kwa kahawa na sangara zetu, lakini hawaachi kusema, Zanzibar ni dola ndani ya Jamhuri ya Muungano.

  Hawa, wako radhi Tanzania izame Bahari ya Hindi ili Zanzibar yao irejee zama za Sultani aliyepinduliwa (hawakupenda) Januari 12, 1964.

  Nyerere alishasema Wazanzibari watakapoanza kudai Uzanzibari, basi Wapemba nao wajiandae kudai Upemba, wakati Wazanzibara watakapoanza kutimuliwa!

  Yapo matatizo ya Muungano yasiyowasibu watu wa upande mmoja tu wa Muungano. Matatizo na changamoto za Muungano havikuanza leo. Tungali tunalikumbuka Kundi la Wabunge 55 (G-55) wa CCM walivyowahi kuchachamaa kudai Tanganyika, wakazimwa kwa maslahi ya Muungano.

  Amani Abeid Karume, Benjamin Mkapa, Pinda, Shamsi Vuai Nahodha, Jakaya Kikwete, Mohamed Seif Khatib na wenzao, wote wanajua matatizo ya Muungano. SMZ na ile ya Muungano wanajua shida na wanaandaa njia ya kutokea katika malumbano ya sasa.

  Wakati tunasubiri kuona hatima yake, tunawasikia akina ‘Zanzibar ni nchi’ wakisisitiza: “Hata iweje, lazima Zanzibar ni dola na ina hadhi ya kuwa hivyo hata Umoja wa Mataifa.” Kisha wanasema kwamba raia wa Visiwani wanapaswa kutambulika kama Wazanzibari hata huko New York na wala si Watanzania!

  Huu ndiyo Muungano wenye umri wa miaka 45. Mwisho wa siku, tunajiandaa kufukua kaburi la pamoja lililovizika vyama vya Afro – Shirazi (ASP) na TANU ili kuvifufua na kuvipa uhai.

  Ndicho kitakavyokuwa kifo cha CCM na njama za watu wake kutaka kugawana mbao – jahazi lizame.

  ‘Ncha’ ya nchi inapodai urithi wa nchi kamili, akina Waziri Mkuu Pinda wanakabwa koo Bungeni, ili wakubali kusema huu si Muungano wa nchi mbili, bali viliungwa vipande viwili (vya jahazi?) kwa kutumia gundi ili wapate kusafiria muda huo tu, kutoka Zanzibar hadi Bara, na hata kutoka Pemba hadi huko waliko Ughaibuni!  source: Rai
   
Loading...