TANGANYIKA HAINA THAMANI, ZANZIBAR YA NINI?

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Nov 22, 2012
1,985
1,282
TANGANYIKA HAINA THAMANI.
1.
Nianze kuwasalimu, kwa jinale Msifika,
Tumshukuru Rahimu, siku hino kuifika,
Hii ni siku adhimu, ya pekee kila mwaka,
Tuyaenzi ya Mwalimu, tuyaenzi kwa vitendo.
2.
Miaka kumi na saba, kamili imetimia,
Tangu atutoke baba, katika hii dunia,
Ulikuwa ni msiba, mkubwa kwa Tanzania.
Tuyaenzi ya Mwalimu, tuyaenzi kwa vitendo.
3.
Kuna mengi alifanya, leo niseme machache,
Yapo aliyo tukanya, ama kutaka tuache,
Aliasa na kuonya, kila aonapo cheche,
Tuyaenzi ya Mwalimu, tuyaenzi kwa vitendo.
4.
Alijenga ujamaa, watu kusaidiana,
Kwa upendo wakikaa, nyoyo zikafungamana,
Tena hawakukataa, kazi kushirikiana,
Tuyaenzi ya Mwalimu, tuyaenzi kwa vitendo.
5.
Pia kujitegemea, katika yetu bajeti,
Tukope palo pungua, kutimiza mikakati
Kuomba kubwa udhia, na kupoteza wakati,
Tuyaenzi ya Mwalimu, tuyaenzi kwa vitendo.
6.
Alisema waziwazi, udini jambo hatari,
Tusifanye ubaguzi, kwa kuichelea shari,
Ukabila upuuzi, hakika hauna heri,
Tuyaenzi ya Mwalimu, tuyaenzi kwa vitendo.
7.
Alikuza Kiswahili, katika awamu yake,
Alifanya kula hali, lugha hii itumike,
Nchini kila mahali, na hata ng’ambo ifike,
Tuyaenzi ya Mwalimu, tuyaenzi kwa vitendo.
8.
Hakuiona thamani, ya nchi ya Tanganyika,
Iloundwa Jerumani, kuigawa Afirika,
Jambo alo litamani, kufuta yote mipaka,
Tuyaenzi ya Mwalimu, tuyaenzi kwa vitendo.
9.
Zanzibari ya Sultani, aliuliza ya nini,
Tanganyika ya Berlini, inaulazima gani,
Tanzania bila soni, liipenda hadharani,
Tuyaenzi ya Mwalimu, tuyaenzi kwa vitendo.
10.
Azimio la Arusha, lilifilia Zanziba,
Sawa kulirekebisha, penye tobo kupaziba,
Ela tukalipotosha, na kulifuta kwa raba,
Tuyaenzi ya Mwalimu, tuyaenzi kwa vitendo.
11.
Msingi kuuwangusha, ilikua ni dhoruba.
Mwalimu alitupasha, tunastahili adhaba,
Hakuchoka kukumbusha, ili tuifanye toba,
Tuyaenzi ya Mwalimu, tuyaenzi kwa vitendo.
12.
Kaditama namaliza, tusizike yake mema,
Lipo nililo bakiza, ninaomba kulisema
Mwalimu tunamliza, kupinga zake kalima,
Tuyaenzi ya Mwalimu, tuyaenzi kwa vitendo.

MWISHO WA SHAIRI.

MWALIMU NYERERE.jpg


Maelezo mafupi.

Katika beti ya nane na tisa nimesema Mwalimu hakuiona thamani ya Tanganyika na Zanzibar mbele Tanzania. Mwalimu alisema watu wanawezaje kuithamini Tanganyika iliyoundwa na wakoloni na kuibeza Tanzania? Kwanini tusijivunie nchi tuliyo itengeneza wenyewe kwa kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar? Kwanini tusijali nchi tuliyoipa jina wenyewe kwa matakwa yetu wenyewe?

Miaka 17 sasa tangu baba wa taifa atangulie mbele ya haki, pamoja mapungufu ya Mwalimu kama binadamu, lakini bado kwangu na kwa watu wengi atabaki kuwa kiongozi bora wa mfano na kuigwa Afrika na Dunia.

Msimamo wake wa serikali mbili kuelekea moja bado msimamo mzuri usio gubikwa na ubinafsi bali umesukumwa na ndoto ya kutaka kufuta mipaka ya kikoloni katika Afrika yetu kwa kuanzia kati ya Tanganyika na Zanzibar baada ya kufeli baina ya Kenya, Uganda na Tanganyika.

Kama kweli tunamuenzi mwalimu, wananchi hasa wanasiasa wafanye juu chini kuhakikisha muungano wetu unabaki kuwa imara na salama kwa kutumia hoja, lakini kubwa wahakikishe AFRIKA MASHARIKI inakuwa shirikisho la kisiasa.

Afrika Mashariki kuwa taifa moja, lenye rais mmoja, ndio ndoto ya Mwalimu, na mwenye kumuenzi kwa vyovyote vile ana wajibu ama deni ya kuitimiza hiyo ndoto, ndoto hii itabaki ndoto tu kama Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ukivunjika! Muungano huu uwe chachu ya Muungano wa Afrika Mashariki.

14/10/2016

Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
Call/ whats app 0622845394 Morogoro.
 
Kila siku nakushauri ubadilishe aina ya uandishi wako
Ndo mana thread zako hazina wasomaji
 
Hilo Wazo la Serikali moja na nchi moja naliunga mkono kwa 100%, tofauti na hapo muungano hauna maana
 
Back
Top Bottom