MAASKOFU NA WACHUNGAJI, KEMEENI MAOVU! MSIWAOGOPE WANASIASA, WATAWALA NA MATAJIRI!
Hawa ni watu ajabu sana! Walipokuwa katika Vyuo vya Theologia na Biblia walisoma sana kuhusu ujasiri wa Askofu Mkuu Janani Luwum wa Kanisa Kianglikana Uganda jinsi alivyomkabili Iddi Amin na kumueleza aache kuua watu wake; wengi wao walisoma na kutiwa moyo na ujasiri wa Askofu Mkuu Desmond Tutu wa Kanisa Anglikana Afrika Kusini jinsi alivyopambana na mfumo wa Ubaguzi wa Rangi ambao ulitweza na kufedhehesha utu, na kuwaua watu weusi kama ndege; wapo waliosoma na kufurahia sana maandishi kuhusu Liberation Theology yaliyotolewa na Padre Gutierrez Gutierrez Gutierrez wa Roman Catholic Church kule Latin America jinsi alivyopinga unyonyaji na ukandamizaji wa wananchi wanyonge uliokuwa ukifanywa na matajiri waliokuwa wameunda ushirika muovu na watawala wakandamizaji; wapo waliotamani sana wamuone Martin Luther King Jr., yule Mchungaji wa Kibatisti jinsi alivyopambana kutokomeza ubaguzi na ukandamizaji kule Marekani, mbengu za haki zilizopiganiwa na yeye zilizopelekea Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika Barack Obama kutawala Marekani bado inasimuliwa hadi sasa; wengine wamejaza maandishi ya Padre Profesa Martin Luther jinsi alivyotetea wanyonge na kusimamia matengenezo ya Kanisa kule Ulaya hasa Ujerumani; wengine hadi leo wanatukuza ujasiri wa Padre Profesa Jan Huss yule mwanzilishi wa u-Moravian alivyopinga uovu hadi akachomwa moto hadharani. Wengi wanafundisha na kuhubiri nadharia kuhusu haki kwa mujibu na mtazamo wa ki- Biblia huku wakikesha kusoma vitabu vya manabii kama Amos, Yeremia, Ezra, nk.
Kinachoshangaza ni kuwa wanaposikia na kuona maovu ya aina hiyo hiyo au hata yanayokithiri katika jamii zao wanafumba macho. Waumini wao wanapofanyiwa maovu na kuonewa na hata kupoteza maisha hawafumbui kinywa. Watu wengine wasiokuwa waumini wao wanapofanyiwa ukatili ndio haiwahusu kabisa! Wanasahau kuwa Nabii Amos alikemea maovu yaliyokuwa yakitendwa hata nje ya mipaka ya Nchi yake ya Yuda kwani aliwaonya watawala wa Damaska, Gaza, Tiro, Edomu, Amoni, Moabu, Israeli, nk.
Watumishi wengine wachache wakijitokeza kukemea maovu basi wao (wasiotaka kukemea) hugeuka kuwa watesi wa watumishi wanaokemea maovu! Maaskofu wengine wanadiriki hata kuwatishia kuwatimua katika makanisa Wachungaji walio majasiri wa kukemea uovu! Wanawanyamazisha kiaina. Kwao ujasiri wa Yohana Mbatizaji aliyemkemea Herode ni nadharia ya kuisoma Kanisani tu lakini isiyofaa kuiishi. Wanafikiri kuwa kukemea uzinzi na ulevi madhabahuni ndio wito pekee walioitiwa lakini ubadhilifu na uporaji wa mali ya umma pamoja na ukandamizaji na utekaji na unyanyasaji wa watu siyo dhambi ya kukemewa madhabahuni. Kwao kutumia madhabahu kukemea ulevi na uzinzi kila Jumapili ndio utumishi lakini kutumia madhabahu hiyo hiyo kukemea watu wanaoeneza chuki katika jamii na wanaotesa, kuteka na kuua watu wengine ni 'kuingiza siasa Makanisani'! Kwao kutumia madhabahu kukemea unyanyasaji katika familia ndio utumishi lakini kutumia madhabahu hiyo hiyo kukemea unyanyasaji mahali pa kazi, na katika mifumo ya kisiasa na uendeshaji wa serikali ni kufanya siasa. Kwao wanaona ni ujasiri kuwaambia waumini kuacha kuwasingizia majirani zao kama moja ya Amri Kumi za Mungu inavyotaka lakini kuwaambia wanasiasa na watendaji katika mifumo ya kiserikali na kisiasa kuacha kuwasingizia watu na kuwabambikia kesi na kuwachafua wenzao ni 'kuleta siasa Kanisani'!
Ee Mungu uturehemu na ututie ujasiri tusiache kuwaonya hata hawa Wachungaji na Maaskofu wanaoupa kisogo wito wao wa kuonya, kukemea na kushauri katika jamii ulimowatuma kukutumikia kama Maandiko yanavyotaka (Ezekieli 33:1-20). Kama tunao ujasiri wa kuwaonya na kuwakemea matajiri, wanasiasa, na watendaji wa serikali, tupe pia ujasiri wa kuwakemea viongozi wa Makanisa walio waoga. Tupe hekima na neema ya kutokuwachukia tunaowakemea. Tupo uangavu wa kiimani ili tuone pia maovu yanayoweza kutendwa na hao tunaojua wanateswa na kunyanyaswa. Ee Bwana! Fufua kazi yako katikati ya mataifa!
Ujumbe huu nimeutoa leo nikiwa nimetimiza miaka 25 ya utumishi wangu tangu nilipojiunga rasmi katika kazi ya kumtumikia Mungu (full time ministry) siku ile ya tarehe 4 Agosti 1994.
Mwana Kondoo Ameshinda Tumfuate!
Askofu Mkuu Emmaus Bandekile Mwamakula - Mkuu wa Kanisa la Moravian Uamsho Tanzania & Afrika Mashariki na Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian ya Uamsho Duniani
View attachment 1173288