Tamko la Kamati Kuu ya Chadema: Jan 31 Jan, 2011

Mie napenda kufahamu kutoka kwa kiongozi yeyote wa CUF humu ndani hata kama Mtatiro yumo, nikiwa kama mwanaharakati wa maendeleo na ustawi wa Watanzania wenzangu! Ninataka kuhudhuria haya maandamano, ila naomba kujua kama naweza vaa uniform ya chama changu kingine (aidha magwanda, bendera au kofia)! maana naskia huwa wana CUF hukataza hayo nakumbuka kuna wakati waliitisha maandamano kwa sharti ya kutobeba bendera au kuvaa uniform za chama kingine chochote! Naombeni kujua maana nina hofu nisije nikatimuliwa!
 
Sikutarajia waungane at this stage baada ya kuwa wamepishana ktk mambo mengi mara baada ya uchaguzi wa spika, mameya na mdahalo.
 
Serikali kivuli maana yake ni serikali ya upinzani kusingekuwa na maana kama CDM wangeshirikisha chama kinachoshirikiana na chama tawala. Hizo ni habari mbaya kwa HR huwezi kuwa mguu mmoja huku mwingine huko ukilazimisha matokeo yake ni kupasuka msamba.
 
Hurusiwi kuvaa nguo za chama chengine zaidi ya zile za cuf. Kama unashida ya maandamano njoo la kama unashida ya kuvaa magwanda ya wafungwa subiri maandamano ya chadema keshatangaza padri slaa mda si mrefu.
 
Ni kweli nimeona. Ndo sawa
Bila shaka CUF atakuwa ni nyoka wa hatari sana kisiasa nchini.

Kwa Zanzibar kikae kwa pamoja na CCM kama serikali na kutolea maamuzi mambo mbalimbali ambayo tunayalalamikia hapa halafu bado wanatarajia tunapoteremka tu kwenye boti pale Ferry basi tuungane nao kupinga yaleyale mambo walioshiriki kuyaunda.

CUF kijichunguze vema nafsi yake; chama hakiwezi kikawa cha baridi ya barafu na wakati huo huo kituaminishe kuwa wa moto kama mvuke kwenye mtambo wa gesi ya Songosongo pale Ubungo njia pamba.

CUF ama kikubali kuwa upande wa serikali na kujitayarisha kupokea gharama yake kutoka kwa Umma wa Tanzania au kijiunge jumla upinzani ndio tuweze kufanya kazi kwa kushirikiana.
 
TAMKO LA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) KUHUSU HALI YA TAIFA.

Kamati Kuu ya CHADEMA katika kikao chake cha kawaida kilichofanyika tarehe 29-30 Januari 2011 jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa Taifa Mheshimiwa Freeman Aikael Mbowe (Mb), pamoja na mambo mengine, imepokea, kujadili na kutolea maazimio Taarifa ya Hali ya Siasa na Taifa kwa ujumla. Maazimio haya yapo katika maeneo matano yafuatayo.

1. Mchakato wa Upatikanaji wa Katiba Mpya.

Kamati Kuu imezingatia na kupongeza juhudi za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pamoja na wadau mbalimbali wa demokrasia nchini za kudai Katiba Mpya. Aidha, Kamati Kuu imejadili na kutafakari kwa kina maoni ya wadau mbalimbali juu ya mchakato unaofaa katika kupata Katiba Mpya, na kuzingatia kuwa njia sahihi ni ile itakayowashirikisha wananchi kikamilifu na kwa dhati bila kujali tofaui zao za kisiasa, dini, umri, elimu, kabila wala jinsia zao. Kamati Kuu imezingatia pia kwamba Tume ya Rais sio njia sahihi itakayowezesha upatikanaji wa Katiba Mpya yenye kuzingatia utashi, matakwa na mahitaji ya wananchi wa Tanzania. Hivyo basi:

  1. Kamati Kuu imepinga utaratibu wa kuunda Tume ya Rais katika uundaji wa Katiba Mpya
  2. Kamati Kuu imeunga mkono utaratibu wa kutumia Bunge katika kutengeneza na kusimamia mchakato utakaoletekeza upatikanaji wa Katiba Mpya
  3. Kamati Kuu imeipongeza Sekretariati yake kwa kumwagiza Mheshimiwa John Mnyika kuandaa na kuwakilisha Hoja Binafsi inayolitaka Bunge kuandaa sheria itakayoweka utaratibu na mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya
  4. Kamati Kuu imewahimiza na kuwaomba wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunga mkono Hoja Binafsi ya Mheshimiwa Mnyika kwa maslahi ya Taifa.

2. Mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi Jijini Arusha

Kamati Kuu imepokea kwa masikitiko taarifa ya vifo vya wananchi watatu wasio na hatia kwa kupigwa Risasi na askari wa Jeshi la Polisi kufuatia vurugu zilizosababishwa na Jeshi hilo katika harakati zao za kuzuia maandamano halali na yenye Baraka zote za Kamanda wa Jeshi la Polisi Wilayani Arusha. Aidha, Kamati Kuu imesikitishwa na uvurugwaji wa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha kulikofanywa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa maelekezo ya Chama cha Mapinduzi na Serikali yake. Katika maazimio yake:

  1. Kamati Kuu imewapa pole ndugu wa wafiwa wa vurugu za Arusha pamoja na wananchi wa Arusha na watanzania kwa ujumla
  2. Kamati Kuu imewapongeza Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Mhe Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Willibrod Peter Slaa, Mbunge wa Arusha Mjini Mhe Godbless Lema na viongozi wengine wa CHADEMA kwa juhudi zao kubwa za kuepusha shari na kutoa uongozi wa kisiasa pale ambapo wananchi wa Arusha walitelekezwa na viongozi wa Serikali ya CCM katika kipindi chote cha matatizo ya Arusha
  3. Kamati Kuu imeiagiza sekretariati ya CHADEMA kuendelea na harakati za kudai haki za wananchi wa Jiji la Arusha kwa njia za kisiasa.
  4. Kamati Kuu imewaagiza madiwani wa CHADEMA katika Halmashauri ya Jiji la Arusha kuendelea kuingia katika vikao vya Baraza la Halmahauri hiyo na kuwawakilisha wananchi waliowachagua kikamilifu na wahakikishe kuwa wanatumia nafasi yao kufanikisha uchaguzi wa Meya.

3. Matatizo ya Nishati ya Umeme na Gesi na Malipo kwa Kampuni Hewa ya Dowans

Kamati Kuu imesikitishwa na kupanda holela kwa bei za nishati muhimu za umeme na gesi, pamoja na kushindwa kwa serikali ya CCM katika kuwekeza kikamilifu katika sekta ya nishati hapa nchini. Aidha, Kamati Kuu imesikitishwa na kufadhaishwa sana na uamuzi wa CCM na serikali yake kuridhia kuilipa Kampuni hewa ya Dowans fedha za walipa kodi wa Tanzania zipatazo Shilingi bilioni 94, pamoja na kwamba Kampuni hii ilikwishaharamishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya wananchi.

Kamati Kuu imetambua kuwa sakata la Dowans ni mwendelezo wa vitendo vya kifisadi ndani ya CCM na serikali yake ambavyo vimeligharimu taifa hili kwa miongo mitano iliyopita. Hivyo basi:

  1. Kamati Kuu imewahimiza wana CHADEMA, wabunge na wananchi kwa ujumla kuendelea kupinga kwa nguvu zote malipo ya Dowans
  2. Kamati Kuu imewaelekeza viongozi pamoja na wabunge wa CHADEMA kuendelea kuwahamasisha wananchi kupinga kwa njia mbalimbali za kisiasa na kisheria malipo ya Dowans na ufisadi mwingine hapa nchini
  3. Kamati Kuu imewapongeza na kuwashukuru wanaharakati wa taasisi za kiraia kwa ujasiri na moyo wao wa kizalendo kwa uamuzi wao wa kufungua kesi mahakamani ya kupinga malipo ya Dowans
  4. Kamati Kuu imeiasa Serikali ya CCM kutokuona aibu kutekeleza sera za CHADEMA zilizofanyiwa utafiti kuhusu namna ya kujenga na kuimarisha sekta ya nishati ya umeme na gesi hapa nchini ili nchi yetu iondokane na tatizo la kudumu la umeme.
  5. Kamati Kuu imeiagiza Secretariat yake kuanza maandalizi ya maandamano ya nchi nzima ya kupinga ongezeko la bei ya umeme, gesi na kuilipa Dowans. Na tarehe 24/02/2011 itakuwa siku ya kuanza maandamano kwenye Jiji la Mwanza na miji mingine kadiri ratiba itakavyotolewa.

4. Matokeo ya Kidato cha Nne

Kamati Kuu imeyapokea kwa masikitiko makubwa matokeo ya Kidato cha Nne yanayoonyesha kuwa nusu ya watahaniwa wote wamefeli Mtihani huo. Aidha, Kamati Kuu imezingatia na kusikitishwa na taarifa kuwa ni asilimia 11.5 tu ya watahiniwa ndio waliopata daraja la I hadi la III. Ndio kusema kuwa karibu asilimia 90 ya vijana wote waliomaliza kidato cha nne mwaka 2010 hawawezi kuendelea na elimu yeyote ya juu na itakuwa ni vigumu sana kwa vijana hawa kupata aina yeyote ya ajira ya uhakika.

Aidha, Kamati Kuu imezingatia kuwa matokeo mabaya ya Kidato cha Nne yamesababishwa na sera dhaifu za serikali ya CCM zenye kulenga kughilibu wananchi kwa ajili ya mafanikio ya kisiasa kwa kukazania wingi wa majengo ya shule badala ya ubora wa walimu na ubora wa shule. Kutokana na hali hii:

  1. Kamati Kuu imeyatangaza matokeo ya Kidato cha Nne ya mwaka 2010 kuwa ni Janga la Kitaifa
  2. Kamati Kuu imeitaka Serikali ya CCM isione aibu kutekeleza sera za elimu za CHADEMA zilizoanishwa katika ilani yake ya mwaka 2010, ikiwemo sera ya kutoa elimu bure na kuboresha maslahi na mazingira ya kazi ya walimu ambazo zilielezwa na wataalamu wa elimu kwamba ndio sera sahihi za kufufua ubora wa elimu ya nchi yetu
  3. Kamati Kuu imeunda timu maalumu ya wataalamu wa elimu kwa ajili ya kutafiti kwa kina sababu za matokeo mabaya ya Kidato cha Nne na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu katika kikao chake kitakachofanyika kabla ya Mwezi Mei 2011.

5. Kuhusu propaganda za udini hapa nchini

Kamati Kuu imesikitishwa na propaganda zinaendelezwa na viongozi wa juu wa Chama cha Mapinduzi, hususani Rais Kikwete, kuhusu kuwepo kwa mfarakano wa kidini hapa nchini. Kamati Kuu imezingatia kuwa wananchi wa Tanzania wameendelea kuishi kwa amani, upendo na mshikamano mkubwa bila kujali tofauti zao za kidini. Kamati Kuu imezingatia kuwa Viongozi wa juu wa CCM, na hasa Rais Kikwete, ameamua kuficha udhaifu wake wa kiuongozi chini ya zulia la udini ili wananchi waache kujadili mambo ya msingi ya Taifa hili, ikiwemo kushindwa kwa CCM kutekeleza ahadi ambazo imekuwa ikizitoa katika miongo mitano iliyopita. Hivyo basi:

  1. Kamati Kuu imewahimiza wananchi wa dini zote hapa nchini kuendelea kuishi kwa amani na mshikamano na kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii bila kujali tofauti zao za dini, ukabila wala itikadi ya siasa
  2. Kamati Kuu imewataka viongozi wa juu wa CCM na hasa Rais Kikwete kuacha kuchochea mgawanyiko wa dini hapa nchini kama njia ya kuficha udhaifu wake wa uongozi
  3. Kamati Kuu imewahimiza viongozi wa dini zote hapa nchini kuendelea kukemea maovu yeyote katika jamii bila woga wala upendeleo kwani hilo ni jukumu lao la msingi.

6. Kuhusu Ushirikiano wa Vyama vya Siasa vya Upinzani

Kamati Kuu imeendelea kuzingatia umuhimu wa vyama vya siasa kushirikiana katika kuimarisha nguvu ya upinzani hapa nchini. Hata hivyo, Kamati Kuu imezingatia kuwa Chama cha Wananchi (CUF) wamejiunga na CCM kuunda Serikali ya Umoja Kitaifa Zanzibar, na kwa kuwa Sheria inayoruhusu uwepo wa vyama vya siasa inahusu pande zote za Muungano, na kwa kuwa vyama vingine vya upinzani vyenye wabunge wamo katika ushirikiano na CUF, Kamati Kuu imeona kuwa CHADEMA haiwezi kuwa na ushirikiano wenye tija na vyama hivyo. Hivyo basi Kamati Kuu imemwagiza Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kuunda Baraza la Kivuli kwa kuhusisha wabunge wa CHADEMA pekee.




7. Kuhusu mpango mkakati wa chama 2011-2016.

Kamati Kuu ilijadili na kupitisha mapendekezo ya mpango kazi wa chama kwenye Baraza kuu la chama .Pia ilijadili na kupitisha mpango kazi wa mwaka 2011-2012.

Tamko hili limetolewa leo tarehe 31/01/2011.

Dk Willibrod Peter Slaa
Katibu Mkuu




[source - chadema.or.tz]
 
Cuf ina viti 2 bara(tanganyika) ie lindi mjini na kilwa kusini na pia cuf ina madiwani karibu 200 huku tanganyika,
jee chadema wana viti vingapi zanzibar? Chadema Wana madiwani wangapi zanzibar?

Wingi sio jambo kiivyo. Angalia jongoo ana miguu mingi lkn hana mbio. Ni sawa na wingi wa watanganyika hauna maana yeyote ktk mambo ya muungano iko sawa na zanzibar iliyo na watu milion moja? Upo mlevi?
 
Safi kabisa zama za siasa za uongo na unafiki zimepitwa na wakati.Cuf ombeni viti CCM huko ndiko mnako fit si mmejiunga nao? Sasa mbona mnataka kutuletea mkanganyiko wananchi? You guys belong to serkali ya CCM ....Go figure!
 
Tulichotangaza ni maandamano, tena ya amani na siyo uniform, au magwanda.

Kama umechoshwa na yale yanayoendelea nchini mwetu basi njoo utuunge mkono. Njoo na bango lako lililo na message kwa watanzania. Usije na silaha. Tunawasiliana na CDM na NCCR ili watuunge mkono na waandishi wa habari na wakereketwa wooooote ili dunia nzima ielewe kinachoendelea kwetu. Kuja na simu iliyo na internet RUKHSA
 
Cuf ina viti 2 bara(tanganyika) ie lindi mjini na kilwa kusini na pia cuf ina madiwani karibu 200 huku tanganyika,
jee chadema wana viti vingapi zanzibar? Chadema Wana madiwani wangapi zanzibar?

Wingi sio jambo kiivyo. Angalia jongoo ana miguu mingi lkn hana mbio. Ni sawa na wingi wa watanganyika hauna maana yeyote ktk mambo ya muungano iko sawa na zanzibar iliyo na watu milion moja? Upo mlevi?

We ukianza dharau za kijinga kwa watanganyika eti wengi lakini sio kitu basi vumilia pia ukirushiwa vijembe kama hivi,
Kuna mdau mmoja hapa JF aliwahi kuandika hivi:


quote_icon.png
Originally Posted by Nguruvi3

5. Kwa uchumi wa bilioni 500, wabara wanafaidika nini kutoka Zanzibar? Hii ni sawa na bajeti ya wizara ya akina mama na watoto au mapato ya soko la kariakoo.
 
Hurusiwi kuvaa nguo za chama chengine zaidi ya zile za cuf. Kama unashida ya maandamano njoo la kama unashida ya kuvaa magwanda ya wafungwa subiri maandamano ya chadema keshatangaza padri slaa mda si mrefu.

Si utambulisho wa kuwa tuko pamoja kwenye masilahi ya taifa hata kama itikadi tofauti? Kwa hiyo unamaana hata vibarakashia, mitandio, vizubao, kanzu, vijambakoti na vikoi navyo havitakuwapo sio? Si haki jamani identity muhimu...au maandamano ni yana CUF tu na masilahi yao tu?
 
Hili jipu la UNDUMRAKUWILI WA KISIASA litawatesa sana sana tena sana Chama Cha CUF katika jamii yetu. Sijui kama kweli wanaliona hili au mpaka jahazi ligote chini ya bahari kusikofikika kiuokozi.

Vile vile wao kujaribu kufanya lolote kisiasa nchi kamwe haitoheshimika bila kwanza kuchagua gamba lipi la kuvua; je CUF wako tayari kulivua lile la userikali au la upinzani??

Uamuzi kwenu kabla ya muda kuyoyoma kwa sana kwani watu vichwa kama Prof Safari washaliona hilo mapema sasa wasisubiri mpaka wale wanachama wao wa uelewa wa chini nao waje wakaliona hili kasoro kwani hivyo hawafiki mbali licha ya kubahatika kifaa kwa jina la Duni Haji Duni na Julius Mtatiro.

CUF tambueni kwamba watu vichwa + Mbinu Rojorojo = Kifo na Kutoweka kwa Cha Chama bila Taarifa kwa namna iliyo sawa tu kuwa na hali itakavyoweza kuonekana pindi CUF kitakapokua na Watu Vichwa Maji + Mbinu Rojorojo inavyoweza kutokea.

Yakumbukeni maneno haya kabla hakujachelewa sana kwenu, CHADEMA tunawahitaji sana lakini kwa SURA INAYOKUBALIKA.
 
Kwa muda mrefu watu wamekuwa na kiu ya kuandamana. Kiu hiyo imeongezeka zaidi baada ya mafanikio yaliyopatikana huko Tunisia ana yale yanayoendelea Misri.

Kila hoja inayotolewa hapa jamvini watu wamekuwa wakionyesha wazi wazi nia yao ya kutaka kuandamana.

Kuna njia nyingi za kuandamana ili kufikisha ujumbe kwa wahusika. Ukweli ni kwamba hapa kwetu bado hatujawa na muamko wa kutosha kuingia barabarani. Nia na sababu zipo ila the spark is still lacking......pale pa kuanzia ndio bado!!

Jambo la msingi ni kuanza kutoa mafunzo ili wananchi waelewe kuhusu non-violent struggles. Hata kwa wengine wetu humu jamvini tunaweza tukawa hatujui nini maana ya maandamano na yanawezaje kuwa successful. Kwa nini inawezekana bila umwagaji damu. Tukiendelea na tabia ya kuingia barabarani wachache basi itatuchukua muda mrefu kufanikiwa. Lakini kama tukitoka ina numbers hakuna polisi wa kutosha kuzuia!!

Jaribu kufikiria kwamba kila mji kila kijiji watu wametoka wanatembea barabarani kupinga kupanda kwa bei ya nishati, malipo ya dowans, kufeli kwa wanafunzi nk. Pia kumlazimisha Waziri wa Elimu achukue hatua za haraka kuhusu kufeli kwa wanafunzi nk. Ikitokea hivyo ni lazima matokeo yataonekana tu!!

Ushauri wangu;

Tuandae waraka wa kiswahili utakaoelezea jinsi ya kufanya maandamano ya amani and how tow age non-violent struggles in a Tanzanian situation. Waraka huu tuusome wote na tuuelewe. Mapendekezo yatolewe ya nini cha kufanya kwa kuangalia mazingira yetu, elimu ya watanzania, kutokuwepo kwa ukabila na udini isipokuwa huo unaopandikizwa na baadhi ya viongozi etc.

Tukikurupuka kupeana tarehe za maandamano bila kujipanga mwisho wake utakuwa hauna matunda!! Waandaji lazima wajipange na Great Thinkers wa JF lazima watoe michango yao ya kitaalamu kulingana na mazingira yetu ili maandamano yafanikiwe!!
 
Kamati kuu ya CDM ina vichwa haijibu kwa jaziba hebu angalia baadhi ya maamuzi yake........

Kamati Kuu imepinga utaratibu wa kuunda Tume ya Rais katika uundaji wa Katiba Mpya


Kamati Kuu imeiagiza sekretariati ya CHADEMA kuendelea na harakati za kudai haki za wananchi wa Jiji la Arusha kwa njia za kisiasa.

Kamati Kuu imewaagiza madiwani wa CHADEMA katika Halmashauri ya Jiji la Arusha kuendelea kuingia katika vikao vya Baraza la Halmahauri hiyo na kuwawakilisha wananchi waliowachagua kikamilifu na wahakikishe kuwa wanatumia nafasi yao kufanikisha uchaguzi wa Meya.


Kamati Kuu imeunda timu maalumu ya wataalamu wa elimu kwa ajili ya kutafiti kwa kina sababu za matokeo mabaya ya Kidato cha Nne na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu katika kikao chake kitakachofanyika kabla ya Mwezi Mei 2011.

Kamati Kuu imewataka viongozi wa juu wa CCM na hasa Rais Kikwete kuacha kuchochea mgawanyiko wa dini hapa nchini kama njia ya kuficha udhaifu wake wa uongozi
 
Back
Top Bottom