JUMAMOSI, AGOSTI 04, 2012 05:38
NA GABRIEL MUSHI
*CWT yatangaza rasmi kurudi darasani
*Yakusudia kukata rufaa ngazi za juu
* Mukoba asisitiza madai yao yako palepale
*Alia na polisi wanaotisha walimu waliogoma
HATIMAYE Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kimesalimu amri na kutangaza kusitisha mgomo wa walimu uliodumu kwa siku kadhaa nchi nzima.
Kutokana na kauli hiyo, CWT imewataka walimu wote kurudi kazini ili kutekeleza agizo la Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, lililotolewa juzi mjini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Rais wa CWT, Gratian Mukoba, alisema pamoja na mambo mengine, hukumu hiyo imewakatisha tamaa kwa kiasi kikubwa, hivyo wanajipanga kwa ajili ya kukata rufaa.
Alisema maagizo yaliyotolewa na mahakama yatekelezwa na CWT, baada ya kuipitia kwa umakini hukumu hiyo.
"Leo (jana), nimewaita kwa ajili ya kutekeleza sehemu ya maagizo ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, yaliyotolewa na Jaji Sophia Wambura kwenye Shauri Na. 96 ya mwaka 2012. Katika hukumu hii, mahakama imeagiza chama kitoe maelekezo kwa wanachama wake kurudi kazini kuanzia leo (jana) Agosti 3, mwaka huu.
"Kwa maelekezo hayo, chama kinawaagiza wanachama wake kurudi kazini kuanzia leo (jana) kutekeleza majukumu yao ya kila siku, maagizo mengine ya mahakama yatatolewa maelekezo, baada ya kupitia hukumu kwa makini na kupata ushauri wa wakili wetu na wanachama watajulishwa," alisema.
Alisema kuhusu kulipa fidia ya hasara waliyoipata wanafunzi, chama kinasubiri taarifa rasmi ya Serikali, kwa kuwa CWT haina uwezo wa kufahamu hasara waliyopata wanafunzi.
Alisema mwenye uwezo wa kuwasilisha hasara hiyo, ni mlalamikaji katika kesi hiyo, ambaye ni Serikali.
"Kwa kuwa hukumu hii, imewakatisha tamaa walimu wanarudi kazini, huku mwajiri wao akionyesha kutowajali kutokana na madai yao kutopewa kipaumbele katika kuboresha maslahi yao.
"Walimu wanamwangalia mwajiri wao ambaye ni Serikali amewapuuza akifahamu kuwa kwa vyovyote vile atakimbilia mahakamani…hii haijafuta cheti cha kutopatikana kwa suluhu ya mgogoro wa Julai 25, mwaka huu, haiondoi ukweli kwamba maslahi ya walimu ni duni.
"Pamoja na walimu kuendelea kupuuzwa na mwajiri wao kwa kuwapa maslahi duni, chama kitaendelea na majadiliano na Serikali kuhusu nyongeza ya mishahara na posho kama kilivyowasilisha. Chama kina imani hukumu hii imetoa somo kwa mwajiri ili atambue umuhimu wa kuzungumza na walimu wote nchini," alisema.
KUKATA RUFAA
Kuhusu kukata rufaa, alisema chama hicho kinawasiliana na wakili wake ili kuona uwezekano wa kukata rufaa.
"Baadhi ya vipengle vya hukumu, vinahitaji ufafanuzi wa Mahakama ya Rufaa ili kuondoa utata wa kisheria, wanachama wanaombwa kuwa wavumilivu wakati huu.
"Kwa sababu mahakama, imetuonea kwa kipengele wanachodai tulitoa muda kwa Serikali kabla ya kuitisha mgomo katika siku za mapumziko, wakati wao wenyewe walishawahi kutoa saa 3:48 usiku," alisema.
WATAKA KULINDWA
Kuhusu usalama wao, Mukoba alisema katika kipindi cha mgomo baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya, waliamuru wanachama wa CWT na viongozi wake kukamatwa bila na sababu za msingi.
"Baadhi yao, wamefikishwa mahakamani kwa kuhamasisha mgomo wa walimu, chama kina wasiwasi kuhusu usalama wa viongozi na wanachama walioshiriki na kuhamasisha mgomo wa walimu.
"Chama kinatoa rai, kwa Serikali na vyombo vya dola, wakiwamo maofisa usalama na makamanda wa polisi wa mikoa na wilaya, kuhakikisha viongozi wa chama na wanachama waliohamasisha mgomo wanakuwa salama bila kudhurika.
MAZUNGUMZO NA SERIKALI
Alisema walimu wanarudi kazini bila kuwa na mawazo yaliyotulia, juu ya utendaji wao wa kazi.
"Chama kinatoa wito kwa Serikali, kukutana na CWT haraka kuendeleza majadiliano ya madai ya walimu, msimamo wetu tangu mwanzo ulikuwa ni kujadiliana na Serikali kupitia kwa msuluhishi, aliyeteuliwa na Tume ya usuluhishi na uamuzi.
"Tatizo lilikuwa ni serikali ambayo haikuwa tayari kuzungumza na CWT, ushahidi umeonekana kuwa muda wa siku 50 za mgogoro huu, hakuna mwakilishi wa Serikali aliona umuhimu wa kukutana na viongozi wa CWT kuzungumza nao, badala yake waliamua kutumia vyombo vya habari kukishambulia chama.
"Chama kinashauri Serikali ichukue hatua za haraka kutibu majeraha ya walimu kwa kujadiliana na CWT kuhusu madai yao na kufuta barua zote zilizosambazwa kwa walimu kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua za kinidhamu," alisema.
Julai 30, mwaka huu, CWT kiliitisha mgomo wa walimu nchi nzima ili kuishinikiza Serikali kutekeleza madai yao ambayo ni nyongeza ya mshahara kwa asilimia 100, posho ya walimu wanaofundisha masomo ya sayansi asilimia 55, walimu wa sanaa 50 na mazingira magumu 30. Lakini Rais Jakaya Kikwete akihutubia taifa katika utaratibu wake aliojipangia, alisema Serikali haina uwezo wa kulipa madai ya walimu kutokana na bajeti ndogo iliyopo.