Tahrir Square Fundisho Kwa CCM ( Makala, Raia Mwema) | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tahrir Square Fundisho Kwa CCM ( Makala, Raia Mwema)

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by maggid, Feb 17, 2011.

 1. m

  maggid Verified User

  #1
  Feb 17, 2011
  Joined: Dec 3, 2006
  Messages: 1,084
  Likes Received: 397
  Trophy Points: 180
  Na Maggid Mjengwa,

  UKOMO wa uvumilivu wa kukandamizwa umewafanya WaMisri kuandamana kwa mamilioni na kumtimua Hosni Mubarak madarakani.
  Waarabu wale walikuwa na kiu ya uhuru, kiu ya haki . Ni kiu ya zaidi ya miongo mitano, miaka 50. Kule Misri, tuliwaona WaMisri wenye furaha kuu usiku ule wa mkesha wa ’Tahrir’ ikiwa na maana ya ukombozi.

  WaMisri walikesha wakiimba na hata kutoa machozi ya furaha. Misri , kama ilivyokuwa kwa Tunisia, hatukuziona bendera za vyama. Tulioziona bendera za mataifa hayo. Kwao, ilikuwa ni sawa na mataifa yao kuzaliwa upya. Furaha ile ya Wamisri ni sawa kabisa na taifa lao kushinda kwa mara ya tano, fainali za Kombe la Dunia.

  WaMisri wale hawakuchoshwa tu na Hosni Mubarak. Walichoshwa na mfumo mzima na hususan chama chao tawala. Ndio, tulishuhudia, kuwa jengo la kwanza kutiwa kiberiti na waandamanaji lilikuwa ni jengo la Makao Makuu ya Chama tawala cha nchi hiyo, NDP- National Democratic Party. Kilikuwa chama kikongwe na kilichoshika hatamu za uongozi.

  Kwa WaMisri, NDP kilikuwa ni chama walichokihofia hata katika maisha yao ya kila siku. National Democratic Party kwa maana ya Chama Cha Taifa Cha Demokrasia hakikuwa cha Taifa na wala Demokrasia ndani yake. Kilikuwa chama cha wateule wachache akiwemo mwana wa Hosni Mubarak aitwaye Gamal Mubarak aliyepewa cheo cha Ukatibu Mkuu na aliandaliwa na baba yake kumrithi madaraka ya Urais.

  Ndio, WaMisri walifikia ukomo wa uvumilivu. Kwa mwanadamu , unapoukandamiza mpira uliojaa na hata ukabonyea, basi, kuna mawili yanayoweza kutokea. Mosi, kama mpira umebonyea, basi, yaweza kuwa upepo umetoka kidogo. Pili, kama umebonyea, basi, yaweza kuwa mpira huo umefutuka upande wa pili.
  Na kibaya zaidi, kama mpira huo ukakandamizwa kwa nguvu nyingi, basi, utapasuka. Ndio tuliyoyashuhudia kule Misri. Tumeyashuhudia pia Tunisia. Tutakuja kuyashuhudia kwingineko.

  Vijana wale wa Tunis, Cairo na Suez hawana tofauti na vijana wa Kigali,
  Nairobi, Dar es Salaam na Kampala. Tofauti ni kwenye viwango vya uvumilivu. Ni kama kabati la nguo. Kabati likijaa nguo, na mwenye nalo akazidi kuweka nguo, basi, sio tu mwenye nalo atashindwa kulifunga, bali nguo zitaanza kuanguka.

  Makabati ya vijana wa Tunisia na Misri yalishajaa. Ndio maana, tumewaona vijana wale wakilala mbele ya vifaru vya jeshi . Walikuwa tayari kwa lolote, liwalo na liwe. Makabati ya vijana wetu bado yana nafasi ya kuweka nguo. Busara kwa watawala wetu ni kutosubiri yajae.

  Ndio, binadamu anayekandamizwa sana hufikia kikomo cha uvumilivu. Miaka kumi iliyopita hakuna aliyefikiri vijana wale wa Tunisia na Misri wangefanya waliyoyafanya. Hata mjusi ukimwandama sana anaweza kugeuka nyoka kwako. Na paka naye unaweza kumfuga na ukamlisha vyote akanenepa. Lakini, siku ile utakapojifungia kwenye chumba kidogo, wewe na paka wako. Kisha ukachukua rungu uanze kumpiga nalo , hakika, ukali wake utazidi wa chui. Atakurarua, paka wako mwenyewe!

  Yaliyotokea Misri ni darasa kubwa kwa watawala na vyama barani Afrika. Kuwa unapoukandamiza mpira uliojaa na ukabonyea, basi kuna matokeo ya upepo kupungua, mpira kufutuka upande mwingine au kupasuka. Mawili ya mwisho ni lazima yatokee, ni suala la wakati tu.

  Viongozi Afrika wanapaswa kutambua sasa, kuwa Mwafrika wa mwaka 1975 si Mwafrika wa mwaka 2011. Waafrika wameamka. Viongozi Afrika wana lazima ya kuendana na mabadiliko ya wakati. Hizi ni zama za mabadiliko. Na Mabadiliko ya amani Afrika yanawezekana, mwenye kuyazuia mabadiliko ya amani, atambue, kuwa mabadiliko yenye vurugu hayaepukiki. Hilo la mwisho lina hasara kubwa.

  CCM ina cha kujifunza?

  Ni ukweli, idadi ya Watanzania, na hususan vijana waliokichoka Chama tawala, Chama cha Mapinduzi, inaongezeka kila kukicha. Kufikiri kingine ni kujidanganya. Leo kuna vijana wenye kiu kubwa ya kuindoa CCM madarakani ili waone tu itakuwaje wakija wengine. Maana, CCM pia imejitengenezea mazingira ya kuhofiwa badala ya kuheshimiwa.

  Mathalan, kuna wengi leo wananing’iniza bendera za CCM kwenye biashara zao, au kujiita WanaCCM. Si kwa sababu wanakipenda na kukiheshimu chama hicho, wanakihofia.

  Ni ukweli, leo kuna Watanzania wenye kukihofia zaidi Chama Cha Mapinduzi kuliko Mungu wanayemwamudu. Na lipi jema kwa mtawala na chama; kuhofiwa au kupendwa? Mwingine angependa vyote, lakini haiwezekani. Jema ni kupendwa na kuheshimiwa.

  CCM itambue sasa, kuwa, Tahrir inakuja hata Tanzania, ni suala la wakati tu. Na vijana wa Tanzania huenda wasiingie mitaani wakafanya kama wenzao wa Misri na Tunisia. Watasubiri siku ile ya kwenda kupiga kura ifikapo 2015. Tahrir ya vijana wa Kitanzania yaweza kuwa vituo vya kupigia kura. Wataandamana kwa wingi wakiwa na vitambulisho vyao vya kupigia kura. Wataandamana kwenda kuiondoa CCM kwa nguvu za kura.

  Salama ya CCM?
  CCM inahitaji sasa ‘ Tahrir’ yake ya ndani ya chama. Nimepata kuandika, kuwa ili CCM isalimike na kubaki madarakani katika chaguzi zijazo, sio tu inahitaji kufanya mabadiliko makubwa, bali mabadiliko makubwa yenye kishindo.
  CCM inahitaji kurudi kwenye misingi iliyoanzisha chama hicho. Huu ni wakati wa kurudisha misingi ya kimaadili ya chama na uongozi. Misingi iliyokuwapo huko nyuma. Angalia, iko wapi Miiko ya Uongozi? Imevunjwa, na ndio maana ufisadi umetamalaki.

  Kwa MwanaCCM, sasa sio suala la kushinda uteuzi wa ndani ya Chama na kujihakikishia kuingia Ikulu au Bungeni, kuna umma unaotaka mabadiliko utakaomkabili mgombea wa CCM, awe mgombea Urais, Udiwani au Ubunge. Kuingia ulingoni na ‘ CCM ile ile’ itakuwa ni hatari kwa wagombea wengi wa CCM siku zijazo.

  Ni ukweli, kuwa ndani ya CCM imeanza kuporomoka, misingi iliyopelekea kuanzishwa kwa Chama hicho tukianzia na vyama mama vya TANU na Afro- Shiraz. Hili ni jambo la hatari sana. Ikumbukwe, Vyama mama kwa CCM, TANU na Afro- Shiraz, vilikuwa ni kimbilio la makabwela, kimbilio la wanyonge.

  Lakini, CCM ya sasa inakimbiliwa na wafanyabiashara, wasomi na wajanja wengine. Wasomi hapa kwa maana ya hata wale wenye taaluma zao. Wako tayari kuzikimbia taaluma zao na kuingia kwenye siasa za vyama, hususan Chama cha Mapinduzi. Baadhi yao wanasukumwa huko kwa ajili ya kutafuta maslahi zaidi. Maslahi binafsi. Na kuna wanaoambiwa; "Mkitaka mambo yenu yawanyokee, njooni CCM". Si mambo ya wananchi, ni mambo yao binafsi!

  .
  Kuna wanaokimbilia ndani ya CCM kwa kuamini katika malengo na madhubuni ya kuanzishwa kwa chama hicho. Lakini, kuna wanaokimbilia ndani ya CCM wakiwa na malengo na madhumuni ya kwao binafsi yasiohusiana kabisa na ya CCM. Kwao wao, CCM ni sawa na daraja la miti la kuwasaidia kuvuka na kufika wanakotaka kwenda.


  CCM ina nafasi ya kujisahihisha. Si udhaifu kwa kiongozi au wanachama wa chama cha siasa kukiri udhaifu na kujisahihisha. Mwl. Nyerere katika kijitabu chake cha " Tujisahihishe" anaandika; "Nataka kutaja makosa machache ambayo mara nyingi huzuia Umoja wowote kuwa imara hata ushindwe kutimiza madhumuni yake. Ukiondoa matatizo wayapatayo binadamu kwa sababu ya mambo kama mafuriko, nzige, kiangazi, nk, matatizo yao mengi hutokana na ubinafsi"

  "Swali ambalo twalisikia mara kwa mara; " Hali yetu ya baadaye itakuwaje? Mtu anayeuliza anafikiri kuwa TANU iliundwa kwa faida yake yeye binafsi. Ni kama kwamba TANU ilipoundwa ilimwahidi kwamba ikiwa atakubali kuwa mwanachama, au kiongozi, basi, TANU itamfanyia yeye jambo fulani kama tuzo! Anasahau kabisa, kuwa TANU inajishughulisha na haja za jumuiya kwa ujumla.

  Lakini, kwa mtu wa aina hiyo, hata kama TANU inatimiza madhumuni yake ya Jumuia, ataona kuwa ni umoja ambao hauna maana kwa sababu haumtimizii haja zote za nafsi yake! Huu ni ubinafsi. Kama wanachama wa TANU, na hasa viongozi, hawatakiuhukumu chama chetu kwa mahitaji ya jamii yao, bali watakihukumu kwa mahitaji ya nafsi zao wenyewe, chama hakitadumu. Wanachama wa aina hiyo ni ugonjwa katika chama" (J.K Nyerere "Tujisahihishe",1962).

  Maggid,
  Iringa

  Alhamisi, Februari 17, 2011

  mjengwa
   
Loading...