Taharuki: Mgodi uliofungwa kwa kuua watu zaidi ya 20 Arusha wafunguliwa kinyemela

buswelu moja

JF-Expert Member
Aug 24, 2014
226
147
Utata imeibuka baada sintofahamu kuhusu mgodi wa Moramu uliopo eneo la Moivaro ambao ulisababisha vifo vya zaidi ya 20 kwa nyakati tofauti kufunguliwa kinyemela huku mamlaka mkoani Arusha zikitupiana mpira juu ya nani aliyehusika kufungua mgodi huo.

Mgodi huo umekuwa na historia ya kusababisha maafa mbalimbali kama vifo kwa nyakati tofauti hususani kipindi cha mvua ambapo mwaka huu umesababisha vifo vya watu watatu baada ya kufukiwa na vifusi vya moramu.

Baadhi ya Watumishi wanaodaiwa kufanya kazi katika mgodi huo wameonekana Leo wakiwa na mashine mbalimbali huku wakichimba moramu katika mgodi huo hali ambayo imeibua maswali mengi kwa wakazi mbalimbali jijini Arusha.

Hatahivyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk Madeni Maulid alipohojiwa na waandishi wa habari kuhusu taarifa hizo leo nje ya ofisi yake alikanusha vikali ofisi yake kutoa idhini ya kufunguliwa kwa mgodi huo.

Mbali na kukanusha taarifa hizo Dk Madeni alimpigia kwa simu yake ya mkononi afisa mazingira wa jiji la Arusha, Mbuya na kumuuliza kuhusu madai hayo ambapo afisa huyo alikanusha taarifa hizo huku akiutupa mpira kwa ofisi ya afisa madini mkazi mkoani hapa kwamba ndio wameidhinisha kibali cha kufunguliwa kwa mgodi huo.

"Wewe Mbuya naomba unieleze ni nani amesema kwamba mimi nimeruhusu mgodi huo ufunguliwe? naomba uwaambie hao watu wasitishe shughuli zote sasa hivi "alisema Dk Madeni huku akimwelekeza afisa huyo kwa njia ya simu

Ofisa huyo alimjibu kwa simu mkurugenzi huyo kwamba kwa taarifa alizonazo ofisi ya afisa madini mkazi ndio imeidhinisha kibali cha kufunguliwa kwa mgodi huo ambapo pia wametoa masharti mbalimbali ambayo wahusika wanapaswa kuyatekeleza wakati wanachimba moramu katika mgodi huo.

Hatahivyo, Dk Madeni alisisitiza kwamba kwa taarifa alizonazo mgodi huo ulifungwa na kamati ya ulinzi na usalama wilayani Arusha na kudai kwamba endapo wahusika walitaka kuendelea na shughuli zao walipaswa kwanza kupata barua kutoka kwa kamati hiyo.

Alipotafutwa afisa madini mkazi mkoani Arusha, Hamis Kamando ili ajibu madai ya ofisi yake kutoa kibali cha kufunguliwa kwa mgodi huo alisema kwa kifupi ofisi yake haijatoa kibali chochote cha kufungua mgodi huo.

"ni nani aliwapeleka huko? hakuna kibali chochote nilichotoa kufungua mgodi huo kifupi sijaruhusu "alisema Kamando kwa njia ya simu huku akisisitiza kwamba yuko Mererani kwenye vikao

Baadhi ya Waandishi wa habari walifika kutembelea mgodi huo uliopo nje kidogo ya jiji la Arusha na kukuta watu mbalimbali wakiendelea na kazi ya kuchimba moramu kama kawaida kwa kutumia mashine ya Excavator.

Mkazi wa eneo hilo, Ayoub Stephen Mollel alisema anashangaa kuona serikali imefungulia shughuli katika eneo hilo ihali baadhi ya ndugu zake walifariki baada ya kufukiwa na vifusi na hajawahi kupata fidia yoyote kuhusu maafa hayo.

"Mimi binafsi nashangaa Sana serikali imefungulia mgodi huo wakati kwanza huu mgodi una historia ya kuua watu alafu nina ndugu zangu walishakufa na mpaka Leo hatujawahi kuona fidia yoyote "alisema Mollel

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Maria Saitoti alisema kwamba amesononeshwa na hatua ya kufunguliwa kwa mgodi huo kwasababu binafsi alipoteza watoto wake wawili ambao walifariki wakichimba moramu baada ya kufukiwa na kifusi cha moramu.

Mgodi huo umekuwa na historia ya kusababisha maafa mbalimbali ya vifo ambapo serikali mkoani Arusha imekuwa ikiufunga mara kwa mara na kisha kuufungulia jambo ambalo limekuwa likipingwa vikali na wananchi kwa kuwa linahatarisha uhai wa wananchi.

Mwisho.

Pichani chini ni mashine ya excavator ikionekana Leo katika mgodi huo uliofungwa na serikali mkoani Arusha hivi Karibuni ikichimba moramu, mgodi ambao umekuwa ukipelekea maafa ya vifo vya watu mbalimbali mkoani Arusha kwa nyakati tofauti.

IMG_20200324_144026.jpeg
IMG-20200324-WA0062.jpeg
IMG_20200324_143955.jpeg

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom