Majuzi Fredrick Sumaye, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Mwungano wa Tanzania, aliwaita waandishi wa habari kuwaelezea kile kilichoitwa rushwa mpya katika chaguzi za ndani za CCM. Katika kulijadili hili, tuiangalie dhamira na uadilifu wa SUMAYE, na kisha nafasi ya SUMAYE katika kuenzi au kuipiga vita rushwa.
Katika mkutano wake na waandishi, SUMAYE alitaka kuwaaminisha waandishi na watanzania kuwa yeye ni mtu safi, mtu asiyependa rushwa. Na kwa maneno yake alitamka kuwa atapigana ndani ya CCM kuondoa mfumo unaopalilia uongozi wa rushwa.
Katika kuitafakari kauli hiyo ya SUMAYE, tumjadili SUMAYE kama kweli ni mtu mwenye uwezo wa kupigana na rushwa, na pia tuangalie, na kisha tujiulize: Je, SUMAYE atapigana na rushwa za ndani ya CCM ili yeye SUMAYE asiye na uwezo wa kupata hela ya kutosha kuhonga aweze kushinda, au atapiga vita rushwa kwa sababu anaichukia rushwa?
Napenda kuwakumbusha wachambuzi kuwa ni huyu SUMAYE akiwa waziri mkuu ndiye aliyekuwa mtetezi mkuu wa ile rushwa walioianzisha CCM na kuiita TAKRIMA. Hakuna aliyekuwa mtetezi mkuu wa TAKRIMA wakati ule kumzidi SUMAYE. Ni huyu SUMAYE ndiye aliyewaambia vijana na wafanyabiashara mara kadhaa kuwa, 'ukitaka biashara yako istawi, lazima uwe ndani ya CCM'. Ni wakati wake vijana wengi ili wasisumbuliwe na polisi, askari wa jiji na TRA waliamua kuchomeka bendera za CCM ili kuepuka usumbufu. Na kwa upande mwingine, kauli yake ilidhihirika kwa wale wafanyabiashara ambao walionekana kushabikia upinzani, baadhi yao walifilisiwa kwa kuitumiaa TRA, na wengine kupitia mamlaka za miji.
Ndani ya CCM hakuna kiongozi hata mmoja ambaye hajawahi kupokea rushwa au malipo yasiyo halali. Ni CCM ndiyo walioasisi malipo ya kukaa (sitting allowance), ambao ni wizi uliopewa kanuni ya kuulinda. Ni CCM ndiyo walioasisi malipo anayopewa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri na Manaibu, ambayo wanaiita officiation allowance. Hii ni posho ya kukata utepe wanapofungua miradi au kuizindua. Huu nao ni wizi wa hela ya Watanzania unaolindwa na nyaraka zilizoandaliwa na wezi wenyewe, akiwemo Sumaye.
UKWELI: Sumaye hana tofauti na viongozi wengine wa CCM. Hakuwahi kuwa na tofauti na hata sasa haonekani kuwa ni tofauti. Kauli alizozitoa ni za chuki kwa wana-CCM wenzake watoa/wapokea rushwa baada ya kuona hana uwezo wa kuwashinda. Ni vema Watanzania na waandishi wa habari mngemwuliza ushiriki wake wa kuanzishwa na kupalilia rushwa kwa kuipamba kwa neno, 'TAKRIMA'. Tunamshukuru Mtikila aliyeipinga kwa nguvu zote, na kueleza wazi kuwa TAKRIMA ni rushwa, na kisha mahakama kuridhia kuwa kinachoitwa na CCM TAKRIMA, ndicho watu waadilifu hukiita RUSHWA.