Taazia: Buriani Mja wa Kheri Sheikh Salim bin Ahmed Bajaber

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,920
30,263
TAAZIA: MJA WA KHERI SHEIKH SALIM BIN AHMED BAJABER

Nimepata taarifa hii leo mchana kuwa Mzee Salim Ahmed Taib Bajaber Mkurugenzi Mkuu wa Pembe Flour Mills (PFM) amefariki Mombasa na kazikwa Markaz Madina, Amkeni Kikambala.

Nilimfahamu Mzee Salim mwanzoni mwaka wa 2004 yeye na wakurugenzi wenzake PFM walipokuja Tanga kutoka Kenya kujenga kiwanda cha unga wa ngano.

PFM ni wasagishaji wakubwa wa unga Kenya na wana jina linalotajika nchi nzima.

Pamoja na kusaga unga wanatengeneza pia vyakula vya wannyama. Wakati huo mimi nikiwa mfanyakazi wa Tanzania Ports Authority nikawa karibu sana na kiwanda hiki kikazi kwani wao walikuwa kati ya waagizaji wakubwa wa ngano kupitia bandari ya Tanga.

Hivi ndivyo nilivyokuja kufahamiana na viongozi wakubwa wa PFL ambao wote ni kutoka familia moja.

Nikamfahamu Salim Abubakar aliyekuwa akiendesha PFM, Nairobi maarufu katika duru zetu za kazi bandarini tukimwita Salim wa Nairobi kwa kuwa yeye kituo chake cha kazi Kilikuwa Nairobi.

Nikamjua na Mzee Abdallah ambae mwanae, Salim Abdallah ndiye aliyekuwa Meneja wa PFM, Tanga.

Wote hawa watu wema wasio na mfano.

Walipoingia Tanga Mkoa wa Tanga ukajua kuwa wameingia watu barabara na wa kisawasawa.

Bandari ikachangamka na mji pia ukachangamka na barabara ya kuelekea kiwandani kwao Kange ikachangamka.

Ndani ya dala dala utasikia kondakta ananadi, ‘’Pembe, Pembe, Pembe,’’ kuwagutua wanaoshuka kiwandani ama wawe wafanyakazi au wafanya biashara ndogondogo nje ya langu kuu la kiwanda.

Lakini lililowafanya wakazi wa Tanga waitambue na kuijua PFM lilikuwa jambo ambalo lilinyanyua jina la Pembe mbinguni na litakumbukwa daima ilikuwa kwa wao kujenga chuo kusomesha watoto na vijana Uislam.

Baada ya kifo cha Sheikh Muhammad Ayub muasisi wa TAMTA kufariki, mwanafunzi wake mkubwa Sheikh Muhammad Bakari alifundisha TAMTA au kwa jina lingine Shamsiyya kwa muda kisha alitoka hapo chuoni na kwenda kuanza kusomesha Magomeni kwenye msikiti mdogo.

Sheikh Muhammad Bakari akaendelea kusomesha chini ya taasisi yake mpya aliyoiita Shams Maarif akisaidiwa na walimu wachache kutoka Shamsiyya mmojawao akiwa Mwalimu Miraj na mwengine Sheikh Said Makata.

Hiki kilikuwa kipindi kigumu sana kwake na kwa wanafunzi waliomfuata kwani alijaza wanafunzi wengi katika mahali finyu.

Waislam wa Tanga hawakupenda kuona hali ile lakini hawakuwa na la kufanya.
Kujenga chuo kipya inataka fedha nyingi.

Sheikh Muhammad Ayub aliendelea kusomesha na mara kwa mara alikuwa anapopewa pole akisema kuwa ile hali iliyokuwa ikimkabili katika kusomesha ilikuwa ni qadar ya Allah.

Kipindi hiki ndipo Mzee Salim alipofika Tanga kujenga kiwanda na akapata habari kuwa Sheikh Muhammad Bakari amefungua chuo anasomesha Magomeni katika msikiti mdogo na ana wanafunzi wengi kutoka sehemu mbalimbali za nchi na hana pa kuwaweka.

Mzee Salim hata kabla hajakamilisha ujenzi wa kiwanda wala hajauza hata mfuko mmoja wa kilo moja ya unga wa ngano, kwa kasi ya ajabu akaleta mkandarasi kujenga chuo kikubwa na msikiti kwa ajili ya Waislam wa Tanzania.

Kitendo hiki kiliwagusa watu wa Tanga kwani kwa kawaida taasisi zote Tanga zilijengwa na wenyewe Waislam kwa michango yao na msaada wa wafadhili wachache.

Sharif Maarif ilijengwa na Mzee Salim na nduguze.

Nakumbuka siku ya ufunguzi wa majengo ya chuo cha Sharif Maarif na Masjid Bajaber tarehe 2 May, 2004.

Ugeni mkubwa kutoka Mombasa akiwemo Sharif Khitami na mwanae Sharif Mundhari Khitami walihudhuria shrehe hiyo ya ufunguzi wa msikiti na madrasa ya Shams Maarif.

Ugeni huu kutoka Kenya ulipokelewa na ndugu zao wa Tanzania, Iddi Simba, Bakari Mwapachu na umma mkubwa wa Waislam wa Tanga na pembezoni yake pamoja masheikh maarufu wa Tanga na Waislam wa kawaida.

Siku ile watu wa Tanga kwa mara ya kwanza ndiyo waliwatia machoni Mzee Salim Bajaber, Mzee Abdalah wa Mombasa na Salim Abubakar wa Nairobi.

Sheikh Alhad Omar bingwa wa kusoma Qur’an kutoka Dar es Salaam ndiye aliyesoma Qur'an kufungua hafla hii.

Hakika hii ilikuwa siku ya kukumbukwa.

Alikuwa akija Tanga kwa shughuli za kiwanda atakuja ofisini kwa Meneja wa Bandari ya Tanga ambako wakuu wote wa idara tutakuwapo.

Ikiwa nitajua yuko Tanga na hakutokea bandarini nitakwenda kumuona kiwandani ofisi za PFM au nitakwenda nyumbani kwa mwanae Salim Abdallah Meneja wa PFM Tanga alipokuwa akifikia.

Juu ya utajiri aliokuwanao ukiwa na yeye kama humjui wala hutoweza kuhisi nguvu zake.

Mzee Salim alikuwa mtu wa maskhara sana na Allah alimjaalia unyofu nisioweza kuwa na naneno kueleza.

Siku moja tuko ofisini kwa Menaja wa Bandari na tukawa tumemaliza kikao tumekaa tunazungumza hili na lile mfano tuko barzani tuna bariz.

Bwana Fedha wa Bandari akamwambia Mzee Salim, ‘’Mzee Salim kwanza nimekumbuka unadaiwa hapa.’’

Mzee Salim hakujua kuwa Bwana Fedha wetu alikuwa akimtania.
Chini ya kiti alichokalia alikuwa na ''briefcase,'' akainama kaiweka juu ya meza akaifungua.

Mimi nilikuwa nimekaa pembeni yake.
Nilichokiona mle ndani nilikuwa nakiona kwenye picha tu.

Bwana Fedha na yeye alikiona pia kama mimi.
Sote tulikuwa wawili tumeshtuka na wenzetu waliiona hali ile yetu.

‘’Mzee Salim funga mimi nakutania huna deni hapa bandarini.’’
Mzee Salim akaufunga mkoba wake.

Wale ambao hawakuona kilichokuwa ndani ya mkoba ule walisubiri Mzee Salim aondoke ndipo walipotuuliza sisi tuliokuwa karibu nini tulishuhudia.

Siku moja nimekwenda kumwamkia Mzee Salim kiwandani nikamkuta yuko ofisini kwa Salim Abdallah Meneja wa PFM.

Baada ya kumtokea salamu akaitika na yeye muda wote ni mtu wa tabasamu na bashasha akaniambia hata sijatulia kitini, ''Mohamed ehe sasa nini unataka, ndugu zako wote nimewapa kazi usinambie sasa umekuja unataka nimpe kazi mama watoto wako.''

Sote tukaangua kicheko.

Mwaka wa 2010 Mwezi wa Ramadhani Salim Abdallah kanipigia simu kunialika futari nyumbani kwake akanambia kuwa wazee wote wako hapo kwake na itapendeza ikiwa tutafuturu pamoja.

Ilikuwa nimefanyiwa upasuaji mkubwa siku si nyingi na nilikuwa nimekonda sana.

Mzee Salim aliponiona akashtuka huku akiwa katika tabasamu kama kawaida yake akaniuliza nimekumbana na dhoruba gani hata kunifanya vile.
Basi nikamfahamisha na akaniombea dua.

Ile namna ya Mzee Salim alivyokuwa akizungumza na wewe ilikuwa inakufanya utulie na uondokwe na hofu kuwa hapa nilipo nipo mbele ya mtu mzito kwa maana khasa ya uzito kama uzito ulivyo.

Tunamwomba Allah awape subra wafiwa wote Tanga hususan walimu na wanafunzi wa Sharif Maarif na jamaa walioko Mombasa.

Tunamwelekea Allah na tunamuomba amghufirie mzee wetu dhambi zake na amtie Pepo ya Firdaus.

Amin.
1661203191696.png

1661203265285.png
 
Mohamed kipindi kile hapakua na benki? Kwanini sheikh alitembea na minoti mkononi, tudokolee hali ilivyokuwa
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom