Kumbukumbu ya Ramadhani 8

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,918
30,259
KUMBUKUMBU YA RAMADHANI 8 : MFUNGO MOMBASA NA SHARIFF SALIM ABDALLAH (SAL DAVIS) NA SHARIFF MUHDHAR KHITAMI 2009

Ndugu zangu hawa masharifu wawili wote wanatoka katika koo kubwa na maarufu mjini Mombasa.

Baba yake Shariff Salim Abdallah maarufu kwa jina la Sal Davis alikuwa memba wa LEGCO, (Baraza la Kutunga Sheria la Kikoloni) kwa takriban miaka 30.

Shariff Khitami alikuwa kiongozi wa Waislam na tabibu maarufu.

Nilimfahamu Muhdhar Khitami Dar es Salaam katika Maonyesho ya Saba Saba, Kilwa Road yeye na wenzake walipokuwa katika banda moja wakitangaza shule yao Mombasa Coast Academy kutoka Kenya.

Mimi nilikuwa mmoja wa maofisa katika banda la Bandari na wakati mwingine ili kunyoosha miguu ninapokuwa sipo zamu nikawa natembelea mabanda mengine kuangalia wanaonyesha kitu gani.

Hivi ndivyo nilivyofika katika banda la shule ya Mombasa Coast Academy nikafahamiana na Shariff Muhdhar Khitami nikawa kutoka siku ile nimepata rafiki-ndugu.

Hii ilikuwa katika miaka ya mwishoni 1990s.

Nilikuwa bado sijafahamiana na Shariff Salim Abdallah.

Nikaja kukutana na kaka yake Shariff Muhdhar Khitami, Dr. Ahmed Binsumeit Kampala mwaka wa 2003 kisha nikakutananae Johannesburg mwaka wa 2006 lakini sikujua kama hawa walikuwa ndugu kwa kuwa Dr. Sumeit sikuona jina la Khitami katika majina yake.

Dr. Sumeit alikuwa amenialika Maulid ya Lamu tulipokutana Kampala lakini sikujaaliwa kwenda na tulipokutana tena Johannesburg akanikumbusha mwaliko wake.

Mwaka uliofuatia 2007 nikahudhuria Maulid ya Lamu na ndipo nikakutana na Dr. Sumeit na mdogo wake Muhdhar na nilishangaa Dr. Sumeit aliponifahamisha kuwa Muhdhar ni mdogo wake.

Dr. Sumeit yeye alishangaa kuwa mimi na mdogo wake ni marafiki toka Tanzania na tukijuana kitambo.

Hawa ndugu wawili nikawa nalala na wao chumba kimoja kwenye nyumba yao ya Lamu.

Hii ilikuwa heshima kubwa sana kwangu.

Mwaka wa 2016 nilikwenda Dubai na safari yangu hii ilikuwa kwenda kuwapa mkono wa taazia watoto wa Aman Thani ambao walikuwa wamefiwa na baba yao.

Hiki ni kisa kinachohitaji muda makhsusi kukiieleza lakini kwa ufupi ni kuwa nilikuwa nina hariri kitabu kipya cha Aman Thani na nilikuwa nimekusudia kusafiri kwenda Dubai kwa Aman Thani kukikamilisha kitabu na tiketi ninayo mkononi.

Nikaletewa taarifa kuwa Aman Thani kalazwa hospitali.
Haukupita muda mrefu akafariki.

Nikaenda Dubai kutoa mkono wa pole.

Nikiwa Rashidiyya, Dubai nilikwenda kusali Maghrib msikiti wa jirani nilipokuwa nakaa.

Hapa Rashidiyya ndiyo sehemu walipofikia Wazanzibari baada ya mapinduzi ya Zanzibar mwaka wa 1964.

Kiongozi wa Dubai Sheikh Rashid aliwapa hifadhi Wazanzibari na aliwajengea nyumba na huo msikiti.

Kitongoji hiki kina historia kubwa sana katika historia ya Zanzibar.
Tulipomaliza kusali pakawa na kisa cha Isra na Miraji.

Sheikh aliyekuwa anatusomea kisa hiki alikuwa Dr. Ahmed Sumeit akitokea Muscat.

Alifurahi sana kuniona pale msikitini.
Allah ana shani yake.

Nimekutana na Dr. Sumeit kwa mara ya kwanza Kampala Nile Hilton mwaka wa 2003, tukakutana tena Johannesburg 2006, Mombasa, Lamu 2007 na Dubai 2016.

Kuna kitu nataka nieleze hapa.

Nilipofika Mombasa 2007 kuelekea Lamu kwenye Maulid niliona nilale Mombasa na asubuhi ndiyo nielekee Lamu.

Nikawa nimepanga hoteli moja inaitwa Saphire.

Sijui Dr. Sumeit alijuaje usiku akanifuata hotelini na jamaa wengine kwa nia ya kunihamisha na kunipeleka nyumbani.

Nilimtaka radhi nikamsihi asitaabike.
Hawa ndiyo ndugu zangu.

Ramadhani mwaka wa 2009 mwezi wa Ramadhani niliamua niende Mombasa kwa Shariff Salim Abdallah Salim maarufu kwa jina la Sal Davis nikamalize kuandika kitabu cha maisha yake.

Kitabu kilikuwa kimekamilika ila nilitaka tukipitie pamoja niweke sawa baadhi ya mambo.

Sal Davis alikuwa anakaa Nyali Beach.

Mahali patulivu panapofaa sana kwa kazi yangu inayotaka utulivu.
Sal Davis alikuja Mwembe Tayari stendi kuu ya mabasi kunichukua kwenda Nyali Beach.

Ilikuwa kiasi cha saa nne asubuhi.

Mombasa Mwezi wa Ramadhani inakuwa kama vile wakazi wake wameambizana kuwa wote wavae kanzu.

Kila unapotupa jicho watu wamevaa kanzu na mkononi wameshika tasbihi.
Ratiba yetu ilikuwa nyepesi.

Asubuhi tutakipitia kitabu na baada ya hapo tutapumzika na mchana nitafatana na Sal Davis kwenda Nyali Golf and Country Club.

Shariff Salim Abdallah ni mchezaji mkubwa wa golf.

Siku ya kwanza mimi kufika Nyali Club wakati tunaingia Shariff akasimamisha gari akazungumza na bwana mmoja kwa kiasi cha dakika mbili tatu.

Tulipopita akaniambia kuwa yule mtu jina lake ni Duncan Ndegwa.

Duncan Ndegwa nilikuwa nimemsoma sana kwani alikuwa mtu maarufu katika serikali ya Kenya toka enzi za Jomo Kenyatta.

Mimi nitarudi nyumbani na jioni nitarejea Golf Club kumchukua Shariff kwenda Makadara kufuturu.

Tulikuwa tunafuturu hoteli moja Shariff akiipenda sana.

Njiani tukitokea Nyali Beach kuingia Mwembe Tayari Mombasa imependeza kwa meza zilizopangwa zilizosheheni mapochopocho ya kila aina kuanzia kaimati, sambusa, kababu, katlesi viti vingi sana vya kutamanisha.

Meza zimezungukwa na wanunuzi.

Watu wakinunua kwa kufungulia mwadhini au kama nyongeza katika futari.

Iko siku Shariff Salim Abdallah Salim akaniambia kuwa atanipeleka kwa Shariff Muhdhar Khitami.

''Mohamed leo nakupeleka kwa Muhdhari najua utafurahi sana.''

Nyumba ya Shariff Muhdhar Khitami iko jirani sana na Fort Jesus, Stone Town.
Inasemekana barabara mkabala na nyumba ya kina Khitami alipita Vasco da Gama alipofika Mombasa.

Sharif Muhdhar alifurahi sana kunipokea na kuanzia mchana ule hadi maghrib alinipitisha misikiti miwili kusali Dhuhr na Asr na akaniomba nizungumze na Waislam historia ya East African Muslim Welfare Society (EAMWS).

Baada ya Isha Shariff Muhdhar alinipeleka kufanya kipindi Mubashara katika FM Station moja na aliniomba niendelee na mada ya historia ya EAMWS.

Ramadhani hii ilikuwa makhsusi sana kwangu kwani nilikuwa mgeni wa masharifu wawili na wote wakanifuturisha.

Picha: Shariff Salim Abdallah Salim na Mwandishi, Mtwapa, Mombasa 2009, Kushoto Shariff Khitami kulia Sheikh Mohamed Bakari na kati ya hawa wawili nyuma ni Shariff Muhdhari Khitami, Tanga, Kitabu chanDuncan Ndegwa, Kitabu cha Sal Davis.

1710941796139.png

1710941832507.png

1710941862358.png

1710941890578.png
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom