Taarifa ya CUF kuhusu matendo yanayoendelea ya uvunjwaji wa Haki za Binadamu nchini

  • Thread starter Mwanahabari Huru
  • Start date

Mwanahabari Huru

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Joined
Mar 9, 2015
Messages
13,491
Likes
27,349
Points
280
Age
48
Mwanahabari Huru

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Joined Mar 9, 2015
13,491 27,349 280
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu zangu waandishi wa Habari,
Awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na uzima wa afya na tukaweza kukutana hapa asubuhi hii ya leo. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu pia kwa kuijaalia nchi yetu kuendelea kubaki katika hali ya amani na utulivu licha ya matatizo mengi yanayotukabili.

Pili, nichukue fursa hii kukushukuruni nyinyi waandishi wa habari kwa kuitikia wito wetu na kuja kutusikiliza. Naamini mtatusikiliza kwa makini, hususan kutokana na uzito wa suala tulilowaitia na, kwa kuzingatia hali ya nchi yetu, mtawafikishia wananchi yale ambayo tutawaeleza.

Kwa aina ya kipekee, tuanawashukuru wananchi wan chi yetu kuendelea kubakia katika hali ya amani na utulivu, licha ya kuwepo kwa matendo mengi ya makusudi wanayotendewa ili yawapelekee kusababisha uvunjifu wa amani na kuondoa utulivu uliopo.

Tumewaita leo hii ili kuzungumzia kwa kina kuhusiana na matendo yanayoendelea ya uvunjwaji wa Haki za Binadamu na njama zinazoratibiwa na kutekelezwa na Mamlaka mbali mbali za serikali, ikiwemo vyombo vya Ulinzi na Usalama hasa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vikosi vya Zanzibar, kwa lengo la kuonea, kudhalilisha na kukandamiza raia wasio na hatia kwa madhumuni ya kudumaza na kuviza mfumo wa demokrasia nchini.

Naomba mnivumilie wakati nasoma maelezo haya niliyoyaandaa. Maelezo haya ni ya kina na bila ya shaka yatakusaidieni kufahamu historia na chanzo, wafadhili na waratibu, wasimamiaji na watekelezaji na athari za matukio haya kwa raia wasio na hatia na heshima ya taswira ya nchi yetu mbele ya taasisi mbali mbali za ulimwengu na jumuiya ya kimataifa.

1. KUANZISHWA KWA MFUMO WA VYAMA VINGI VYA SIASA
Mabadiliko ya mfumo wa siasa duniani yaliilazimisha Tanzania, kama zilivyokuwa nchi nyingi za kiafrika na zile za ulaya ya mashariki, kuachana na mfumo wa siasa ya chama kimoja na kuingia katika mfumo wa siasa za vyama vingi.

Mwaka 1992 serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliunda Tume kuratibu maoni ya watanzania juu ya mfumo wa siasa ulio muafaka kwa mazingira ya Tanzania. Baada ya Tume iliyoongozwa na Jaji Francis Nyalali, kukamilisha kazi yake iliwasilisha ripoti yake serikalini.

Baada ya kukamilika kwa hatua zote muhimu serikali ya Tanzania ililazimika kufuata mageuzi na kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, vyama vingi vya siasa viliruhusiwa, kwa tamko la Sheria namba 5 ya vyama vya siasa, tangu kupatikana kwa uhuru na muungano wa Tanzania.

Kutokana na kauli na matendo ya wakuu wa serikali na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) dhidi ya mfumo huu mpya wa siasa, iliashiria tokea mwanzo kuwa CCM na Seriali zake ilikubali mfumo huu shingo upande na kwa hivyo mwanzo wa safari ya kuelekea demokrasia ya kweli ulifanywa uwe mgumu na hivyo hata safari yenyewe imekuwa ya kusuasua hadi hivi leo.

Kwa kuwa haikuwa hiari ya watawala, ndio maana Tanzania haikuwa mstari wa mbele duniani kuanzisha na kushawishi nchi nyingine zifuate mfumo huu kama ilivyofanya katika jitihada zake za kiukombozi. Badala yake, kiasi kikubwa cha rasilimali fedha, rasilimali watu na wakati vilitumika kuandaa mipango na kutekeleza mikakati miovu ya kuzorotesha maendeleo ya demokrasia ya kweli nchini.

Mipango na mikakati hiyo miovu imepalilia kutokea kwa matukio ya ukiukwaji wa Haki za Binadamu na kutamalaki kwa dhulma, unyanyasaji na udhalilishaji wa raia wa umri mbali mbali na kuondoa murua wa watu walio na historia ya asili ya kuishi kwa umoja, upendo na maelewano makubwa.

2. MBINU ZA KUKANDAMIZA DEMOKRASIA

Pamoja na kukubali yenyewe, bila ya kushurutishwa, kufuata mfumo wa demokrasia ya siasa za vyama vingi, serikali iliyo chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliendesha mkakati wa kufanya ukatili na kunyanyasa wapinzani na kuwajengea taswira ya uadui kwa wananchi ili waonekane wamepotoka na kupotea, na kwamba hawana haki wala hawastahiki kupewa dhamana ya uongozi wa nchi.

Kilichodhihirika tangu kusajiliwa vyama vya upinzani ni ubabe wa chama kimoja unaofanywa na viongozi wa CCM na wafuasi wake dhidi ya vyama na wafuasi wa upinzani badala ya kuonesha ustaarabu wa demokrasia ya kweli. Hali hii imesababisha mageuzi ya kisiasa Tanzania kuwa katika mazingira machafu, yaliyoambatana na madhila, mateso na unyanyasaji kwa wananchi wanaoonekana kuwa na maoni ya upinzani.

Kwa kuwa unyanyasaji, udhalilishaji na ukandamizaji raia unahitaji kutumia Mamlaka za Serikali kukandamiza haki za binadamu ili kuwarejesha nyuma wananchi na kuwavunja moyo katika harakati zao za kuondosha utawala kandamizi kwa kufuata sheria za nchi na kwa kutumia njia za kistaarabu na za kidemokrasia, Mamlaka za serikali, ikiwemo vyombo vya Dola vimekuwa vikitumika kuratibu mipango hiyo miovu, kuitekeleza na kuikamilisha kwa kuwadhibiti wananchi hao.

MATUMIZI YA VYOMBO VYA DOLA DHIDI YA DEMOKRASIA
Vyombo vya Dola, hasa Jeshi la Polisi, limekuwa mstari wa mbele katika kuandaa mipango mbali mbali ya kudumaza demokrasia kwa kutekeleza mikakati ya kutisha raia kwa kuwakamata, kuwabambikizia kesi na kuwafungulia mashtaka, kama ilivyoshuhudiwa nykakati tafauti za uwepo wa vyama vingi vya siasa, ili kuzima sauti za wananchi hao na kushusha morali yao ya kudai mabadiliko kupitia njia za kidemokrasia.

Kwa mikakati hiyo miovu, kila wakati, Zanzibar imekuwa ikishuhudia kushehenezwa mamia ya askari wa Jeshi la Polisi na maelfu ya wanajeshi wa JWTZ walio tayari kufanya maangamizi ili kusimika utawala usio na ridhaa za wananchi.

Matokeo ya ushiriki wa vikosi vya Ulinzi na Usalama katika kuandaa na kutekeleza hujuma dhidi ya wananchi wasio na hatia kwa lengo la kurejesha nyuma maendeleo ya demokrasia ni matukio ya mauwaji ya Januari 26-27 2001 yaliyoratibiwa na kuchochewa na CCM ambapo silaha nzito za kivita kama vile RPGs, RRs na risasi za moto zilitumika kuzima sauti za wananchi walioamua kutumia haki yao ya kikatiba kuonesha hisia zao kwa kuandamana ili kudai Tume huru ya Uchaguzi na kuheshimwa kwa matakwa ya wananchi kupitia njia za kidemokrasia.

Matumizi haya ya nguvu za vyombo vya Dola yalipelekea wananchi 46, wasio na hatia, kuuawa, 658 kujeruhiwa vibaya, watoto wadogo kubaki mayatima, wanawake kuachwa vizuka na wengine 135 kupata na kubakia na ulemavu wa kudumu.

Zaidi ya yote, matukio haya yaliiondoshea hadhi Zanzibar kuwa ni nchi yenye ustaarabu uliotukuka yenye watu waungwana na rahimu wa nafsi na kuipeperusha heshima ya Tanzania, kwa Afrika na Dunia, kutokana na mchango wetu katika harakati za kusaidia kuondosha udhalimu na ukandamizaji wa kikoloni kwa nchi ambazo zilichelewa kujitawala.

Kuchochea dhulma dhidi ya raia wasio hatia na kunyamazisha sauti za wananchi waliokataa dhulma na ukiukwaji wa demokrasia kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015, hivi karibuni kumekuwa na hatua kadhaa za uendelezaji wa jinai dhidi ya utu wa wananchi unaofanywa na vyombo vya Ulinzi na Usalama vikiongozwa na Jeshi la Polisi.

Hivi tunavyozungumza Jeshi la Polisi limo katika mkakati maalum wa kudhalilisha na kunyanyasa raia wasio na hatia kwa kuwakamata, kuwabambikizia kesi na kuwashikilia katika vituo vya Polisi. Katika baadhi ya matukio ya kamata kamata wananchi wasio na hatia wamekuwa wakuzuiliwa katika vituo vya Polisi kwa muda mrefu.

Kwa mfano, katika Wilaya ya Mkoani, watu watatu ambao ni Said Ali Abdalla, Othman Yahya Said na Twahir Mohamed Mussa walikamatwa tarehe 12 Juni, 2016 na kushikiliwa katika vituo vya Polisi hadi tarehe 17 Juni, 2016. Baada ya kushikiliwa kwa muda wote huo, walifikishwa mahakamani ambapo wamerudishwa rumande hadi tarehe 12 Julai, 2016.

Mfano mwengine wa dhulma dhidi ya raia wasio na hatia kwa lengo la kuwanyanyasa na kuwadhalilisha kwa mateso ni ule wa Wilaya ya Chake Chake ambapo watu watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi tangu tarehe 28 Juni, 2016 na hadi leo hii haijulikani sababu ya kuzuiliwa kwao katika vituo hivyo vya Polisi wala hawajafikishwa mahkamani.

Aidha, watu wanne wanaokabiliwa na kesi namba 70/2016 wanaendelea kusoteshwa rumande hadi tarehe 12 Julai, 2016 kwa kosa la eti kukata mikarafuu. Mpango wa kuwakamata na kuwasweka wananchi hawa rumande kumesababishwa na Hakimu aliyepewa dhamana ya kusikiliza shauri hilo kukataa kutoa dhamana kwa watuhumiwa hao hata baada ya mwendesha mashitaka wa serikali kusema hana pingamizi dhidi ya dhamana ya watuhumiwa hao.

Kupigia chapuo uhalifu huu dhidi ya ubinadamu, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DDCI) Salum Msangi, aliendeleza utekelezaji wa mkakati wa kulihusisha Jeshi la Polisi katika kukandamiza haki za raia.

Ifahamike kuwa vitisho hivi vya Salum Msangi, ambaye kimsingi amepoteza heshima na uaminifu wa kulitumikia Jeshi la Polisi kutokana na kuweka mbali maadili ya Jeshi hilo na badala yake kufanya kazi kwa ushabiki, vimelenga kuwatisha wananchi wenye mawazo tafauti na misimamo ya CCM na wafuasi wa CUF walioko maeneo mbali mbali ya Zanzibar na wanaounga mkono jitihada za wananchi kupinga uonevu na udhalilishaji unaofanywa na Jeshi hilo dhidi ya raia wasio na hatia, na hivyo kuamua kuendesha mgomo dhidi ya kila anayeonekana na kuaminika kuwa chanzo cha dhulma hizo.

Aidha, Salum Msangi alikwenda mbali zaidi kwa kuwatisha wasaidizi mbali mbali wa kisheria, ikiwemo mawakili, na kuahidi kuwa atawachukulia hatua wale wote wanaoonekana kuwa mstari wa mbele kujihusisha na matukio hayo kama vile kufuatialia mienendo ya kesi zinazohusiana na matukio ya aina hiyo.

Kauli hii ya Salum Msingi imelenga kuwarejesha nyuma wadau wa Haki za Binadamu na mawakili wanaoonekana kupinga dhulma na uhuni unaofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya raia wasio na hatia na kuamua kutoa msaada wa kisheria kwa watuhumiwa hao.

Kitendo hichi cha Salum Msangi situ kinachochea na kuendeleza unyama wa Jeshi la Polisi dhidi ya wananchi wanyonge lakini pia kinakwenda kinyume na Katiba zote mbili, ile ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kinyume na Sheria za nchi kama kama inavyoelezwa katika Sheria za mwenendo wa makosa ya jinai S. 41 ya CPA No. 7/2004. Kuwazuia mawakili na wadau wengine wa Sheria kutekeleza wajibu wao wa kikatiba na kukandamiza Sheria maana yake ni kuidhalilisha fani hiyo na kuwakosesha raia hai ya kupata utetezi kwenye kesi zinazowakabili.

Kauli hii ya Salum Msangi, inadhihirisha usahihi wa kauli na matamko mbali mbali ya The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) kuwa wengi wa watendaji waliopewa dhamana katika Jeshi la Polisi wamekuwa wakiburuzwa na ushawishi binafsi na utashi wao wa kisiasa na kwamba wako tayari kufanya jambo lolote kuhakikisha na kufanikisha maslahi yao kwa kukandamiza raia kwa gharama yoyote kama inavyobainika katika utendaji huu wa Salum Msangi.

KUSAKAMA NA KUWAPAKA MATOPE WAPINZANI
Mkakati wa kuviza demokrasia umekuwa pia ukihusisha mipango ya kuchafua mazingira ya ushindani ulio huru na wa haki kwa kuwasakama na kuwapaka matope wapinzani. Baadhi ya shutuma nzito ambazo zimekuwa zikielekezwa kwa CUF ni pamoja na:
• CUF ni chama cha Ukabila
• CUF ni chama cha Udini
• CUF inataka kuvunja Muungano
• CUF inataka kuleta vita vya wenyewe kwa wenyewe
• CUF ni chama cha vibaraka wa mataifa ya nje
• CUF inataka kurejesha utawala wa kisultani Zanzibar
• CUF ni chama cha Wapemba
• CUF ni chama cha magaidi, n.k.

Kutokana na kutekelezwa kwa mpango huu wa kuwasakama na kuwapaka matope wafuasi na viongozi wa upinzani, wafuasi wa vyama vya upinzani hasa CUF, wamejikuta katika mazingira magumu. Mifano ifuatayo inadhihirisha matendo ya kuwasakama wapinzani kwa lengo la kuwakomoa na kuwavunja moyo ili kurahisisha na kufanikisha mpango wa CCM kuendelea kujibakisha madarakani:

• Kuchezewa kwa demokrasia na kusalitiwa kwa maamuzi ya wananchi yaliyofanywa kidemokrasia, zaidi ya mara tano katika historia ya Chaguzi za vyama vingi nchini Tanzania kwa lengo la kulazimisha kwa nguvu kubwa kuipa ushindi CCM, hata kwa maeneo iliyokataliwa wazi wazi, kama ilivyobainika katika Uchaguzi Mkuu wa 25 Oktoba, 2015.

• Kudhulumiwa kwa kunyimwa haki za msingi za kikatiba kwa baadhi ya raia kutokana na kuwa na msimamo wa kukubaliana na mfumo wa kihuni katika uendeshaji wa nchi. Kwa mfano, serikali katili na isiyojali haki za raia inayoongozwa na CCM iliwafukuza wanafunzi zaidi ya 1500 wa kidato cha nne baada ya kugoma kuonesha kuwaunga mkono wenzao waliofukuzwa kutokana na kutokubaliana na ukiukwaji wa demokrasia nchini. CUF iliwasaidia wanafunzi hawa kufanya mitihani hiyo Tanzania Bara kwani serikali ya Zanzibar iliwazuia kabisa hata kuchukuwa fomu za Private Candidates.

• Kushamirishwa kwa manyanyaso dhidi ya wananchi waliohisiwa kuwa na imani na itikadi ya siasa za upinzani. Kwa mfano, wafanyakazi wengi walifukuzwa kazi kutokana na taarifa zao za kutiliwa mashaka kuunga mkono upinzani kuwasilishwa kwa viongozi wa juu wa serikali. Wananchi wasiokuwa na hatia wamekuwa wakikamatwa, kuswekwa rumande na kubambikiziwa kesi ili kuwatisha na kuwaogopesha kwa lengo la kuzima sauti za wananchi wanaolalamika kunyanyaswa na kudhalilishwa na vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Zanzibar na vile vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

• Kutengwa na kubaguliwa kwa baadhi ya wananchi ambapo hata leseni za biashara zilitolewa kwa mujibu wa itikadi na misimamo ya kisiasa. Maeneo ya biashara yalikuwa meupe kwani ukionekana au kujulikana kama ni CUF au kuunga mkono mawazo ya upinzani kuhusiana na masuala mbali mbali ya nchi ulinyimwa leseni na wachache waliofanikiwa kupata leseni hizo wakinyang’anywa na kuporwa vitu vyao na mali za biashara baada ya kugunduliwa itikadi zao za kisiasa.

• Kusukwa na kutekelezwa kwa mipango ya kugombanisha wananchi kwa lengo la kupata kisingizio cha kuwakamata baadhi ya watu na kuwaweka kizuizini ili kuwafungulia mashitaka

• Kuharibiwa kwa mali za wafuasi wa upinzani kwa kutolewa amri za kubomolewa makaazi ya raia hao maeneo ya Mtoni na kuwataka wamiliki wake kurudi kwao. Katika matukio mengine, nyumba za wafuasi wa CUF zilizotumiwa kwa makaazi ya wananchi ziliteketezwa kwa kuchomwa moto na kuharibiwa vibaya huku mamlaka zenye kukabiliana na matukio ya aina hii zilkikataakwa makusudi kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kwa kuwa kumekosekana dhamira njema miongoni mwa viongozi wa CCM na wameonesha dhahiri kuwatayari kufanya lolote ili kuendelea kushika hatamu za Dola kwa kutumia mbinu za kidikteta, na kuwaamrisha mamluki wao katika Mamlaka za nchi, hasa vyombo vya Ulinzi na Usalama, kutekeleza mipango yao miovu iliyopelekea Zanzibar kuwa katika mtanziko mkubwa na kuifanya irudi katika historia ya unyanyaswaji na udhalilishwaji wa raia wasio na hatia, The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi):

1. Inalaani matendo ya hujuma dhidi ya mali binafsi za wananchi yanayofanywa kwa lengo la kuvipa sababu vyombo vya Ulinzi na Usalama kuwakamata wafuasi na viongozi wa upinzani hasa wafuasi wa Chama Cha Wananchi CUF. Pia CUF inalaani vikali kauli za vitisho na lugha za kibabe zinazotolewa na Jeshi la Polisi Zanzibar, kama ile iliyotolewa tarehe 28 Juni, 2016 na DDCI Salum Msangi kisiwani Pemba kwa lengo la kuwanyamazisha wananchi ili kukisambaratisha Chama Cha Wananchi CUF.

2. CUF inaunga mkono tamko la Zanzibar Law Society (ZLS) lililotolewa kulaani tamko la DDCI Salum Msangi na kukataa aina zote za ukiukwaji wa Sheria na taratibu za kidemokrasia zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi. Aidha CUF inaziomba Jumuiya na Taasisi zote kuendelea kupaza sauti na kuungana na wananchi kupinga aina zote za ukandamizaji na matendo yaliyopitwa na wakati unaofanywa na watendaji waliopewa mamlaka ya kusimamia vyombo vya Dola kama inavyoendelea kutokea katika maeneo mbali mbali ya nchi ambapo wananchi wanyonge wanadhalilishwa na kunyanyaswa kutokana na watendaji hao kuweka mbali maadili ya taasisi wanazoziongoza na kujitwika ushabiki wa kikereketwa kwa lengo la kulinda maslahi yao binafsi.

3. CUF inamtaka IGP, Ernest Mangu, na Mamlaka zote zinazohusika ndani ya Jeshi la Polisi kuchukua hatua za kimaadili dhidi ya DDCI Salum Msangi na wale wote waliopewa dhamana za juu kulinda raia na mali zao na wakashindwa kufanya hivyo kama inavyoendelea kutokea katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar kama vile: Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mkoa wa Kusini Pemba na Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo ilifikia wananchi watano wasiokuwa na hatia kufyatuliwa na kujeruhiwa kwa risasi za moto sehemu tafauti za miili yao. Kuendelea kunyamazia unyama wa aina hii si tu kunachochea kuendelea kwa matukio haya, lakini pia yanatoa mwanya kwa watawala waovu kuendelea kuwatumia watendaji wa aina hii kuratibu na kutekeleza mipango itakayokuwa na athari mbaya kwa nchi yetu.

4. Kinawataka wananchi wote wasio kubaliana na matendo ya dhulma na wanaounga mkono jitihada za kidemokrasia kukabiliana na aina zote za matendo yasiyokuwa ya kistaarabu na uonevu dhidi ya raia wanyonge, walioamua kutumia njia za kisheria kuweka madarakani viongozi wanaowataka, kutorudi nyuma na kutotishika na kauli za ovyo ovyo, zisizokuwa na mantiki na zinazotolewa kishabiki na watendaji wa Jeshi la Polisi Zanzibar, kama ile iliyotolewa hivi karibuni na Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya jinai Salum Msangi. CUF inawataka wananchi wote kuendelea kutekeleza maazimio na maamuzi ya Chama ya kuonesha msimamo wao wa kutoitambua serikali haramu iliyojiweka madarakani kwa mtutu wa bunduki na kutoipa mashirikiano ya aina yoyote.

5. Kinatamka wazi kuwa kitaendelea kuyasimamia maazimio halai ya Vikao vya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa yaliyotolewa 25 Oktoba, 2015 na lile lililofanyika 3 Aprili, 2016 na kutekeleza mkakati wa Chama na kamwe hakitabadilisha msimamo uliotokana na maamuzi halali ya vikao vyake ya kutoitambua serikali haramu iliyojiweka madarakani kwa mtutu wa bunduki. Aidha, CUF itaendelea kuunga mkono jitihada zote za wananchi, kwa kuzingatia sheria za nchi na utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa katiba, kuonesha hisia zao dhidi ya matendo ya udhalimu wanayofanyiwa kwa lengo la kuzima sauti zao za kudai demokrasia ya kweli na ustaarabu wa kuendesha nchi kwa mujibu wa sheria tulizojiwekea.

6. Kinawataka wananchi wote kuendelea na msimamo madhubuti wa kukiunga mkono Chama na kuendelea kushikamana kwa pamoja na kutoa mashirikiano kwa wale wote wanaopatwa na matatizo yanayoandaliwa na kutekelezwa kwa makusudi ili kuwarudisha nyuma na kuwavunja moyo.

7. Chama Cha Wananchi CUF kinawataka wananchama wake, wananchi na wapenda amani kuendelea kuvifichua vitendo vyote vya kinyama vinavyofanywa na vyombo vya Dola dhidi ya raia pamoja na kuorodhesha matukio yote na kuweka kila aina ya ushahidi, ikiwa ni pamoja na kuwatambua watekelezaji wa vitendo hivyo vya unyama dhidi ya raia, na kuwasilisha taarifa hizo katika Ofisi za Makao Makuu ya CUF kwa lengo la kuongeza taarifa hizo katika ushahidi uliokusanywa kwa ajili ya Mahkama ya Uhalifu dhidi ya Ubinadamu (ICC) iliyopo The Hague kwa hatua za kimataifa.

HAKI SAWA KWA WOTE

SALIM BIMANI
MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI NA MAWASILIANO NA UMMA
 
M

Mapya Yaja

JF-Expert Member
Joined
Feb 8, 2013
Messages
562
Likes
343
Points
80
M

Mapya Yaja

JF-Expert Member
Joined Feb 8, 2013
562 343 80
Sidhani matamko kama yanaishtua hii serikali ya ccm. Yametolewa mengi hadi wanaona kama ni ngonjera tu zinaimbwa.
 
Erythrocyte

Erythrocyte

JF-Expert Member
Joined
Nov 6, 2012
Messages
54,111
Likes
44,556
Points
280
Erythrocyte

Erythrocyte

JF-Expert Member
Joined Nov 6, 2012
54,111 44,556 280
Mungu ibariki CUF .
 
MOTOCHINI

MOTOCHINI

JF-Expert Member
Joined
Jan 20, 2014
Messages
24,483
Likes
13,108
Points
280
MOTOCHINI

MOTOCHINI

JF-Expert Member
Joined Jan 20, 2014
24,483 13,108 280
Hehehe
Mtaishia Taarifa awamu hii

HAPA TULIA
KULE MAGUFULI!!!
 
kipara kipya

kipara kipya

JF-Expert Member
Joined
May 2, 2016
Messages
5,395
Likes
5,401
Points
280
kipara kipya

kipara kipya

JF-Expert Member
Joined May 2, 2016
5,395 5,401 280
Tamko kama hili lilitakiwa litoke ile siku alipozuiwa maiti kuswaliwa na yule waziri shamba lake lilipofyekwa!
 

Forum statistics

Threads 1,235,782
Members 474,742
Posts 29,235,409