Taabini: Hashil Seif, mpigania haki asiyeyumba (Januari 12, 1938 – Oktoba 27, 2023)

Hamid Rubawa

Member
May 23, 2018
72
202
Gazeti La Dunia

Taabini: Hashil Seif, mpigania haki asiyeyumba (Januari 12, 1938 – Oktoba 27, 2023)
Ahmed Rajab
Ahmed Rajab

Na Ahmed Rajab

UJUMBE wa simu ulipoingia asubuhi ya Ijumaa iliyopita, ulikuwa na maneno machache: “Ndugu yetu ameshatangulia mbele ya Haq leo saa moja na dakika arobaini na tano kwa saa za hapa. Tunangoja daktari aje kumtizama mara ya mwisho.”

Aliyeleta ujumbe alikuwa Hamed Hilal, mmoja wa makomredi wa chama cha zamani cha Umma Party cha Zanzibar, kilichokuwa kikifuata itikadi ya Umarx. Huyo “ndugu” yetu aliyetutoka alikuwa komredi mwenzetu, Hashil Seif Hashil, aliyefariki saa hizo jijini Copenhagen, Denmark.

Ujumbe wa Hamed ulitanguliwa na aya ya Qur’ani isemayo, “Inna liLlahi wa inna ilayhi rajiun” (Hakika sisi ni wa Mungu na hakika Kwake tunarudi). Nilipoisoma tu aya hiyo hata kabla ya kuusoma ujumbe wenyewe nilikwishajua kwamba

Hashil, komredi wetu, kipenzi chetu na cha wengi wengine wasiokuwa wafuasi wa Umma Party, ametutoka.

Siku tatu kabla ya mauti kumkuta Hashil, komredi wetu mwengine, Aboud Abdallah, anayeishi Copenhagen, alitupasha habari kwamba hali ya mwenzetu ilibadilika ghafla na alikuwa mahtuti hospitalini. Moyo ulinipwaya na machozi yakanilenga huku nikiwaza kwamba mwenzetu ambaye kwa miaka kadhaa akiyadhihaki mauti sasa alikuwa anakaribia kuyaonja, kama kila mmoja wetu atavyoyaonja.

Siku ya pili yake Aboud alitujuza tena kuwa hali ilizidi kuwa mbaya. Taarifa hiyo ya pili ndiyo iliyomtoa Hamed kutoka maskani yake ya huko Maskati, Omani, akarudi Copenhagen alikokuwa akiishi na Hashil kwa miaka 44.

Baada ya kuwasili Copenhagen, Hamed alifululiza moja kwa moja hospitalini. Alimkuta Hashil dhaifu sana lakini akiwa na kauli yake na walizungumza.

Hamed alikuwa komredi wa mwisho kuonana na Hashil. Mwaka 1996, yeye na mimi tulikuwa wa mwisho kuzungumza na kufanyiana mizaha na aliyekuwa kiongozi wetu wa Umma Party, Abdulrahman Mohamed Babu, katika hospitali ya Chest Hospital, London, siku chache kabla hajafariki mnano Agosti, 5.

Hamed alipotujuza kwamba Hashil ametutoka nilikuwa kama niliyepigwa na mughuma. Kwa muda sikuweza kufanya kitu. Nikiyakumbuka masikhara ya Hashil na kauli yake aliyokuwa heshi kuikariri, kama wimbo uliokwama kwenye sahani ya santuri na uliokuwa ukijirejearejea, kwamba kitendawili cha mauti ni kuwa hakuna aliyefariki akarudi na kueleza kakutana na nani na alifanya nini upande wa pili.

Hapa duniani, katika umri wake wa miaka 85, Hashil aliyapitia na kuyaonja mengi. Aliwahi kuwa askari wa forodha zama za ukoloni, muuguzi wa wagonjwa hospitali, baharia — wa kiraia na wa kijeshi — mpigania wanyonge, mwanajeshi, mwanaharakati wa haki za binadamu na wa mengi mengine yaliyokuwa ya kimaendeleo, mwandishi wa vitabu, mshairi, mwandishi wa riwaya na mfungwa wa kisiasa.

Kwa miaka sita, yeye na Hamed na makomredi wengine, akiwemo kiongozi wetu Babu, walisota katika jela za Tanzania kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa kwanza wa Rais wa Tanzania, Sheikh Abeid Amani Karume. Walipoachiwa huru na Rais Nyerere kufuatia shinikizo na kampeni kubwa ya kimataifa, Hashil na Hamed walipata hifadhi ya kisiasa Denmark.

Hashil akipenda kuyatafakari maisha, ulimwengu na walimwengu — hayo yanadhihirika zaidi katika tungo zake za kishairi kama mashairi yaliyo kwenye diwani zake “Sauti ya Muhajirina” na “Kurunzi”. Tafakuri zake zimo pia katika riwaya alizozitunga, zikiwa pamoja na “Mke mmoja, Waume wawili” na “Kiroboto na Mzimu wa Majini na Marmar” au kile kitabu alichokiandika kwa Kiingereza cha tafakuri za kumbukumbu zake za gerezani kiitwacho “Reflections from My Prison Notebook.”

Kitabu kingine cha Kiingereza alichoandika kwa kushirikiana na mwanasayansi Dakta Ahmed Faris wa Chuo Kikuu cha Uppsala huko Sweden kinaitwa “Living under the shadow of terror: Zanzibar caught off guard” kinachozungumzia mateso ya utawala wa Zanzibar. Tafakuri zake zinaonekana pia katika kitabu chake chenye anuwani ya “Uchu na utamu wa Kutawala kwa Mabavu.” Na bila ya shaka, maoni yake juu ya maisha na siasa ameyamwaga, hapa na pale, katika kitabu chake cha mwisho kinachohusu historia na kiitwacho “Mimi, Umma Party na Mapinduzi ya Zanzibar.” Ni fahari kubwa kwangu kwamba niliupitia mswada wa kitabu hicho na kuuhariri.

Nilijifunza mengi ya ziada kutoka kwa Hashil kwa kuuhariri mswada wake. Kabla ya hapo nikiyajua mengi kuhusu maisha yake kwa sababu tuliingiliana kwa miaka mingi sana — nikishukia kwake nikenda Copenhagen na akifikia kwangu akija London. Tumewahi kuwa pamoja Zanzibar, Dar es Salaam, Dubai, na katika miji hiyo miwili ya Ulaya. Zaidi ya hayo kwa miaka tulikuwa ama tukiandikiana au kupigiana simu takriban kila siku. Fikra zake nikizijua fika. Nathubutu kusema kwamba Hashil alikuwa mwanafalsafa wa mapambano n awa maisha.

Miongoni mwa wanafalsafa aliokuwa akiwahusudu yeye ni mwanafalsafa wa kale wa China, Laozi (au Lao Tzu, kama anavyoitwa na wengine) na aliye maarufu kwa kutunga kitabu kiitwacho “Tao Te Ching,” ingawa wanahistoria wanatia shaka iwapo yeye ndiye mtunzi hasa wa kitabu hicho. Hata hivyo, Hashil aliziramba fikra za kifalsafa za Lao Tzu kama alivyoziramba zile za Mao Zedong, aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti cha China na ambazo tukizifuata kama dira ya muelekeo wetu wa kiitikadi — kutoka nadharia za Karl Marx na Vladimir Lenin hadi fikra za Mao Zedong.

Juu ya yote hayo, Hashil atakumbukwa zaidi na historia, ingawa si na watawala wa sasa wa Zanzibar, kwa namna alivyoshiriki katika Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari, 12, 1964. Yeye ndiye aliyeongoza kikundi cha wapinduzi wasiopungua 15 waliokiteka kituo cha mawasiliano cha Cable & Wireless. Kituo hicho kilikuwa pekee cha aina yake katika Zanzibar ya miaka hiyo na kilikuwa kwenye jengo ambalo sasa ni hoteli ya Serena, hapo Kelele Square. Miongoni mwa vijana wengine aliokuwa nao walikuwa komredi Kadiria Mnyeji, Adam Mwakanjuki na kijana mmoja aliyekuwa akiitwa Fuko.

Kabla ya hapo, alishirikiana na makomredi wenzake, kina Amour Dugheish na Ahmed Maulidi Haji pamoja na Musa Maisara, kutoka chama cha Afro-Shirazi (ASP), kujaribu kuiteka steshini ya polisi ya Malindi, iliyokuwa ngome ya mwisho na madhubuti ya serikali iliyopinduliwa ya Zanzibar Nationalist Party (ZNP) au Hizbu. Lakini walishindwa ingawa baadaye askari wa ZNP walitoroka wakakimbilia gatini. Baadhi ya hao askari na raia waliokuwa wafuasi wa ZNP walipanda meli wakaihama Zanzibar pamoja na sultani, Seyyid Jamshid bin Abdallah al Said.

Hashil alikuwa mshabiki mkubwa wa mapinduzi, akiamini kwa dhati kwamba yataleta usawa na mageuzi chana katika jamii. Haikuchukua muda matendo ya wengi wa wapinduzi yalianza kumkirihisha na mapinduzi yenyewe yakamtumbukia nyongo. Hashil ameyaeleza hayo kwa ufasaha mkubwa katika kitabu chake cha mwisho.

Ndani ya kurasa za kitabu hicho, ameeleza jinsi yeye na makomredi wenzake walivyoshiriki katika mapinduzi na kwa nini walishiriki. Muhimu ni kwamba ameonesha makosa yaliyofanywa na makomredi pamoja na kuutathmini mchango wao katika tukio hilo lililoibadili taswira ya Zanzibar kwa makovu na majaraha yake.

Hashil aliweza kushiriki katika mapinduzi kwa sababu, pamoja na Hamed na mkaazi mwengine wa Copenhagen Abdulrahim Mahmoud (Handsome), alikuwa miongoni mwa vijana wa Umma Party waliopatiwa mafunzo ya kijeshi, Havana, Cuba. Huko walifunzwa mbinu za kupindua serikali. Na ndio maana jukumu lake la kwanza alilopewa siku ya Mapinduzi lilikuwa kuwafundisha wapinduzi namna ya kutumia silaha. Kazi hiyo aliifanya yeye na makomredi wenzake, Dugheish pamoja na Abdalla Juma (Bulushi).

Hashil alikuwa mtu wa mikasa. Hata uzawa wake ulikuwa wa mikasa — haukuwa wa kawaida. Alizaliwa baharini, ndani ya ngarawa iliyokuwa inaelekea Mtambwe huko Pemba, mnamo Januari 12, 1938. Kwa hivyo, kama alivyoandika kwenye kitabu chake cha mwisho kilio chake cha mwanzo kilisikika ndani ya ngarawa iliyokuwa ikiyumbayumba juu ya mawimbi ya bahari ya Pemba.

Babake, Seif bin Hashil, alikuwa “Mmanga ndevu” aliyezaliwa Ibra, mji wa pili kwa ukubwa katika jimbo la Ash Sharqiyah, huko Omani. Nasaba ya bwana huyo ilikuwa ya ukoo wa al Busaidi na alihamia Unguja alikokuwa akiuza duka Mwembe Kiwete, Mkokotoni, Mkoa wa Kaskazini A, Unguja.

Mamake akiitwa Bibi Mwanadawa binti Jadi Khamis, mzawa wa Kwale, Pemba. Alitokana na kabila la Zarai. Bibi Mwanadawa akifanya kazi za nyumbani na mara nyingine akilima mazao kama viazi na mihogo.

Hashil alikulia Mwembe Kiwete na ndo maana mwenyewe akitafahari kujiita “mshamba wa Mkokotoni.” Alipotimia umri wa kwenda skuli alipelekwa Skuli ya Mkwajuni iliyokuwa karibu na Mwembe Kiwete. Alipofika miaka 13 babake alimrejesha Pemba kwa ami yake aliyemsomesha Qur’ani huko Konde. Alipokuwa barobaro wa miaka 16 alirejeshwa Mwembe Kiwete, Unguja, na aliendelea kusoma Mkwajuni.

Alipomaliza masomo ya msingi, Hashil alifanikiwa kuingia skuli ya Seyyid Khalifa Technical School, iliyokuwako Beit-el-Ras, nje kidogo ya Mjini, Unguja. Huko ndiko alikozivaa siasa, ingawa mwenyewe akiamini kwamba alizianza siasa za kuwapigania wanyonge tangu utotoni mwake. Alikuwa hapendi kuonewa wala kuwaona wengine wakionewa. Mara chungu nzima akiingilia ugomvi usiomkhusu, usiokuwa wake, kwa nia ya kuwasaidia walioonewa.

Msimamo wake wa siasa ulikuwa ni muendelezo wa utetezi wake wa watoto waliokuwa wakionewa, halafu kuupiga vita ukoloni alipokiunga mkono chama cha ZNP, baadaye kupigania haki za wafanyakazi na hatimaye kuzikumbatia siasa za Umma Party. Siasa hizo alizisikia mwanzo kwenye baraza yake ya Mtendeni, Unguja, nyumbani kwa kina komredi Ali Khatib Chwaya. Hapo ndipo alipokutana na komredi Ali Mshangama, ambaye ndiye aliyependekeza kwamba Hashil aingizwe kwenye kundi lao la vijana waliokuwa wanapelekwa Havana, kwa mafunzo ya kijeshi.

Katika nyakati tofauti huko Havana, Hashil alikutana, ingawa kwa muda mchache, na Che Guevara na Fidel Castro. Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hashil alipelekwa Indonesia kwa mafunzo ya uanajeshi wa majini. Aliitumikia Tanzania akiwa katika jeshi la wanamaji. Ughaibuni alirudia kuwa baharia wa kiraia lakini kazi ya mwisho aliyoifanya na aliyokuwa akijivunia nayo ilikuwa katika Kituo cha Haki za Binadamu cha Denmark.

Nina mengi ya komred Hashil na hata nikipewa gazeti zima kuyaandika sitoyamaliza. Naitoshe nikisema kuwa Hashil alikuwa mshupavu, mpigania haki asiyeteteleka na kwamba Zanzibar ilimjaa moyoni. Kila mara akitushajiisha kuandika barua za wazi za kuonesha madhila yaliyokuwa yakifanyika huko. Tukisitasita akisema: “Kama mnaogopa wekeni jina langu.”

Hashil hakuwa akipigania Zanzibar tu. Barua zake zikichapishwa kwenye magazeti ya Tanzania na ya nchi za nje ya Afrika akiwasemea waliokuwa wakidhulumiwa nchi mbali mbali duniani.

Nisingependa kumaliza taabini hii ya Hashil bila ya kukitaja kisa kimoja. Kuna wakati ambapo Tanzania ilitangaza kwamba inampeleka Bwana mmoja aitwaye Juma Ameir awe mwanabalozi wake katika ubalozi wa Sweden. Habari hizo niliandika kwenye jarida la “Africa Analysis” nilokuwa nikilihariri London. Hashil baada ya kuisoa taarifa hiyo aliwapigia simu waandishi habari wa Denmark na Sweden na kuwaeleza kwamba bwana huyo alikuwa mmoja wa watu waliomtesa yeye na wengine walipokuwa wamefungwa jela Tanzania. Hashil alihojiwa na televisheni ya Sweden na habari zake za mateso katika jela za Tanzania ya siku hizo zikatangazwa. Serikali ya Sweden hakuwa na hila ila kumkataa huyo bwana asipelekwe Stockholm kuwa mmoja wa wawakilishi wa Tanzania.

Huyo ndiye aliyekuwa Hashil. Hakuwa na upuuzi katika kupigania haki.

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com/@ahmedrajab X

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.

Gazeti la Dunia ni Jukwaa Huru la Fikra kwa wasomaji wa lugha ya Kiswahili lenye lengo la kuchapa makala za kichambuzi kuhusu masuala mbalimbali muhimu kwa Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla. Waandishi wa kwenye jukwaa hili ni maveterani na wabobezi kwenye maeneo watakayokuwa wanaandikia. Kama unajua unachokiandika, hili ni jukwaa lako.

2022 Gazeti La Dunia | Website by Kinara TechnologiesView attachment 2800842
IMG_20231027_131349_976.jpg
 
Sasa yuko mbele ya haki hakuna janja.
Mlioyafanya kuuwa maelfu ya watu wasio na hatia sasa ndio kesi inaanza na Mola ndie jaji.
 
mapinduzi yenyewe aliwasaidia John Okelo, lakini hadi leo mnachukua ninyi sifa. mwandikeni kwenye vitabu hata ukurasa mmoja tu basi.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom