Suala la posho za wabunge liishe

Sumasuma

JF-Expert Member
Jun 23, 2011
342
110
JANA katika gazeti hili lilichapisha habari iliyokuwa ikimkariri Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai akieleza kuwa nyongeza ya posho za vikao vya wabunge kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 zimefutwa.Kauli hiyo imetolewa na Ndugai huku kukiwapo taarifa za kutatanisha kuhusu posho hizo zilizotolewa na Ikulu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Spika wa Bunge, Anne Makinda na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah.

Alianza Dk Kashililah mwishoni mwa mwaka jana akikanusha kuwa posho za wabunge hazijapanda baada ya gazeti la hili kuchapisha habari iliyokuwa ikieleza kuhusu kupanda huko.

Hata hivyo, baada ya siku chache, Spika wa Bunge alipinga kauli ya katibu wake na kusisitiza kuwa posho za wabunge zilikuwa zimepanda.Alisema sababu kubwa ya kupandisha posho za wabunge hao ni ili kuwawezesha kumudu kupanda kwa gharama za maisha katika Mji wa Dodoma ambako ndiko Bunge lililopo.

Kauli hizo za kupingana baina ya Spika na Katibu wake ziliwachanganya wananchi. Mbali ya kuwashangaza, pia ziliibua hisia mbalimbali katika jamii.

Baadhi ya wananchi walishangaa kusikia wabunge wakipandishiwa posho hizo, wakati wa kipato cha chini wakiishi kwa mlo mmoja na hospitali nyingi za Serikali zikiwa hazina uwezo wa kutoa huduma inavyostahili.
Baadhi ya viongozi walijitokeza hadharani kupinga ongezeko hilo akiwamo Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye ambaye alionya kuwa nyongeza hizo za posho zisizofuata utaratibu wa watumishi wa umma ni hatari na ni utawala mbaya kwa nchi.

Alisema suala la posho ni jambo ambalo sasa limekuwa tatizo kwa Serikali na kuwa imefika wakati ofisi za Serikali zimehamia hotelini lengo likiwa ni watumishi wa umma kutafuta mwanya wa kulipana posho.

Lakini kama hiyo haitoshi, Waziri Mkuu Pinda pamoja na Spika waliwaambia wabunge mjini Dodoma hivi karibuni kuwa ongezeko la posho za wabunge lina baraka za Rais Jakaya Kikwete.

Lakini siku moja baada ya kutolewa kauli hiyo, Ikulu ilikanusha taarifa hiyo ikieleza kuwa Rais hajabariki ongezeko la posho hizo, isipokuwa aliwataka wabunge kutumia hekima na busara katika kulitafakari suala hili.

Hata hivyo, juzi Ndugai alisema kibali kilichopo ni cha malipo ya posho za zamani ambazo hata yeye mpaka sasa analipwa huku akisisitiza, hajawahi kulipwa hata senti moja ya posho hizo mpya zilizoibua mjadala mpana nchini.

Tunatumia nafasi hii tena kuungana na watu wote wanaopinga kwa nguvu zote ongezeko hilo la posho za wabunge, tukiamini kuwa jambo hilo halina tija kwa nchi hivi sasa.

Lakini pamoja na kusema hayo, tunadhani kuwa suala hili la ongezeko la posho za wabunge bado limegubikwa giza na halijawekwa wazi likaeleweka.Yapo maswali mengi ya kujiuliza ambayo Serikali na Bunge vinapaswa kuyatolewa ufafanuzi. Je, posho zimefutwa au zimesitishwa? Kama zimefutwa, Spika aliwahi kusema kuwa posho mpya zilishaanza kulipwa, waliochukua watarejesha?

Tunadhani maswali haya na mengine yanayohusiana na posho hizi yanapaswa kuwekwa wazi ili kuondoa hisia kuwa kundi fulani la jamii linaneemeka zaidi ya mengine wakati hali ngumu ya maisha inawakabili wote na haichagui.

Ni vyema sasa pande zote zinazohusika yaani mihimili hii miwili ya Serikali na Bunge kuliweka wazi hili ili wananchi wajue hatima yake.
 
Mh. Raisi JK alishalitoleaga maamuzi suala hili na limeshaishaga muda mrefu. Labda kuwe na longolongo nyingine katika kauli zao.


MIZAMBWA
INANIUMA SANA!!!
 
Back
Top Bottom