Story ya wapenzi maarufu, Bonnie and Clyde

geraldincredible

JF-Expert Member
Mar 26, 2017
2,036
7,195
NANI MWENYE MAPENZI KAMA YA BONNIE NA CLYDE?

Kuna msemo wa Kilatini unasema Hostis Publicus, ukiwa na maana ya adui wa watu (enemy of the people).

Aprili 1930, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uhalifu ya Chicago, Marekani, Frank Loesch, aliutumia msemo huo wa Kilatini, kumtangaza haramia Alphonse Capone ‘Al Capone’ kuwa adui wa watu wa Chicago.
Al Capone au Scarface kwa jina lingine, alikuwa mtu hatari mtu kwa wakati wake, alimiliki kundi la uhalifu wa kupangwa (organized crime), lililoitwa Chicago Outfit. Aliihenyesha dola, mpaka Loesch akaamua kumtangaza kuwa adui wa watu.

Baada ya tangazo la Loesch kuhusu Al Capone, maeneo mbalimbali ya Marekani yaliitika, majina ya wahalifu yakitajwa kwenye mamlaka za majiji. Umma wa Wamarekani walijulishwa kuhusu maharamia mbalimbali.

Matamko hayo kwa wingi wao kuwalenga maharamia mbalimbali waliokuwa wakiitikisa Marekani kwa wakati huo, yalisababisha kipindi hicho kiitwe Zama za Adui wa Umma (Public Enemy Era) kwa Marekani.

Public Enemy Era ni kipindi cha kati ya mwaka 1930 mpaka 1935. Wahalifu wakubwa zaidi waliosababisha miaka hiyo iitwe Zama za Adui wa Umma Marekani ni Al Capone, John Dillinger (siyo DJ JD), Baby Face Nelson, vilevile Bonnie na Clyde.
Maharamia wengine ni Pretty Boy Floyd, Machine Gun Kelly, Ma Barker na Alvin Karpis. Kwa pamoja, majina hayo yalitamba sana, wakitafutwa na Serikali, wakiihenyesha dola. Watu hao walimiliki makundi makubwa na hatari.

Public Enemy ni nyakati zilizoibuliwa kipindi cha mdororo mkubwa wa kiuchumi (Great Depression) kati ya mwaka 1929 mpaka 1939. Mdororo huo ulisababishwa na anguko la uchumi wa viwanda na kuporomoka kwa soko la hisa kwenye nchi za Magharibi.

Hivyo, Marekani ikiwa inateswa na hali mbaya ya kiuchumi, vilevile ilikuwa ikisumbuliwa na uhalifu wa mipango uliokuwa ukitekelezwa na makundi hayo hatari. Mashushushu wa FBI walipelekwa puta na maharamia hao ambao walijijengea umaarufu mkubwa wa kuogopwa.
Maneno Public Enemy yamekuwa yakirudiwa mara kwa mara na kutamkwa kwenye vipindi tofauti.

Rais wa 37 wa Marekani, Richard Nickson, mwaka 1969 alitangaza matumizi ya dawa za kulevya kuwa ni Public Enemy, hata hivyo Public Enemy ya ukweli inabaki nyakati hizo za mwaka 1930 mpaka 1935.

BONNIE AND CLYDE
Utakuwa umewahi kuwasikia wakizungumzwa au kuimbwa. Walikuwa vijana wadogo na waliuawa wakiwa na umri mdogo lakini majina yao yameendelea kuandikwa, kutamkwa na kutazamwa.

Bonnie na Clyde wana historia ya kusisimua mno kuhusu mapenzi yao, walivyoshirikiana katika matukio ya uhalifu kisha wakauawa siku moja.

Historia hiyo ndiyo huwafanya wanamuziki mbalimbali kuwaimba. Rapa Tupac Shakur katika wimbo wake Me and My Girlfriend, anaimba kiitikio kuwa kitu pekee anachohitaji katika ulimwengu huu wa dhambi ni yeye kuwa na mpenzi wake.

Ndani ya wimbo huo Tupac anajifananisha yeye na mpenzi wake kuwa ndiyo Bonnie na Clyde wa mwaka 1996. Alijifananisha mwaka huo kwa sababu wimbo huo ulirekodiwa mwaka 1996 kisha kuwemo kwenye albamu ya tano ya rapa huyo, inayoitwa The Don Killuminati: The 7 Day Theory.

Mwaka 2003, Rapa Shawn Carter ‘Jay Z’ aliurudia wimbo huo wa Tupac, alimshirikisha girlfriend wake wakati huo ambaye sasa ni mkewe, Beyonce Knowles. Wimbo huo waliupa jina 03 Bonnie and Clyde, wakimaanisha kuwa wao Jay Z na Beyonce ndiyo Bonnie na Clyde wa mwaka 2003.

Mwaka 1967, wakali wa Pop na Jazz kutoka Ufaransa, Serge Gainsbourg na Brigitte Bardot, walitoa wimbo Bonnie and Clyde, wakiimba kuyafananisha mapenzi yao kama Bonnie na Clyde.

Mwaka huohuo, mwanamuziki Georgie Fame, alitoa wimbo ambao ulitikisa sana, unaitwa The Ballard of Bonnie and Clyde. Mwaka 1968 mwanamuziki Mel Tamel alitoa wimbo A Day in the Life of Bonnie and Clyde.

Mwaka 1968, mwanamuziki Merle Haggard alirekodi na kuachia wimbo The Legend of Bonnie and Clyde. Mwaka 1996, bendi maarufu ya Die Toten Hosen, walitoa wimbo Bonnie and Clyde ambao ulikuwemo kwenye albamu yao ya saba, inayoitwa Opium Furs Volk.

Bonnie na Clyde wapo Hollywood. Mwaka 1958, iliachiwa filamu yenye jina The Bonnie Parker Story, iliyoongozwa na William Witney. Mwaka 1976, Arthur Penn aliongoza filamu inayoitwa Bonnie and Clyde.

BONNIE NA CLYDE NI NANI?
Nyimbo zimeimbwa, filamu zimetengenezwa, vitabu vimeandikwa kuhusu Bonnie na Clyde, je, watu hao ni akina nani? Maisha yao yalikuwaje mpaka iwe ni historia ya kusimuliwa na vizazi vyote?
Bonnie na Clyde ni vijana wawili wapenzi wenye roho mbaya, katili kweli lakini walipendana.

Ni Bonnie Parker na Clyde Barrow. Walipanga mipango mingi ya uhalifu na kutengeneza fedha nyingi ambazo ziliwawezesha kuishi maisha ya starehe.
Kuna wale huitana Partner In Crime, wakimaanisha ushirika au urafiki ulioshibana. Partner In Crime ya kweli maana yake ni Mapatano ya Uhalifu. Ndani ya Bonnie and Clyde ndipo unaweza kuwaona waliopatana na kushibana katika uhalifu.

Bonnie and Clyde ni kundi kubwa la uhalifu, ila Bonnie na Clyde wanatajwa sana kwa ukinara wao. Bonnie ni mwanamke, Clyde ni mwanaume. Katika kundi hilo la uhalifu, alikuwepo pia Buck Barrow ambaye ni kaka mkubwa wa Clyde.

Buck kwenye kundi hilo alikuwa pia na mke wake, Blanche. Hivyo maisha waliyoishi Bonnie na Clyde yalikuwa sawa na yale ya Buck na Blanche, ingawa Blanche alikuwa anapelekwapelekwa tu, wakati Bonnie mwanamke mwenzake alikuwa mtaalamu wa kupanga na kutekeleza.

Memba wengine wa kundi hilo walikuwa ni Raymond Hamilton, William Jones ‘WD’, Joe Palmer, Ralph Fults na Henry Methvin. Wote hao walikuwa kundini na waliongozwa na vijana wawili waliopendana sana, Bonnie na Clyde.

STORI YA BONNIE AND CLYDE
Mapenzi ya Bonnie na Clyde ni uhusiano ambao haukuwa na usaliti. Wawili hao walipendana bila unafiki na waliishi kwa kutegemeana, vilevile waliogopana.

Bonnie ashikwe na kiranga mpaka amsaliti Clyde, angekuwa anajitaka? Clyde ajifanye kupapatikia warembo halafu Bonnie ajue, angeponea wapi? Wote wawili hawakuwa na kusita linapofika jambo linalohitaji kuua.
Hofu hiyo ilisababisha Bonnie na Clyde wasisalitiane lakini kikubwa ni kuwa hakuna ambacho Clyde alipanga na kutekeleza bila Bonnie wake kujua. Vivyo hivyo kwa Bonnie, hakuwa na mpango wowote nje ya Clyde wake.

Bonnie na Clyde walipanga pamoja na kutekeleza uharamia wao pamoja. Walitembea pamoja, ilipotakiwa kujificha walijificha pamoja. Walipofanikisha mipango yao ya uhalifu na kutengeneza fedha, walikwenda kujirusha pamoja.

Mahali popote ungemkuta Bonnie, ungezungusha macho ungemwona Clyde yupo. Ungekutana na Clyde njiani, ungetazama vizuri lazima ungemwona Bonnie. Hawakupeana nafasi. Walikuwa na mapenzi ya kugandana kama kupe. Mapenzi yao yalikuwa ya kufuatana kama kumbikumbi.

Kilevi alichotumia Bonnie na Clyde alitumia. Waliishi kwa tafsiri kamili ya jozi (pea). Kila baada ya kufanikisha mipango yao ya uhalifu hakuna ambacho Bonnie alikihitaji zaidi ya kula maisha akiwa jirani na mwanaume wa maisha yake, Clyde. Vivyo hivyo kwa Clyde dhidi ya mwanamke wa maisha yake, Bonnie.
Mapenzi ya Bonnie and Clyde hayakuwa na kuambiana “I Miss You”, maana hakuna nukta ilipita wakiwa wapo mbalimbali.

Walinyimana njozi tu walipokuwa usingizini, hapo ndipo kila mmoja aliota za kwake, lakini kitanda walicholala kilikuwa kimoja.
Kama shughuli za Bonnie na Clyde zingekuwa za halali, basi wangekuwa mfano bora zaidi kwa wapendanao duniani kote, kutokana na ushirikiano wao kikazi na mapenzi yao yenye nguvu. Tatizo Bonnie na Clyde mapenzi yao yalidumishwa zaidi na uhalifu wao.

Bonnie na Clyde walipenda maisha ya juu kwa njia ya mkato, na kwa vile walishirikiana ilibidi wagandane zidi kwa kufichiana siri na kulindana. Hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya kuwa na mfano wa kipekee katika mapenzi.

MJUE CLYDE
Jina la kundi ni The Barrow Gang, lakini umaafu wa Bonnie na Clyde ni sababu ya jina hilo la kundi kutokuwa maarufu kwa kumezwa na majina ya wapenzi hao wawili.
Historia inamwonesha Clyde kuwa kijana mshenzi aliyeota kuwa jamabazi la kutisha tangu akiwa kijana mdogo. Wakati Bonnie yeye alikuwa mwanamke mrembo kijana, jasiri na mwenye uthubutu, hivyo alipokutana tu na Clyde kipaji chake cha uharamia kikaonekana na kukua.

Clyde alizaliwa Machi 24, 1909, katika familia ya kimasikini iliyojiendesha kwa kutegemea kilimo cha kihohehahe. Alizaliwa na kuishi na familia yake kwenye mji wa Ellis County, Texas, Dallas.

Wazazi wa Clyde, Henry Barrow (baba) na Cumie Talitha Walker (mama) walifariki dunia wakiwa wameshuhudia matukio ya kutikisa nchi ambayo Clyde aliyafanya pamoja na kaka yake, Buck.

Clyde akiwa na umri wa miaka 17, tayari alikuwa mwenye hekaheka na polisi. Mwaka 1926, alikamatwa na polisi kwa kosa la kuazima gari na kutokomea nalo jumla. Kesi hiyo wazazi wake walimsaidia ikaisha, lakini hazikupita siku nyingi Clyde akakamatwa tena kwa kosa la kumiliki mali za wizi.

Clyde alikuwa mwenye tamaa sana, kwani kati ya mwaka 1927 mpaka 1929, alikuwa akifanya kazi halali yenye kumpa riziki, lakini alijishughulisha na ujambazi wa kuvamia maofisi na kufungua masanduku ya pesa (cracked safes).

Ujambazi mwingine ambao Clyde alijihusisha nao ni kuvamia na kuvunja maduka na maghala, kisha kupora, vilevile kuiba magari. Na kati ya mwaka 1928 na 1929, alikuwa anakimbizana na polisi wakitaka kumkamata bila mafanikio.

Aprili 1930, Clyde alitupwa jela kwenye Gereza la Eastham Unit, lililopo Texas. Akiwa gerezani, Clyde alikutana na mfungwa mshenzi, Ed Crowder ambaye walichangia chumba.

Crowder kwa kumwona Clyde ni mdogo, alimbaka kinyume na maumbile mara kwa mara nyakati za usiku. Crowder hakujua kuwa Clyde ni mdogo lakini katili kuliko alivyoweza kumtazama kwa macho.
Siku moja Crowder kama alivyozoea, alitaka tena kumbaka Clyde, kumbe Clyde alikuwa ameshajipanga, alichukua bomba lilikuwemo kwenye chumba chao na kumpiga kichwani Crowder, akapoteza maisha. Hilo lilikuwa tukio la kwanza la Clyde kuua.

ROHO NGUMU YA CLYDE
Akiwa gerezani, Clyde alimshawishi mfungwa mwenzake kumkata vidole viwili vya miguu ili awe mlemavu, aweze kukwepa kazi ngumu za jela. Kwa uamuzi huo, Clyde alimaliza maisha yake yote akiwa mlemavu asiye na vidole viwili miguuni.

Baada ya tukio hilo mama yake alifanikiwa kuandikisha hati ya kumwombea msamaha Clyde ili aachiwe huru. Clyde aliachiwa siku sita baada ya tukio lake la kukata vidole vya miguu.

Clyde aliachiwa Februari 2, 1932. Matarajio yalikuwa kwamba kwa siku alizokaa gerezani angeweza kuwa amejifunza kuwa raia mwema, lakini haikuwa hivyo. Clyde aliyetoka jela alikuwa sawa na mnyama.
Wanasaikolojia walisema kitendo cha Clyde kubakwa na mfungwa mwenzake gerezani ni sababu ya kumfanya ageuke kuwa mnyama. Maana alitawaliwa na roho ya kihalifu na kisasi.

Wapo wanasaikolojia walibainisha kuwa tabia ya asili ya Clyde na roho ngumu aliyokuwa nayo, ilipoongezewa ukatili aliotendewa gerezani, ilitosha kumfanya abadilike jumla, kutoka binadamu aliyefaa kutazamika na kumtumaini kuwa angeweza kubadilika, hadi kuwa mnyama kabisa.
Dada wa Clyde, Marie Barrow, aliwahi kuhojiwa na vyombo vya habari baada ya Clyde kuuawa mwaka 1934, alisema: “Kitu kibaya bila shaka kitakuwa kilimtokea alipokuwa jela, kwa sababu alipotoka hakuwa tena mtu wa kawaida.”

MJUE BONNIE
Bonnie alizaliwa Oktoba Mosi, 1910, Rowena, Texas. Baba yake, Charles Parker alifariki dunia mwaka 1914, wakati huo Bonnie alikuwa na umri wa miaka minne tu. Hivyo Bonnie kwa maisha yake alilelewa tu na mama yake, Emma Parker.

Kama ilivyokuwa kwa Clyde, Emma alishuhudia vitimbo vyote vya Bonnie, vurugu zake na polisi mpaka alipouawa. Emma alifariki dunia mwaka 1944, ikiwa ni miaka 10 baada ya kumshuhudia mwanaye akiuawa.

Nyakati za mwanzo Bonnie alipoanza kukua, alionesha kipaji kikubwa cha kuandika mashairi. Tungo mbili za mshairi ambazo zilipata umaarufu mkubwa ni The Story of Suicide Sal na The Trail’s End ambayo hujulikana zaidi kama The Story of Bonnie and Clyde.

Bonnie akiwa mwaka wa pili high school, alikutana na Roy Thornton, wakaacha shule na kuoana. Ndoa yao ilifungwa Septemba 25, 1926, wakati huo alikuwa na umri wa miaka 16 tu.

Ndoa yao haikuwa na maelewano kabisa na Januari 1929 walitengana, ingawa hawakuachana kwa talaka rasmi. Miaka mitano baadaye, Bonnie alipouawa akiwa na Clyde, alikutwa amevaa pete ya ndoa aliyovalishwa na Thornton mwaka 1926.
Baada ya kutengana na Thornton, Bonnie alirejea kuishi na mama yake, akaanza kufanya kazi kama mhudumu kwenye mgahawa mmoja uliopo Dallas. Katika mgahawa huo, mmoja wa wateja wake alikuwa ofisa usalama wa Dallas, Ted Hinton.
Huyo Ted Hinton ndiye baadaye alishirikiana na maofisa wenzake wa Dallas, kuwashambulia na kuwaua Bonnie na Clyde mwaka 1934.

BONNIE NA CLYDE WALIVYOKUTANA
Bonnie na Clyde walikutana Januari 1930, ikiwa ni miezi mitatu kabla Clyde hajafungwa jela. Walikutana Mtaa wa Herbert, Oak Cliff, Dallas, wakati Clyde alipomtembelea rafiki yake, anayeitwa Clarence Clay.

Nyumba ambayo Clarence alikuwa akiishi, kulikuwa na rafiki wa Bonnie aliyekuwa anaumwa. Bonnie ili kumsaidia ‘shosti’ wake, aliamua kuhamia pale kipindi akimuuguza. Ikawa kila akitoka kazini anakwenda kwa rafiki yake na analala hapohapo.

Siku hiyo Clyde alipokwenda kumtembelea Clarence, alikutana na Bonnie. Kuanzia hapo mapenzi kati ya watu hao wabaya wawili yalianza. Wanasema mapenzi hayavutwi kwa winchi, Bonnie alipomwona tu Clyde akaona tayari amemnasa mwanaume wake.
Bonnie na Clyde walitengana baada ya Clyde kufungwa jela. Februari 1932 baada ya Clyde kuachiwa huru, waliunga tena ndipo Bonnie na Clyde waliandika historia yao nzito. Vurugu zote, stori nyingi kuwahusu, kila kitu kinaundwa na matukio waliyofanya kwa miaka miwili tu.

Ilikuwa tamthiliya ndefu ya miaka miwili tu; Bonnie na Clyde wakiwa na kundi la The Barrow, walipora magari, walivamia mabenki na kuiba pesa, waliteka wasafiri na kuwaibia, walivamia maduka na kufanya matukio ya kila aina.

Aprili 30, 1932, Clyde akiwa dereva wa gari, kundi lao lilivamia duka moja eneo la Hillsboro, Texas. Katika uvamizi huo, mmiliki wa duka, J.N Bucher alipigwa risasi na kuuawa. Mke wa mwenye duka alimtambua Clyde kuwa ndiye aliyepiga risasi ingawa yeye alikuwa kwenye gari.

Kutokana na tukio hilo, Bonnie alikamatwa lakini alikaa miezi miwili jela kabla ya kuachiwa. Clyde aliendelea kusakwa kwa tuhuma za mauaji hayo ya mmiliki wa duka. Juni 17, 1932, Bonnie aliachiwa kisha wakaendelea na shughuli zao za uporaji.
Machi 22, 1933, Buck aliachiwa kutoka jela alikokuwa amefungwa kwa makosa ya ujambazi, baada ya hapo naye akiwa na mkewe, Blanche walijiunga na kundi hilo.
Wakati huo, Bonnie na Clyde walikuwa wakitafutwa sana, kwa hiyo Buck na Blanche walifanya kazi ya kuwahudumia walipokuwa wamejificha kwenye gereji moja, iliyopo Joplin, Missouri.

Baadaye chimbo hilo lilishitukiwa. Majirani waliona hali isiyokuwa ya kawaida na kutoa taarifa polisi ambao walivamia. Mapigano makali yalitokea ya kurushiana risasi na askari wanne waliuawa, mmoja alijeruhiwa.
Bonnie na Clyde pamoja na kundi zima la The Barrow walitoroka eneo hilo. Baada ya kutoroka, polisi walirejea na kukagua. Walifanikiwa kupata picha ya Bonnie akiwa anavuta sigara, vilevile mkononi akiwa na bunduki. Walikuta pia shairi la Bonnie, The Story of Suicide Sal.

Picha hiyo ya Bonnie na shairi la The Story of Suicide Sal, vilipamba kwenye magazeti na kuwa kivutio cha wasomaji wengi kwa wakati huo. Ni kuanzia hapo ilithibitika kweli Bonnie alikuwa haramia mwanamke, moto wa kuotea mbali.

MWISHO WA BUCK
Bonnie na Clyde waliendelea kuongoza kundi lao. Kukawa na ‘kapo’ mbili zenye kufanana, Bonnie na Clyde, vilevile Buck na Blanche. Matukio ya uharamia wa kuteka na kupora yaliendelea kama kawaida.

Julai 1933, kundi hilo lilivamia jengo ambalo huitwa Red Crown Tourist Court, lililopo Jiji la Platte, Missouri. Waliteka walinzi wa jengo hilo kisha wakafanya makazi ya kujificha kwa muda.

Wakati wanaingia hapo, Buck alikuwa ameshajeruhiwa kwa risasi kichwani na kupata madhara mpaka kwenye bongo, vilevile Bonnie alikuwa amejeruhiwa na maji ya betri ya gari, kwa hiyo walijificha hapo huku wakiwatibu.

Clyde akawa anatoka kwenda kununua dawa na kurudi kuwatibu Bonnie na Buck. Kwa Bonnie ilikuwa rahisi kupona. Buck walikata tamaa. Wakati huohuo, Blanche alipata matatizo ya macho baada ya kudondokewa na vipande vya kioo machoni wakati wa mashambulizi ya risasi na polisi, yaliyomjeruhi mume wake (Buck).

Julai 24, 1933, kundi zima la The Barrow lilihamia kwenye jumba la starehe lililokuwa limetelekezwa, lililoitwa Dexter Park, lililopo Iowa. Mpaka wakati huo Bonnie alikuwa ameshapona.

Clyde aliamini kaka yake (Buck) angekufa wakati wowote, kwa hiyo alichofanya ni kushirikiana na WD kuchimba kaburi. Walichimba wakiamini wakati wowote Buck angekufa wamzike kisha waendelee na safari yao ya kujificha na kupora.

Bahati mbaya, bandeji zenye damu zilizotupwa baada ya kumbadilisha Buck, zilionwa na majirani ambao walitoa taarifa polisi. Kwa taarifa hizo polisi walihisi watu hao bila shaka ni timu nzima ya The Barrow.
Polisi walivamia Dexter Park, walimpiga risasi Buck na kumkamata Blanche. Clyde, Bonnie na WD walifanikiwa kutoroka.
Buck baada ya kukamatwa na polisi, alipelekwa Hospitali ya Kings Daughter, iliyopo Perry, Iowa. Siku tano baada ya kufikishwa hospitalini hapo alifariki dunia. Ilikuwa Julai 29, 1933.

Blanche alijitetea kuwa yeye hakuwa jambazi, isipokuwa alimpenda sana mume wake (Buck), hivyo hakuweza kuishi mbali naye, akawa hana namna zaidi ya kujiunga naye kwenye kundi.

Hata hivyo, Blanche alifungwa jela miaka 10 na akiwa jela, alipokea taarifa za vifo vya Bonnie na Clyde.

TAMATI YA BONNIE NA CLYDE
The Barrow walibaki watatu, kwa maana ya Bonnie, Clyde na WD, hivyo walijiona ni wachache. Walichofanya ni kuvamia Gereza la Eastham ambalo Clyde aliwahi kufungwa na kutorosha wafungwa ambao walikuwa wakitumikia kifungo cha maisha ili kuongeza nguvu.

Clyde alijua watu wabaya ni akina nani ambao wangeweza kusaidia kuimarisha kundi. Ilikuwa Januari 1934, The Barrow walifanikiwa kuwatorosha wafungwa, Raymond Hamilton, Henry Methevin na wengine wengi.

Mwanahistoria John Phillips ambaye ni msimuliaji mzuri wa habari za Bonnie na Clyde, alisema kuwa tukio la The Barrow kuvamia Gereza la Eastham na kutorosha wafungwa, ni mafanikio ya Clyde kulipa kisasi dhidi ya Idara ya Magereza ya Texas kwa kumfunga mwaka 1930.

Idara ya Magereza ya Texas, iliamua kumshawishi mlenga shabaha maarufu, Frank Hamer na kumpa kazi ya kuwafuatilia The Barrow na kuwaua. Vilevile Mkuu wa Idara ya Magereza Texas, Lee Simmons, aliwapa kazi walenga shabaha wengine wawili kwa ajili ya kazi hiyo.

Hamer ndiye aliyekuja kuwa mtu maya kwa Bonnie na Clyde. Maana baada ya kupewa kazi hiyo, hakulala nyumbani kwake. Maisha yake yalibadilika kuwa ya kwenye gari, muda wote aliwafuatilia Bonnie na Clyde.

Aprili Mosi, 1934, ilikuwa Jumapili ya Pasaka, siku hiyo Clyde na Methvin waliua vijana wawili wauza mafuta ambao ni H. D Murphy na Edward Wheeler. Baada ya hapo waliendelea kufanya mauaji na kupora mali mfululizo.

Hali ilikuwa mbaya, mamlaka za usalama Texas na Marekani yote, ziliamka na kutoa tangazo la zawadi nono kwa atakayefichua siri kuhusu mahali walipo The Barrow.
Nyumba zote za starehe, hoteli, baa na kadhalika, polisi waliwekwa ili kupambana na The Barrow. Majina ya Bonnie na Clyde yalitangazwa kila kona. Hali ilikuwa ya wasiwasi, kwani nao kadiri walivyosakwa ndivyo walivyoua na kupora.

Mwanahistoria James Knight, alisema kuwa kipindi hicho cha machafuko, Bonnie alionekana mkomavu wa kutumia bunduki, akishambulia sawasawa na Clyde. Knight aliandika: “Hakika Bonnie alionekana muuaji, akiwa na bunduki hakutaka kupoteza muda.”

SIKU YA KIFO
Kuanzia Februari 12, 1934, Hamer alianza kusoma nyenendo za The Barrow, aliwafuatilia na kujua walikuwa wakitembea kama wakimbizi katika majiji matano tofauti ya Marekani lakini makao yao yalibaki kuwa Texas.

Mei 21, 1934, Hamer baada ya kufuatilia kwa miezi mitatu mfululizo, aliweza kugundua kuwa siku hiyo Bonnie, Clyde na Methvin walikuwa na safari ya kwenda Parokia ya Bienville, Lousiana kwa ajili ya kuwatafutia makazi wazazi wa Methvin.
Siku hiyo pia waligundua kuwa Bonnie na Clyde wangerudi peke yao Shreveport, Lousiana. Siku ya pili, yaani Mei 22, ilipita kimya. Kumbe polisi walikwenda kumteka baba yake Methvin ili wamtumie kuwakamata Bonnie na Clyde.

Mei 23, 1934, saa 3:15 asubuhi, Bonnie na Clyde wakiwa kwenye gari aina ya Ford V8 Fordor Delux Sedan toleo la mwaka 1934. Clyde akiwa ndiye anaendesha, alimkuta njiani baba yake Methvin, alipoanza kuzungumza naye, polisi wanne wataalamu wa shabaha walimshambulia Clyde na kumuua hapohapo.

Baada ya hapo walimgeukia Bonnie aliyekuwa kwenye gari, siti ya abiria na kumwagia risasi kisha naye akafa. Hadithi ya Bonnie na Clyde ikaishia hapo.

Hamer, Ted Hinton, Bob Alcorn na B.M Gault ‘Manny’ ndiyo askari wabaya waliohitimisha tamthiliya ya Bonnie na Clyde duniani.
Hao ndiyo ma-partner in crime wa ukweli. Mfanano wao ni Buck na Blanche. Baada ya kutoka jela, Banche alishuhudia mengi na alilizwa mno na watu walivyoigiza uhusika wake katika filamu mbalimbali.

Kila alipoona filamu iliyoigizwa kuhusiana na Bonnie na Clyde na kushuhudia kipande chake kilivyochezwa, alikiri kweli hakuwa binadamu wa kawaida. Blanche alifariki dunia Desemba 24, 1988 kwa maradhi ya kansa.

Clyde alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 25, Bonnie miaka 23, Buck miaka 30, Blanche ambaye alipotoka jela aliachana na uhalifu, aliishia miaka 77. Kweli, ukiwa mhalifu lazima uishi umri mfupi.

Ukifika Gibsland, Louisiana, Marekani kuna jumba la makumbusho ya mapambano ya Bonnie na Clyde yaliyotokea Mei 23, 1934. Jumba hilo linaitwa Bonnie and Clyde Ambush Museum. Kumbukumbu zote zipo, hata gari hilo lipo na matundu yake ya kuchakazwa na risasi siku ya kifo cha wapenzi Bonnie na Clyde.

Safari yao ilihitimishwa Dallas, Texas lakini kwenye makaburi tofauti. Bonnie alizikwa makaburi ya Crown Hill Memorial Park na Clyde alihifadhiwa Western Heights Cemetery.



maloto
 
Mods rekebisheni title isomeke

BONNIE NA CLYDE: Wapendanao Maarufu Walifanya Ujambazi Enzi za Muanguko wa Kiuchumi (Economic Depression)
 
Back
Top Bottom