Stori: Usife haraka mpenzi wangu

Ambiele Kiviele

JF-Expert Member
Dec 29, 2014
15,267
29,906
USIFE HARAKA MPENZI WANGU

HANA haraka anapotembea, ukimtazama anaonekana kujiamini sana. Tabasamu mwanana linaupamba uso wake, lakini mavazi yake yanaonesha asivyo mtu wa dhiki! Hata kama siyo sana, lakini uwezo wa kubadilisha mboga ulikuwa mikononi mwake!

Anatoka kwenye duka hili maalum kwa kuuza kadi na zawadi mbalimbali lililopo ghorofa ya saba, katika jengo moja la KPC Towers, katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Anatembea taratibu kuifuata lifti iliyokuwa mita chache sana mbele yake.

Anatabasamu!

Ni kweli anatabasamu!

Tena basi alikuwa na kila sababu ya kutabasamu, maana zilibaki wiki tatu tu, kabla ya ndoa yake na mpenzi wake wa siku nyingi Cleopatra ifungwe.

Mkononi mwake ana bahasha ya khaki ambayo ndani yake kuna zawadi kwa ajili ya Cleopatra wake. Alijua anachotakiwa kumfanyia Cleopatra!

Siku zote alikuwa akinunua apple tu, mambo yanakuwa sawa! Huo ulikuwa ugonjwa mkubwa zaidi kwa Cleopatra.

Alipoifikia, akabonyeza kitufe fulani mlangoni, mlango ukafunguka. Akaingia na kusimama, punde mlango ukajifunga, akabonyeza kwenye herufi G akimaanisha kwamba anataka kushuka chini!

Ni kijana mtanashati sana, anayevutia kwa kila mwanamke aliyekamilika.

Anaitwa Deogratius Mgana. Mfanyakazi wa shirika moja lisilo la kiserikali jijini Dar es Salaam. Ana furaha moyoni mwake, maana anakwenda kufunga ndoa na chaguo lake.
Kwanini asitabasamu!

Hakika ana haki ya kutabasamu!

“Ni kweli lazima nitabasamu, kwanza nusu ya ndoto zangu tayari zipo kwenye mstari. Lazima nijisikie vizuri,” akawaza mwenyewe akiwa kwenye lifti.

Akabaki ametulia kimya akiwa amesimama kwenye lifti ile, ikaanza kushuka taratibu kwenda chini. Ghorofa ya sita, ghorofa ya tano, ghorofa ya nne...

alipofika ghorofa ya tatu, lifti ikasimama. Hapo akajua kuna mtu aliyekuwa akitaka kushuka chini. Mlango ulipofunguka, wakaingia wanaume watatu, wote wamevaa miwani za jua.

“Mambo bro?” Mmoja akasalimia.
“Poa,” akaitikia Deo.

Lifti ikaanza kushuka taratibu, walipofika ghorofa ya tatu, ikasimama. Mlango ulipofunguka tu, ghafla wale vijana watatu wakamsukuma hadi nje. Mara mlango ukafunga.

“Paaaaaa!” Mlio wa risasi ukasikika.
Deo akaanguka chini, akianza kuvuja damu!


* * *

Alisikia vizuri sana mlio wa simu yake, lakini aliamua kupuuzia! Si kwamba hakutaka kwenda kupokea, lakini alikuwa na kazi muhimu sana aliyokuwa akiifanya, zaidi ya kwenda kupokea simu!

Cleopatra alikuwa anapika!

Chakula kizuri ambacho mpenzi wake alikuwa anakipenda sana. Alikuwa anapika viazi vya kukausha, maarufu kama maparage, ambavyo Deo alikuwa akipenda sana.

Siku hiyo Deo alipanga kwenda nyumbani kwa akina Cleopatra, Mikocheni.

Ilikuwa zimebaki wiki tatu tu ndoa yake na Deo ifungwe. Siku ambayo alikuwa akiitamani sana na kuomba ifike haraka.

Mlio wa simu yake ukaisha ghafla. Akaendelea na mapishi yake jikoni, lakini baada ya muda mfupi sana, simu ikaita tena kwa mara nyingine...

“Nani huyo aaah!” Cleopatra akasema kwa hasira kidogo.

“Mi’ nampikia Deo wangu bwana alaaah!” Akasema tena, akifunika kile chakula jikoni na kufunga kanga vizuri.

Yap! Kama ungekuwepo, ungeamini kweli Cleopatra alikuwa mwanamke mrembo.

Pamoja na kwamba alikuwa amevaa kanga, lakini umbo lake lenye namba nane liliweza kuonekana vyema kabisa. Cleopatra alijaaliwa umbo zuri sana la kuvutia.

Ona anavyotembea...
Kama anaionea huruma ardhi. Ana hips pana zinazozidisha uzuri wake, ana macho mazuri yenye uwezo wa kumchanganya mwananaume yeyote yule. Labda niseme kwamba, Cleopatra alikuwa mwanamke mrembo sana.

Alivyofika sebuleni, simu ikaacha kuita. Akachukia sana, lakini akiwa anainua ili aweze kujua aliyekuwa akimpigia ili aweze kumpigia tena, akashangaa simu yake ikianza kuita tena. Kwenye kioo cha simu yake likaonekana jina ‘My Deo’!
“Jamani, kumbe ni sweetie!”

Akasema akibonyeza kifufe cha kijani ili kumsikiliza.
Ilikuwa ni namba ya Deo ikionekana kwenye kioo cha simu yake..
.
“Yes baby, najua hujasahau kuninunulia apple na napenda kukujulisha kwamba, maparage yako yanakaribia kuiva, ila sijui ungependa nikuandalie juice ya nini?

Machungwa, maparachichi, maembe au mananasi? Maana kila kitu kipo kwenye friji!” Cleopatra akasema kwa sauti iliyojaa mahaba mazito sana.

“Samahani dada, mimi siyo mwenye simu!” Sauti hii ya kiume, tulivu yenye mikwaruzo kwa mbali ilisikika kwenye simu ya Cleopatra.
“Sasa kama wewe si mwenye simu, kwanini umepiga? Kwanini unakosa ustaarabu?”

Cleopatra akamwuliza yule mtu akiwa na hasira sana.

“Samahani sana dada’ngu, lakini nadhani ni vyema ukawa mtulivu na kuuliza kilichotokea. Si kawaida mtu kupiga simu isiyo yake kwa watu ambao wamehifadhiwa kwenye simu hiyo.

Hiyo ingetosha kabisa kukufanya ugundue kwamba kuna tatizo!” Mtu huyo akasema akizidi kuonesha kwamba anahitaji utulivu wa Cleopatra.

“Ndiyo...enhee kuna nini?

Hebu niambie, maana tayari nahisi nimeanza kuchanganyikiwa!”
“Sina shaka wewe ndiye Cleopatra!”
“Ndiyo!”

“Ni nani wako?”

“Ni mchumba’ngu, kwani vipi?”

“Usijali, tuliza moyo dada yangu.

Mimi ni Dk. Palangyo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili. Huyu ndugu mwenye simu, ameletwa hapa na wasamaria wema, baada ya kupitishwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay!”
“Anaumwa na nini dokta?” Cleopatra akauliza akianza kulia kwa huzuni.

“Amepigwa risasi na watu wasiojulikana katika Jengo la KPC Towers.

Hata hivyo, hana hali mbaya sana, matibabu yanaendelea, lakini nimeona ni vyema kukujulisha ili uwafahamishe na ndugu wengine!”

“Asante dokta kwa taarifa, baada ya nusu saa nitakuwa hapo,” Cleopatra akajibu akizidisha kilio chake.

Akatoka mbio, hadi chumbani kwake. Hakukumbuka kwenda kuipua chakula jikoni. Akavaa haraka na kutoka hadi getini! Ghafla kumbukumbu zake zikarudi!

“Mama yangu, nimeacha chakula jikoni na jiko linawaka,” akawaza akirudi ndani mbio.

Ilikuwa ni hatari sana, maana alikuwa anapikia jiko la umeme. Mara moja akarudi ndani na kuzima jiko, akaipua kile chakula na kutoka kwa kasi sana.

“Wewe vipi mwenzetu, mbona hivyo?” Mama yake Cleopatra akamwuliza baada ya kumuona mwanaye anaonekana kuwa na haraka ambayo hakujua ni ya nini.
“Nitakupigia simu mama!”

“Unakwenda wapi?”

“Mama nitakupigia!”

“Patra, mwenzako si anakuja au haji tena?”

“Mama Deo amepigwa risasi, yupo hospitalini,” akasema Cleopatra akiwa tayari ameshaingia kwenye gari.

Akapiga honi kwa nguvu, mlinzi akafungua haraka. Cleopatra akaondoa gari kwa kasi sana. Alikuwa anakwenda Muhimbili, huku nyuma akiwa amemuacha mama yake akiwa mwenye mawazo.

Episode Ya 2 Inakuja
 
USIFE KWANZA MPENZI WANGU......

EPISODE 2.


Akiwa jikoni anaandaa chakula kwa ajili ya mpenzi wake, Cleopatra anapokea simu kutoka Muhimbili, akipewa taarifa kwamba Deo, mpenzi wake amepigwa risasi na amelazwa. Taarifa hizo zinamshtua sana. Anatoka na gari haraka kwenda hospitalini. Nini kitatokea? Endelea...

CLEOPATRA aliendesha gari kwa kasi sana, hakujali ajali barabarani, alikuwa tayari kwa lolote litakalotokea! Aliendesha kwa kasi ya ajabu sana. Kutokea nyumbani kwao Mikocheni hadi Muhimbili, alitumia dakika ishirini!

Hakukubali kukaa foleni, aliendesha kama daladala, kwani alipenyeza pembeni, sehemu zilizokuwa na foleni kubwa.

Alipofika hospitalini, akaegesha gari lake kisha akapiga zile namba na kuzungumza na yule daktari.

“Nimeshafika dokta!”

“Ok! Uko wapi?”

“Kwenye maegesho!”

“Tukutane MOI!”

“Sawa dokta.”

Bila kupoteza muda, Cleopatra akachanganya miguu hadi ilipo wodi ya Taasisi ya Mifupa (MOI).

Akiwa kwenye lango kuu la kuingilia, akamwona mwanaume mmoja mrefu aliyevaa koti jeupe na miwani, akahisi angekuwa ndiye daktari aliyekuwa akimfuata.

“Sorry, ni dk. Pallangyo?”

Cleopatra akauliza akimkazia macho.
“Yes, karibu!”

“Ahsante!”

“Nifuate!”

Dk. Pallangyo akatangulia na Cleopatra akimfuata nyuma. Safari yao ikaishia ofisini kwa daktari yule.

“Karibu sana dada yangu!”
“Ahsante!” Cleopatra akajibu na kuketi kwenye kiti, kwa mtindo wa kutazamana na daktari.
“Ulisema mgonjwa ni nani wako?”

“Mchumba wangu!”
“Oh! pole sana...kilichotokea ni kwamba, mwenzio amepigwa risasi ya begani, lakini inaonekana kutokana na mshtuko alioupata, umesababisha apoteze fahamu.

Tunashukuru kwamba risasi haijatokeza upande wa pili, kwahiyo tumefanikiwa kuitoa, lakini bado hajazinduka!”

“Mungu wangu, atapona kweli?”

“Uwezekano huo ni mkubwa sana, lakini tuombe Mungu, naamini atakuwa sawa.”
“Naweza kwenda kumuona tafadhali?”

“Bila shaka!” Dokta akamjibu na kusimama.
Akaonesha ishara kwamba Cleopatra amfuate. Akasimama na kumfuata nyuma yake.

* * *

Deogratias alikuwa amelala kimya kitandani, Cleopatra akiwangalia kwa jicho la huruma, simanzi tele ikiwa imemjaa moyoni mwake. Moyo wake unashindwa kuvumilia, macho yake yanazingirwa na unyevunyevu. Chozi linadondoka!

Chozi la huzuni!

Deo ametulia kitandani, mwili wake ukiwa umefunikwa kwa shuka jeupe, isipokuwa kuanizia kifuani, bandeji inaonekana mkononi mwake. Mapigo ya moyo wake yanakwenda taratibu kabisa!

“Deo wangu...Deo...Deo jamani...amka mpenzi wangu. Naomba usife kwanza mpenzi wangu jamani. Hebu amka baby, tufunge ndoa...bado nakupenda...” akasema Cleopatra akilia kwa uchungu..

Deo hakusikia kitu, alikuwa katika usingizi mzito akiwa hajui chochote kinachoendelea. Alikuwa amepoteza fahamu na hakuwa na uwezo wa kusikia chochote.

Wasiwasi wa Cleopatra ulikuwa mmoja tu; Kwamba Deo akifa asingeweza tena kufunga naye ndoa, tendo ambalo alikuwa akilisubiria kwa muda mrefu sana.

Cleopatra akazidi kulia. Alitamani sana kuliona tabasamu la Deo.

Alitaka kuona akiongea, akimbusu, akimkumbatia na kumwambia maneno matamu ambayo amekuwa akimwambia mara nyingi sana.

Hilo tu!
Lakini Deo hakuweza kufanya chochote kati ya hivyo.

Alikuwa amelala kitandani kama mzigo, hana taarifa kama mpenzi wake Cleopatra alikuwa kitandani kwake akilia.

“Basi dada yangu, mwache apumzike, usijali, huna sababu ya kulia. Atapona tu!”

“Lakini inaniuma dokta, bado wiki tatu tufung ndoa. Tayari ndoa imeshatangazwa mara ya kwanza kanisani, bado mara tatu ili nifunge ndoa na Deo wangu,

sasa itawezekanaje tena? Si ndiyo nimeshamnpoteza? Si tayari nimeshapoteza ndoa?” Cleopatra akasema akionekana kuwa na uchungu sana.

“Hapana, hana hali mbaya, wiki tatu ni nyingi sana, kabla ya muda huo atakuwa amesharejea katika hali yake ya kawaida, bila shaka atapanda madhabahuni kufunga ndoa na wewe!”

Maneno ya Dk. Pallangyo kidogo yalimpa moyo Cleoptara, lakini ndani ya moyo wake, aliendelea kuwa na uchungu mwingi sana, kwani Deo alikuwa kila kitu katika maisha yake.

Yeye ndiye aliyekuwa wa kutimiza ndoto zake za kuingia kwenye ndoa, lakini sasa zinakaribia kuzimika!

Lazima aumie!

Lazima ateseke!..

Episode 3 inakuja
.
 
USIFE KWANZA MPENZI WANGU.....

EPISODE.3.

leopatra analia mbele ya kitanda cha Deogratius, ambaye alikuwa amelazwa baada ya kupigwa risasi. Zilibaki wiki tatu tu, kabla ya ndoa yao. Machozi machoni mwa Cleopatra yaligoma kabisa kufutika!

Dokta akamtoa nje, akimbembeleza na kumpa moyo kwamba asijali, mgonjwa wake angepona.

Cleopatra haamini hilo, anazidi kulia kwa uchungu, mawazo tele kichwani mwake yakizidi kumzonga.

Alichowaza yeye ni ndoa tu! Atafungaje wakati mpenzi wake alikuwa amelazwa wodini? Endelea kufuatilia...

AKIWA katika mawazo ya kumuumiza moyo, simu yake ikaita. Akaangalia jina la mpigaji akakutana na jina lililoandikwa ‘My Mumy’.

Alikuwa ni mama yake mzazi akimpigia. Kwa muda akaiangalia ile simu akijishauri kupokea, lakini alisita.

Alijua sababu ya simu ya mama yake, kwa vyovyote vile, angetaka kujua kuhusu Deo, jambo ambalo aliamini lingeweza kuamsha machozi upya, kitu ambacho hakutaka kabisa kitokee.

Lakini baadaye akaamua kupokea...
“Patra uko wapi?” Ndiyo neno alilokutana nalo baada ya kupokea simu ya mama yake.

“Hospitalini!”

“Upo sehemu gani, maana na mimi tayari nimeshafika hapa Muhimbili!”

“Nipo huku MOI mama!”

“Nakuja!”.

Muda mfupi baadaye, mama yake akatokea. Cleopatra alipokutanisha uso na mama yake, machozi kama maji yakaanza kumwagika machoni mwake.

Akamkimbilia na kumkumbatia.

“Mama Deo wangu anakufa mama...” akasema kwa hisia za uchungu sana..

“Hapana mwanangu, hutakiwi kuwaza hayo mama...yupo wapi?”

“Wodini!”.

“Twende...”.

“Hawaruhusu kwenda sasa hivi, muda wa kuwaona wagonjwa umepita!”
“Tatizo ni nini hasa lakini?”

“Amepigwa risasi!”

“Na nani?”

“Hawajulikani mama.”
“Wapi?”

“Mjini. Daktari anasema aliletwa na wasamaria wema baada ya kumuokoa!”
“Maskini, ana hali mbaya sana?”
“Haongei mama, amepigwa risasi ya bega, lakini dokta anasema imekuwa vizuri maana haijatokeza upande wa pili.”

“Mungu ni mwema mwanangu.”
“Namuomba sana amponye ili tufunge ndoa yetu kwanza.”

“Sote ndiyo dua yetu!”
Kwakuwa muda ulikuwa umeshapita wakaondoka kwa ahadi ya kurudi jioni kumuona.

****

Saa 11:00 jioni, Cleopatra na mama yake walikuwa wanaingia katika wodi aliyolazwa Deo. Hawakuamini walipofika kitandani mwake na kumuona akiwa amefumbua macho yake. Cleopatra akalia kwa furaha.

“Pole sana sweetie!”

“Ahsante!” Deo akajibu kwa sauti ya taratibu sana.

“Shikamoo mama...”

Deo akasalimia.

“Marahaba mwanangu, pole sana!”
“Ahsante mama!”

“Ilikuwaje?” Cleopatra akauliza akiketi kitandani kwa Deo.

“Hata sielewi, nakumbuka nilikuwa kwenye lifti, nilipofika ghorofa ya tatu lifti ikasimama, wakaingia wanaume watatu,

tukaanza tena kushuka hadi ghorofa ya pili, ikasimama tena.

Ghafla nikasukumwa nje, kilichofuata ilikuwa ni mlio wa risasi.

“Nikashtuka sana na kupoteza fahamu. Nilipozinduka, nikajikuta nipo hapa hospitalini.”

“Unaweza kumkumbuka kwa sura hata mmoja wao?”

“Hapana.”

“Pole sana, lakini unajisikiaje sasa?”

“Siwezi kujielezea, nahisi maumivu ya mkono na bega, lakini sielewi hali yangu hasa!”

“Pole sana, utapona usijali,” mama yake Cleopatra akasema.

“Nashukuru sana mama.”

Cleopatra akamlisha chakula huku akimwambia maneno matamu ya kumtia moyo!

Kidogo Deo akaanza kujisikia vizuri baada ya kupata faraja kutoka kwa mpenzi wake.

Muda wa kuwaona wagonjwa ulipopita wakaondoka zao.

“Ugua pole dear, kesho asubuhi nitakuja kukuona.”

“Ahsante sana mpenzi wangu, nakupenda sana. Ahsante kwa kujali kwako!”

“Ni wajibu wangu...utapenda kula chakula gani asubuhi?”

“Chochote tu baby!”

“Chagua mwenyewe mpenzi wangu!”

“Nadhani mtori utanifaa zaidi.”

“Ok! lala salama, ugua pole, you will be okay!”

“Thank you baby!”

Cleopatra na mama yake wakaondoka, wakamuacha Deo akiwa ametulia kimya kitandani, akisikilizia maumivu yake ya bega. Mpaka wakati huo, hakuelewa ni kwanini watu wale walimpiga risasi, maana hakuwa na fedha na wala hawakumwibia!

Hilo liliendelea kuzunguka kichwani mwake bila kupata majibu.

***
Anahisi kama ameguswa na mkono wa mtu, anajaribu kuyafumbua macho yake kwa shida kidogo kutokana na mzigo wa usingizi aliokuwa nao!

Alilala sana siku hiyo. Uchovu na usingizi ulisababishwa na mambo mawili; Deo alikuwa hajalala usiku mzima kwa maumivu ya bega, ndiyo kwanza asubuhi hiyo alianza kuhisi usingizi.

Dawa alizokunywa, zilikuwa kali na zilimchosha sana mwili wake. Hayo yalitosha kabisa kumfanya, saa moja hii ya asubuhi, macho yake yaendelee kuwa mazito.

Anajaribu kuyafumbua kwa shida na kumtazama mtu huyo!

Akashtuka sana!

Hakutegemea kukutana na sura hii hospitalini. Nani amemwambia kwamba amelazwa?

Ni jana tu, alipata matatizo, leo hii amejuaje?

Nani amempa taarifa za yeye kuumwa?

Yalikuwa maswali yaliyofumuka mfululizo kichwani mwake, bila kupata majibu stahiki!
Anazidi kumwangalia mwanamke huyu ambaye naye amesimama kama ameganda...
“Pole Deogratius...pole sana kwa matatizo!” Mwanamke huyo akatamka kwa sauti ya taratibu sana.

Deo hakuitika!

“Maskini Deo, najua ni kiasi gani unaumia, najua kwamba ni jinsi gani ndoa yako itakavyokuwa na ugumu wa kufungwa. Bila shaka mmebakiza wiki tatu tu, sidhani kama utaweza kupanda madhabahuni ukiwa katika hali hii...pole sana...ni majaribu tu ya shetani,” akatamka kwa yakini, akiongea kwa mpangilio mzuri sana.

Deo hakujibu neno!

“Huyu vipi? Amejuaje nipo hapa?

Amejuaje natarajia kufunga ndoa? Amejuaje mambo yangu?...

amejuaje?”

Akazidi kujiuliza Deo, lakini majibu hakuwa nayo.
“Nakupa pole huitiki, kwanini?

Au hujapenda mimi kuja hapa?” Mwanamke yule akasema, akionekana kusononeka na mapokeo ya Deo.

Kwa ghafla sana, macho ya Deo yakaanza kupatwa na unyevunyevu, baadaye machozi yakaanza kuchuruzika machoni mwake.

Ubongo wake ukasafiri miaka kumi nyuma. Akayatupa macho yake juu ya dari, kisha kumbukumbu zote za maisha yake yaliyopita zikaanza kumjia kama anatazama sinema ya kusisimua...

Sinema ya maisha yenye kila aina ya machafuko na mataabiko.

Mateso, dhiki na kuonewa. Masimango, kutukanwa na kudhalilishwa. Ilikuwa sinema mbaya, lakini yenye mwisho mzuri wa kupendeza, mwisho ambao baadaye uliingia shubiri.

Ikawa chungu!
Sinema ikaanza...
 
USIFE KWANZA MPENZI WANGU.....

EPISODE.4.

Cleopatra analia mbele ya kitanda cha Deo aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, hali yake ni mbaya na anatamani sana kuona Deo wake akiamka ili waende wakafunge ndoa yao kanisani.

Baada ya saa kadhaa, Deo anazinduka, Cleopatra na mama yake walipoenda baadaye, walimkuta Deo akiwa ameshazinduka, hawezi kuzungumzia vizuri jinsi alivyopata ajali ile.

Wanaondoka kwa ahadi ya kurudi tena asubuhi inayofuata.

Muda mfupi baada ya wao kuondoka, anaingia mwanamke mmoja na kumpa pole kwa matatizo aliyoyapata.

Deo hajibu kitu muda wote mwanamke yule alipokuwa akizungumza. Lakini baadaye, Deo akaonekana kuwa na mawazo ya ghafla!

Akili yake ikasafiri miaka kumi iliyopita, akaanza kukumbuka matukio yote yaliyotokea katika maisha yake.

Kila kitu kikaanza kuonekana kama sinema ya kusisimua.
Je, anakumbuka nini?

Endelea....

Oktoba 22, 1999 – Dar es Salaam
Ni siku nyingine ya pilikapilika, kama ilivyokuwa kwa siku zilizotangulia, leo pia Deo ameamka saa 11:00 alfajiri kama kawaida yake.

Alipoamka kitu cha kwanza kufanya ni kumwagilia maji maua, kufanya usafi wa mazingira na kuwapeleka watoto shule.

Aliporudi, alitoka nyumbani kwa bosi wake Mburahati, akaenda sokoni Tandale, kilometa zaidi ya kumi na tano kwa miguu.

Hapo ndipo anapofanya kazi ya kuuza mchele hadi saa 11:00 jioni, anapoanza safari nyingine ya kurudi nyumbani kwa miguu.

Siku yake humalizika kwa kufunga mifuko ya barafu hadi saa sita za usiku anapopata muda wa kupumzika, kabla ya kukurupushwa tena alfajiri inayofuata.

Hayo ndiyo maisha yake!

Deogratius Mgana, kijana mchapakazi, hajawahi kupumzika hata siku moja tangu alipoanza kazi katika nyumba ya mzee

Maneno, miaka mitatu iliyopita. Alikuja Dar es Salaam, akitokea nyumbani kwao Kiomboi Singida kwa lengo moja tu, kutafuta maisha. Mshahara wake ukiwa ni shingili elfu arobaini na tano tu, kwa kazi zote anazofanya.

Akiwa ametulia kwenye ubao wake sokoni, anatokea dada mmoja mrembo sana. Si mgeni machoni mwake, ni mteja wake wa kila siku, ambaye amekuwa akimhudumia mchele karibu mara mbili au tatu kwa wiki!

“Mambo kaka?” Dada yule akamsalimia.
“Poa, karibu!”

“Ahsante, nipimie kilo tano!”
“Usijali!”.

Deo akampimia mchele aliohitaji na kumuwekea kwenye mfuko, kisha akampa. Yule msichana akalipa na kuondoka...baada ya hatua nne, akarudi tena.

“Samahani kaka, nimeshakuwa mteja wako wa kudumu sasa, nadhani ni vizuri kujua jina lako. Mimi naitwa Levina, wewe je?”
“Deogratius, lakini wengi wanapenda kuniita Deo!”
“Nashukuru kukufahamu, sasa nimeridhika, kwaheri!”

“Poa!”

Deo alimwangalia Levina hadi alivyoishilia, namna alivyokuwa akitembea, namna alivyokuwa akiongea vilimpa picha ya tofauti sana.

Alianza kuhisi eti huenda Levina anampenda, lakini alijishangaa, maana lilikuwa jambo gumu kidogo!

Levina ampende yeye?

Muuza mchele?

Mbona alikuwa anawaza mambo makubwa sana? Lakini bado hakutaka kuuhakikishia ubongo wake moja kwa moja juu ya hilo.

Aliamini kwamba lazima kulikuwa na kitukinaendelea. Kwanini atake kujua jina lake? Ana umuhimu gani hasa?

“Au zali la mentali nini?

Si kawaida mteja kutaka kujua jina langu bila sababu za msingi. Lazima kuna kitu kinaendelea, lazima....”

akawaza Deo akiwa anamwangalia mpaka anavyoishilia mbali.
Akabaki akiwa na mawazo mengi kichwani mwake, tayari hisia za mapenzi dhidi ya Levina zilianza kumuingia, lakini aliwaza sana namna ya kumuingia, hakuwa na hadhi ya kutoka na Levina.

****

“Mambo Deo?”

“Poa Levina, mzima?”

“Nipo poa!”

“Za nyumbani?”

“Salama kabisa.”

“Ngapi leo?”

“Pima kilo kumi!”

“Wewe kwani mna sherehe?”
“Hapana ni bajeti tu!”

Deo akapima mchele alioagizwa, akamimina kwenye mfuko na kumkabidhi Levina, aliyeupokea huku akiachia tabasamu mwanana kabisa.
“Ahsante sana Deo!”

“Nashukuru pia!”

“Samahani Deo, naweza kupata namba zako za simu?” Levina akamwuliza.
“Simu?”

“Ndiyo!”
“Mimi sina, labda nikupe namba za nyumbani!”

“Hapana, nataka namba zako mwenyewe!”
“Sina.”
“Kwanini?”
“Maisha Levina!”

“Ok! basi chukua zangu...ukimaliza kazi zako nipigie kwenye kibanda cha simu, nahitaji kuzungumza na wewe!”

Levina akasema akiandika namba na kumkabidhi Deo akiambatanisha na noti ya elfu tano.

“Ahsante sana Levina, nitakupigia!”
“Usiache tafadhali, ni muhimu sana!”
“Sawa.”

Levina ni nani hasa?

Anataka kumwambia nini Deo?

Fuatilia..
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom