SoC02 Sote tuwajibike ulinzi wa miundombinu

Stories of Change - 2022 Competition

Abeida

Member
Jul 14, 2022
13
7
Abeid Abubakar

Asubuhi moja mwaka huu namuona utingo wa lori lenye tela, akihangaika kuvuta kibao kilichowekwa barabarani kuashiria kuwa hapo kuna kituo cha abiria.

Lengo lake ni kukipindisha ili dereva wake aweze kukata kona eneo hilo ambalo kwa hakika barabara yake ni ndogo kwa gari hilo kupita.

Ninapomtazama kijana huyu na anapopigiwa kelele na watu jirani, anaacha shughuli yake, akimwachia dereva wake akihangaika kulipitisha lori hilo katika barabara hii ya mtaani ambayo kwa hakika isingetarajiwa aina ile ya gari kupita hapo.

Hili ni tukio moja kati ya mengi ambayo nimeshuhudia kwa malori makubwa kupita katika barabara za mtaani ambazo naamini hazina uwezo wa kuhimili uzito wa magari hayo ambayo aghalabu huwa yamebeba shehena hasa za bidhaa kama nafaka na saruji.

Kwa sababu ni makubwa na barabara zetu nyingi za mtaani ni finyu kieneo, kinachotokea ni uharibifu wa miundombinu katika maeneo mengi. Ni mazoea ya kila siku, lakini hakuna hatua zozote zinazooonekana kuchukuliwa na mamlaka husika.

Ni miundombinu inayojengwa kwa mabilioni ya fedha ya walipa kodi, lakini ni sisi wenyewe tunaoihujumu. Kibaya zaidi hakuna anayejali si wananchi wala mamlaka zinazosimamia barabara.

Jirani tu na niliposhuhudia na tukio hili la lori mitaa ya Ukonga jijini Dar es Salaam, kuna barabara ya Chunge iliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kutoka makutano ya Gongo la Mboto kuelekea Markazi hadi Kota.

Barabara hii pamoja na uzuri wake unaonakshiwa na uwepo wa taa zinazoendeshwa kwa nishati ya jua, lakini sasa uzuri huo unakaribia kutoweka. Nguzo za taa zinaharibiwa, baadhi zimeanguka, nyingine ziko katika wakati mgumu kwa sababu ya kukumbana na masaibu ya watumiaji wasiojali.

Unabaki unajiuliza miezi inapita nguzo zimeharibiwa, hakuna ukarabati wowote. Ni dhahiri kuwa hakuna ufuatiliaji na usimamizi wa miundombinu hii.

Unaweza kujionea picha ya nguzo hiyo niliyoipiga hivi karibuni kuonyesha namna tusivyojali miundombinu yetu. Nguzo hiyo inaeeleka sasa kudondoka na ipo hivyo kwa miezi mingi hapo.

Wako wapi watendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), wako wapi watendaji wa manispaa, halmashauri, serikali za mitaa?

Hawa ndio watu ambao nadhani wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kufuatilia uharibifu unaofanywa kwenye miundo mbinu.

Ikiwa barabara ina shimo dogo lakini linaachwa mpaka linakuwa kubwa na hatimaye kuwa kero kwa watumiaji; hii ni dalili kuwa watendaji wa mamlaka zinazosimamia barabara hawajali majukumu yao. Pengine hawana utaratibu wa kufanya ukaguzi wa miundombinu.

Inawezekenaje kukawa na ukaguzi, halafu shimo dogo likaachwa hadi kuwa shimo kubwa na kuwa kero kwa watumiaji wa barabara?

Au inawezekanaje nguzo ya taa kuangushwa na ikabaki hivyo kwa miezi nenda rudi? Huu ni uzembe uliofurutu ada.

Tuna maofisa walizoea kukaa ofisini wakipulizwa na upepo wa kutoka kwenye viyoyozi. Hawana habari kuwa majukumu yao ni pamoja na kufuatilia miundombinu, ili pale panapoibuka tatizo, wawe wa kwanza kulifuatilia na kutoa ufumbuzi.

Nguzo hizi za taa katika barabara niliyoitaja hapo awali, zimeharibiwa kwa miezi mingi, hazijafanyiwa matengenezo.

Hii ni ishara kuwa barabara hiyo pamoja na uzuri wake na fedha zilizomwagika hapo, hakuna anayeithamini, hakuna ukagauzi wa kujua barabara hiyo inaendeleaje.

Ukaguzi ungekuwapo, nguzo hizi zingeshughulikiwa mapema. Kinachonisikitisha nimewahi kuwasiliana na aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri ambaye sasa amesimamishwa. Pamoja na kuniahidi kuwa angelifanyia kazi suala la taa hizo, hakuna kilichofanyika mpaka anatoka ofisini.

Kwa upande mwingine, najiuliza upi wajibu wa viongozi katika ngazi za mitaa, kata, tarafa na nyinginezo. Nguzo hizi zimefanyiwa uhuni sio hewani, zimefanyiwa uhuni katika barabara ambayo watendaji hawa wanapita kila siku. Wamechukua hatua gani angalau kuripoti kwa mamlaka husika?

Hivi serikali za mitaa zina majukumu gani kama sio pamoja na kufuatilia usalama wa maeneo husika? Hivi hawajui kama usalama huo ni pamoja na barabara na matumizi yake.

Inawezekanaje mtaa wako umependelewa kwa kujengwa miundombinu iliyo bora, lakini viongozi wanashindwa kuilinda? Tutaamka lini Watanzania na kuanza kujali vitu vyetu tulivyojenga kwa gharama kubwa?

Hebu tutazame leo hii namna malori yanavyoharbu barabara zetu, Tanroada wapo, mamlaka nyingine za kiserikali zipo, lakini madereva wanaachwa wakitamba huku kila siku wakiharibu barabara zetu.

Kingo za barabara, alama za barabara katika maeneo mengi zimeharibiwa na madereva, lakini hatuoni jitihada zozote zinazochokuliwa na wahusika. Na wanawezaje kuchukua hatua ikiwa wanashindwa kufanya ukaguzi wa miundombinu hiyo?

Tufanyeje?

Moja nishauri Tanroads iwe na desturi makini ya kukagua barabara zake mara kwa mara.

Watendaji wanapojifungia ofisini kwa muda mrefu, ndipo hata kunapotokea tatizo barabarani, inachukua muda mrefu kulishughulikia

Kwa mfano, kunaweza kukawa na shimo dogo tu barabarani, lakini kwa kuwa wahusika hawakagui na kuligundua, baada ya muda shimo hilo linageuka kuwa handaki na hivyo kusabaisha usumbufu zaidi kwa watumiaji wa barabara. Wakala lazima uamke kwa hili.

Lakini pia ni wakati sasa mamlaka ya ulinzi wa miundombinu yetu ikakasimiwa hata kwa serikali za mitaa ambazo ndizo zilizo karibu na miundombinu.

Kupitia kamati za mitaa kuwe na timu maalumu ya wajumbe ambao moja ya majukumu yao itakuwa kukagua hali ya barabara zetu na kisha kutoa ripoti kwa mamlaka husika kama vile Tanroads, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (Latra) na hata Wizara mama ya Ujenzi na Uchukuzi.

Pili, tufike hatua sasa miundombinu yetu ilindwe kiteknolojia ili kubaini wanaofanya uharibifu kisha kuchukuliwa hatua ikiwamo ya kulipishwa. Picha ya Julai 25, 2022 gazeti la Mwananchi ukurasa wa 11, imenisikitisha mno. Inaonyesha kingo za daraja letu la kisasa la Tanzanite jijini Dar es Salaam, zikiwa zimegongwa. Kwa daraja nyeti kama hili, nadhani matumizi ya teknolojia hasa taa za usalama ni muhimu ili kubaini wahusika wanaochafua mandhari mazuri ya daraja.

Aidha, ni wakati sasa wa kuwa na mabalozi wa ulinzi wa moundombinu yetu kama ilivyo kwa mabalozi wa usalama barabarani ambao wakiona jambo la hatari wanawasiliana. Mamlaka zinazozimamia miundombinu zinaweza kukopa mfumo huu wa mabalozi na kuwa na mtandao wake wa kupea taarifa dhidi ya uharibifu wowote.

Kwa upande mwingine, ulinzi wa miundombinu hii unabaki pia kuwa wajibu kwa kila mwananchi. Unapoona walakini mahala toa taarifa kwa wahusika kama mimi nilivyomtaarifu mkurugenzi wa jiji lakini akashindwa kuchukua hatua mpaka nimefikia hatua ya kutumia maandishi kama njia ya kufikisha ujumbe kwa wahusika.

taaban nguzo.jpg


Mwandishi ni mkazi wa Dar es Salaam. Anapatikana kwa simu barua pepe: abeidothman@gmail.com
 
Back
Top Bottom