Soko la Uhindini Mbeya lawaka moto

Soko la Uhindini Mbeya lawaka moto

Soko kuu Mbeya lateketea kwa moto.

SOKO kuu la Uhindini jijini Mbeya, limeteketea kwa moto na kusababisha vilio, simanzi na watu kadhaa kujeruhiwa, huku baadhi yao wakipoteza fahamu baada ya mali zao za mamilioni ya fedha kupotea.
Wakati baadhi ya mali zikiteketea, inadaiwa baadhi ya askari polisi waliofika katika eneo la tukio kwa lengo la kulinda usalama na mali, waligeuka na kuanza kujihusisha na vitendo vya uporaji, wakishindana na vibaka waliotumia nafasi hiyo kuiba na kupora kiasi kikubwa cha mali zilizookolewa.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, waliofika mapema baada ya tukio hilo kutokea, walidai kuwa moto huo ulianza majira ya saa 2:00 usiku, ambapo moja ya kibanda kilichokuwa kikitumiwa na dobi ndicho kilianza kuwaka moto kabla ya kushika kasi na kuteketeza nusu ya vibanda katika soko hilo.

Mwandishi wa habari wa Tanzania Daima, alishuhudia magari mawili ya kikosi cha zimamoto cha Halmashauri ya Jiji la yakifika mapema katika eneo la tukio, lakini hayakuweza kuzuia kasi hiyo ya moto baada ya kudaiwa kufika hapo yakiwa hayana maji ya kutosha.

Mbali na hilo, baadhi ya mashuhuda hao walisema, licha ya kikosi cha zimamoto kukosa vifaa, miundombinu mibovu ni moja ya vikwazo ambavyo vilisababisha kushindwa kukabiliwa kwa tukio hilo la kuungua kwa soko la Uhindini, ikiwa ni tukio la pili la kuungua kwa soko kubwa ambapo mwaka 2006 soko la Mwanjelwa jijini hapa nalo liliteketea kwa moto na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi milioni 800.

Wakati moto huo, ukiendelea kuteketeza mali za wafanyabiashara hao, ambao wengi walionekana kuchanganyikiwa usiku huo wa tukio, kundi la vibaka lilivamia eneo hilo na kufanya uvunjaji wa vibanda na kupora mali.

Licha ya polisi kupiga mabomu kwa lengo la kuwatawanya vibaka hao, bado walionekana kuzidiwa na kuruhusu kiasi kikubwa cha mali zilizookolewa kubebwa na vibaka hao.

Tukio la vibaka lilionekana kama sinema, kwani baadhi yao walifika na magari na kujifanya wasamalia wema mbapo waliwataka wenye mali kujaza mali zao ndani ya magari hayo kwa lengo la kuwasaidia kuziondoa katika eneo la tukio, lakini cha ajabu punde gari lilipoonekana kukaribia kujaa waliondoa na kuwaacha wenye mali wakiangua vilio.

Mwenyekiti wa soko hilo, Emily Mwaituka, alipozungumza na gazeti hili, alisema soko hilo lina jumla ya vibanda na maduka 1000 ambapo katika tukio hilo, nusu ya vibanda hivyo viliteketea kwa janga hilo moto.

Baadhi ya wananchi wa jiji hilo, waliozungumza na Tanzania Daima walishangazwa na tukio hilo la moto kutokea kipindi kinachofanana na tukio la namna hiyo la kuungua kwa soko lingine la mjini hapo la Mwanjelwa, ambalo liliungua Desemba 2, 2006.

Miongoni mwa magari yaliyoonekana yakipakia bidhaa kwenye maduka mbalimbali ni T 543 aina ya Nissan Patrol, T432 AEF, T 256 AEM, T 822, AGX, T 643 AMS aina ya Center, T 373 BBB aina ya Center, T257, ACK na T 695 ATS.

Tanzania daima 03/12/2010.

Pia soma: Soko la Kariakoo lateketea kwa moto
 
Back
Top Bottom