TANGAZA MGOGORO WA KIKATIBA
 Hutuba ya Mhe. Seif Sharif Hamad
 Aliyoitowa Uwanja wa Malindi Zanzibar 11/12/1994
Mheshimiwa Katibu Mkuu,
Waheshimiwa Viongozi,
Waheshimiwa Wanachama na Wananchi,
Ningependa niungane na Katibu Mkuu kukushukuruni wananchi muliofika hapa kwa wingi leo, ili kuja kuyasikiliza yale ninayoamini yanatukera sote.
Waheshimiwa; mkutano huu siyo mkutano wa kawaida. Huu ni mkutano wa maombolezi. Tunaomboleza kuteketezwa kwa Serikali na nchi yetu. Tunaomboleza kwa kuwa kuna dalili zinazoonyesha njama za Julius Kambarage Nyerere za kuhakikisha kuwa Zanzibar inatoka kwenye ramani ya Dunia. Inaonekana kama hatukukazana atafanikiwa.
Kwa hivyo, wananchi wa Zanzibar hatuna furaha, tuna majonzi, tuna masikitiko makubwa sana. Lakini tunaomba majonzi hayo na masikitiko hayo tuyageuze kuwa ndiyo silaha ya kuitetea Zanzibar yetu.
Waheshimiwa; nitajaribu kueleza kwa kifupi nini kimetokea katika siku hizi za karibuni. Hivi karibuni katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumewasilishwa mswada wa marekebisho ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungao. Katiba ile ilitungwa mwaka 1977, hadi sasa tayari yamekwishafanywa marekebisho 11. katiba ya Marekani imetungwa karne 2 nyuma, hadi sasa wamefanya marekebisho yasiozidi 6. Sisi chini ya miaka 30 yameshafanywa marekebisho 11. hiyo pekee itoshe kuona aina ya katiba uliyonayo Mtanzania. Inatiwa viraka tu.
Juzi Bunge lilipelekewa marekebisho ya katiba ya 11. yamo mambo mengine mule (katika Katiba) lakini moja ambalo linamkereketa na kumuuma kila mwananchi wa Zanzibar, ni hili ambalo linatamka kwamba Rais wa Zanzibar asiwe tena Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hilo ndilo kubwa katika rekebisho liliofanywa juzi (katika Bunge).
Badala yake, eti kwa kutumia kisingizio cha vyama vingi, ni kwamba kila mgombea awe na mwenza. Kila chama kisimamishe mgombea na mwenza. Ikiwa mgombea anatoka bara mwenza atoke visiwani, na akichaguliwa Rais, yule mwenza moja kwa moja anakuwa Makamo wake. Ndivyo sheria hiyo inavyosema.
Kabla ya sheria hiyo au mapendekezo hayo kuwasilishwa katika Bunge tulisikia vishindo vingi hapa Zanzibar. Tunasikia minongono kuwa Rais Salmin Amour wa Zanzibar hakubali. Tukashuhudia Wabunge kutoka Zanzibar wanafanya mikakati kukataa suala hilo. Wakaitwa kwenye Afisi Kuu ya CCM tukaambiwa wameshapewa mkakati waende wakapinge mswaada huo.
Ndipo Dokta Omar Ali Juma, Waziri Kiongozi akathubutu kusema kwenye mkutano wa hadhara Mfenesini kwamba wananchi musiwe na wasi wasi, musikubali fitina na chokochoko za hawa. Sisi ni wafupi lakini uwezo wa kuitetea Zanzibar tunao. Akasema Dokta Salmini hayupo peke yake katika hili. Sote tupo pamoja naye. Kwa hivyo wananchi musiwe na wasi serikali yenu ipo, na hatukubali hatukubali Hatukubali. Hivyo ndivyo alivyosema Dokta Omar Ali Juma kwa waliomsikia.
Mimi nilimsikia vile vile kwenye Televisheni. Wenzangu wakasema mara hii Serikali ya Zanzibar imekusudia. Mimi nikawambia ingalikuwa kuwakandamiza CUF Basi ahadi ile ingalikuwa ni kweli. Ingalikuwa ni kufukuza watu kazi ahadi ya Omar ingalikuwa ni kweli. Ingalikuwa ni kutoa amri ya watu watiwe ndani ahadi ya Omar ingalikuwa ni kweli. Nikawambia, kwa suala la kutetea maslahi ya Zanzibar mutaona wenyewe.
Nasikia mara hii Wabunge wa Zanzibar hawakupita hata Dar es Salaam, wakaletewa ndege hapa hapa, wakapelekwa moja kwa moja Dodoma, mkakati huo, ili wasipite Dar es Salaam wakaharibiwa mawazo. Nikasema mambo makubwa mara hii. Nini kilichotokea Dodoma.
Waheshimiwa; kwanza katika mwezi huu wa Oktoba iliyopita, Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilichapisha katika gazeti Rasmi la Tanzania, mswada wa kufanya marekebisho ya sheria hiyo. Yule aliyetoa notisi ya kuchapishwa na kutangazwa ni Paul Rupia, ambaye ni Katibu wa Baraza la Mawaziri, ndiyo kusema kuwa mswada huo ulikuwa umeshakubaliwa na Baraza la Mawaziri.
Mheshimiwa Salmini Amour Juma akiwa ni Makamo wa Pili wa Rais, yeye moja kwa moja ni Mjumbe wa Kebineti, kwa hivyo alikuwa ANAUJUA, mswaada huo.
Baada ya kuweka mkakati hapa, nadhani Mheshimiwa akamuomba Rais Mwinyi, kwamba Wazanzibari hawajaridhika na mswaada huo. Tunaomba tuujadili upya. Mwinyi kwa sababu anasikilizana sana na Mheshimiwa Salmini akamkubalia ombi lake. Kwa hivyo, Rais Mwinyi akaitisha tena Baraza la Mawaziri. Wakakutana tena kwenye kebineti yao. Wakalizungumza tena. Wabara wakashikilia msimamo wao ule ule, kuwa rais wa Zanzibar asiwe Makamo wa Rais.
Mheshimiwa Salmini akajiona labda peke yake akasema mimi nimeshafahamu jamani lakini naomba tukutane na Baraza langu la Mapinduzi tulizungumze kwa pamoja. Mwinyi akamkubalia. Baraza la Mapinduzi likachukuliwa mbio mbio likapelekwa Dodoma. Wakakutana Baraza la Mawaziri na Baraza la Mapinduzi. Nasikia ulikuwa mkutano wa pata shika, vidole machoni, kejeli na kutukana. Wote hao ni wana CCM.
Baraza la Mapinduzi, nasikia wakashikilia kwamba lazima Rais wa Zanzibar aendelee kuwa Makamo. Baraza la Mawaziri la Muungano likasema hilo haliwezekani. Rais mwenyewe kama ndiye mwenyekiti wa kikao akajidai kuwaunga mkono Wazanzibari. Nasema akajidai, mimi siamini kwamba kwa kweli alifanya kwa dhati ya moyo wake. Rais Mwinyi alijidai kuwaunga mkono Wazanzibari. Wazanzibari wakacheza ngoma kuwa wameshinda.
Sasa akatakiwa Waziri wa Sheria na Katiba Samuel Sitta abadilishe mswaada apeleke mbele ya Kamati ya Bunge na Sheria mswaada uliobadilishwa kwamba Rais aendelee kuwa Makamo.
Mara nyingi kabla ya mswaada haujaenda kwenye Bunge ni lazima upitiwe na Kamati yake (sheria na Katiba). Kwa sababu mswaada huu ulihusu Katiba basi ni Kamati ya Sheria na Katiba ya Bunge.
Wanakamati hawa wakiongozwa na Mbunge Marmo wakakataa kujadili mswaada huo. Wakasema haiwezekani. Ikawa mvutano baina ya Sitta kwa upande mmoja na Kamati ya Bunge kwa upande wa pili. Suala likamfika Spika wa Bunge Mheshimiwa Pius Msekwa. Msekwa akawambia kwa mujibu wa kanuni za Bunge mswaada unaofaa kufikishwa kwenye Kamati ni ule uliochapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali. Kwa hivyo kamati ijadili mswaada ule.
Ikiwa Waziri anataka kufanya marekebisho, afanye wakati wa kuwasilishwa kwenye Bunge. Kwa hivyo Kamati ikafanya kazi hiyo. Wakati kamati inafanya kazi hiyo, Waziri Mkuu akajaribu kutafuta mawazo ya Wabunge wa Bara.
Kwa hivyo akawaita Wabunge, Wakuu wa Mikoa na Mawaziri wa Bara, kutaka msimamo wao. Mawaziri wakamwambia kinaga ubaga, sisi katu hatukubali kuunga mkono mswaada unaosema kuwa Rais wa Zanzibar aendelee kuwa Makamo. Wakamwambia kuwa watendelea kuwaunga mkono Wabunge wa Bara kaika jambo hili. Kwa hivyo mswaada haupiti.
Baada YA Mallecella kuambiwa hivyo yeye na Kolimba wakaenda moja kwa moja kwa Rais huko Chamwino. Wao (Malecella na Kolimba) wakamueleza Rais kuwa, hali ni ngumu na kwamba Wabunge wa Bara, Wakuu wa Mikoa na Mawaziri wa bara wanashikilia msimamo wao kuwa Rais wa Zanzibar asiwe Makamo wa Rais. Kwa hivyo, kama tutalazimisha mswaada huu upite, basi tutashindwa na itabidi tulivunje Bunge. Ndiyo hapo ulipopangwa mkakati mpya.
Ikakubalika kuwa atafutwe Rais Salmini na ambiwe kuwa ilivyokuwa yeye ni mwana CCM basi lazima akubali mswaada huo wa kutaka Rais wa Zanzibar asiwe Makamo upelekwe kwenye Bunge. Akaelezwa kuwa wao (Malecella na Kolimba) hawataki kusikia kuwa yeye (Rais Salmini ) na watu wake wanaupinga mswaada huo. Salmini akatishwa na kukumbushwa yaliompata Aboud Jumbe.
Rafiki yangu (Salmini ) akaanza kulegea, na haukupita muda Julius Nyerere akamwita Salmini mbele ya Rais Mwinyi na Daktari Omar Ali Juma. Nyerere akamwambia Salmini, unajua kuwa sisi tunazo taarifa za usalama na taarifa zetu za Usalama ni za kuwaminika kuliko zenu. Akaambiwa kuwa wewe kule Zanzibar huna Usalama kuna watu wanaokudanganya tu.
Salmini akaambiwa na Nyerere kuwa, maana ya mswaada ule ni kumlinda yeye (Salmini), kwa kuwa madaraka yote yanaondolewa kwa Rais wa Zanzibar na kuwekwa kwenye Serikali ya Muungano. Kwa hivyo, hata kama CUF waliamuwa kukushitaki wewe (Salmini) haitawezekana, kwani hata Polisi wataamrishwa wapuuze amri ya kukukamata. Salmini akakubaliana na maneno ya Nyerere.
Baada ya hapo Salmini akalazimishwa kuweka saini yake kwa vile aliambiwa kuwa haaminiki kwa sababu yeye ni kigeugeu. Salmini akaweka saini yake, kama watu walivyosikia. Hivyo ndivyo mambo yalivyotokea katika suala hili.
Baada ya hapo Salmini akawaita Wabunge wake na akawaeleza hali ilivyo kwa hivyo ule msimamo waliondoka nao Wabunge wote ukawa hauna maana. Kuna Wabunge wengine wakatishwa, wakaambiwa kuwa wakiwa hawataki gari zao na kazi zao basi wapinge mswaada ule. Wakatishiwa kufukuzwa. Kuna wengine waliahidiwa vyeo vikubwa zaidi na wengine wakaahidiwa kuwa wao watakuwa hao wenza. Inasemekana wengine walipewa fedha ili wakubali suala hili lishe.
Baada ya kuona hali ni hivyo, waziri Mkuu Malecella akatoa kauli kuwa suala hilo litamalizwa kidugu na kuhakikisha kuwa upinzani umekwisha. Kwa hivyo, mswaada huo ukawasilishwa kwenye Bunge. Ni kweli wabunge 88 walichangia mswaada huo (rekodi katika Bunge kwa mswaada mmoja kuchangiwa na Wabunge wengi kama hao).
Lakini ni kweli, ule upinzani ambao Wazanzibari mulidhani utakuwepo, uliyayuka kama mshumaa. Mswaada ule uliwasilishwa.
Wananchi, mpaka hivi sasa ni kwamba Makamo wa Rais ni wawili na hii ni kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri kifungu 47 mpaka 40, kwamba Makamo ni wawili; mmoja ni Rais wa Zanzibar na mwengine ni Waziri Mkuu. Vifungu hivyo sasa vimefutwa na badala yake kutakuwa na Makamo na huyu atatokana na mwenza. Pili; Rais wa Zanzibar anakuwa mjumbe moja kwa moja kwenye Baraza la Mawaziri.
Kwa hivyo, kukapigwa kura (katika Bunge) na Spika akatangaza kwamba mswaada huu unatakiwa uungwe mkono na theluthi mbili za Wabunge wote. Theluthi mbili za Wabunge ni Wabunge 167. wabunge waliounga mkono 186 na waliopinga ni Wabunge 5. ukijumlisha hesabu hizo, kama theluthi mbili ni 167, basi Bunge lote lina Wabunge 250. kama 186 waliunga mkono na 5 kuukataa maana yake ni kuwa Wabunge 191 ndiyo waliopiga kura zote. Wabunge 60 walikuwa wapi? Wabunge 60 hawakupiga kura.
Wananchi; lililotokea ni nini? Baada ya kuonekana mambo yanakwenda vizuri, Wabunge wengine walilaghaiwa na kuambiwa kuwa wao hawana haja ya kupiga kura. Wabunge wetu wengine wakarudi hapa Zanzibar.
Tunaambiwa walioukataa mswaada huo ni Wabunge 5, na mmoja wa Wabunge hao ni kutoka Kyela (Mkoa wa Bara). Kwa hivyo ni kuwa kuna Wazanzibar walioupinga mswaada huo ambao ni Wabunge 4 tu. Mswaada huo ulipita kwa hadaa, kwa sababu utaratibu ulivunjwa kwa makusudi.
Katiba ya Jamhuri ya muungano kifungu 98 (2), kinasema kwamba, mambo ambayo kupitishwa kwake ni lazima yaungwe mkono na Wabunge wasiopungua idadi ya theluthi mbili ya wabunge wa Tanganyika (au Tanzania Bara) na theluthi mbili ya Wabunge wa Zanzibar, ni yale mambo ambayo yataathiri madaraka ya Serikali ya Zanzibar.
Mswaada huo unaathiri madaraka ya Zanzibar, kwa sababu unamvua madaraka yake rais wa Zanzibar katika Serikali ya Muungano. Kifungu hicho 98(2) ilibidi kitumike. Wabunge wa Zanzibar peke yao waulizwe na wapatikane. Wabunge wa Bara pia waulizwe peke yao na wapatikane theluthi mbili kwa kila upande. Hapo tu ndiyo mswaada huo ungalipita kihalali.
Wabunge wa Zanzibar walikuwa wanao uwezo wa kuuzuia (blocking power) mswaada huo, kwa sababu Wabunge wa Zanzibar katika Bunge wapo 77. theluthi moja ya Wabunge hao wa Zanzibar ni Wabunge 26. kwa hivyo kama wangalitokea Wabunge 27 tu, wakasema kuwa hawautaki mswaada basi usingalipita, kwa sababu theluthi mbili zingalikuwa hazikutumia.
Kwa hivyo, kama Wazanzibari wangalikuwa macho mswaada usingalipita kabisa; Wazanzibari wangalisema tu , Bwana Spika; ni lazima Watanganyika waulizwe mbali na Wazanzibar waulizwe mbali. Ndiyo matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini Wabunge wetu hawakufanya hivyo.
Kwa kweli kama Wabunge wa Zanzibar wangalikuwa na maslahi ya Zanzibar na wana msimamo, wangalitokea Wabunge 27 tu au 28 wangaliuzuia mswaada.
Wabunge wetu wa Zanzibar walishindwa kufanya hivyo na matokeo yake ni kuwa Rais wenu wa Zanzibar anakuwa ni Meya tu. Baraza la Mawaziri na Baraza la Wawakilishi ni Madiwani tu, hawana uwezo wowote. Hii ni kwamba ule uwezo na mamlaka ya Ki nchi yanaondoka Zanzibar. Huo ndiyo ukweli wa mambo yalivyo. Kitendo hicho siyo kwamba kinamdhalilisha Rais wa Zanzibar tu, lakini kinaidhalilisha Serikali ya Zanzibar.
Kazi yao hivi sasa (Mawaziri na Serikali ya Zanzibar) ni kuangalia mambo ya afya na kuangalia mambo ya elimu ya msingi na hawana zaidi ya hapo.
Hivi juzi, siku ya Alhamisi tarehe 8/12/94, Dokta Salmini aliitisha mkutano wa viongozi (Wabunge wa Zanzibar, Wawakilishi na Viongozi wa Chama CCM na wa Serikali). Wazanzibar sote tulikuwa na hamu kubwa ya kusikia nini kiongozi wetu atatwambia. Ametwambia mambo matatu.
Jambo moja la kwanza; Salmini anasema kuwa Serikali ya Zanzibar haikushirikishwa katika suala hili. Mimi nasema pengine ni kweli. Ukichukulia kwamba Baraza la Mapinduzi na Baraza la Wawakilishi hayakushirikishwa. Ukichukulia kwamba Mwanasheria wa Zanzibar pengine hakushirikishwa kwenye suala hili. Hapo unaweza kusema kuwa Dakta Salmini yuko sahihi.
Lakini si kweli kuwa yeye Dokta Salmini alikuwa hajui, kwa sababu suala hili si jipya. Miaka miwili nyuma Rais Ali Hassan Mwinyi aliteua Tume chini ya uongozi wa Marka Bomani. Tume hiyo ilikuwa na kazi moja tu, yaani kutafuta mfumo huu, ambao ni huu wa kumfanya Rais wa Zanzibar asiwe Makamo wa Rais wa Muungano. Mfumo huu (mapendekezo ya Bomani) ukafikishwa kwenye Kamati Kuu ya CCM na Halmashauri Kuu ikaujadili, na walipingana juu ya mfumo wa kumpata Makamo wa Rais. Mwisho walikubaliana kuwa wapeleke kwenye Bunge mswaada wa kumpata Rais peke yake na hili la Makamo waliahirishe kwa miaka 2. Tangu wakati huo Mheshimiwa Salmini analijua.
Hivi juzi tu, Julius Nyerere alipotoa kitabu chake alilizungumzia kwa uzito wote. Nyerere alisema kuwa viongozi hawa wameshindwa hata kumpata Rais na Makamo na kwamba utaratibu ulikuwa mzuri. Mimi nimeshawambia wafuate utaratibu huu bado wanapinga anasema Julius Nyerere. Katika kitabu chake.
Kwa hivyo wakakutana tena kwenye Kamati Kuu wakakubaliana kuwa wapeleke mswaada huo kwenye Bunge mara hii. Hoja hiyo ikapelekwa kwenye Baraza la Mawaziri, ambalo Salmini ni mjumbe. Hata tuseme kuwa siku hiyo Salmini hakuwepo. Lakini mimi naamini kuwa kila mjumbe wa Baraza hilo la Mawaziri anapelekewa nyaraka za mambo yatakayozungumzwa kwenye Baraza hilo. Kwa hivyo, hata kama mjumbe anakuwa hayupo basi atajua nini kinazungumzwa kwenye Baraza hilo. Kwa hivyo, tulitazamia kuwa yeye (Salmini) angaliwaambia wenziwe kwamba suala hili vile vile liingizwe kwenye mambo yatakayozungumzwa. Wewe (Salmini) si ulikuwa ukijua, kwa nini hukushikilia kwamba Serikali ya Zanzibar ijulishwe. Maelezo hayo ya Salmini ni ya kitoto.
Pili; Mheshimiwa Salmini, katika maelezo yake anawatoa wasiwasi Wazanzibari musiwe na wasi wasi Serikali yenu ya Zanzibar ipo na akasema pengine hata serikali ya Muungano itakuwepo. Sasa hii pengine maana yake nini? Kitandawili hicho.
Wananchi; mimi nasema suala siyo kuwepo jina la Zanzibar. Jina linaweza kuwepo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Lakini Jee ina madaraka gani? Wazanzibari wanataka kujua madaraka ya serikali yao, siyo jina la Serikali ya Zanzibar. Hilo ndilo suala ambalo Mheshimiwa Salmini angalitwambia kwamba Serikali yetu itakuwepo na madaraka yake yatakuwa haya na haya. Lakini itakuwepo tu unadhani Wazanzibari wataridhika kuwa na Baraza la Mji. Hawataridhika hata siku moja. Hawataridhika kuwa na Meya. Hawataridhika Wazanzibar!
Tatu; alilolisema (Salmini) eti kuomba Serikali ya Zanzibar na Rais apewe mamlaka ikiwepo Polisi na kwamba kikao cha Bunge cha Mwezi February kitafafanua yote hayo.
Sasa tunamwambia, Mheshimiwa Salmini kwamba, kwanza ameomba na anayeomba anaweza akapewa au asipewe. Kwa hivyo, hapo hukuondoa wasi wasi wa Wazanzibari. UNAOMBA, tena kinyonge!!! Wewe Salmini una dola, unaomba? Unaomba nini? Hapa kila siku munatwambia kuna dola. Dola hiyo ya kuwakandamiza wana CUF tu, ndiyo kazi yake?
Pili; Mheshimiwa Salmini kasema kwamba Bunge litaeleza utaratibu mzima wa mambo ya itifaki (Protocol) ya uhusiano wa mambo ya nje na mambo mengine.
Mimi nasema, jambo la msingi kuwa maelezo hayo ya Salmini kuwa ni ufafanuzi. Katiba imeshasema Serikali ya Zanzibar haina madaraka. Hiyo ndiyo sheria mama, hayo mengine yote ni ngonjera. Mimi naichukulia kauli hiyo ya Salmini kama kauli ya kujinawa uso.
Mtakumbuka kwenye suala la OIC, Mheshimiwa Salmini alitikisa vibiriti na akasema (kuwambia wabunge wa bara) kwamba musitikise vibiriti. Salmini akaitwa Butiama na akatolewa ukali mmoja tu. Akaja hapa na akawaita watu wote na akawambia kuwa Zanzibar imejiondoa kutoka katika OIC. Kwa maelezo yake akasema tumejiondoa kuipa nafasi Serikali ya Muungano kutafuta uwezekano wa kujiunga. Tangu wakati ule mumesikia nini juu ya Serikali ya Muungano kujiunga na OIC?
Nyerere katika kitabu chake alisema kuwa yeye aliichukulia kauli ile ya Salmini ni kuwa (face washing device) kauli ya kujinawa uso tu. Hii ya juzi pia ni kauli ya kujinawa uso kwa Wazanzibar. Kama angalikusudia, angalisema kama ni hivyo, basi taratibu zitumike kwenye katiba hivi sasa, kwenye marekebisho haya ya 11. Hatutazamii kuwa Bunge hilo litafanya marekebisho ya 12 hapo Februari. Utakaotokea ni utaratibu tu.
Waheshimiwa; Salmini anatufanya watoto wadogo na mazungumzo yake ya juzi hayakusaidia chochote ila yameongeza hasira za Wazanzibari. Matokeo ya kupitishwa kwa marekebisho hayo ni kuweka mchanga katika maiti wa Muungano. Muungano kwa Mujibu wa Sheria ya Zanzibar haupo. Iliyopo ni nguvu na magube.
Waheshimiwa; muungano huu ni baina ya nchi mbili Zanzibar na Tanganyika. Serikali ya Jamhuri ya watu wa Zanzibar na Serikali ya Watu wa Tanganyika, na zilitiliana mkataba tarehe 22/4/64 hapa Ikulu Zanzibar. Kwa niaba ya Serikali ya Tanganyika aliweka saini Julius Kambarage Nyerere na kwa niaba ya Zanzibar aliweka saini Mzee Abeid Amani Karume.
Wananchi; mkataba ule ni wa Kimataifa (International Treaty) baina ya nchi mbili. Mkataba ule ndiyo unaojenga mihimili ya Muungano. Muhimili mmoja wa muungano ule unaosema hivi kwamba haya makubaliano ambayo sisi Marais wawili tunaotia saini, yataweza kutumika na kuwa sheria katika nchi mbili zetu mpaka kwanza Bunge la Tanganyika, kwa upande wake na Baraza la Mapinduzi na baraza la Mawaziri kwa pamoja, wapitishe sheria, kila mmoja kwa upande wake kuyafanya makubaliano haya kuwa sheria. Hiyo ndiyo itakuwa Muungano huu umethibitishwa. Hicho ni kufungu cha (8) cha makubaliano hayo katika Articles of Union.
Tunao ushahidi kuwa Bunge la Tanganyika lilikutana na kupitisha sheria hiyo. Lakini hakuna ushahidi kuwa Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri la Zanzibar lilikutana na kupitisha sheria hiyo.
Mimi ninamchallenge Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar atutolee sheria hiyo ya Zanzibar kuthibitisha Muungano. Ninamtaka yeye na Waziri Kiongozi atwambie sheria gani. Hatutaki kumsikia Moyo (Hussan Nassor Moyo) akisema kuwa yeye alikuwepo wakati wa Muungano. Vipi jambo kubwa kama hili pasiwepo na sheria?
Wananchi; kilichofanyika tangu mwanzo ni hadaa na magube anayotufanyia Nyerere katika nchi yetu. Nyerere alimfanya yule Mwanasheria aliyeiandika Sheria ya Tanganyika ndiye aliyeiandika sheria ya Zanzibar. Penye Tanganyika alitia Zanzibar, na Penye Zanzibar alitia Tanganyika. Mzee Karume alitia saini bila ya sheria hiyo kupelekwa kwenye Baraza la Mapinduzi mpaka leo. Aliyekuwa mwanasheria wa Zanzibar wakati huo Bwana Dourado alikuwa shahidi.
Tangu awali Nyerere ameichukua nchi yetu kwa hadaa na nguvu si kwa mujibu wa sheria. Kwa hivyo, Muungano huu tangu awali ni BATILI.
Wanasheria wa Zanzibar simameni mutetee, Dr. Omar Ali Juma asimame atetee uhalali wa Muungano, Radio na Televisheni chambueni na mutwambie suala hili.
Tunasema kuwa si Muungano, kwa sababu sharti nambari (8) la makubaliano ya Muungano mpaka hii leo halijakamilishwa.
Kifungu nambari (7) cha Mkataba wa Muungano kinasema kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano akishirikiana na Makamo wake ambaye ni kiongozi wa Zanzibar, atateua Tume ya Kufanya mapendekezo ya Katiba Tume yenye Wajumbe kutoka Zanzibar na Wajumbe kutoka Tanganyika. Baada ya hapo Rais ataitisha mkutano wa Katiba, ambao wajumbe wake watatoka Zanzibar na Tanganyika. Mkataba unaeleza kuwa kazi hiyo ifanyike mnamo mwaka mmoja kuanzia tarehe ya Muungano. Tarehe ya Muungano ni tarehe 26/4/64, mwaka mmoja ulimalizika tarehe 25/4/65. Hata kama Zanzibar iliidhinisha lakini jambo la pili halikufanywa. Tume haikuundwa wala mkutano wa katiba haukuitishwa. Kilichofanyika, ni kuwa ilipofika tarehe 25/4/65, Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipitisha sheria ya kuwahirisha kuundwa kwa tume na kuitishwa kwa Mkutano wa katiba.
Wananchi; tunamhoji Nyerere na kuwa mkataba uliofanya Muungao ni (International Treaty) Mkataba wa Kimataifa baina ya nchi mbili. Katika mkataba huo, serikali moja mamlaka yake yalichukuliwa na Serikali ya Muungano na ikawa haipo (serikali ya Tanganyika ikawa haipo). Lakini Serikali ya pili (Serikali ya Zanzibar) ilibaki pale pale.
Lakini, kwa sababu mkataba huo ulikuwa wa Kimataifa sheria hiyo ya kuwahirisha ilibidi ifanywe na Bunge la Tanganyika, ambalo sasa ndilo hili la Muungano. Vile vile sheria hiyo ifanywe na Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri la Zanzibar, kwa wakati huo.
Ninamtaka Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Idi Pandu atwambie sheria nambari ngapi iliahirisha kuundwa kwa Tume ya kuwahirisha kufanya marekebisho ya katiba hiyo na kuitishwa mkutano wa katiba. Sheria hiyo imerekebishwa na upande mmoja tu. Nyinyi Zanzibar munakokotwa. Kwa hivyo tunasema Muungano ni BATILI.
Tunaambiwa mwaka 1977, munakumbuka, wakati wa kuunganisha TANU na AFRO. TANU na AFRO eti waliunda Tume ya Kufanya katiba ya CCM, iliongozwa na Mzee wetu Sheikh Thabit Kombo. Wajumbe wake walikuwa kina Sheikh Ali Mzee ALI, Sheikh Hassan Nassor Moyo na watu kama hao.
Upande wa pili unamkuta mtu aliyebobea kwa mambo ya Katiba, Pius Msekwa, Warioba na watu kama hao. Huku kwetu Nyerere alikataa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar asiingie kwenye Tume hiyo. Akawekwa Sheikh Thabit Kombo, hatumdharau Mzee wetu hyo kafanya mchango mkubwa. Lakini tukubali tusitake, mambo ya katiba ni mambo ya kisomi. Unatazamia nini kwa mambo hayo? Hiyo ilikuwa ni Tume iliyoundwa kuunda Katiba ya CCM.
Baada ya kumaliza hiyo, Nyerere akasema kuwa Tume hiyo ndiyo itakayokuwa na kazi ya kuunda Katiba ya nchi Aboud Jumbe akakubali. Kwa hivyo Tume ile ile ya akina Thabit Kombo kwa upande mmoja na Msekwa kwa upande mwengine ikafanya katiba ya mwaka 1977. Nyerere huyo huyo akasema badala ya kutafuta watu wengine wa kuunda mkutano wakatiba, basi Bunge hilo ndilo litakalokuwa mkutano wa Katiba. Tunazongwa tu.
Wananchi; kwa kweli mpaka leo sharti hili la kuundwa Tume ya kufanya mapendekezo ya kuunda Katiba ya Muungano na baadaye kuitishwa mkutano wa Katiba halijatekelezwa. Uhalali wa Muungano uko wapi? Hilo ni la pili.
Waheshimiwa; jambo la tatu, kifungu nambari (4) cha Mkataba wa Muungano kilitaja mambo 11 (kumi na moja) ya Muungano. Leo ukiiangalia katiba kwenye nyongeza kuna mambo zaidi ya 22 (ishirini na mbili). Haya mambo 22 yanatoka wapi? Hii ni kuvunja katiba, na wakati wote ni kuinyima Zanzibar uwezo na kuipa Bara uwezo. Hakuna kuipa uwezo Zanzibar. Mambo yote 11 (kumi na moja) ya nyongeza ni kinyume na katiba ya nchi.
Nimefurahi kusikia rafiki yangu Dakta Salmini kuwa alimuandikia barua Proffessor Shivji na kumwambia kuwa anamuunga mkono kuwa yale mambo 11 mengine ni haramu. Lakini Dakta Salmini alimalizia hapo tu, hakuchukuwa hatua nyengine ya kurejesha mambo hayo mikononi mwa Zanzibar.
Jambo la nne, ni hili la juzi; mkataba wa muungano kifungu cha (3) (b) kinaeleza wazi kwamba kutakuwa na Makamo wawili wa Rais, mmoja kati ya Makamo hao atakuwa ndiye kiongozi wa Serikali ya Zanzibar. Makamo huyu ndiye atakayekuwa msaidizi wa Rais wa jamhuri ya Muungano katika kutekeleza madaraka yake kwa Zanzibar. Ndivyo mkataba unavyosema. Hiii ilitafsiriwa katika katiba ya sasa kwa kuongezwa vifungu (47) mpaka (50). Tafsiri hiyo ina maana kuwa huyu Makamo mmoja siyo awe Mzanzibari tu, lakini awe Mzanzibari bila kuwa Rais wa Zanzibar?
Kubadilisha vifungu hivyo vya mkataba ni kwenda kinyume na katiba. Pia kifungu hicho kinasema kuwa Rais wa Zanzibar atakuwa ndiye Msaidizi Mkuu wa Rais wa Jamhuri kwa upande wa Zanzibar, kwa sababu ilionekana kuwa Muungano huu ndiyo wenye Majeshi, Polisi na mambo yote ya Kidola ndani ya Muungano. Kwa hivyo, ili kumpa uwezo Rais wa Zanzibar, ndiyo akafanywa moja kwa moja awe Makamo wa Rais na msaidizi wa mambo yote ya Muungano. Leo Rais wa Zanzibar anaondolewa na badala yake anawekwa Mzanzibari mwengine ili awe Makamo wa Rais.
Mimi ninawambia hawa kwamba hata huyo atakayechaguliwa mwenza (Makamo wa Rais) hatakuwa na kazi. Kwa mfumo wanaotaka wao Makamo wa Rais hana kazi. Kazi yake nini? Atumwe kwenda mahala fulani,kazi ya pili angoje Rais asafiri achukuwe kile kiti kwa siku mbili tatu. Hana uwezo wa kubadilisha mawaziri, hana uwezo wa kufanya maamuzi makubwa. Tatu angojee Rais afariki ili akamate madaraka ili amalizie kipindi cha Rais aliyefariki. Ikiwa Salmini unaambiwa utakuwa mwenza au wengine watakuwa wenza, utakuwa na madaraka uwongo. Hutokuwa na madaraka yoyote. Madaraka yote yatakuwa kwa Amiri Jeshi Mkuu (Commander in Chief) mmoja tu; (Rais wa Muungano).
Wananchi; huo ndiyo ukweli kwamba ilifanywa makusudi kubadilisha mambo. Kwa hivyo tunasema kuchukuwa hatua hiyo, maana yake maiti ni kumzika. Muungano Haupo Wananchi. Kutokana na Nyerere na magube yake Muungano ulivunjwa na TANU, ASP, na CCM na juzi Bunge lilifukia maiti.
Kwa mujibu wa sheria za Kimataifa, Muungano haupo, hivi sasa tunaendeshwa kwa nguvu za Nyerere na ulazima.
Wananchi; sasa tunajiuliza tufanye nini katika hali kama hii?
CUF tufanye nini na muda ni mfupi?
Kwanza: sisi CUF tunamwambia Mheshimiwa Salmini Amour Juma, Rais wa Zanzibar ikiwa unataka Wazanzibari wakuamini kwamba jambo hili wewe kweli hulitaki, hulipendi, tunakushauri; TANGAZA MGOGORO WA KIKATIBA. Tangaza! Serikali ya Zanzibar inao uwezo huo. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, kifungu (125) mpaka (128) vya katiba ya Jamhuri vinatoa uwezo kwa Serikali ya Zanzibar ama ya Muungano kuitisha Mahkama maalum ya Katiba.
Kwa hivyo njia ni hiyo ndugu yangu, rafiki yangu. Kama kweli hupendi basi tunakwambia Tangaza mgogoro wa katiba. Unaogopa nini?
Mimi nataka nikuhakikishie, tangaza tuone kama wataleta vifaru kuja kukuchukuwa. Tunakuhakikisha kuwa Umma usiozidi watu laki moja watazunguka Ikulu wasifike pale tunakuhakikishia. Kama kweli wewe ni mwananchi unataka kuzuia hili Tangaza mgogoro wa Katiba.
Wananchi; jambo la pili, tunalolikusudia kufanya kwa niaba yenu ni kumtaarifu msajili wa vyama vya siasa, kwamba kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa nambari (5) ya mwaka 1992, CCM imepoteza sifa ya kuwa chama halali katika nchi yetu. Ushahidi ni kwamba, kifungu (9) (2) (b) cha sheria hiyo kinasema Chama chochote ambacho kinataka kuvunja Muungano kinapoteza sifa ya kuwa chama cha siasa. Kwa hivyo, tunasema kuwa CCM wamevunja Muungano kifunge chama cha CCM!
Jambo la tatu tunasema kuwa CUF itawashawishi wananchi watano (5) wa kila wilaya ya Unguja na Pemba wafungue mashtaka dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Tunafungua mashtaka kwa kusema kuwa marekebisho yaliyofanywa na bunge yanakwenda kinyume na mkataba wa Muungano, kwa hivyo ni BATILI. Pili utaratibu uliotumiwa na Bunge katika kupiga kura ulikuwa si sahihi, kwa hivyo, uamuzi wao ni BATILI. Kwa hivyo, tunawaomba watu watano wajitokeze katika kila wilaya ili tuweze kufungua mashtaka dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Wao wanajua kuwa wamefanya dhulma, wamezungumza kwamba watakutana na Wanasheria wa Bara na Visiwani kuangalia vipi wataweza kwenda kujitetea katika Mahkama. Wanajua kuwa CUF hawatokubali. Wasema wao hawana hofu na mahkama Kuu ya Zanzibar, hawana hofu ya mahkama Kuu ya Tanzania.
Wananchi; sisi tutaanza hapa katika Mahkama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam, tutafungua mashtaka yetu. Tukishindwa tutakwenda kwenye Mahkama ya Rufaa. Tukishindwa tutakwenda katika Mahkama ya Kimataifa (International Court of Justice). Hizo hatua tutazichukuwa sasa. Tukiingia kwenye Serikali ikiwa mambo hayo hayakufanywa tunalosema ni nini.
Kwanza, Rais wetu abadan hatoingia katika Baraza la Mawaziri la Bara. Haingii!
Pili; mara moja tunayachukuwa yale mambo yote ambayo yameongezwa baada ya mwaka 1964, ambayo hayamo kwenye Mkataba wa Muungano. Moja kwa moja tunayarejesha Zanzibar kwa wenyewe. Tunawambia hilo walijue.
Tatu; ikiwa mpaka wakati huo (Salmini kashindwa kutangaza mgogoro wa Katiba) CUF wakati huo itatangaza mgogoro wa Katiba, kwa sababu Mahkama maalum ya Katiba ina wajumbe majaji walioteuliwa na Serikali ya Muungano sawa sawa. Hao watajadiliana. Tutafanya hivyo wakati huo, ikiwa bado hawajamaliza. Tutamtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wakati huo atimize masharti ya kifungu cha (7) cha Mkataba wa Muungano, kwa kufanya mapendekezo ya Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwa mazingira ya sasa, vyama vyote vya siasa na taasisi nyengine lazima washirikishwe. Pili, kwa sababu jambo hili ni baina ya Zanzibar na Tanganyika, wajumbe lazima wawe sawa Bara na Visiwani katika Tume itakayoundwa. Likimaliza hilo (Rais huyo wa jamhuri) atapaswa kuitisha mkutano wa katiba ambao sasa hivi utakuwa na wajumbe kutoka katika vyama vya siasa na taasisi zote nchini. Hapo tutakuwa tunatimiza masharti ya Mkataba wa Muungano.
Wananchi; sisi tunatambua kuwa kwa mfumo huu, Rais huyu (Rais wa Zanzibar ) kuwa Makamo ni tabu. Kwa hivyo tuheshimu mkataba kwa kuunda Serikali ya Zanzibar na Kuunda Serikali ya Tanganyika. Viongozi wake hawa wanakuwa pamoja katika Baraza la Uongozi, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano. Sehemu zote mbili zitashiriki katika Muungano. Tatizo la kutoweza kuheshimu Serikali zote mbili litamalizika hapo.
Endapo yote hayo watagomea, tutafanya lile ambalo halina budi kutendwa. Hatuvunji Muungano HAPANA. Kwanza, tutaunda Polisi yetu, tutaunda Uhamiaji yetu, tutaunda Forodha yetu na Fedha tutafanya sarafu yetu.
Tunamwambia Julius ikiwa utakuja kuvamia Zanzibar na majeshi yako Wazanzibari wako tayari kufa kwa hilo. Hatukubali nchi yetu kuuzwa. Mwisho wenu ni mwaka huu
Waheshimiwa; kwa kumaliza ninasema Wazanzibari tuache tafauti zetu. Tuungane tuinusuru nchi yetu.
Ikiwa Mzanzibari unataka Zanzibar ibaki na iendelee kustawi huna budi kuiunga mkono CUF. Ikiwa unataka nchi yetu (Zanzibar) ipotee kaa kwenye CCM
Nataka nimwambie Dokta Omar, wenzake na Nyerere kwamba HALITOTI.
Imetolewa na Kurugenzi ya haki za Binaadamu na mahusiano na Umma
Tarehe 10th Julay,2008
Zanzibar.
KHABARI NDIO HIYO