Slaa mpiganiaji haki na maslahi ya Watanzania

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,015
Posted Date::1/13/2008
Dk Slaa sasa aitwe mwongo au mzalendo? --Uchambuzi
Na Theodatus Muchunguzi
Mwananchi

BAADA ya Mbunge wa Karatu, Dk Wilborad Slaa kuhutubia mkutano wa hadhara Mwembe Yanga, Temeke jijini Dar es Salaam Septemba 15 na kueleza tuhuma za ufisadi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhusu ubadhirifu wa mabilioni ya walipa kodi, baadhi ya wanasiasa wastaafu na baadhi ya vigogo aliowatuhumu walijitokeza kukana tuhuma hizo na kumwita Slaa kuwa ni mwongo.

Baadhi yao walitishia kwenda mahakamani kumshitaki, ingawa hadi leo hii hakuna aliyediriki kufanya hivyo. Wengine walitoa kauli za kumkashifu. Kuna mtuhumiwa mmoja aliyewaambia waandishi wa habari kuwa Dk Slaa alikuwa anafanya kazi zisizomhusu kwa kuwa alikimbia utumishi wa Mungu.

Kabla ya kufikia hatua hiyo ya kuwataja hadharani watuhumiwa wa ufisadi katika BoT, Juni 25, Dk Slaa alitoa alitoa tuhuma nzito za ubadhirifu ndani ya BoT bungeni na kutaka aliyekuwa gavana, Daudi Ballali ajiuzulu. Wakati wa kikao cha bunge la bajeti, Slaa alitaka kuwasilisha hoja binafsi kuhusiana na ubadhirifu ndani ya BoT lakini Agosti 16 aliondoa hoja yake akidai kukosekana kwa nia njema.

Siku mbili baadaye Spika wa Bunge, Samwel Sitta alimtuhumu Dk Slaa kuwa alikuwa ameghushi nyaraka alizotaka kuzitumia dhidi ya BoT na kutishia kumshitaki. Kwa ujumla, Dk Slaa alipitia wakati mgumu sana wakati akijaribu kuhalalisha utafiti alioufanya kwa ushirikiano na baadhi ya viongozi wenzake wa upinzani, Hamad Rashid Mohamed na Tundu Lissu kuhusu.

Kimsingi, tuhuma za Dk Slaa, ambaye pia kuna wakati alizielezea kwa nchi wahisani zilichangia kwa kiasi kikubwa kuishinikiza serikali mwezi Septemba kuipa kampuni ya Ernst&Young kupitia hesabu za BoT katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kwa lengo la kubaini ukweli kuhusu ubadhirifu wa fedha.

Kwa ujumla kampuni ya Ernst & Young imebainisha kuwa ni kampuni makini yenye kudhihirisha kuwa inakidhi viwango vyote vya kimataifa kwa kuwa ilifanya kazi ya kupitia hesabu za akauti ya EPA kwa tija na ufanisi na kuikabidhi kwa kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh Desemba 23 na yeye kuikabidhi kwa Rais Jakaya Kikwete Januari 7.

Ukweli hatimaye umebainishwa na Rais Kikwete mweyewe wakati alipoitoa ripoti hiyo ya uchunguzi hadharani kwamba tuhuma zilizotolewa na Dk Slaa, aliyebezwa na kuitwa muongo na baadhi ya watu zilikuwa za kweli. Slaa alidai kuwa kiasi cha zaidi ya Sh 300 bilioni zilifujwa katika EPA, ingawa ripoti ya uchunguzi imebainisha upotevu wa Sh 133bilioni zilizchochotwa na kampuni 22.

Rais Kikwete mara moja ametangaza hatua mbalimbali kwa lengo la kurejesha imani ya wananchi kwa serikali yake na nchi na mashirika wahisani, ambao. Miongoni mwa hatua hizo ni kumfukuza Ballali, kuagiza ufanyika uchunguzi ili wamiliki wa kampuni na maofisa waliohusika kuchota fedha hizo washitakiwe na fedha hizo kurejeshwa ndani ya miezi sita.

Rais wetu amechukua uamuzi mzuri na wa busara lakini kuna baadhi ya mambo ambayo yanaacha mashaka kwa umma. Moja ni kutozungumziwa hatua za kinidhamu dhidi ya Ballali, ambaye ni mhusika mkuu, kwa kuzingatia kuwa ndiye aliyekuwa mtendaji na mwajibikaji kwa masuala yote yanayohusu BoT.

Hapa ninamaanisha kuwa Rais angeamuru gavana huyo wa zamani kuwekwa chini ya ulinzi popote aliko huko Marekani hata kama ni hospitalini ili ahojiwe na kufunguliwa mashitaka. Huyu ana taarifa nyingi na muhimu sana kuhusu mambo yote yaliyotendeka. Kama Ballali anakamatwa na kurejeshwa nchini umma utaweza kuelewa mengi.

Kwa mfano, tumeambiwa kuwa kampuni nyingi zilichotewa fedha bila kuwasilisha vielelezo muhimu kama anuani, usajili na mambo mengine. Hata kama taarifa muhimu zinakosekana, lakini Ballali kwa vyovyote vile wamiliki wake na taarifa zao na mambo mengine atakuwa anayaelewa vizuri.

Hapa nakubaliana na Slaa kwamba Ballali anapaswa kukamatwa na kupelekwa mbele ya sheria. Bila kumkamata Ballali na kumshitaki, baadhi ya wananchi wanaweza kubaki na mashaka kuwa amefichwa ili kuficha ushahidi muhimu.

Pili, kwa habati nzuri Katiba ya Tanzania inampa madaraka makubwa Rais Kikwete kama ya kuteua watumishi wa umma, kuwahamisha, kuwafukuza, kutumia miongozo mbalimbali ambayo ina nguvu za kisheria. Kwa hiyo anao uwezo kisheria kuwachukulia hatua mara moja watumishi wengine wa BoT ya kuwasimamisha kazi waliohusika kabla hata kuanza kuchunguzwa na vyombo vya dola.

Tatu, muda wa miezi sita uliotolewa na Rais Kikwete kwa vyombo vya dola kukamilisha kazi hiyo ni mrefu kulinganisha na kiasi cha fedha zilizopotea hivyo kuna uwezekano mkubwa baadhi ya wahusika; yaani wamiliki wa kampuni zilizohusika na watumishi wa serikali kutorokea nje.

Nne, kwa kuwa Dk Slaa alitoa tuhuma za ubadhirifu wa mabilioni ya fedha ndani ya BoT kwa upande wa ujenzi wa minara pacha, Kampuni za Meremeta na Mwananchi Gold, ingekuwa vizuri basi matumizi ya fedha hizo pia yakachunguzwa ili kubainisha ukweli huo badala ya kuishia kwenye EPA peke yake.

Tukio la tuhuma za ufisadi zilizotolewa na Dk Slaa ndani ya BoT na ukweli wake kubainisha upotevu wa Sh 133bilioni linapawa kuwa fundisho kwetu kuwa viongozi wa serikakali, na chama tawala na umma kwa ujumla wajenge tabia ya kuheshimu maoni yanayotolewa na pande zingine kama vyama vya siasa, watu binafsi na vyama vya kiraia badala ya kuwabeza na kuwaita waongo pale wanapozungumzia masuala yanayohusu maslahi ya taifa letu.

Kazi ya vyama vya siasa na vyama vya kiraia siyo kuitetea serikali bali kukosoa utendaji wake mbaya. Mtu anaweza kuuliza swali kama Dk Slaa sasa anastahili kuitwa mwongo au mzalendo? Binafsi jibu nitakalolitoa mimi ni kuwa Dk Slaa ni mzalendo wa kweli.

Nitapendekeza pia kuwa nchi yetu ianzishe tuzo ya maana kwa raia kama yeye wenye uchungu na nchi yao kama ilivyo kwa tuzo ya Amani ya Nobel, ambayo hutolewa kwa watu wanaodiriki kupigania amani duniani. Wewe msomaji wangu sijui utamuitaje?

E.mail:theodatusm@yahoo.com Simu: 0752450235
 
Mimi naona aitwe Muongo, maana kusema Viongozi wa kitaifa na wengine toka Chama Dume ni waaongo ni Kukosa adabu???xxxx???
 
Back
Top Bottom