Kauli kama hizi za baadhi ya wanasiasa na pia viongozi waandamizi wa serikali lazima zichunguzwe kwa umakini sana.
Mh. Sitta anaongea kama nani kwa sababu kwa Tanzania, yeye ni mwakilishi wa Watanzania bungeni (Mbunge) na pia ni mtendaji wa serikali (Waziri) bila kusahau kama ni mjumbe wa halmashauri Kuu ya CCM.
Kuna watu watanunua maneno yake kwa vile tu wamesikia kile ambacho wanapenda kukisikia bila kujali athari zake.
Lazima tujiulize chanzo, sababu na mazingira ya yeye kusema maneno haya ambayo ni mazito kwa nafasi aliyonayo ndani ya CCM na serikalini.
Mtafaruku au kadhia hii chanzo chake ni serikali ambayo yeye ni mjumbe pia wa baraza la Mawaziri ambapo kisheria hukaa chini kama baraza la Mawaziri kuuchambua mswaada wa serikali kabla ya kupelekwa bungeni halafu pia akiwa kama mjumbe katika kamati ya wabunge wa CCM ambao serikali huwa inafanya mawasiliano nao kabla haijapeleka mswaada bungeni ili kupata mawazo yao. Kwa kifupi, Mh. Sitta yuko sehemu zote ambazo mswaada hupita kabla ya kufika kwenye kamati za bunge.
Je, alikuwa wapi katika kuliona hilo ndani ya baraza la mawaziri na wabunge wa CCM mpaka mswaada umefika bungeni na kupitishwa. Kikubwa zaidi, misingi ya uongozi bora unatuasa kuwa, kikitokea kitu cha kuburuzwa au kinafanyika kinyume na sheria, maadili au misingi ya uongozi wako basi lazima ukikemee na kama kitaendelea kufanyika basi lazima uonyeshe political statement kwa kuachia ngazi za kisiasa na serikali ambazo zilikuwa zinakufunga katika kulisemea nje ya misingi ya kazi na ndani ya chama.
Mh. Sitta kwa sasa anachofanya ni kutenda kosa la maadili ya kiwaziri na pia ndani ya kamati ya CCM huku akijiondoa kwa kusema "WASIKILIZWE" wakati yeye ndiye anatakiwa kuwasikiliza kulingana na nafasi yake ndani ya CCM na serikali yake.
Huyu mzee anapiga ngoma na kuicheza yeye mwenyewe huku washabiki wa kisiasa kama ilivyo kwa watanzania wengi wakimzunguka na kushangilia.
Mzee Sitta anatafuta nini na kwa manufaa ya nani katika statement yake hii wakati yeye ndiye mwenye lungu la kisiasa na kiutendaji serikalini.
Siasa za Tanzania ni majanga.