...Wengi wetu tu wepesi kusimulia hadharani kama si kwa mashostito basi hata humo saluni au maofisini tunasimulia mambo yetu ya chumbani au waume wetu. Utasikia ah shost mie wangu mlevi sana bwana hadi anakera akirudi ye ni kukoroma tu hata hakumbuki ka kalala na mwanamke, au mh nimechoka leo, maana shughuli niliyopewa na shemeji yenu hata si ndogo!n.k...
...Hebu fikiria mara mbili, unawasimulia udhaifu wa mume wako, mara: Mimi mume wangu akiona paja tu basi, wazaramu wanampanda, bila kumpa staftahi hapo ujue network hazitosoma. Kesho, shoga yako akikuta bar atamkaribisha shemejiye na kumfunulia paja hiyo ni kumdatisha, si umeshamuambia kuwa wazimu wake upo kwenye mapaja?
Habari hii imenifanya nijiulize kama wanaume nao huwa wanazo tabia kama hizi, hivi huwa wanatusema kwa marafiki zao? Au wao mazungumzo yao ni tofauti?
Bila ya shaka kuwa mwanamke ndiye mtu wa karibu sana kwa mume wake, mwanamke huyu, anakuwa ndiye mwanamke aliyefanikiwa katika uhusiano wake wa mapenzi na mume wake...
Hivyo basi, suala la kuhifadhi siri ni jambo zito kwa mtu na ni amana aliyoichukua. Sisi ambao tuna imani na dini zetu tunafundishwa kuwa ...ikiwa mtu atazungumza na mtu mwengine kisha wakaachana basi huwa ni amana (yaani mazungumzo yale waliyozungumza huwa ni amana kwa kila mmoja) Haifai kwenda kuyasimulia mbele bila idhini ya yule uliye zungumza naye kwanza.
Tunafahamishwa kuwa:
Hakika katika watu wabaya wenye shari siku ya Qiyaamah ni mtu aliyefanya tendo la ndoa na mke wake kisha mume au mke akatoa siri ile ya mume wake au ya mke wake
Jambo la kuhifadhi siri ni la wajibu kwa mume na mke na ni jambo lililokuwa muhimu sana katika jamii na ndilo linalohifadhi amani na maadili mema katika jamii husika. Kwa hakika kutoa siri za mwanamme ndani ya nyumba yake au mwanamke, matengamano ya mume kwa mkewe, watoto wake, na kila alichokuwa nacho katika mali yake na mengineyo itakuwa ni fedheha kwa watu wengi. Uislamu umemuusia Muislamu kumsitiri na kumfichia siri nduguye Muislamu, na ya kuwa, Muislamu atakayemsitiri nduguye Muislamu basi Mwenyezi Mungu Atamsitiri yeye siku ya Qiyaamah.
Pamoja na kuwa kuhifadhi siri kwa ujumla ni jambo muhimu sana na ni wajibu, hata hivyo kuhifadhi siri ya unyumba baina ya mume na mke ni jambo la wajibu zaidi na ni jambo tukufu ambalo halifai kutolewa kwa hali yoyote ile. Ama wajinga wa zama zetu leo hii hawapendezwi na maneno isipokuwa ni maneno haya na yote hayo yanatokana na ukosefu mkubwa walionao wa imani na udhaifu wao.
Mtume (Saw) ametahadharisha hali hii ya kutoa siri ya jimai (tendo la ndoa) kwa watu, aliposema,
Huenda mtu akasema anachomfanyia mke wake, na huenda hilo likafanywa na mwanamke pia (watu wakanyamaza baada ya maneno hayo) mwanamke akauliza, ee, kweli kabisa na wengi hufanya hivyo katika wanawake na wanaume, Mtume (Saw) akasema, Basi msifanye hivyo, mfano wa jambo hilo ni kama Shaytwaan aliyekutana na Shaytwaan mwenzake wa kike na akawa anamuingilia hapo njiani na watu wakiwa wanamwangalia
Kwa hakika huu ni mfano mbaya sana wa kufananishwa na shetani. Hivyo hili ni onyo kali kwa wenye tabia hiyo waiache ili wasiwekwe katika daraja ya chini Siku ya Kiyama wala wasifanane na mashetani.
Jamii zinavunjika kwa tabia hii ambayo imezagaa katika vigaro na mabaraza yetu kwa kuzungumzia mas-ala nyeti na ya ndani kama haya.