Siri ya chumba namba 39

isubamen

Member
Jul 12, 2017
7
9
KIJANA mmoja mtanashati aliingia kwenye hoteli moja kama mteja, akaomba aonane na bosi. Baada ya kuruhusiwa, mazungumzo yalikwenda kama hivi;

Mteja: Samahani, naomba kujua kama chumba namba 39 kiko wazi.

Bosi: Ndiyo, kiko wazi.

Mteja: Naweza kupata chumba hicho?

Bosi: Ndiyo unaweza kupata.

Mteja: Ahsante sana.

Baada ya mazungumzo hayo, kijana alilipia chumba alichohitaji, kisha kabla ya kwenda chumbani alimwomba bosi amletee kisu cheusi, uzi mweupe wenye urefu wa sentimita 39 na machungwa 39.

Bosi alikubali, japo alishangazwa sana na vitu alivyoagizwa na mteja wake. Baada ya hapo, mteja alikwenda chumbani bila kuagiza chakula wala kitu kingine chochote.

Kwa bahati, chumba cha bosi kilikuwa jirani na cha mteja huyo. Usiku wa manane, bosi alisikia sauti za ajabu na kuogofya. Sauti kama za wanyama mwitu wakishambuliana, pamoja na sauti za vyombo vikivunjwa sakafuni. Siku hiyo bosi hakupata lau lepe la usingizi - hakulala kabisa. Alibaki akistaajabu na kutafakari sababu za sauti zile.

Asubuhi ya siku iliyofuata, wakati mteja akikabidhi funguo za chumba kwa ajili ya kuondoka zake, bosi akaona hapana, huyu si wa kumwacha. Akamtaka wafuatane hadi chumbani kuhakiki usalama.

Walikwenda pamoja hadi chumbani na kukuta kila kitu kikiwa sawa bin sawia. Zaidi, alikuta na kile kisu cheusi, uzi mweupe na machungwa vikiwa juu ya meza. Bosi alibaki mwenye huzuni na taharuki, asijue siri ya mkasa ule.

Mwaka mmoja baadaye, mteja yule aliibuka tena hapo hotelini.

Akaomba tena kuonana na bosi. Bosi alihamanika vilivyo kumwona mteja wake wa siku nyingi, utadhani ameona jini. Kama awali, mahitaji ya mteja yalikuwa yale yale; chumba namba 39, kisu cheusi, uzi mweupe sentimita 39 na machungwa 39. Safari hii bosi aliazimu kuutafuta ukweli kwa njia yoyote iwayo. Alimkirimu mgeni wake kama ilivyo ada, kisha usiku alibaki macho kusubiri sauti zile za ajabu.

Usiku wa manane balaa likaanza: sauti za ajabuajabu na ghasia vilianza, safari hii kwa sauti ya juu maradufu ya ile ya mwaka mmoja nyuma.

Asubuhi kulipopambazuka, mteja aliondoka akiwa na furaha na bashasha. Chumba kilikuwa salama u salimini. Bosi alihamaki baada ya kushindwa kubaini siri iliyogubikwa na mkasa ule.

Alijiuliza kwanini chumba namba 39? Kwanini machungwa tisa? Kwanini kisu cheusi? Kwanini uzi mweupe? Basi, kwa kukosa majibu ya maswali hayo, bosi aliomba uzima tu kwa Mungu wake ili mwaka utakaofuata, mteja huyo afike tena hotelini hapo.

Kama mzaha vile, mwaka uliofuata, mteja yule alirejea na mahitaji yaleyale kama ya miaka miwili iliyopita. Kama kawaida, usiku bosi alitaabishwa na hali ileile ya sauti za kelele na za kutisha.

Ilipotimu asubuhi wakati mteja akiondoka, bosi alimtaka radhi na kumwomba amweleze siri iliyo nyuma ya yote yaendeleayo chumbani kila afikapo hotelini hapo.

Mteja: Ni siri kubwa mno. Je, nikikwambia utaweza kuitunza na kuidhibiti bila kuivujisha?

Bosi: Nakuahidi sitaivujisha siri hiyo, nijulishe!

Bahati mbaya, mpaka hivi niandikavyo habari hizi, bosi hajavujisha siri aliyosimuliwa.

Tuombe uzima, siku akiisimulia tu nami nitaiandika hapa kwa ajili yenu.

Sent from my GT-I9060I using JamiiForums mobile app
 
Sasa wewe umejuaje wakati wewe siyo huyo jamaa au huyo boss?
1.Jamaa alimwambia boss
2.Boss alikuambia wewe.
3.Wewe umetumbia sisi.
Hakuna tena siri hapo..tuambie tu.
 
Back
Top Bottom