Chama cha Mapinduzi kilifungua dirisha lake la watia nia kwa ngazi ya urais. Wanachama wengi wamejitokeza hadi sasa wanakaribia kufikia 40. Miongoni mwao wameshakamilisha zoezi la kutafuta wadhamini wasiopungua 450 kwa mikoa isiyopungua 15 ya Tanzania. Katika mchakato huo, baadhi wametumia fursa hiyo kujiuza toka mkoa mmoja hadi mwingine huku wapambe wao wakisherehesha mikutano ya kusaka saini za wadhamini kwa mikutano mikubwa sana. Na baadhi yao wamefanya na kukamilisha mchakato huo kimya kimya.
Aidha, kwa watia nia wengine miongoni mwa waliojitokeza inaonesha kuwa fursa hii ya kusaka wadhamini waliisubiri kwa kwa shauku kubwa. Ni fursa ambayo ilikusudiwa kujiuza kwa taifa kwa maana kabla ya hapo hawakuwa na wala wasingeipata fursa kama hii. Hii ni fursa adimu ya kuzunguka nchi nzima ukisema makusudio yako ni nini kwa umma. Fursa adimu iliyotumika kuvuka mipaka ya zoezi hata kufikia kuitangulia NEC ya Jaji mstaafu Lubuva.
Inavyoelekea, kuna watia nia hao waliokuwa wamepanga kimkakati kabisa kutumia mchakato huo kuanza kampeni za kuusaka urais mapema. Na kwa mujibu wa Katibu Mwenezi wa CCM ndugu Nape Nnauye mchakato wa kutia nia na kusaka wadhamini sio muda wa kampeni. Hata hivyo, kwa sisi tulio wengi mchakato huu kwa baadhi ya watia nia umegeuzwa muda na msimu wa kampeni kiaina. Kampeni ambazo si kwa wanachama tu, bali sasa ni kwa taifa zima.
Tunapenda kuelewa, kwa mujibu wa kanuni za CCM. Je! Ni sahihi kwa mwenendo kuwa hivi?