Simulizi ya kipelelezi: Document number 72 (Nyaraka namba 72)

STORY: DOCUMENT NUMBER 72
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
EPISODE 5.

Mwanamama huyo Dainesi Mtandu, alikuwa kwenye gari yake akiwa mwingi wa wasiwasi asiye na amani kabisa kwenye moyo wake. Gari alikuwa anaipeleka kwa mwendo ambao haukuwa rafiki sana kwa upande wake mpaka alipofika nje ya mji kabisa eneo ambalo lilikuwa na msitu.

Palitulia sana kiasi kwamba palitisha na mtu mwenye roho yake nyepesi asingeweza kusimama eneo kama hilo akiwa mwenyewe kutokana na historia ya eneo hilo. Alishuka kwenye hiyo gari yake na mbele yake walitokea vijana wawili ambao walijifunika vichwa vyao kwa vitambaa vyeusi, waliinama kumpa heshima mama huyo kisha wakamuongoza njia mpaka ndani ya msitu huo ambako huko kulikuwa na jengo moja kubwa ambalo lilionekana kuwa la muda mrefu ila bado lilokuwa kwenye ubora mkubwa.

Walifika mpaka ndani ambapo walimkuta mwanaume mmoja aliyekuwa amejifunika shuka jeusi kwenye mwili wake wote akiwa amekaa chini kwa namna ya kupiga magoti.

"Kuna mtu ambaye ameanza kuifuatilia historia ya mwanangu na anaonekana kuna taarifa nyingi sana anazo kitu kilicho pelekea mpaka mwanangu kuanza kuniuliza kuhusu baba yake"
"Whaaaat?"
"Ndiyo maana nimefika hapa saivi"

"Anaitwa nani huyo mtu?" Mwanaume huyo aliuliza kwa sauti yake nzito huku akiwa analifunua hilo shuka lake. Mwanaume huyo alilifunua shuka lake hilo, usoni kwake hakuwa na jicho moja ambalo lilikuwa limetolewa huku usoni akiwa na alama za visu ambavyo bila shaka viliwahi kupitishwa usoni.

"Anaitwa mzee Balezi"
"Unamaanisha yule mfanyakazi wake"
"Ndiye huyo"
"Unatakaje mama?"
"Nadhani unajua cha kufanya"

"Kama niliwahi kupoteza jicho langu kwa sababu ya kumlinda bosi mdogo huyu tangu zamani basi kwa sasa pia siwezi kuruhusu kitu chochote kiingie kati na kuharibu mambo ambayo tulipoteza mpaka damu za watu kuyajenga"

"Usije ukaruhusu ujinga wowote utokee maana sitakusamehe" mwanamama huyo aliongea huku akiwa anasimama ili aondoke humo ndani.

"Mama mpaka kesho asubuhi kazi itakuwa imeisha punguza wasiwasi kabisa" walimaliza maongezi yao kisha mwanamama huyo akawa ameondoka, kazi akiiacha mikononi mwa huyo mtu ambaye makazi yake yalikuwa porini huko.

Asubuhi na mapema kulikucha, Calvinjr kama kawaida yake alikuwa amewahi ofisini kwake kwa ajili ya kujiandaa na kikao ambacho alikipanga siku hiyo ili kuwataarifu watu wote kuhusu mkataba ambao walikuwa wamekubaliwa kupatiwa. Lakini kuna kitu aliona kwamba hakipo sawa, ilikuwa imefika mpaka saa mbili ila hakubahatika kupata taarifa ya msaidizi wake, mzee Balezi.

Haikuwa kawaida kwa mzee huyo kutofika mapema kazini hata siku moja na kila akifika ilikuwa ni lazima kwanza akaripoti kwa bosi wake ambaye ndiye alikuwa Calvinjr mwenyewe. Alipotezea na kuhisi huenda kuna tatizo tu la ghafla limetokea na mzee huyo angerudi, kwa sababu kama angekuwa na tatizo kubwa basi angemtaarifu kwenye simu ila kabla hajafanya chochote kile, simu yake ya mkononi iliita

Alivyo angalia kwa umakini alishtuka sana, kwa sababu ilikuwa ni namba ya mke wa mzee huyo ambaye alitoka kumuwazia muda sio mrefu. Aliipokea akiwa na wasiwasi maana hakutamani kusikia taarifa yoyote mbaya kutoka upande wa pili lakini hata hivyo hilo halikusaidia kitu, kwani ukweli ilikuwa ni lazima aupate.

Upande wa pili, mke wa mzee huyo alikuwa analia kwa uchungu sana huku akiwa anatoa machozi. Alitoa taarifa kwamba Asubuhi ya siku hiyo mumewe amekutwa amenyongwa na kutupwa kwenye mtaro akiwa pamoja na Yasin. Yasin ndiye aliyekuwa msaidizi wake ndani ya ile ofisi yake na ndiye yule kijana ambaye jana yake alikuwa anamsimulia kwamba ana wasiwasi sana na bosi wao kwa sababu anafanana na mtu fulani.

Hizo habari zilimpa mshtuko usiokuwa wa kawaida, sasa alielewa kwamba ni kwanini watu hao mpaka huo muda hawakuwa wamefika kazini na wasingefika milele. Alikuwa na maswali mengi sana ila alimjibu mwanamke huyo kwamba angefika huko muda mfupi ujao kisha akakata simu.

Alikaa chini kinyonge sana, hakuelewa kipi kilikuwa kimewakuta watu hao na kwa sababu zipi hasa mpaka wafe pamoja, "kwani kuna mambo ya siri ambayo huenda walikuwa wanashiriki bila mimi kujua ndiyo yamewaua?" Alikuwa anajiwazia mwenyewe lakini hakupata jibu zaidi ya kubaki kuumia tu kwenye moyo wake.

Mzee Balezi licha ya kuwa mfanyakazi wake lakini kwake alikuwa anamuona kama baba na alikuwa akimheshimu sana isivyo kawaida, suala la mzee huyo kufa lilimuuma sana. Hakuweza kukaa ofisini tena kwa wakati huo, akaamua kuifunga ofisi na kutoka ili aelekee kwa mzee huyo kuweza kupata taarifa zaidi wa nini kilitokea na pia kujua ni kwa namna gani anaweza kuisaidia hiyo familia.

Alikimbiza sana gari yake mpaka alipofika maeneo ya Mwenge ambapo ndipo palikuwa nyumbani kwa mzee huyo, baada ya kufika alitaka kuingia getini lakini alizuiwa na maaskari ambao walimwambia kwamba eneo hilo lote lipo chini ya ulinzi kwa sababu za kiusalama hivyo hakuna mtu anatakiwa kuingia kwa sasa mpaka baadae watakapotoa taarifa nyingine maana hata familia imehamishwa kwa muda ili kupisha tatizo kama hilo lisijirudie tena.

Basi hakuwa na namna zaidi ya kukubali kuondoka kishingo upande kichwa kikiwa kinamuuma kwa mawazo na maswali mengi sana ambayo alihisi kwamba huenda familia hiyo ingemsaidia kumpa majibu ili ajue kwamba mzee huyo kilicho muua kilikuwa ni nini hasa. Aliondoka kuelekea njia ya Mikocheni, huko alikuwa anaenda kumuona dada yake wa damu kwake.

Alipita eneo kilipo kituo cha radio ya Clouds fm na kutembea na gari kama dakika tano tu, akakunja mkono wake wa kulia na kupaki karibu na geti moja ambapo alifunguliwa baada ya kupiga honi moja tu. Hata hivyo hakuweza kuingia na gari, aliiacha nje yeye akaingia kwa mguu mpaka uani ambako alisikia kama mtu anahesma.

Alifika huko na kumkuta dada yake akiwa anafanya mazoezi kwa nguvu kubwa, alitabasamu kwa mbali. Huyo ndiye alikuwa Valentina mwenyewe, waweza kumuita Tina, alivyo muona tu mdogo wake alicheka na kumrushia fimbo moja ngumu ambayo ilikuwa chini, walitakiwa kuvipasha viungo vyao kwanza kabla ya kuongea.

Calvinjr aliidaka fimbo hiyo lakini kabla hata hajatulia alikoswa na fimbo nyingine baada ya kurudi nyuma, alitaka kusogea mbele alipishana na teke kwenye uso wake lakini alipigwa bonge la mtama. Wakati anahangaika kunyanyuka, fimbo ilikuwa kwenye uso wake, kwa maana hiyo kama dada yake angeamua kumdhuru angesha mharibu uso muda mrefu sana.

"Mhhhh sijui hao watu walikufundisha nini huko kwenye mafunzo yako, mbona umekuwa mzito sana namna hiyo? Utaweza hata kujitetea ukikutana na watu wenye uwezo kama wangu wewe?" dada mtu aliongea akiwa anajifuta jasho na kuelekea sebuleni ambapo mdogo wake alitabasamu tu na kusikitika huku akimfuata dada yake nyuma.

"Haya nambie kulikoni last born wetu? maana nakujua, hiyo sura yako ilivyo lazima kuna tatizo huko ulikotoka" Tina aliongea akiwa anampatia Calvinjr maziwa kwenye kikombe, walimjua alivyokuwa akiyapenda maziwa ndiyo maana hawakucheza naye mbali.

"Una taarifa zozote kuhusu hawa watu ambao wamewaua wafanyakazi wangu?" swali lake lilimfanya dada yake amwangalie kwa umakini sana.

"Najua tu kwamba wamekufa ila kuhusu aliye waua sijajua bado, mtaani kuna makundi mengi sana ya kihalifu na siku hizi watu wanauana hata kwa kudaiana shilingi elfu kumi tu hivyo ni ngumu moja kwa moja kujua kirahisi hivyo na kingine hakuna hata mtu mmoja ambaye anahisiwa"

"Lakini dada, wewe kila siku upo kazini, nina imani kwamba hakuna taarifa za siri ambazo zinakupita. Unajuana na watu wengi sana, sasa suala dogo kama hilo unakosaje taarifa zake?"

"Mhhhh usijisahau sana kwamba hata wewe ni nani? Wewe na mimi tuna tofauti gani? Wote tunafanya kazi hii ya siri ambayo hata mama hajui, sasa kwanini uhisi mimi ndo napaswa kuwajibika? Okay kuna utofauti wowote ambao uliuona kwa watu hao kuanzia kazini labda au mazingira ambayo ulikuwa huyaelewi au hata wakiwa wanakutana na mtu ambaye hukuwa na taarifa zake?"

"Hapana hakuna kitu kama hicho zaidi ya jana tu ambapo niliwasikia wakiongea mambo ambayo hayakuwa ya kawaida kwangu"

"Yapi hayo?"
"Nilimsikia mzee Balezi anadai kwamba mimi kuna mtu wa zamani kidogo ambaye alikuwa muuaji nafanana naye kwa kila kitu"
"Mhhhh ukafanyaje baada ya hapo?"
"Nilienda kumuuliza mama"
"Hey unataka kuhisi kama mama ndiye kawaua au mbona unakuwa na akili za kitoto Calvinjr?" Dada mtu aliuliza kwa jazba.
"Sisiter sio hiv....." Calvin kabla hajajibu simu yake ilianza kuita, alikuwa ni mke wa mzee Balezi akiwa anapiga simu.
"Naomba leo usiku uje tafadhali nina mambo nataka nikwambie, naogopa sana kuhusu usalama wa wanangu" mwanamke huyo aliongea kwenye simu akiwa anaonyesha dalili ya uoga.
"Wewe uko wapi?"

"Sawa nakuja " mwanaume alikkata simu baada ya kuelekezwa mahali ambapo mama huyo alikuwepo, hakukaa tena humo ndani alitoka bila hata kuaga, akihitaji kuwahi ofisini kwanza ili baadae awepo kwa mke wa mzee huyo, hata dada yake alibaki anamshangaa mdogo wake.

Tuendelee kufuatilia kwa ukaribu, episode ya 5 inafika tamati.
Kalamu ni yangu mwenyewe.

Febiani Babuya.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
STORY: DOCUMENT NUMBER 72
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
EPISODE 6

Saa mbili ya usiku ilimkutia Calvinjr njiani akiwa anaelekea Mbande, huko alikuwa anaenda kukutana na mke wa mzee Balezi ambaye alimuahidi kwamba kuna kitu alikuwa anahitaji kumwambia. Mwanaume alitumia dakika 40 tu pekee kufika Azam Complex, huo ni uwanja wa timu ya mpira wa miguu wa Azam.

Aliongeza spidi maana ilibakia muda mchache sana mpaka kufika hapo Mbande. Dakika chache sana zilizo fuatia alikuwa ndani ya hilo eneo, alisimamisha gari yake na kugeuka sehemu zote mpaka alipo iona nyumba yenye rangi ya blue, alitabasamu maana alielekezwa eneo hilo na hiyo ndiyo ilikuwa nyumba pekee yenye bati la blue ndani ya hilo eneo.

Alisogea mpaka ulipokuwa mlango wa getini ila alihisi upo wazi, alichungulia kwa ndani, hakuona kitu zaidi ya taa za ndani ya nyumba hiyo ambazo zilikuwa bado zinawaka. Baada ya kuingia tu alisimama kwanza, mwili ulimsisimka mno ndipo alipogeuka upande wake wa kushoto, alishangaa sana baada ya kuona mwili wa mlinzi ukiwa upo chini.

Alisogea kwenye eneo hilo kisha akamgusa pua mlinzi huyo ili kujua kama alikuwa hai au amekufa lakini kitu cha ajabu mlinzi huyo alikuwa amezimishwa tu. Alishangaa sana, ni mvamizi gani ambaye amekuja na anaonekana kabisa hakuwa na lengo la kumuua mtu huyo? Sasa kilicho mleta ni kipi? Hakuelewa.

Akiwa bado ameinama hapo alihisi kama kuna kivuli kinakuja upande ambao yeye alikuwepo. Aliinuka ghafla sana kisha akarudi nyuma, alipishana na buti ambalo kama lingempata huenda angetumia kama wiki moja hivi kuweza kuzinduka na kurudi kwenye hali yake ya kawaida.

"Kaa mbali na hii familia utailetea matatizo makubwa sana. Endelea kuishi maisha yako ya kawaida kama unavyo ishi siku zote na usitake kujifanya unaanza kukuza kuza mambo utawaletea matatizo watu wanao kuzunguka bure" sauti yenye mamalaka ilipenya vizuri kwenye masikio yake. Ina maana huyo mtu alikuwa anamfahamu vizuri ndiyo maana alimpa huo ushauri.

"Kwa maana hiyo wewe unanifahamu mimi vizuri sio? Kwahiyo wewe ni nani?" Mwanaume huyo aliyekuwa amejifunika na shuka jeusi kwenye mwili wake hakujibu kitu zaidi ya kukimbilia ulipo mlango wa geti ili atoke. Nani wa kumruhusu? Alikutanishwa na viganja kwenye kifua chake.

Alirudi nyuma kwa hatua kadhaa huku akionyesha mshtuko mkubwa wa kijana huyo kuwa na uwezo wa namna hiyo, Calvinjr alitabasamu na kuikunja suti yake kwenye mkono. Mwanaume huyo alitakiwa kutoa maelezo yeye ni nani na anamjuaje Calvinjr.

"Kitu cha ajabu kilitokea, mwanaume yule alivua shuka lake kwa kasi na kulirushia upande ambao alikuwepo Calvin, lilimfunika mwenye mwili wake wakati anahangaika kulitoa, mwanaume yule alijibinua na buti lake na kujizungusha kwa double kick nzito ambapo mateke yote yalitua kwenye kifua cha Calvinjr na kumuachia maumivu.

Kasi ya yale mateke ilimfanya yeye mwenyewe kuachia lile shuka huku akijibamiza ukutani. Alidondoka chini akiwa na maumivu ya kutosha. Alijigonga kwa nguvu kwenye mguu wake wa kulia kwa kutumia mkono wake, alijigeuza na kusimama kwa sarakasi lakini alikutana na hewa tu na utulivu wa humo ndani, mwanaume huyo alikuwa ametoweka zamani.

Aliinama na kumgusa yule mlinzi kwenye mshipa wa shingoni kwa nguvu na kumfanya ashtuke kama ametoka usingizini.

"Kuna nini! Kuna nini kwani?" aliongea mlinzi huyo akiwa kama mtu aliyetoka usingizini.
"Aliyekuwa hapa ni nani?" Calvinjr aliuliza baada ya kugundua kijana huyo alimtambua vizuri maana alikuwa bosi wa bosi wake.

"Sikumbuki chochote kile, maana kwa mara ya mwisho nakumbuka kuna mtu aligonga mlango lakini nilivyo fungua sikuona mtu, sijaelewa tena kilicho endelea mpaka saivi nilivyo shtuka hapa" ilionekana kwamba mtu aliyekuwa kwenye hilo eneo alikuwa akifanya mambo yake kwa kasi mno na kwa ufanisi mkubwa.

Calvinjr aliamua kumuacha mlinzi huyo na kuelekea ndani ambako hakuwa na uhakika kama familia hiyo ilikuwa kwenye usalama ila kitu ambacho kilimshangaza sana ni baada ya kukuta mlango umefungwa kumaanisha kwamba hakuna mtu aliyekuwa ameingia hapo ndani kabisa.

Ina maana hata yule mgeni aliyepishana naye hakuingia ndani, sasa alikuwa amekuja kufanya nini? Hata yeye hakuelewa ila alikuwa akiikumbuka sana ile kauli ya kwamba kaa mbali na hii familia maana utailetea matatizo makubwa sana.

Calvinjr aligonga mlango huo ambao ulienda kufunguliwa na mama huyo moja kwa moja. Sebuleni palikuwa kimya sana ni wao wawili tu ndio ambao walikuwa hapo.
"Poleni sana kwa matatizo makubwa ambayo yameweza kuwatokea"

"Tunashukuru sana kwa hilo na samahani sana kwa kukusumbua maana hata mchana nimepata taarifa kwamba ulikuja kule, niseme tu asante kwa sababu mume wangu alibahatika sana kupata bosi mwenye moyo kama wako maana kwa majukumu uliyo nayo sikudhani kama unaweza kukubali kupoteza muda wako kwa sababu ya familia yetu"

"Huu msiba ni wetu sote, yule aliyekufa kwangu hakuwa mfanyakazi tu bali kwangu nilikuwa namuona kama baba. Amekuwa mwema kwangu siku zote na kutimiza majukumu yake kwa asili miamoja, hivyo mazishi yake kampuni itasimamia lakini pia mtalipwa stahiki zenu zote mpaka kesho asubuhi malipo yatakuwa tayari"

"Ahsante! sana mwanangu, MUNGU aendelee kukupigania siku zote. Mume wangu amekufa lakini kuna mambo ambayo siyo ya kawaida na siyaelewi, sijamwambia mtu yeyoye hata polisi nimewaambia sijui lolote maana siwaamini sana hivyo nikahitaji kukufikishia wewe ili uone ni sehemu gani unaweza kutusaidia" mama huyo aliweka kituo kidogo kabla ya kuendelea kumsimulia mwanaume huyo kwamba ni kipi hasa kilikuwa kinamtatiza au ni siri ipi ambayo alikuwa nayo kwenye moyo wake.

"Jana baada ya mume wangu kurudi nyumbani, kuna watu walifika hapa nyumbani..."
"Samahani unasema watu?"
"Ndiyo"
"Ikawaje?"

"Hawa watu walifika kule tulipokuwa tunaishi wakidai kwamba ni wageni wa mume wangu hivyo walihitaji kuongea naye na kufanya mazungumzo ya siri hivyo walitoka na kwenda upenuni mwa nyumba ambako huko walikaa kwa dakika thelatini tu kisha wakatoka. Baada ya kutoka kule mume wangu alikuja kuniaga kwamba anatoka mara moja na hao watu na angerudi baada ya muda fulani"

"Wakati anakuja kuniaga alirudi akiwa tofauti sana, maana hata hali yake ilionekana kubadilika na kuwa kama mtu aliye na wasiwasi isivyokuwa kawaida. Alinipa ishara ya kukataa jambo ila sikumuelewa maana watu wale walikuwa wamefika tulipokuwa tumesimama hivyo wakaongozana naye na kutoka wakiwa pamoja"

"Baada ya hapo mume wangu hakurudi tena mpaka asubuhi ambapo tulikesha kumsubiri, zimetoka taarifa kwenye vyombo vya habari kwamba kuna miili miwili imepatikana kwenye mtaro ikiwa imekufa, nilipata wasiwasi mkubwa kwa maana mume wangu alikuwa bado hajarudi tangu jana yake na simu yake alikuwa ameiacha nyumbani.

Baada ya kuona miili ile ndipo nikagundua kwamba alikuwa ni yeye na kijana ambaye alikuwa anafanya naye kazi kwenye kampuni yako" mama huyo alimaliza maelezo yake ambayo Calvinjr alikuwa akiyahitaji sana na ndiyo sababu kubwa ambayo alikuwa anaisubiri kwa hamu kubwa.

"Ulifanikiwa kuwaona hao watu?"
"Hapana sikufanikiwa kuwaona sura zao maana walikuwa wamejifunika na mashuka meusi kwenye miili yao mpaka usoni"

"Unasema walijifunika mashuka meusi?" Calvinjr aliuliza kwa mshangao kwa sababu dakika chache tu alitoka kupambana na mtu ambaye alikuwa ndani ya mavazi meusi kama ambayo alikuwa anayazungumzia mama huyo.

"Ndiyo"
"Je kuna ishara zozote kwa mumeo ambazo labda uliziona siku kadhaa kutoka kwake kabla ya kifo chake ambazo ulikuwa huzielewi?"

"Hapana mume wangu alikuwa muwazi sana hivyo kama kungekuwa na kitu cha tofauti basi mimi ni lazima angeniambia kwa namna yoyote ile, ila.....!" mama huyo akiwa anaendelea kueleza ni kama alikumbuka kuhusu jambo fulani ambalo lilimfanya agande akiwa kama anavuta kumbukumbu fulani za nyuma, Calvinjr alikuwa makini sana kumsikiliza.

"Nakumbuka siku chache kabla hajafa, aliniambia kwamba kuna jambo anahisi kwamba halipo sawa. Alidai kuna kitu kinamkumbusha sana maisha ya huko nyuma ambapo kuna mambo yaliwahi kufanyika kwenye nchi hii na huenda yakajirudia kwa mara nyingine tena. Aliniambia kwamba kuna mtu amemuona, anamkumbusha sana maisha yaliyopita japo hana uhakika sana ila atakapokuwa ana uhakika ataniambia"

"Hivyo nilikuwa nasubiri kwa hamu kubwa sana aweze kuniambia ni kitu gani hicho ila kwa bahati mbaya sana hajanambia chochote mpaka anafariki" mama huyo aliongea akiwa ameinama chini kwa maskitiko makubwa.

"Kuna mtu yeyote yule ambaye umeongea nae kuhusu hizi taarifa?"
"Hapana wewe ndiye mtu wa kwanza"

"Sasa kwa sasa cha kufanya, inatakiwa siri zote ambazo unazo kumhusu mumeo inabidi uzizike kwenye moyo wako na kifua chako, yaani usije ukathubutu kumwambia mtu yeyote mwingine kwa gharama yoyote ile.

Kama kuna mtu atakutafuta na kuhitaji kujua mwambie kwamba hakuna unalo lijua lolote lile, na kwa sasa usije ukanipigia simu kwa namna yoyote labda tu pale ambapo unahisi kwamba upo kwenye hatari ndipo nipigie simu haraka sana.


Nimefanya hivyo kwa sababu nahisi huenda kuna watu wanatufuatulia hivyo huu muda mimi nitautumia kufanya uchunguzi ili nijue tatizo liko wapi"

"Pesa zenu zote nawaingizia kwenye akaunti zenu asubuhi na kwa sasa najua mtakuwa chini ya jeshi la polisi hivyo jiangalie sana na uyazingatie niliyo kwambia kwa ajili ya usalama wa familia yako" Calvinjr alimaliza maongezi na mama huyo huku akiwa anaaga na kuondoka hilo eneo kichwani akiwa na mambo mengi sana ambayo alikuwa anajiuliza kuhusu hao watu wanaovaa hayo mashuka meusi na mambo ambayo yapo nyuma yao.

Episode ya 6 inafika mwisho.

Kalamu ni yangu mwenyewe,

Febiani Babuya.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom