HADITHI: THE ODYSSEY OF GAVIN LUCA (LIONELA)
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
********************
UKURASA WA AROBAINI NA MOJA
SONGA NAYO................
******
JNIA.
Saa nne na dakika zake kumi na sita usiku ni wakati ambao ndege kutoka kwenye shirika kubwa la ndege duniani la FLY EMIRATES ilikuwa inatua ndani ya viunga vya ardhi ya uwanja ambao waliupatia jina la muasisi wa taifa la Tanzania Mwl. Julius Kambarage Nyerere kama urithi na heshima ambayo alilipatia taifa kwa uwepo wake kuanzia siku ambayo alizaliwa mpaka siku ambayo alitoweka duniani.
Ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria wa kutosha ambao wengi wao walikuwa ni wageni kutoka kwenye mataifa mbali mbali duniani wakiwa wanakuja kwa ajili ya biashara lakini wengine walikuwa wamefika Tanzania kwa sababu ya kupumzika na kufanya utalii. Ndani ya ndege hiyo kubwa pia walikuwepo wazawa ambao walitabasamu kurudi tena ndani ya ardhi yenye amani, ardhi ambayo ilikuwa inamiliki watu wajuaji kuzishinda hata kompyuta.
Kwenye ndege hiyo alionekana kushuka mwanamke mmoja ambaye alikuwa ni mrembo mno, uso wake ulikuwa kama umejichonga kiasi, ngozi yake ilikuwa nyororo ambayo hata kuishika na mkono ungehisi kwamba inateleza! Rangi yake mwanamke huyo ilikuwa ni ile chocolate ambayo ilikolea sana kiasi kwamba akawa kama anataka kuwa mweupe ila weupe uligoma. Ilikuwa ni burudani kuweza kumtazama mwanamke huyo hata wale ambao walikuwa wanamuona akiwa anatoka ndani ya hiyo ndege waliduwaa na wengine wakajikwaa.
Kwenye mwili wake alikuwa amevaa nguo aina ya suti ambayo ilikuwa na rangi nyeusi, kwenye miguu yake alivaa viatu vya kisasa vifahamikavyo kama high heels. Usoni alikuwa na miwani na nywele zake za asili ambazo zilitunzwa vyema na kuchanwa kwa ustadi wa hali ya juu kisha zikasindikizwa na kofia ya kike ambayo iliacha sehemu ya nyewele hizo kuwa zinaonekana kwa mbali. Alikuwa na madaha, alitembea kwa kuringa kwani alikuwa ardhi ya nyumbani kwake ambako yeye alizaliwa, nyumbani ambapo alikuwa anapapenda kuliko sehemu yoyote ile duniani.
Mrembo huyo alikuwa ana muda mrefu tangu atoweka ndani ya Tanzania, muda ambao ulimfanya kuishi mbali na nyumbani kwa kipindi kirefu kidogo lakini wakati huo ilimlazimu kurudi haraka kwa sababu hapakuwa pema sana, kulikuwa na tatizo ambalo lilikuwa linauhitaji uwepo wake yeye kuweza kulimaliza tatizo hilo. Mwanamke huyo hakuwa mwenyewe wakati anashuka kwenye ile ndege, alikuwa ameongozana na wanaume wawili ambao nao walikuwa na mavazi meusi kama yeye ila wao walionekana kuwa wafanyakazi wake kwa sababu hata mizigo yake waliishika wao. Alionekana kutulia, hakuwa na papara kubwa bali ni furaha tu ilitawala ndani yake.
Alitembea taratibu kwenda mpaka sehemu ya mapokezi huku akiwa amewaacha watu ambao walikuwa jirani midomo wazi, kila mtu alikuwa akimshangaa lakini wakati huo hata yeye alionyesha tabasamu kidogo kwenye uso wake. Tabasamu ambalo lilitokea baada ya kumuona mtu ambaye huenda hakuwa ametarajia kuweza kumkuta eneo hilo kwa wakati huo. Alikuwa ni baba yake mlezi, mwanaume wa kazi alikuwa hapo kumpokea mwanamke huyo, hakuwa mwingine zaidi ya Othman Chunga.
LIONELA GAVIN LucA, ndiye mwanamke ambaye nilikuwa namzungumzia hapa! Mtoto wa damu na mtoto wa pekee kabisa wa yule mwanaume ambaye dunia ilikuwa inahangaika kutambua kama alikuwa amekufa ama bado yupo hai Gavin Luca na mkewe Norah Hassan. Lionela ndiye alikuwa amefika hapo uwanja wa ndege akiwa anatokea China, na mtu ambaye alikuwa ameenda kumpokea alikuwa ni Othman mwenyewe kama ambavyo mama yake na mwanamke huyo alihitaji bwana huyo afanye. Bado alikuwa ni binti ambaye alikuwa anavutia mno, umri wake ulikuwa ni wa miaka ishirini na hivyo alikuwa kigoli ambaye anaita.
Alimkimbilia Othman na kwenda kumkumbatia kwa mahaba, watu walibaki wamepigwa na butwaa kwani furaha ambayo ilionekana kwa hao wawili ilikuwa ni kubwa mno, haikuwa rahisi kuweza kuielezea kwa lugha rahisi na kila mtu akaielewa. Hawakupoteza muda kwani walitoweka ndani ya eneo hilo kwa msafara wa gari tano za kifahari ambazo zilikuwa zinawasubiri kwenye eneo la kupaki magari. Watu hao waliingia hapo na kuondoka bila kugundulika na mtu yeyote yule.
Kutokana na mambo ambayo yalikuwa yanaendelea nchini kila sehemu ilikuwa imewekewa ulinzi wa kutosha ili kuhakikisha maeneo hayo yanakuwa salama kabisa hususani eneo hilo la uwanja wa ndege. Kesi za zamani zilikuwa zimeanza kurudishwa nyuma tena ili kuwapata wale ambao serikali ilikuwa inwahitaji kwa wakati huo, jambo hilo ndilo liliwapa umakini maafisa usalama wa uwanja huo wa ndege kwani sura ya mtu mmoja ambaye alionekana ndani ya eneo hilo ilionekana kutambulika na ilikuwa kwenye orodha ya watu ambao serikali ilikuwa inawatafuta kwa muda mrefu mno. Mtu huyo alipotea kwa takribani miaka ishirini akiwa hatambuliki kwamba alikuwa wapi lakini siku hiyo alionekana eneo hilo kwa sababu sura yake iliweza kujidhihirisha wazi.
Othman Chunga ndiye mtu ambaye sura yake ilitambulika, ni muda mrefu ulipita lakini sura yake haikuwa imebadilika sana zaidi ya kuwa na ndevu za kutosha usoni kwake. Dredi zake zilikuwa ni zile zile hakuna ambacho kilibadilika kwake, kutambulika kwa sura yake ndiko ambako kulimfanya kiongozi wa maafisa usalama wa eneo hilo kutoa amri ya mtu huyo kukamatwa haraka iwezekanavyo lakini kwa bahati mbaya mpaka wanaligundua hilo walikuwa wamechelewa kwa sababu mtu huyo alikuwa ametoweka. Hali hiyo iliwafanya maafisa hao kupiga simu kwa jeshi la polisi kwa ajili ya kuhitaji msaada na simu hiyo ikampata IGP moja kwa moja usiku huo huo.
IGP Laurien Masapi ndiye aliipokea hiyo simu usiku huo akiwa nyumbani kwake, simu hiyo ilimfanya ajiandae haraka sana kwa sababu alikuwa ni miongoni mwa watu ambao walipewa kazi hiyo na raisi kuweza kuhakikisha wanaipata hiyo familia ili iweze kuhojiwa na kuadhibiwa kwa uhalifu ambao waliufanya kwa zaidi ya miaka ishirini ambayo ilikuwa imepita. IGP aliongozana na msafara wa askari wake mpaka uwanja wa ndege ambapo alifika akiwa anakimbia kuwahi kuona tukio hilo ambalo lilikuwa limetokea hapo.
“Heshima yako kiongozi”
“Umenishtua na simu yako ya usiku huu, una uhakika uliye muona ni yeye?”
“Ndiyo mkuu, picha zake zipo mtandaoni kwa miaka mingi, baada ya kamera kuinasa sura yake ni kwamba hizi picha zimeonyesha mfanano kwa asilimia tisini na tisa ikiwa ni ishara kwamba huyu ni mtu mmoja”
“Nionyeshe hilo tukio na namna lilivyoweza kutokea” IGP alisogea kwenye skrini kubwa ili aweze kumuona mtu huyo kwa usahihi. Nyakati zilikuwa zimeenda, alikuwa ni mtu mzima lakini mwili wake ulikuwa unalipa na hata sura yake haikuwa imebadilika, alikuwa mtu wa mazoezi mno hivyo alijitunza vyema ndiyo maana bado alikuwa anaonekana kama kijana wa juzi tu.
“Mhhhh huyu ni yeye kabisa, kuna kitu gani hasa mpaka amekuja uwanja wa ndege bila uoga tena akiwa amejiachia namna hii?”
“Kuna mtu alikuja kumpokea mheshimiwa”
“Nani?”
“Vivienne Gavin” jina ambalo lilitajwa pale lilimshtua, la kwanza halikuwa na shida kwake ila lile la pili.
“Una uhakika na hilo jina?”
“Ndiyo mheshimiwa”
“Nionyeshe tukio zima” bwana yule hakuongeza neno zaidi ya kurudia tukio zima mpaka lilipofika mwisho, bado IGP ni kama alikuwa haamini lile jambo ambalo lilikuwa linatokea. Alilirudia zaidi ya mara tatu ili kuwa na uhakika zaidi.
“Huyu atakuwa ndiye mtoto wa yule Gavin Luca ila ameamua kubadili jina la kwanza kwa sababu ya kutotambulika kirahisi. Alikuwa wapi miaka yote hii na kwanini aje kuonekana hadharani wakati huu? Othman alikuwa anaweza kulifanya jambo hili kwa siri, sasa kwanini akahitaji sura yake ionekane? Ina maana kuna ujumbe alikuwa anautuma kwetu? Hakuna namna hawa ni lazima wapatikane kwa gharama yoyote ile, huu ni mwanzo mzuri, kama alikuwa amepanga kututisha kwa kujitokeza basi nasema kwamba amefanya moja kati ya makosa makubwa kwenye maisha yake ambayo atayajutia mno”
41 Inafika mwisho.
Febiani