SIMULIZI: Tubu

SIMULIZI: Tubu

Wakati Mrisho akilia hapo dining room , alichokuwa hajui ni kwamba kulikuwa na
mtu aliyemsikia jinsi alivyokuwa ameamka na kutoka hadi hapo dining room usiku
huo na kuanza kulia na kuongea peke yake.

Huyo mtu alikuwa ni dada yake, yani Bi
Khadija. Khadija alikuwa macho usiku huo, na alikuwa katoka kwenda kunywa maji, na ndio
akamkuta kaka yake akiwa hapo dining room , akiongea peke yake.

Hakutaka kumshtua, alitaka kwanza aelewe kaka yake alikuwa anaongea nini peke
yake usiku huo, alisimama nyuma akimtazama jinsi kaka yake alivyolia kama mtu
aliyechanganyikiwa, ambaye mikono yake alikuwa kaiweka usoni huku akiendelea
kuongea mwenyewe peke yake, “Unanitafutia nini wewe Rebecca, umefariki miaka
mingi sana?”, alilia Mrisho huku Khadija akisikiliza huku akijawa na maswali, huyo
Rebecca alikuwa nani?, na anamtafutia nini kaka yake hadi analia hivyo peke yake usiku, na hasa alijiuliza huyo Rebecca kafa miaka mingi, alikuwa ni nani hasa.

Uso wa Khadija ulikuwa na maswali, moyo wake ulikuwa na maswali kichwa chake
pia kilikuwa na maswali, hadi akashindwa kujizuia ikabidi amuulize kaka yake.

“Kaka kulikoni?, mbona unazungumza peke yako usiku wote huu?”, aliuliza Khadija
kwa Mrisho, ambaye alishtuka na kugeuka haraka, hakutarajia kuwa kuna mtu yuko
macho usiku huo mahala hapo.

Uso wa Mrisho ulikuwa umejawa na machozi kwa kulia, huku akiwa na mshtuko wa
uwepo wa dada yake mahala hapo. Uso wa Khadija ulikuwa ni uso wenye maswali
mazito.

Kimya kikatawala kati yao. “Unafanya nini hapa usiku huu, huu si muda wa kulala”, aliongea Mrisho kwa dada
yake, akiondoa kimya kilichojitokeza. “Nimeamka kuja kunywa maji, nimekukuta unalia na kuongea peke yako mahala
hapa”, alijibu BiKhadija,

“Kwanini unalia hapa?, usiku huu, kwanini unaongea peke
yako?”, aliendelea kuuliza
Mrisho alikosa majibu ya kujibu, akaona njia pekee ya kutoka hapo ni kujitia kisirani
kisicho na sababu,

“Achana na mimi, naenda kulala, achana na mimi” aliongea Mrisho
kwa hasira na kuanza kusonga ili atoke hapo dining room, ila kabla hajampita dada
yake, Khadija kwa kutumia mkono wake wa kushoto alidaka mkono wa kulia wa
Mrisho na kuzuia asiondoke,

“Mrisho, acha kutaka kukwepa maswali yangu. Nimekukuta unalia hapa usiku huu, huku ukiongea peke yako, juu ya mwanamke anaitwa Rebecca na nimekusikia kwa
masikio yangu vizuri kabisa, ukilia ukisema, unanitafutia nini, unanitafutia nini wewe
umefariki miaka mingi iliyopita”,

aliongea Bi Khadikja huku uso kakaza akitaka hasa
kujua yaliyokuwa yanamsibu kaka yake.

Mrisho akawa kabaki kasimama hana majibu zaidi ya kueleza.

“Au umeanza
kuchanganyikiwa, maana hata Rahim na Omari wameniambia kipindi nimesafiri uliwahi
kuamka usiku hadi nje kwenye ule mti mkubwa na kuitilia mwanamke kwa jina la
Rebecca usiku wa manane ukidai kuwa ulimuona huyo mwanamke, ilhali hakukuwa na mwanmke yeyote usiku huo” aliongea Bi Khadija,

alikuwa kashasimuliwa na watoto
wake jinsi mjomba wao alitoka usiku hadi nje mbele ya nyumba kwenye mti mkubwa
akidai kusikia sauti ya kulio ya mwanamke aliyeitwa Rebecca
 
Bi Khadija, alihofia kuwa ndugu yake alikuwa ameanza kupata tatizo la ugonjwa wa
akili, ambalo moja ya dalili zake huwa ni mtu kusikia sauti kichwani mwake, ilhali
hakuna sauti zozote.

“Kaka, au umeanza kuugua shezofrenia, ugonjwa wa akili wa kusikia sauti
zisizokuwepo na kuona vitu hovyhovyo ambavyo havipo”, aliongea Bi Khadija, usoni
akionesha kutoelewa kabisa shida ya kaka yake.

Walikuwa wamezaliwa wawili tu, walikua pamoja na hadi umri huo waliishi nyumba moja.

Siku zote kama kaka yake
alikuwa na tatizo lolote basi kwake lilikuwa ni suala lake ambalo alikuwa tayari
kushughulika nalo kwa namna yoyote ile kulitatua.

“Kaka itakuwa unaumwa akili , sio kawaida”, aliongea BiKhadija huku machozi
yakimlenga lenga machoni, Mrisho hakupenda hiyo kauli ya dada yake kuwa huenda
ugonjwa wa akili ulikuwa umemuanza, ilimtia hasira, alijijua yeye sio mgonjwa akili ama
chizi kama waitavyo waliokosa busara ya lugha.

“Mimi sio chizi”, aliongea Mrisho kwa sauti kubwa kumkomesha dada yake na dhana
yake ya kuwa huenda yeye ameanza kuumwa ugonjwa wa akili, mara akatoa mkono
wake wa kulia toka mkononi mwa Khadija ambaye alikuwa kamshikilia asiondoke
mahala hapo, na kuanza kuondoka akielekea kwenye ngazi na kupandisha juu
ghorofani hadi kwenye chumba chake na alipoingia alijifungia.

Chini alibaki Bi Khadija na uso wake wenye maswali mengi na machozi kumlenga, akiwaza alichokiona, na aliyosimuliwa na watoto zake. Alihofia kuwa kaka yake alikuwa
anawehuka akili, maana haikuwa kawaida.

Inaendelea………………………………………….
 
Unaweza pia kusoma simulizi hii kupitia telegram kwa link hii [emoji1541]

 

Similar Discussions

Back
Top Bottom