Kwa hofu kubwa Rahim akaanza kupiga mayowe na kukimbilia sehemu ile ambayo
Sarah alikuwa amejizamisha.
“Anajiuaaaa, anajiua jamani, anajiua”, watu kadhaa
waliokuwa karibu na eneo hilo waliweza kumuona Rahim akikimbilia eneo hilo na wao
wakaanza kukimbia wakimfuatia.
Rahim akajitupa kwenye maji, akamuona Sarah akiibuka kwenye maji akisukumwa
na mawimbi ya maji huku akitapatapa, macho akiwa ameyatoa, maji yakiingia puani na
midomoni.
Kwa ujasiri Rahim akaogelea hadi akamfikia Sarah na kuanza kumvuta kumrudisha
ufukweni. Sarah, mwenyewe alikuwa yuko hoi.
Kikundi cha watu kilikuwa kimekusanyika kumsaidia Rahim kumuokoa binti huyo
ambaye wao wote hawakuwa wakimjua hata jina.
Baada ya kumfikisha ufukweni, Rahim alimlaza Sarah na kuanza kuminya tumboni,
ili kumtoa maji mengi aliyomeza, huku akiwa na wasiwasi mkubwa.
Sarah alionekana kupoteza fahamu. Rahim akaanza kuhisi kuwa huenda binti huyo
amekufa hivyo akaanza kupaniki, huku akiendelea kumkamua tumbo na kumpulizia
hewa mdomoni.
Mara Sarah akazinduka na kucheua maji mengi, kisha akaanza kukohoa.
Rahim na
kikundi cha watu waliokuweko hapo wakafurahi kuona kuwa binti huyo kazinduka.
Pia walitaka kufahamu huyo binti ni
nani?,anatokea wapi?, na kapatwa na nini hata akataka kujiua.
Hivyo wakabaki hapo pembeni kumsubiri apate nguvu ili wamuhoji.
Baada ya dakika kadhaa kupita Sarah akaanza kuonekana kupata nguvu, taratibu
akaanza kuinuka na kusimama, bila kuzingatia watu waliomzunguka.
“Tulia kwanza, ni vyema uendelee kupumzika, tulia”, aliongea Rahim akimsihi Sarah
atulie. “Achana na mimi, hunijui, sikujui kwanini umeniokoa?”, alijibu Sarah kwa hasira
iliyoambatana na uchovu wa baada ya kumezaa maji mengi na kuzimia, aliwaangalia
Rahim na wezake, huku akianza taratibu kuondoka, aliwaona kuwa ni watu
waliokwamisha mpango wake wa kutaka kujiua.
“Wewe unaitwa nani?, umetokea wapi na kwanini unataka kujtoa uhai wako wa
thamani?” alihoji Rahim kwa shauku na pengine hasira, kichwani mwake hakuweza
kuelewa kabisa iweje binti kama huyo alitaka kujiua.
Pia wale watu wengine
waliokusanyika walikuwa na nyuso zenye maswali kama Rahim, nao walitaka kujuu
kulikoni binti huyo kafikia hatua ya kutaka kujitoa uhai wake.
“Wewe na wenzako, sijawatuma mnisaidie, mniache niondoke”, alijibu Sarah kwa
hasira na kuanza kuondoka eneo hilo akiwaacha Rahim na wale mashuhuda wengine wakibaki
na maswali yao yaliyokosa majibu.
Inaendelea….………………….