SIMULIZI: Tubu

SIMULIZI: Tubu

Juma moja lengine likapita bila ya Rahim kupokea simu ama ujumbe toka kwa
Sarah. Alitegemea binti huyo kuwa atampigia simu ama japo atamtumia ujumbe.


Taratibu akaanza kuhisi kuwa pengine Sarah hatomtafuta. Hisia hiyo ilianza
kumkwaza, kwa maana sasa ilikuwa dhahiri kwake kuwa alikuwa anampenda.

Naalitamani waonane tena kwa mara nyengine, pengine hata amuambie lililo moyoni
mwake. Lakini siku zilikuwa zimepita na Sarah hakumtafuta kabisa Rahim.
Ila pasina kutarajia siku moja, Rahim akiwa bize na mambo yake simu iliita. Ilikuwa
ni namba ngeni. Kupokea hakuamini masikio yake , alisikia sauti ya Sarah, hatimaye
Sarah aliamua kumpigia.


“Habari, nimekukumbuka, za toka siku ile?”, alisalimia Sarah. Sauti yake ambayo
pengine ni ya kawaida sana safari hii haikuwa ya kawaida masikioni mwa Rahim.
Alionakuwa sauti hiyo ilikuwa laini na tamu, hata akakosa maneno ya kujibu salamu ya Sarah,
akawa kama amepigwa na bumbuwazi, alihisi hisia za ajabu, hatimaye alikuwa kapokea
simu aliyokuwa akiisubiri kwa hamu toka kwa binti huyo.

“Natamani tuonane, hata mimi nilikuwa nimekumiss, natamani nikuone”, aliongea
Rahim, kwenye simu. “Sawa tunaweza kuonana”, lilikuwa ndilo jibu la Sarah.

Kama ilivyokuwa kwa Rahim kuwa alikuwa ameelemewa na hisia nzito za kumpenda
Srah basi pia ilikuwa hivyohivyo kwa Sarah.

Sarah alimuona Rahim kama mtu wa ajabu. “Sijawahi kukutana na mtu wa aina hii
kwenye maisha yangu”, Sarah alijiambia , “ulikuwa wapi siku zote?, ungekuja mapema
kwenye maisha yangu”, aliendelea kujiuliza Sarah moyoni mwake.
….…………………………………………..


Maisha yake yote Sarah alikutana na watu wa hovyo, kuanzia kwenye familia ya kwao
na ndugu na marafiki, pia hadi wakati huo na umri wake wa miaka ishirini na mitano
alikuwa hajawahi kupendana na mtu na hakuwai kufikiria hapo kabla, kwamba hilo
litatokea, maana watu kadhaa aliowahi kuhisi ni wema kwake wote waligeuka kuwa
wapuzi.

Yaliyomtokea Sarah kwenye maisha yake kuanzia kwenye familia yake na ndugu na
marafiki na mahusiano, yalikuwa ni simulizi ambazo yeye binafsi hakupenda
kuzisimulia kabisa, kwake zilikuwa ni simulizi za kuhuzunisha zilizomtwika donda
ambalo aliona kuwa halina siku ya kupona.
Maswahibu hayo pengine yalielezea kwanini Sarah aliishi maisha aliyoishi. Sarah
aliishi maisha ya peke yake, kwenye chumba chake kimoja alichopanga maeneo ya
Mwananyamala. Hakuwa na familia wala ndugu aliokuwa na ukaribu nao wa
kuwambilia.
 
Wazazi wake wote wawili walikuwa wamefariki akiwa binti mdogo, alichosimuliwa
tu ni kwamba wazazi wake walikuwa ni waharifu na waliojihusisha na magenge ya
kiporaji na waliuwawa katika mazingira ya kutatanisha, alikuwa na picha moja tu ya
wazazi wake ambayo Sarah siku zote aliiweka kwenye mfuko wake wa nguo.

Ndugu wawazazi wake nao walikuwa ni watu wa migogoro na ambao hawakumjali sana, hiyo
ilipelekea Sarah kuacha kuwa karibu nao pale tu alipokua na kuanza kujitegemea.

Sarah alikuwa na mtu mmoja tu aliyemuita rafiki. Naye alikuwa akiitwa Cheusi.

Japowalikuwa na ukaribu na mazoea, kitabia Cheusi hakuwa na mchango chanya kwa Sarah.
Cheusi alikuwa anajiuza. Kazi yake ilikuwa ni kuvalia mavazi mafupi na kusimama
mabarabarani akitafuta wateja wa huduma ya ngono.

Hiyo ndio ilikuwa kazi ya Cheusi,
Cheusi alikuwa anavuta bangi na kulewa sana.

Kama kuna matabia mabaya ambayo
Sarah alikuwa nayo basi inaweza kusemwa kuwa kwa asilimia fulani ilitokana na urafiki
wake na Cheusi.

Kutokana na ukaribu uliokuwepo baina yao, Cheusi alikuwa ndio mtu wa kwanza
kusimuliwa na Sarah kuhusiana na Rahim.

“Ninamuona kuwa ni mtu wa tofauti, aliniokoa nilipotaka kutoa uhai wangu, na
amenipa namba yake. Nimeongea nae anataka tuonane. Hakika anaonesha kunijali na
kunipenda.

Alisema Sarah akimwambia Cheusi. Wakati huo walikuwa ndani ya
chumba cha Sarah wamekaa juu ya godoro, wakiwa mikononi mwao wameshika glasi
za pombe wanakunywa, huku Chgeusi akiwa wakati huohuo anavuta sigara.

Uso waCheusi na msuko wa rasta zilizochakaa kichwani mwake kwa kutofumuliwa
ulimuonesha dhahiri kuwa alikuwa binti muhuni sana.
“Wanaume wote ndivyo walivyo, wanonekana wema ukiwa hauwajui vizuri, ila ni fisi
wakishakuramba”, Cheusi alimwambia Sarah, na akamuonya kujaribu kuuendeleza
ukaribu na Rahim.

Sarah hakutaka kuamini kusikia maneno ya Cheusi. “Maisha yangu yote nimekuwa
nikiishi nikiamini watu walionizunguka ni wabaya, sijawahi kuwa na mahusaino seriaz
na mtu yeyote, huyu Rahim ananifanya nione mwanga mpya, ananifanya nione kuwa
inawezekana mimi kuishi kwa furaha”, aliongea Sarah, uso wake ukiwa seiriaz akitaka
Cheusi aelewe kuwa Rahim ni mtu aliyeta nuru kwenye maisha yake.
Cheusi akafikiria jambo kidogo kisha akamgeukia Sarah na kumtazama machoni.

Aliona jinsi gani Sarah alikuwa siriaz kwa kile alichotoka kukiongea.
“Sarah, usiniambie kuwa unampenda huyo jamaa?”, aliuliza Cheusi kwa kushangaa,
“Ndio nimempenda”, alijibu Sarah. Cheusi akaweka glasi yake ya pombe chini nae
Sarah akaweka yake chini pia.
“Unatarajia nini Sarah?, mimi nilitarajia kuwa unataka umchune tu huyo jamaa,
kumbe unawaza mapenzi. Unapoteza focus. Wewe unachohitaji ni pesa kwa sasa.

Usijisahau kuwa uko kwenye matatizo makubwa. Makosa uliyofanya ikitokea
yamejulikana unaweza kupewa hukumu kubwa, wewe unachohitaji ni pesa, ili
kuendeleza ule mpango wako wa kutaka kutokomea kusikojulikana” aliongea Cheusi
kwa msisitizo
 
Cheusi aliona kuwa Sarah anataka kupoteza muda kwa kuwaza masuala ya
mapenzi badala ya kuzingatia kupata pesa na kufanya juu chini kutokomea mbali kabla
makosa yake ya kiharifu aliyofanya hayajajulikana.

“Ukiwa kwenye mahusiano, utakosa kuzingatia kutafuta pesa unazohitaji. Na huyo
mtu unaeanzisha nae mahusiano akibaini ukweli wa makosa uliyofanya na akabaini
kuwa wewe dakika yoyote unaweza kuwa chini ya ulinzi, ama kutokomea
kusikojulikana , unadhani atajali kuhusu wewe, zaidi ya sana naona ukianzisha
mahusiano unatengeneza mazingira ya kujiumiza tu maana mahusiano hayo yanaweza
kutodumu” alisema Cheusi.
Sarah alibaki anamtazama Cheusi huku akijitahidi kutomwaga machozi, Cheusi
alikuwa akimwambia jambo la ukweli.

Hapo alipo Sarah alikuwa katika harakati za
kutaka kukwepa mkono wa sheria. Kulikuwa na mawili atoroke kukimbia asikamatwe,
ama ifike siku moja polisi wanaomtafuta wampate na wamtie chini ya ulinzi kwa makosa
aliyofanya.

Baada ya kuishi miaka mingi akiamini hana nyota ya kupendwa kama watu wengine,
hatimaye Sarah alianza kupata matumaini ya aina hiyo kupitia kwa Rahim, lakini kwa
bahati mbaya haukuwa wakati sahihi.

“Sijali kuwa huu si wakati sahihi wa mimi kuwa kwenye mahisiano. Ninachojua
ninampenda huyu jamaa. Ninakwenda kuonana nae. Nitamwambia jinsi ninampenda.
Sijali kama haya mahusiano yatashindwa kuwa ya kudumu, sijali”, Sarah alimjibu
Cheusi kwa uchungu, alimaanisha kila neno aliloliongea . Yeye aliona kwamba, kuwa na
Rahim ilikuwa ni fursa pekee kwake kuishi maisha ya kawaida kama watu wengine.

Nahakujali kama mahusiano yenyewe yalionekana kutokuwa na mwendo mrefu, alikuwa
tayari kuyaanzisha, hata kama yalikuwa yakudumu kwa siku moja ama mbili.
………………………………………..


Ilikuwa ni usiku wa manane, kwenye jumba la familia ya Bi Fahima, huko
mikocheni.

Wote Rahim, Omari na mjomba wao, bwana Mrisho walikuwa wamelala
kwenye ghorofa ya pili ya nyumba hiyo kwenye vyumba vyao.
Mara katika hali isiyo ya kawaida ikaanza kusikika sauti ya kilio iliyotokea nje ya
nyumba hiyo kupitia dirisha la chumbani kwa bwana Mrisho. Ilikuwa sauti ya
mwanamke.

Awali Mrisho alidhani anaota kusikia sauti hiyo, ila akabaini kuwa yupo macho na
kweli kuna sauti ya mtu akilia, tena ilikuwa sauti ya mwanamke. “Nani analia usiku
huu?”, alijiuliza bwana Mrisho.
Alibaki kitandani akisikiliza sauti hiyo. Katika hali isiyoelezeka, Bwana Mrisho
alihisi sauti hiyo sio ngeni. Ila pia hakung’amua sauti ilikuwa ya nani hasa, akapata
shauku ya kutaka kujua zaidi ni nani huyo anayelia usiku huo wa manane.
 
Ni kama kulikuwa na nguvu ya ajabu iliyomuhamasisha ainuke toka kitandani na
aanze kuchunguza huyo anayelia ni nani.

Taratibu bwana Mrisho akainuka na kuanza kuelekea dirisha la chumba chake ili
kuchungulia huyo aliyeko nje akilia, hakuweza kuona mtu yeyote.

Mwanamke
aliyekuwa analia ilionekana alikuwa yupo upande ambao yeye hakuweza kuuona kupitia
dirisha la chumbani kwake. Mara ghafla akatoka hapo dirishani na moja kwa moja
akaelekea kwenye mlango akaufungua na kutoka nje ya chumba, akaelekea kwenye
ngazi akashuka toka ghorofani hadi sitting room na moja kwa moja akaelekea mlango
mkuu wa nyumba na kuufungua na akatoka nje, yote ilikuwa ni kutaka kujua ni
mwanamke gani huyo alikuwa akilia nje usiku huo, ambaye sauti ya kilio chake ilikuwa
sio ngeni masikioni mwake.

Alipofika nje akaanza kuangaza angaza uwanja wa nyumba
akitumaini kumuona mwanamke anayelia.

Nje ya nyumba hiyo kulikuwa na mti mkubwa wa kivuli, sauti ilikuwa ikitokea
kwenye mti hapo.

Ni kweli kulikuwa na mwanamke.
Alikuwa ni mwanamke aliyevalia mavazi meupe matupu. Alikuwa amekaa chini ya
mti huo, na alikuwa akilia kwa uchungu, huku uso wake akiwa ameuinamisha.

NaMrisho alimuona mwanamke huyo.
Taratibu Mrisho alianza kujongea kuelekea hapo mtini kumtambua huyo
mwanamake.

Taratibu kadri alivyomkaribia Mrisho alizidi kuhisi kuwa anamtambua
mwanamke huyo. Mara yule mwanamke akainua sura yake.
Basi bwana Mrisho akakutana uso kwa uso na yule mwanamke wakawa
wanatazamana.

Bwana Mrisho akatoa macho kwa mshituko. Yule alikuwa ni
mwanamke aliyemfahamu.
Huyo mwanmake mwenyewe , alikuwa ndio yuleyule ambaye alikuwa
akiwatazama Rahim na Sarah kule ufukweni kisha akatoweka.
Yule mwanamke alipoona Mrisho kamtambua aliacha kulia na uso wake wa
huzuni ukabadilika na kuwa wa hasira. Wakawa wako wawili hapo chini ya mti
wanatazamana, Mrisho akiwa na mshtuko huku yule mwanmke akiwa na hasira.
“Rabecca”, Mrisho aliiita jina la huyo mwanamke. Mara kwa ghafla kabisa yule
mwanamke akatoweka.
Mara ikasikika sauti ikimuita Mrisho. “Mjomba. Mjomba kuna nini hapo usiku
huu?”, hiyo ilikuwa ni sauti ya Rahim, akimuita mjomba wake akitokea barazani
kwenye mlango mkuu wa nyumba, huku akifikicha macho kwa mkono wake kutokana
na usingizi.

Mara mlinzi wa nyumba nae akafika eneo hilo maana alisikia sauti zao muda huo
wa usiku wa manane.

“Bwana Mrisho kuna nini?” aliuliza mlinzi, “Nimekusikia unamuita mtu, umeita
Rebecca”. Mrisho akawa hana la kujibu.
 
Rahim akashuka toka barazani alipokuwa kasimama hadi kwenye mti
aliposimama mjomba wake. “Rebecca ni nani? mimi mwenyewe nimesikia ukiita hilo
jina”, Rahim alimuuliza mjomba wake.

Kwa namna fulani Mrisho alionesha kuwa kidogo kachanganyikiwa. Halikuwa
tukio la kawaida kumuona yule mwanamke.

Na aliona kabisa hata kama angewasimulia
bado wasingemuelewa na wangeona anasimulia vitu vya kufikirika.
Ila akaamua kuasimulia, “Kulikuwa na mwanamke analia, alikuwa kakaa hapa
kwenye mti, alikuwa analia ndio maana hata nikawa nimeamka kutoka ndani”.

Rahim na mlinzi wote walikuwa hawamuelewi. Walimuona hayuko sawa.

Mwanamke gani huyo alikuwa analia, wao hawakusikia sauti ya mwanamke yeyote akilia.

“Mjomba Mrisho, ulikuwa unaota”, alisema Rahim, “unajua kama kwenye tivii wale
wanaoota huku wanatembea, basi ndio wewe leo umeota ndoto ya namna hiyo”
alimalizia, huku mlinzi alionekana kukubaliana na ung’amuzi wa Rahim kuwa kweli
Mrisho siku hiyo alikuwa ameota zile ndoto za mtu anaota huku anatembea.

Mrisho alichanganyikiwa zaidi. Alijua kuwa alichokiona hakikuwa ni ndoto kilikuwa
ni ukweli tupu, kwamba kulikuwa na mwanamke anayelia kwa sauti, tena alimfahamu
kwa jina kabisa kuwa aliitwa Rebecca.

Lakini hakuwa na namna ya kuwaaminisha
Rahim na mlinzi kuwa huyo mwanamke alikuwapo hapo kweli. Wao hawakusikia hiyo
sauti, na huyo Rebecca alikuwa katoweka.

Ilikuwa ni hali ya kushangaza na wasingeweza
kumuamini kabisa.
Rahim na mlinzi waliamini kilichotokea ilikuwa ni bwana Mrisho alikuwa anaota, ila
yeye Mrisho alikuwa kaelewa hasa aliloliona.

Yeye alijua ukweli kuwa, mzimu wa
mwanamke aliyefariki zamani ulikuwa umemtokea siku hiyo.
Yani yule mwanamke wa ajabu ambaye Mrisho alikuwa kamtambua kwa jina la
Rebecca kisha akatoweka, ulikuwa ni mzimu wa mwanamke huyo, kwa maana yule
mwanamke, Mrisho alikuwa anamfahamu na alikuwa amefariki miaka takribani ishirini
na tatu iliyopita.



Lililotokea usiku huo halikuwa dogo kwa Mrisho na lilimfanya kuchanganyikiwa,
kwa haraka akawaacha Rahim na mlinzi hapo chini ya mti uwanjani na haraka akapanda
barazani kisha akaelekea mlango wa nyumba na kuingia ndani hadi ghorofani kwenye
chumba chake na kujifungia, huku akiwaza na kuwazua juu ya mzimu aliouona.



Inaendelea.....................
 
Mwandishi: Nasri Mgambo
Simulizi: TUBU
Sehemu: Ya Nne

4. KAZI YA SARAH


Rahim hakuamini kile alichosema mjomba wake kuwa aliona mwanamke akilia
chini ya mti usiku uliopita.

Yeye aliamini kuwa mjomba wake aliota tukio hilo. Ila bado
kichwani mwake alibaki akifikiria mjomba wake alichosedma. Alikuwa akifikiria tukio hilo asubuhi alipokuwa akinywa chai. Omari ambaye jana
yake hakusikia chochote alifika hapo kwenye meza ya chakula ili nae apate kifungua
kinywa.

“Unalala kama umekufa, hukusikia chochote jana usiku”, Rahim alimwambia
mdogo wake huku akimtazama alivyokuwa akimimina chai kwenye kikombe.

“Jana usiku kulitokea nini?, mimi sikusikia chochote maana nilichelewa kulala, nilikuwa hoi, nikalala fofofo, nisingeweza kusikia chochote” aliuliza Omari.

“Usiku wa manane mjomba aliamka na kwenda pale nje kwenye mti na kumuitilia
mwanamke kwa jina la Rebecca, nilipotoka nje hakukuwa na mtu yeyote zaidi yake” alisimulia Rahim, na kuendelea, “hata mlinzi hakumuona mtu yeyote, mimi nadhani
alikuwa anaota, japo yeye anasema ni kweli aliona mwanamke akilia pale”.

Omari aliona hilo ni tukio la ajabu na alikubaliana na Rahim kuwa huenda
mjomba wake alikuwa anaota huku anatembea hadi akatoka huko nje. Baada ya
kumaliza kunywa chai yake, Rahim alimuaga Omari na kutoka na kuelekea kwenye
safari yake ya siku hiyo..

Mchana wa siku hiyo ulikuwa wa furaha kwa Rahim, maana yeye alikuwa
anakwenda kukutana na Sarah. Walipanga watoke out siku hiyo, wazungumze.

….…………………….


Sarah alikuwa amekaa kwenye kitanda, akijipodoa podoa baada ya kutoka kuoga.

Huku kavalia kagauni kazuri kafupi chekundu. Mashuka yaliyotandikwa kwenye
kitanda yalikuwa yameandikwa jina la gesti, ‘Sinza Guests Lodge’.

Chini sakafuni kwenye chumba hicho kulikuwa na nguo za kiume, yani, suruali, mkanda, shati, pia viatu vya kiu
 
Sauti ya maji kutiririka ilisikika toka kwenye bafu la chumba hicho. Kulikuwa na
mtu anaoga.

Kisha sauti ya maji ikakata. Mara mlango wa bafu la chumba
ukafunguliwa, na kutoka bafuni akatoka jamaa, mbaba wa makamo. Kwa kumtazama
tu alikuwa ni sawa na umri wa kuwa mzazi wake na Sarah.

Sarah alikuwa kamaliza kujipodoa, akamrushia macho huyo mbaba aliyetoka bafuni, huku kajifunga taulo kiunoni.

“Nini?, mbona unaniangalia hivyo?”, jamaa huyo alimuuliza Sarah. “Unanichelewesha, kuna sehemu natakiwa niwahi, naomba unilipe hela yangu
niende” alijibu Sarah, uso wake ulionesha kabisa alikuwa anajiamini kwenye mazingira
hayo na ni mzoefu.

Jamaa akacheka na kuendelea kuongea, “Nilidhani labda tutakaa humu pamoja
siku nzima hadi jioni?, kwani unawahi wapi?” jamaa aliuliza.

“Natamani kama ingewezeakana kushinda hapa kutwa nzima, ila nakujua , hela
yako ya mawazo hauna hela ya kunifanya mimi nishinde hapa kutwa nzima, hivyo nilipe
ninchokudai hadi sasa, nisepe”, aliongea Sarah huku kakaza uso.

Jamaa akajikuta kapoteza tabasamu, aliona kuwa Saraha alikuwa yuko siriaz anataka
kupewa hela yake asepe.


Kuepuka shari zaidi akaokota suruali yake toka sakafuni na
kuingiza mikono kwenye mfulko wa suruali na kutoa waleti kisha akatoa humo fedha, notinoti nyekundu na kumpa Sarah.

Sarah nae akapokea pesa hiyo kisha akatabasamu. Akainama kuvuta viatu vyake virefu vyekundu na kuanza kuvivaa. Kwa kifupi ni kwamba Sarah alikuwa anajiuza. Hiyo ndiyo ilikuwa kazi yake.

Naalishakuwa mzoefu wa kazi hiyo. Ilikuwa ni moja ya makandokando mengi ya hovyo
kwenye maisha yake.

Baada ya kuvaa viatu vyake na kuagana, Sarah alitoka kwenye hicho chumba cha
gesti. Ilikuwa ni moja ya gesti kwenye mitaa maarufu ya Sinza.

Sarah alikuwa na miadi ya kuonana na Rahim mchana wa siku hiyo na aliona kama
anakaribia kuchelewa hivyo alipofika kwenye barabara harakaharaka akaita bodaboda
na kuomba apelekwe maeneo ya Mlimani City, mahala ambapo yeye na Rahim
walipanga kukutana

….………………………


Rahim alikuwa ameshafika kwenye mgahawa ambao yeye na Sarah walikuwa
wamepanga kuonana.

Robo saa ilikuwa imepita na Sarah alikuwa bado hajawasili. Mgahawa wenyewe ulikuwa na madirisha makubwa ya kioo. Hivyo Rahim aliyekuwa
kakaa meza ya pembeni aliweza kuona nje kupitia dirishani.

Alikaa hapo akitazama nje
akitegemea kumuona Sarah akiwasili muda wowote.
 
Muhudumu akiwa ameshika sinia ya kubebea vinywaji alifika kwenye meza ya
Rahim na kumuwekea glasi mbili za juisi.

Mara kupitia kwenye kioo Rahim aliona bodaboda iliyombeba Sarah ikiwasili.

Akajikuta akifurahi na kukenua meno, hatimaye Sarah alikuwa amefika.

Akabaki
anamtazama jinsi alivyomlipa bodaboda na kuanza kuelekea kwenye lango la mgahawa
ili kuingia ndani.

Sarah alipofika ndani ya mgahawa aliangaza angaza macho yake kujua
alipokaa Rahim na hatimaye alimuona sehemu aliyokaa akampungia mkono na kuanza
kuelekea kwenye meza hiyo
Gauni lake fupi jekundu na viatu virefu na nywele zake laini alizozichana zilimfanya
Sarah aonekane mrembo sana.

Taratibu aliifikia meza aliyokaa Rahim na kukaa kisha
akavua pochi yake ya begani na kuiweka chini.

“Nimechelewa sana?”, aliuliza Sarah, “Hapana, umechelewa kama dakika kumi na
tano, usijali”, alijibu Rahim, na kuendelea, “ungekubali nikupitie na gari yangu , tungekuwa tumefika mapema ila haukutaka”.

Sarah alikataa kupitiwa na Rahim, ambaye alikuwa na gari yake, kwa madai kuwa
hakutaka kumsumbua. Kumbe alikuwa na mambo yake mengine ya ajabu na
hakutokea alipokuwa akiishi. Rahim alimuona Sarah yuko tofauti mchana huo, kwa mara ya kwanza aliona jinsi
ambavyo binti huyo alivyokuwa mrembo akiwa amevalia mavazi mazuri ya kutoka out.

Sarah alionekana wa kisasa na mrembo kwa jinsi ya alivyokuwa amevalia. Rahim akawa
amevutiwa zaidi na Sarah.

“Nataka kukwambia kuwa nimetokea kukupenda”, alisema Rahim akimwambia
Sarah, “Nataka uwe girlfriend wangu” alimalizia Rahim. Hatimaye alimuambia Sarah
lililokuwa moyoni mwake.

Kauli hiyo ya Rahim ilimfurahisha sana Sarah maana hata yeye binafsi alikuwa
amemzimikia. Sarah alijiona kama yuko ndotoni. Hakuwahi kumpenda mtu jinsi hiyo
kabla ya hapo, na hakuwahi kukutana na mtu ‘gentleman’ kama Rahim kabla ya hapo.

Ndio, alijua kuwa haoti, lakini bado kimoyomoyo alijiuliza kama anaota ama la, hata
akashindwa kumjibu Rahim kama amekubali kuwa girlfriend ama la, akaishia
kumuuliza swali. “Uko siriaz?’, Sarah alimuuliza Rahim, huku uso wake ukiwa umewaka kwa
tabasamu la furaha.

Rahim akamjibu , “Niko siriaz nakupenda sana Sarah”. Kwa hakika wote wawili walikuwa wamezama kwenye hisia nzito za kupendana, ijapokuwa walikuwa wamefahamiana kwa muda mfupi tu.

Basi wakatumia mchana huo kula hapo mgahawani wakiongea na kuulizana mambo
mbalimbali.

Sarah aliepuka kuongelea juu ya familia yake, ama kuhusu watu anaoishi
nao na mitaa anayoishi.

Wakati Rahim alitumia muda mwingi kumsimulia Sarah stori
za kuchekesha kuhusu familia yake, na kumfanya Sarah acheke sana.
 
Rahim alikuwa akisimulia jinsi mama yake alivyokuwa makini kupitiliza,

“Mama
yangu ni mtu ambaye muda wote anaishi kwa kufuata kanuni, kila kitu anataka kiwe
perfect”, alisimulia Rahim, “kuna muda huwa anafurahisha sana, zamani nilipokuwa
shule nakumbuka kuna siku nilikuwa nimepata maksi za juu sana ila nikawa
nimemficha sikumwambia nimepata maksi ngapi, basi kidogo presha impande, alidhani
nimefeli, yuko, Rahim unanichanganya, itabidi nikutafutie shule mpya, tusheni mpya, mara, itabidi nikutengenezee ratiba ya kujisomea, lazima ufaulu kama watoto wa rafiki
zangu huwezi kuwa wewe ndio kilaza”, alimalizia Rahim huku Sarah akiwa anacheka
sana kwasababu ya masimulizi hayo.

Sarah alifurahi sana kusikiliza simulizi za Rahim kuhusu familia yao, ilikuwa ndio
mara ya kwanza kwake, kukutana na mtu wa aina ya Rahim, yani, kijana wa kishua toka
familia yenye uwezo, msomi na mstaarabu.

Yeye Sarah hakuwa na simulizi za aina hiyo, ulimwengu wake ulikuwa wa tofauti sana, yani, ulimwengu wa mjini mjini, wa waharifu, wa kukimbia polisi na maisha ya hali na kipato cha chini. Muda wote wakiwa hapo mgahawani, Sarah aliepuka kusimulia lolote juu ya maisha
yake binafsi, hata Rahim aligundua hilo, akauliza, “Niambie kuhusu wewe, ndugu zako
na unapoishi. Kwanini hutaki kuongea lolote kuhusu wewe binafsi?, kwanini unaficha
sana?”.

Sarah hakutaka kujibu hilo swali, akajibaraguza, kwa kujibu “ aah, mimi stori ya
maisha yangu itakuboa. Na sio msimuliaji mzuri’.

Rahim hakutaka kumuuliza Sarah
zaidi, hakutaka kumbugudhi, alitaka kujua zaidi juu ya maisha ya Sarah lakini alitaka
Sarah afanye hivyo kwa maamuzi binafsi sio kwasababu kamsukuma, alitaka Sarah
ajione yuko salama akiwa naye.

Basi Rahim akanyanyua mikono na kisha kushika viganja kwa Sarah hapo juu meza, wakawa wameshikana mikono, wakitazamana.

“Nataka ujione kuwa uko salama kuwa namimi.

Na sijui umepitia nini kwenye
maisha yako na ninataka kujua, ila pia nataka unisimulie pale utakapoona uko tayari
kunisimulia”, aliongea Rahim akimhakikishia Sarah kuwa yuko salama kuwa nae na
hatomlazimisha asimulie juu ya maisha yake hadi pale Sarah mwenyewe atakapokuwa
tayari kusimulia.

Basi Sarah akazidi kumuona Rahim kuwa ni gentleman, na kuzidi
kuvutiwa nae.
Inaendelea……………………………
 
Jina La Simulizi: TUBU
Mwandishi: Nasri Mgambo
Sehemu ya 5: Sio Chizi



Ulikuwa ni ulimwengu mpya umefunguka kwa Sarah. Rahim alimletea mtazamo
mpya kabisa wa maisha.

Yeye hakuwahi kuwa kwenye hisia nzito za mapenzi wala kuwa
kwenye mahusino siriazi na mtu yeyoyote kabla ya hapo, hivyo mahusiano mapya yake
yeye na Rahim yalimfanya ajione kama yuko ndotoni.

Alijiona yuko kwenye ndoto nzuri ambayo hakutaka kuamka. Mahusiano hayo mapya
yalimfanya asahau shida na visanga vyake vya maisha.

Wiki kadhaa zilipita, na mapenzi baina yake Sarah na Rahim yalipamba moto. Na
Sarah alitamani hali hiyo idumu kuanzia wakati huo hadi milele. Ila, ukweli wa mambo ulikuwa tofauti, ijapokuwa mapenzi mapya yalimpa Sarah
mtazamo mpya juu ya maisha na mahusiano bado moyoni na akilini mwake aliendelea
kubeba mizigo yake ya hofu na uoga na hakuwa huru kuruhusu Rahim ajue undani
hasa wa maisha yake.

Na kubwa kuliko ni kwamba Sarah hakutaka kabisa Rahim ajue yeye anafanya kazi
gani. Hakutaka kabisa Rahim ajue hilo, kuwa alikuwa analala na watu ili apate pesa. Rahim mwenyewe alikuwa kazama kwenye kina kirefu cha mapenzi. Ijapokuwa
alinotisi jinsi Sarah hakuwa huru kuelezea sana juu ya maisha yake na alifahamu wazi
kuwa Sarah hakutaka kabisa yeye apafahamu mahala alipokuwa anaishi, kwake
hakuona kuwa suala hilo ni kikwazo kwenye mahusiano yao.

Moyoni mwake aliamini
siku itafika na Sarah atakuwa huru kumueleza juu ya maisha yake.

Na siku zote Rahim
alikuwa akimhakikishia Sarah kuwa hatomlazimisha kumwambia ukweli juu ya maisha
yake hadi Sarah mwenyewe atakapokuwa huru na hiyari kumueleza kila kitu.

Hakika zilikuwa ni akili za ajabu, ila ndio mapenzi tena yalikuwa yamemkolea Rahim, ni kama alijipachika kibanzi jichoni mwenyewe kwa kutotaka kuchimba habari na
historia ya Sarah.

Rahim hakufahamu hata rafiki yeyote wa Sarah, ila yeye Sarah alifahamu baadhi ya
rafiki wa Rahim ambao alikutana nao mara nyingi walipokuwa wanatoka, ikawa hivyo
hadi siku moja bila kutarajia Cheusi aliyekuwa rafiki yake na Sarah alipokutana nao kwa
bahati mbaya kwenye karamu ya siku ya kuzaliwa ya moja ya rafiki zake na Rahim
 
Ilikuwa ni majira ya jioni siku hiyo, Sarah alifika hapo kwenye bethdei pamoja na
Rahim ili kula, kunywa na kufurahi. Na alikuwa amekalia kwenye kochi huku kashika
kinywani mkononi,

pembeni yake walikaa wasichana wengine ambao nao walikuwa
wakiongea na kufurahi, pembeni yao kulikuwa na wavulana na wasichana wengine
waliosimama, waliokuwa wakiongea wengine wakicheza mziki uliokuwa ukisikika toka
kwenye spika za mahala hapo, huku wakinywa vinywaji, Rahim alikuwa amesimama na
kinywaji chake akipiga soga na baadhi ya rafiki zake, huku mziki mzuri ulisikika toka
kwenye spika za mahala hapo.

Usoni Sarah alionekana kuwa na furaha kuwa mahala
hapo, muda wote alimtumpia macho Rahim na watu wengine wote waliokuwapo hapo
wakifurahi.

Mara ghafla ikasikika sauti, “Joji, Joji mwanngu mwenyewe happy birthday bro”, ilikuwa sauti ya kiume ikitokea toka kwenye mlango wa mahala hapo, wote wakatupia
macho mlangoni, na kumuona jamaa mmoja mrefu mweusi mwenye makelele akiwa na
furaha akiingia ndani huku kaongozana na watu kadhaa, huyo alikuwa ni moja ya
marafiki waliokuwa wakiwasili kwenye hiyo bethdei.

Rahim na marafiki wengine wakawaka kwa furaha kumuona, nao wakayapokea
makelele yake kwa kelele, “Ayaa, mnyama umefika hahaha, mbona unachelewa wewe”, alisikika Joji ambaye hiyo ndio ilikuwa siku ya bethdei yake.

Basi, kukawa na kelele za
furaha tu mahala hapo, macho yote yakawa kwa huyo jamaa aliyeingia na watu
alioongozana nao, mmoja wa watu hao alikuwa ni wa kike.

Sarah alipomtazama huyo dada aliyeingia mahala hapo mara moja alimtambua, kuwa
alikuwa Cheusi, rafiki yake, waliyeishi wote huko mitaa ya mwananyamala. “Cheusi
amefuata nini hapa?”, alijiuliza Sarah.

Cheusi siku hiyo alikuwa kavalia kagauni kafupi, uso wake wake ulionesha dhahiri
kuwa tayari amekunywa kidogo.

Sarah hakutaka uwepo wa rafiki yake huyo mahala hapo, alikaa kwenye kochi na glasi
yake akimtazama Cheusi, huku akiomba rafiki yake huyo asimuone wala asimkaribie.

Sarah alimfahamu rafiki yake kwa tabia ya kuropoka, hakutaka Rahim amfahamu
Cheusi.

Asichokitaka kutokea ndio kikatokea Cheusi alimuona Sarah hapo kwenye kochi na
mara uso wake ukakenua kwa tabasamu na kuelekea hapo Sarah alipokuwa amekaa, alipofika akakaa pembeni yake kabisa, “Sarah unafanya nini huku?” aliuliza Cheusi, Sarah hakuwa na la kufanya , “ nikuulize wewe umefuata nini huku?”, alijibu Sarah kwa
kuuliza swali kama hilo hilo. “Umemuona yule jamaa niliyeingia nae, mteja wangu yule huwa anapitaga kwenye
kona zetu za kazi, anapenda ngono balaa, na ni wa kishua sana, halafu ni kama
nimemuelewa kimtindo na mimi nimemganda”, aliongea Cheusi akimwambia Sarah.

Sarah akaweka glasi kwenye meza, kisha akamgeukia Cheusi akiongea kwa usiriazi, “Cheusi, nakuomba eneo hili usiongelee masuala yahusianayo na kazi tunayofanya, niko hapa na rafiki yangu niliyekwambia anaitwa Rahim, sitaki ajue kuwa ninafanya kazi
ya kujiuza, naomba unyamaze, kama unaongea ongea kama mtu ambaye hatufahamiani sana”,

aliongea Sarah kwa hasira kidogo, alitamani ajifanye hamjui Cheusi kwa wakati
huo lengo likiwa ni Rahim asijetokea kufahamiana na Cheusi na kuja kujua ukweli wa
kazi yao wanayofanya.

Wakati wowote aliokuwa na Rahim, Sarah alifuta na
kujisahaulisha mambo yote yaliyohusu kazi na maisha yake binafsi hakutaka Rahim ajue
sehemu hiyo ya maisha yake.
 
Alichokitaka hakikupangwa kuwa, kwasababu Rahim alikuwa ameshawaona
wakiongea hapo kochini na akang’amua kuwa wanafahamiana, taratibu na glasi yake
yenye kinywaji ikiwa mkononi , Rahim alifika kwenye kochi, “Sarah naona umekutana
na mtu unayemfahamu”,

aliongea Rahim na kukaa kwenye kochi pembeni ya Sarah, basi Sarah akawa yuko kati, kushoto yuko Rahim, kulia yuko Cheusi. Akawa hana la
kufanya akabaki akijibaraguza tu.

“Rahim, huyu ni rafiki yangu, anaitwa Cheusi”, Sarah alimtambulisha Cheusi kwa
Rahim, aliona hakuna namna nyengine tena ya kutaka kujifanya hamjui Cheusi.

Hivyo
ndivyo Cheusi alivyokutana na Rahim, bila ya Sarah kupenda. ….………………….


Wakati dunia ya Rahim na Sarah ilikuwa ikikolea kwenye mahaba baina yao, mambo ya mauzauza nayo yaliendelea kwenye dunia ya bwan mrisho;


Usiku mmoja, Mrisho alikuwa amelala kitandani chumbani kwake akiweweseka, alionekana dhahiri kuwa alikuwa akiota ndoto mbaya. Ghafla akashtuka na kuamka toka kwenye ndoto hiyo., macho yakiwa yamemtoka.

Akajiinua na kukaa hapo kitandani. Hali hiyo ya kuota ndoto mbaya na kushtuka haikuwa kitu cha mara ya kwanza
kumtokea.

Tangu siku ile aliyoamka usiku akisikia sauti ya mwanmke akilia na akatoka
nje hadi chini ya mti na kukutana na mwanamke aliefariki zamani, basi hali hiyo ya
mandoto mabya na mauzauza ikawa ndio ada ya maisha yake. Kichwani mwake bwana Mrisho, kumbukumbu za matukio ya miaka ishirini na tatu
nyuma zilikuwa zikijirudia. Matukio hayo ndiyo ambayo yalikuwa yanapelekea
mauzauza yote yaliyokuwa yanamrandia na kumsumbua Mrsiho, hata usingizi wa amani
hakuwa akiupata tena, ilikuwa ni ndoto za ajabu na kusikia sauti za kilio za mwanamke
ambaye aliitwa Rebecca enzi za uhai wake.

Mrisho alikumbuka jinsi alivyofahamiana na mwanamke huyo zaidi ya miaka ishirini
na tatu iliyopita.

Kumbukumbu ilimjia kichwani, kama video kwenye runinga, alikumbuka siku yeye na watu kadhaa walikuwapo sebuleni nyumbani mtu fulani, wakiongea huku mziki mzuri wa miaka hiyo ya tisini mwishoni ukisikika toka kwa spika
za sebuleni hapo.

Wote sebuleni walikuwa wakiongea kwa furaha wakifurahia mziki, baadhi walisimama na kucheza. Jamaa mmoja aliyekuwa kafurahishwa na wimbo huo
akanyoosha mkono kwa mpezi wake aliyekuwa kakaa kwenye kochi akimuashiria
ainuke ili wacheze wawili pamoja,

huyo mwanamke mwenywe aliyeombwa kucheza
alikuwa ni Rebecca, na jamaa huyo alimuomba kucheza aliitwa Frank Noah Malya.
 
Mrisho alikumbuka vizuri siku hiyo jinsi Rebecca na Frank walisimama na kucheza
kwa furaha huku wao- watu wengine, wakiwaangalia na kufurahia kuwatazama jinsi
walivyokuwa wakicheza kwa furaha.

Mrisho alikuwa amekumbuka mbali sana, alikumbuka enzi za uhai wa Rebecca na
mpenzi wake wa kipindi hicho bwana Malya. Ilikuwa ni enzi zao za ujana. Na Mrisho
alimfahamu Rebecca kupitia kwa Frank.

Yeye Mrisho na Frank walikuwa
wakifahamiana kwasababu walifanya kazi chini ya mtu mmoja. Kazi zenyewe walizomfanyia huyo mtu zilikuwa ni kazi haramu, ambazo baadae
zilikuja kuwaletea mtafaruku mkubwa na kuleta mwisho mbaya.

Mrisho alibaki kitandani akiwaza kumbukumbu hizo za miaka mingi iliyopita, ambazo hakudhania kuwa anazikumbuka, ilikuwa ni miaka mingi sana. Kelele za ajabu
na kutokewa na mzimu wa Rebecaca chini ya mti nje ya nyumba yalikuwa ni matukio ya
ajabu ambayo yalirejesha kumbukumbu za matukio ambayo yeye Mrisho hakutaka
kamwe kuyakumbuka, ilikuwa ni miaka mingi imepita na alishaendelea na maisha yake, ukurasa wa mtindo wa maisha na matukio ya maisha yake ya miaka hiyo alishaamua
kuufunga zamani sana.

Sasa kwanini, kumbukumbu za miaka ya tisini na elfu mbili zilikuwa zinamrejea sasa
na sio kabla ya hapo?, na kwanini mzimu wa Rebecca ulimtokea na kulia kilio sasa na si
miaka yote hiyo iliyopita?, na kwanini ndoto za ajabu ajabu zilikuwa zinamsumbua sasa, baada ya miaka zaidi ya ishirini na zaidi kupita?, kwanini hayo yote hakuyapitia huko
awali mpaka yaanze kuja kumsumbua sasa?, Mrisho alijiuliza maswali hayo.

Kijasho chembamba kilimchuruzika pembeni ya sikio, lilikuwa sio jasho la kazi
ngumu, hapana, lilikuwa ni kijasho cha mawazo, aliyowaza kichwani mwake, akiwa
kakaa kwenye kitanda chake hapo chumbani.

Mara akaanza kuiskia ile sauti ya Rebecca akilia ikisikika tena.

Ilikuwa ni sauti
inayokera, na kutisha, yani sauti ya mtu aliyefariki miaka ishirini na tatu iliyopita. Ilikuwa ni sauti iliyombughudhi Mrisho hapo kitandani.

Na hiyo haikuwa mara ya
kwanza yeye kuisikia hiyo sauti kwa siku kadhaa zilizopita na alifahamu hiyo sauti
haitakoma kusikika chumbani na kwamba hatoweza kulala tena usiku huo. Basi akaamua kutoka humo chumbani, akainuka haraka toka kitandani, akafungua
mlango wa chumba na kutoka akaelekea kwenye ngazi za nyumba na kuanza
kuteremka chini toka ghorofani akafika hadi kwenye sehemu ya chumba cha meza ya
chakula.

Sauti zikawa zimekoma kusikika mahala hapo. Matukio haya ya ajabu yalimtesa sana Mrisho.

Alikuwa kayachoka.

Yalimchanganya
akili na kumfanya aanze kujiona kama kachanganyikiwa, pengine alianza kujiona kuwa
uchizi unamuanza kwa kusikia kelele hizo za ajabu.

Mara machozi yakaanza kumtiririka
toka machoni mwake, akajikuta akiinua mikono yake na kuiweka usoni akilia, na
akaanza kuongea peke yake, “Unanitafutia nini wewe mwanamke, unanitafutia nini, si
ulishakufa miaka mingi imepita, unanitafutia nini?”, alilia Mrisho.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom