Simulizi: Siku yangu ya Kufa Ilipita

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,339
51,884
SIKU YANGU YA KUFA ILIPITA.

Na, Robert Heriel

Siku ile SIRIEL ndiye Huyo mficha Siri za mungu alinijia nyakati za usiku nikiwa nimelala, alikuja kama ndoto usingizini, nami sikujua yakuwa nilikuwa naota au nilikuwa katika matendo halisi. Lakini nilimuona kwa macho yangu, na hata hivi leo ninamkumbuka.

Alikuwa na umbo la kibinadamu lenye pembe tatu, kila pembe kulikuwa na bawa moja, hivyo alikuwa na mabawa matatu. Uso wake ulikuwa wa siri sana. Ulikuwa uso wenye fumbo ambao ulibeba macho mawili, pua na mdomo. Alikuwa na umbo kubwa lenye urefu wa futi kumi na nne kwenda juu na upana wa futi tatu na nusu. Rangi yake ilikuwa ya kijivu. Kichwani alikuwa na Upaa wenye nywele chache za rangi ya huzurungi.

Basi akaitoa mikono yake mitatu iliyokuwa ndani ya mabawa; kwani kila bawa lilikuwa na mkono. Akaninyoshea mkono wake akinikazia macho yake makubwa yenye rangi ya damu na mboni nyeusi. Moyo wangu ukazimia kwa hofu, nikaogopa kwani nilijua ule ndio mwisho wangu, na yule niliyemuona ndiye mtoa roho.
Lakini ajabu ni kuwa Siriel alinyanyua mdomo wake akasema;

"Nimekuja kwa amani Taikon, usiwe na hofu kwa maana nimekuja kukukimbiza na kifo. Nawe utaitwa Aliyekimbia kifo. Jina langu ni Siriel, Mficha Siri za mungu. Amka Tuondoke" Sauti yake ilikuwa kama fumbo lisiloelezeka, maneno yake yalikuwa ya siri, ajabu alinifanya nielewe.

Nikampa mkono wangu wa kuume, naye akanipokea na kunivuta kwa nguvu kutoka kitandani. Kisha nikarushwa kama upepo lakini kumbe bawa lake tayari lilikuwa limenidaka na mkono wake ukanikamata kwa nguvu nyingi. Hapo moyo wangu haukuwa na nguvu tena ya kudunda, wala macho yangu hayakuweza kuona tena, hatimaye nilipoteza akili yangu kwenye giza totoro, hapo nikazirai.

Kitambo kidogo nisichoweza kukumbuka kilikuwa muda gani nikazinduka. Hapo nilijikuta nipo kwenye nchi tambarare yenye ardhi yenye nyufa nyufa: ardhi yenye rangi kama chokaa iliyofifia, mbele yangu kama maili ishirini naliuona mlima mdogo wenye urefu kwenda juu sawa na mita elfu mbili hivi. Hapakuwa na giza wala halikuwepo jua; Nikashindwa kuelewa ile ilikuwa ni alfajiri au ilikuwa ni jioni.

Hapakuwa na upepo, na juu yalikuwepo mawingu yaliyojitenga tenga na kuachia anga la samawati kuonekana.

Nikageuka kushoto na kulia wala hapakuwa na mtu, wala yule Siriel sikumuona. Tena nchi ile ilifanana na nchi ya wafu, nilihisi huenda haya ni makazi mapya ya wafu ambapo mimi ndio nitakuwa mfu wa kwanza kupelekwa mahali pale. Jambo lililonifanya nigundue kuwa nchi ile ilikuwa ni nchi ya wafu ni mazingira yake jinsi yalivyokuwa. Hapakuwa na mti wowote wa kijani isipokuwa visiki vya miti vya zamani vilivyokauka ambavyo vilikuwa vimeachana kwa umbali. Nyasi zilikuwa zimekauka siku nyingi mno.

Nikatembea ningali nikitazama huku na huku nione kama ningemuona mtu yeyote Lakini sikumuona mtu wala sikuona kiumbe yeyote mahali pale. Moyoni mwangu nikajisemea; Nipo nchi ya wafu, sasa wafu wengine watakuwa wapo wapi.

Basi nikatembea nikiufuata ule mlima kwa zaidi ya maili tano mpaka nilipochoka. Nikahisi Mkojo umenibana, nikachojoa nguo kisha nikakojoa. Looh! Nilipokojoa ghafla tetemeko kubwa likapiga. Nyufa za ile ardhi zikaongezeka. Natazama nikaona pale nilipokojolea pakipasuka pasuka na kwa hamaki na tisho Kiganja chenye vidole vilivyogawanyika kikatokea. Hapo wasiwasi ukanivaa kwa nguvu. Nikarudi nyuma nyuma huku nikitazama jambo hilo la kutisha.

Punde ardhi ilipasuka na Siriel alitokea. Alikuwa amejaa matope; Nilifikiri matope yale huenda yamesababishwa na Mkojo wangu. Niliogopa mno, kitendo cha kumkololea Siriel nilikiona kama kosa baya lisiloweza kusameheka.

Nilishangaa kumuona Siriel akicheka kwa nguvu hali iliyosababisha mawingu ya angani kugongana na radi kutokeo. Hii iliniambia jambo moja kuwa Siriel alikuwa na nguvu na uwezo mkubwa sana. Basi akaniambia nimfuate, nami nikamfuata.

Tulitembea kuufuata ule mlima. Wote tulikuwa kimya yeye akiwa mbele mimi nikiwa nyuma yake. Siriel hakuwa na mavazi, Mbawa yake ndio yalikuwa kama nguo kwake. Miguu yake ilikuwa ya pembe tatu, huku akiwa na kidole kimoja kilichokuwa kwenye pembe ya mbele ya nyayo zake. Nilishangaa sana, nilimuona kama kiumbe cha ajabu.

Nikatamani nimuulize kule tunapoelekea ni wapi, lakini akili yangu ikanionya. Ilinibidi nimfuate kama bendera ifuatavyo upepo.

Tulifika. Kisha akasema;
" Nimekukimbiza huku nyuma ya jua, kusiko na giza wala mwanga. Huku nimekuleta ili umkimbie Zeruel ambaye ametumwa kuchukua roho yako"
Hapo nikashtuka kusikia maneno hayo, yalikuwa maneno yaliyoifanya akili yangu ichanganyikiwe.

Kisha akachora pale chini umbo la mstatili lenye urefu wa nchi 50 na upanda wa nchi 30. Kisha akatembea mate lile umbo. Ghafla nikaona picha ya video pale chini kwenye lile umbo la mstatili.

Ilikuwa video iliyowaonyesha viumbe mfano wa malaika wenye mbawa. Viumbe wale walikuwa wamegawanyika, wapo walioluwa na mbawa mbili, wapo waliokuwa na mbawa nne, wapo waliokuwa na mbawa sita. Aliyekuwa na mbawa tatu alikuwa ni mmoja. Huyo nikataka kujua anaitwa nani kwa maana alikuwa akifanana na Siriel kwa maumbile.

" Huyo mwenye mbawa tatu ni nani?" Nilimuuliza " Huyo anaitwa KaaSiriel, ni pacha wangu. Hao wenye mbawa mbili wanaitwa Dharawidi, hawa wenye mbawa nne wanaitwa Fazawidi, wenye mbawa sita huitwa Tauwidi. Sisi wenye Mbawa Tatu tunaitwa Siriuwidi"

Siriel aliongea akitazama ile video pale chini ya ardhi. Maelezo hayo yalinivutia sana, nilitamani kujua habari za viumbe hao.Kisha Siriel akaniambia;
"Huyu ndiye Zeruel, huyu ni mtoa roho"
Hapo nilimtazama huyo Zeruel pale kwenye video. Alikuwa ni jamii ya Tauwidi yaani wenye mbawa sita na mikono miwili. Alikuwa kabiba karatasi iliyokunywa kama bomba.

"Hicho alichobeba Zeruel kinaitwa 'Lauta Bagama' ambayo inamajina ya siku hiyo ya watu atakaowachukua roho zao"
Siriel aliongea akimtazama Zeruel. Hapo nikamuona Zeruel kupitia video akiondoka kwa namna ya ajabu na mbawa zake. Mwendo wake ulikuwa wa ajabu mno, aliruka juu na kuzunguka na kufanya mbawa zake kuwa kama waridi. Kisha akasimama tena, akaondoka akaingia kwenye chumba akiwaacha wale wengine kwenye ukumbi.

" Hicho chumba kinaitwa Otoma, ni chumba cha kuwekea kumbukumbu ya viumbe waliotolewa roho na Zeruel. Chumba hiko anaingia Zeruel na mungu tuu. Umeona jina lako?" Siriel alisema.

Nilishtuka sana baada ya kuona jina langu kwenye ile karatasi baada ya Zeruel kufungua ile Lausta Bagama. Niliona tarehe, siku, mwaka, muda, mazingira ya kifo changu kupitia ile Lausta Bagama.

" Inamaana natakiwa kesho nife?"
Niliuliza huku nikitazama ile video kwa wasiwasi
" Kifo cha mtu hupangwa na mungu, lakini namna atakavyokufa hupangwa na Janalaidana, huyu ndio hupanga namna tukio zima la kifo chako litakavyokuwa. Sisi hupenda kumuita Laidana yaani Mwenye sanaa ya kifo"
Siriel alisema huku uso wake ukikunjuka kwa tabasamu.

Hapo nikamuona Zuriel yaani mtoa roho za watu akitoka na kutembea kwa kasi kuelekea upande wenye giza.
"Anaenda wapi sasa?" Niliuliza kwa hofu nikidhani huenda muda wa Zuriel kuja kunitoa roho umefika.

" Anaenda kwenye chumba kiitwacho X2, ambapo hapo ndio hufanyia shughuli zake. X2 ni chumba ambacho roho zote zilizopo duniani huonekana kupitia mtambo uitwao Dahel. Kila roho iliyopo duniani hupewa code yake, hivyo popote mtu alipo lazima Zuriel amuone kwa mtambo huo"

"Si ninyi mnasema kuwa huwezi kikimbia kifo?"
Siriel aliuliza.
"Ndio, kifo hakikimbiwi" Nikajibu.
" Kifo kinakimbiwa, na kimekimbiwa mara kadhaa. Ili ukimbie kifo lazima uingie chumba hicho yaani X2. Ukifika humo unatakiwa ujue code ya mtu unayetaka asife yaani akikimbie kifo. Ukishajua Code yake basi, umemaliza kila kitu"
" Code ya roho ya mtu ipo kwenye ile Lausta Bagama ambapo kuna jina lake, siku atakapokufa, muda, mwezi mwaka, na namna atakavyokufa, kwa mbele kuna code yenye tarakimu thelasini na sita, hizo ndio code" Siriel alisema.

Hapo nikamuona Zuriel akibonyeza Dahel punde ukafunguka, na hapo akaingiza zile code zilizomo kwenye Lausta bagama, alichukua dakika ishirini.Punde nikaona watu kwenye ule mtambo ndio hiyo Dahel.

" Watu wote unaowaona kwenye huo mtambo watakufa kesho, nawe ukiwemo" Siriel alisema.
Moyo ukapiga paah baada ya kujiona kwenye ule mtambo nikiwa nimelala kitandani.

"Yamebaki masaa kumi na sita roho yako itoke. Nimekuja huku kukusaidia. Sitaki ufe, nina sababu ya kufanya hivi"
Siriel aliongea maneno hayo huku akinitazama na macho yake mekundu yenye mboni nyeusi.

Kisha akasogelea kisiki chenye matawi yaliyokauka na kukata jiti kubwa. Alafua akanambia nilale chini. Nami nikalala. Kisha akachora kupitia pembeni yangu kwa kufuata umbo langu. Alianzia kichwani mpaka kwenye unyao wangu. Kisha akaniambia niamke. Nikaamka, akamalizia kuchora macho, pua na mdomo. Kisha akaniambia niukojolee ule mchoro mdomoni.

Nilisikia aibu kukojoa mbele yake lakini sikuwa na jinsi nilichojoa nikakojoa kwa kujilazimisha lazima kwani sikuwa namkojo muda ule.

Nilipokojoa tuu ghafla ule mchoro ulibadilika ukawa dongo lililosimama bila ya nguo. Lile dongo lilisimama mbele yetu pasipo kusema kitu. Siriel akalimwagia kitu kama maji likabadilika likawa na ngozi kama yangu. Kisha nikaambiwa nilikumbatie. Kwa hofu nikalifuata moyo ukipiga kite. Nikalikumbatia nikiwa nimefumba macho. Nilipofumbua nilishtuka kuona lile dongo limebadilika na kuwa na sura yangu kabisa. lilikuwa limefanana na mimi kama mapacha waliofanana.

Hapo Siriel akachukua damu ya lile dongo ambalo muda huo limekuwa binadamu aliyefanana na mimi. Alipomaliza akasema: " Sasa subiri niondoke niende Tibeli, nikapeleke hii damu kisha nitarudi. Sitakawahi baada ya masaa matano nitakuwa nimewasili"
Siriel aliongea na kisha akaondoka akiniacha mimi na yule dongo ambaye muda huo alikuwa akinitazama bila ya kusema chochote.

Kitambo kidogo kilipita bila ya mimi na yule pacha wangu kuzungumza. Nikaona nimuulize;
"Unajua chochote?"
"Hapa ni wapi? Nawe ni nani unayefanana na mimi?"
Yule Mtu aliongea sauti inayofanana na mimi kabisa.
" Upo nyuma ya Jua, Nami ninaitwa Taikon,"
Nilimjibu.
" Taikon ni mimi, nambie wewe unaitwa nani? Na yule Siriel kaenda wapi?" Yule dongo aliongea kwa sauti ya juu akinifokea.
Niliogopa mno. Pia nikajiuliza alimjuaje Siriel wakati ametengenezwa pale pale nikiwepo.
" Mimi ndiye Taikon, Siriel kaenda Tibeli. Nambie unaitwa nani?" Nilijikaza nikamuuliza tena.
Hapo akanifuata na kunikaba kooni, muda huo alikuwa uchi wa mnyama. Mikono yake ilikuwa ya baridi kama maiti, macho yake bado yalikuwa na mchanga yalinitazama kwa ukali. Alizidisha kunikaba kwa nguvu mpaka nikahisi siwezi tena kupumua.
Kwa upesi nikampiga teke la kwenye kende akaniachia na kuanza kugugumia kwa maumivu lilikuwa pigo baya sana kwake.

Muda hup video ilikuwa ikiendelea pale chini, punde nilimuona Siriel akiingia kwenye ule ukumbi waliokuwamo wale viumbe wenye mbawa mbili,tatu.nne na mbawa sita. Alikaguliwa na moja ya walinzi walindao lango kuu la Tibeli. Niliomba kimoyo moyo asijekutwa na kile kichupa cha damu ya dongo. Bahati ilikuwa yake, kichupa hakikuonekana.

Nilimuona Siriel akimfuata pacha wake Kaasiriel wakakumbatiana kwa upendo, nikajikuta natabasamu. Nilipenda jinsi walivyokuwa wanapendana. Baadaye niliwaona wakizungumza jambo kwa kitambo kisha Kaasiriel akamuacha Siriel pale ukumbini akaenda moja kwa moja kwenye kile chumba cha Otama. Akabisha hodi lakini hakujibiwa. Akajua chumba kile hakina Mtu. Akaondoka akaenda moja kwa moja kwenye chumba kiitwacho X2 ambacho kinamifumo ya roho zote. Hapo akabisha mara moja mlango ukafunguliwa na Zuriel.

Wakaongea kidogo kisha wakatoka wote kuelekea ukumbini, kumbe Siriel alikuwa kajificha kwenye kona, walipopita tuu akaenda na kuingia kwenye kile chumba X2, nikamuona Siriel akabadilisha Code zangu na kuingiza Code za dongo. Kwa haraka sana alipobadilisha, chumba kizima kikatoa alamu ya hatari jambo ambalo lilimfanya Zuriel ajue kuna mtu kaingia kwenye chumba cha X2 na kushika ule mtambo uitwao Dahel.

Siriel alijigeuza ukuta na kubadili Code za ukuta kusudi asionekane. Zuriel alipoingia hakukuta mtu. Akashangaa ni kwa nini alamu ilie. Hapo akawa na mashaka huenda kuna kitu kinaendelea. Akakumbuka ujio wa Kaasiriel alivyokuja na kumchukua akaenda naye ukumbini na hakuwa na jambo la maana. Siriel akatoka pale ukutani akaenda kwa Kaasiriel akamuaga na kuondoka. Yalikuwa yameshaisha masaa manne.

Baada ya lisaa limoja Siriel alirudi na kunikuta pale aliponiacha na dongo wangu. " Kila kitu kimeenda sawa. Sasa Nitaondoka hapa na Huyu alafu baadaye nitarudi kukuchukua" Siriel aliongea kama mtu aliyebakiwa na muda mchache. Ni kweli yalikuwa yamebaki masaa mawili tuu ili roho yangu ichukuliwe na Zuriel.

Aliondoka na moja kwa moja alifika Duniani. Hapo niliwaona kupitia Video iliyokuwepo pale chini.
Nilishangaa kujiona nikiwa duniani nikiendelea na shughuli zangu. Nikajisemea huenda kile ni kivuli changu. Siriel akiwa na Dongo niliwaona wakiwa wamesimama mbele ya kivuli changu kilichopo duniani, Siriel akashika kile kivuli changu ambacho muda huo kilikuwa kinatembea na rafiki zangu ambao muda huo walijua ni mimi kumbe ni kivuli changu.

Alivyokishika kivuli changu kikajikwaa na kupepesuka kama mtu anayetaka kuanguka. Hapo hapo Siriel akamuunganisha Dongo na kivuli changu. Rafiki zangu walinizoza na kuniambia nitembee kwa umakini, wasijue yule hakuwa mimi bali ni kivuli changu.

Zilikuwa zimesalia Dakika kumi Roho yangu ichukuliwe. Siriel alirudi kwa kasi mpaka nyuma ya Jua. Akanikuta nikitazama video. "Kazi imekwisha, subiri tumsubiri Zuriel nafikiri dakika tano zijazo atakuwa eneo la tukio" Siriel alisema. Punde video ilimuonyesha Zuriel akiwa maeneo ya duniani akivizia ule mchanganyiko wa kivuli changu na dongo. Akaitoa roho ya dongo akidhani ni Roho yangu. Basi akamaliza kazi. Nikadondoka, Dongo akafa wakati mimi kivuli changu kikiendelea kuishi.

Baadaye Zuriel akaondoka moja kwa moja mpaka chumba cha Otama ambacho ni maalumu kwa kuhifadhia roho na kumbukumbu za watu waliokwisha kufa.

Siriel akanambia tusubiri siku tatu, kisha zilipoisha siku tatu akanichukua na kunirudisha duniani kwenye kile kivuli changu.

Je, nini kitaendelea? Je, Taikon hatakufa kisa siku yake ya kufa imeshapita?
Usikose mkasa huu wa kusisimua wenye visa matata.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
 
SIKU YANGU YA KUFA ILIPITA 02
Mtunzi: Robert Heriel

ILIPOISHIA.......
Baadaye Zeruel akaondoka moja kwa moja mpaka chumba cha Otama ambacho ni maalumu kwa kuhifadhia roho na kumbukumbu za watu waliokwisha kufa. Siriel akanambia tusubiri siku tatu, kisha zilipoisha siku tatu akanichukua na kunirudisha duniani kwenye kile kivuli changu.
Inaendelea......

Hata baada ya siku nyingi kupita, tangu siku ile nilipochukuliwa na Siriel akanipeleka nyuma ya Jua kunikimbiza na Mkono wa kifo, Mkono wa Zeruel Kiumbe mwenye mbawa sita. Nikasubiri nakusubiri mpaka nikakata tamaa, kwani nilikuwa namsubiri Siriel yule Kiumbe mwenye mbawa Tatu atishaye kama nini.
Miaka ilipita bila kusita, ilienda bila kupenda. Hata nikasahau habari zake na habari za wale viumbe waishio Tibeli.
Kwa habari za Tibeli ndizo hizi; Tibeli ndio makazi ya kina Siriel, Kaasiriel, Zeruel, JanaLaidana, Dharawidi wenye mbawa mbili, Fazawidi wenye mbawa nne, Tauwidi wenye mbawa sita na Siriwidi wenye mbawa tatu. Hiyo ni nyota yenye mbawa mbili yenye kung'aa sana zaidi ya jua letu. Tibeli ndio Nyota inayopaa kutoka Galaxy moja kuelekea Galaxy nyingine. Naam Galaxy(Tamka Galaksi) ni kundi la nyota zipatazo zaidi ya milioni mia moja.

Hivyo Nyota ya Tibeli hupaa na kuzunguka huku na huko kwa kasi kubwa izidiyo kasi ya mwanga. Mbawa zake hung'aa rangi ya dhahabu, nayo hutoa rangi ya Yakuti Samawi ndiyo hiyo rangi ya Bahari. Basi hakuna kiumbe chochote duniani kilichowahi kufika huko, tena waendao huko wote walishakufa kwa Mkono wa Zeruel. Wakahifadhiwa katika chumba cha Otama.
Hayo yote alinisimulia Siriel siku zile alivyonichukua akanipeleka kunificha nyuma ya Jua, huko kusiko na giza wala nuru.
Miaka ishirini ilipita Bila Kumuona Siriel, Taikon nikafikisha miaka thelasini na tano bila kuwa na mke wala watoto. Basi kama ilivyodesturi ya wanadamu nikaazimia nami nitafute mwanamke mzuri wa kufanana nami ili niweze kumuoa. Awe mke wangu nami niwe mume wake. Apate kunizalia watoto wa kufanana nami, wanangu wa damu yangu mwenyewe.

Nikatoka katika mji niliokuwa nikiishi ambao upo kando kando ya ziwa lililopitiwa na bonde la ufa, kusini mwa nchi ya Tanzania. Katika ardhi ya Wanyakyusa. Nikatoka huko nikapanda magari yenye magurudumu ya mpira yaliyotengenezwa na watu wenye ngozi nyeupe kutoka nchi za mbali, nchi za barafu. Kwa maana watu hao walikuwa wakisifika kwa akili na ubunifu, tena walikuwa wakiunda vyombo vyenye kustaajabisha.
Nikapanda katika gari ambalo lilikuwa likielekea mjini, hapo nikaona safu nzuri ya Mlima Livingstone ambayo iliishilizia katika vilindi vya ziwa Nyasa pia huitwa Ziwa malawi. Hapo Nikamkumbuka David Livingstone Mgunduzi na mmishenari mwenye asili ya kizungu kutoka Uingereza ambaye alipata umashuhuri kutokana na mambo aliyoyafanya duniani, moja ya mambo hayo ni kupinga na kupambana na biashara ya utumwa. Mlima Livingstone umepewa jina la mgunduzi.

Baada ya masaa kumi na mbili nilifika katika mji wa Kotobo, wakazi wa mji huu huitwa Wakotobo. Mji wa Kotobo umepakana na Jiji la Dar es Salaam kwa upande wa Mashariki, Magharibi nilipotokea umepakana na Pwani, Kaskazini umepakana na Tanga, na kusini umepakana na Bahari.
Mji wa Kotobo ulikuwa mji mdogo lakini uliojipanga vizuri
Wakazi wake walikuwa wanarangi nyeusi ya kung'aa iliyovutia sana. Walikuwa na sura ndefu na macho makavu.
Wanaume wa kikotobo walikuwa na maumbile marefu yenye futi saba huku wanawake zao wakiwa warefu wa futi sita. Mji wa Kotobo ulikuwa tambarare, sikuona mlima hata mmoja katika mji ule.
Basi nikachukua mizigo yangu nikaelekea nyumba za wageni. Nikapata chumba nakulipia, kisha nikapumzika kwani tayari giza lilikuwa limeshaingia.
Usiku wa manane nilizinduka, nafikiri niliota ndoto mbaya lakini sikuikumbuka hata kidogo. Nilikuwa nikihema kwa pupa huku mapigo yangu ya moyo yakienda kasi. Mwili wote ulikuwa tepetepe kwa jasho. Hakika niliota ndoto mbaya, ndoto iliyozima kumbukumbu zangu hata nisiikumbuke. Ndoto iliyoniachia mashaka na yaliyounyaka moyo wangu.
Punde si punde kwa sekunde upepo mkali ulivuma huko nje. Ulivuma kwa nguvu kubwa mpaka Paa likaezuliwa. Hofu ikanishika, sikuwa na ujanja wowote, nilisubiri litakalotokea.
Nikatoka nje upepo ungali ukiendelea kuvuma, huko nililakiwa na giza nene kwani hapakuwa na umeme. Angani wingu zito lilifunika anga lote, hapakuwa na nyota wa mwezi. Giza ndio lilikuwa limetawala huku upepo ukiendlea kuvuma kwa nguvu kwa kadiri muda ulivyokuwa ukiendelea.

Upepo uliongezeka nguvu na kubomoa mpaka nyumba na kung'oa miti na kuipeperusha angani. Hapo nikawahi kisiki kilichokuwa pale nje. Nilikikumbatia kile kisiki kwa nguvu zangu zote. Upepo nao ulizidi kuvuma mpaka ukawa unachana nguo nilizokuwa nimezivaa. Ulikuwa ni upepo wenye nguvu mno, sikumbuki kama niliwahi hata kuhadithiwa kuwa kuna upepo wa namna ile uliwahi kutokea.
Sasa nguvu za kukumbatia kile kisiki zilianza kuniisha. Nilihisi upepo ukinizidi nguvu, muda huo nilikuwa nimefumba macho. Nikakumbuka mambo yote niliyowahi kuyafanya kwenye maisha yangu. Nilikumbuka ndugu zangu niliowaacha nyumbani. Nilikumbuka habari za Siriel, hapo nikatamani Siriel angekuwepo huenda upepo ule usingenishinda kwani angenisaidia. Majuto yaliniingia, kwa nini nisingetafuta mke kulekule mpaka niende mji wa Kotobo. Kwa nini nije miji ya mbali kutafuta mke mgeni. Looh!
Hapo nguvu ziliponiisha, upepo ukanichukua kwa nguvu zote na kunipeperusha angani kama kikaragosi. Fahamu zikapotea katika mawimbi makali ya upepo ule nikapotelea angani sehemu ambapo upepo ulikuwa ukizunguka kwa kasi na kuunda shimo. Huko ndiko nilipoingia kwenye hilo shimo la upepo na kupotelea huko poteee! Sikukumbuka nini kiliendelea.

**********************

Nilikuwa uchi, ndio tena uchi wa mnyama. Nilizinduka katika fahamu zangu. Nilijikuta nimelala juu ya manyoya mengi kama manyoya ya ndege. Ngoz yangu ilikuwa imeraruka raruka, pengine ilinyofolewa na upepo ule, upepo mkali wenye njaa.
Nikasimama na kuanza kutembea juu ya yale manyoya kama manyoya ya ndege. Yalikuwa manyoya yenye rangi mbalimbali, yalikuwa kamazulia zuri sana. Kila nilipotembea manyoya yalinata chini ya nyayo zangu kwani
nyayo zangu zilikuwa zimenyofoka nyofoka nyama.
Hapakuwa na giza wala hapakuwa na nuru, Nilipotazama juu sikuona anga. Juu palikuwa hapana mwisho, hapakuwa na kitu chochote wala rangi yoyote, labda ningesema sikuona kitu chochote.

"Sasa Huku ni wapi?"
Nilijiuliza huku nikitembea upande niliougeukia. Upande wa mkono wangu wa kushoto kulikuwa na ukuta wa mawimbi uliokuwa unazunguka kwa kasi kama kani ya usumaku. Hapo nikajua kule ndipo nilipotokea, na ule ndio ule upepo ulionikuta kule katika mji wa Kotobo.
Upande wa kulia kama kilometa moja hivi niliona msitu, akili yangu ikaniambia nielekea kwenye ule msitu. Upesi nikaongoza mpaka nikaufikia ule msitu ambao ulikuwa wa kijani sana, mashina ya miti yake yalikuwa ya rangi ya njano.

Nikaingia msituni, jamani kulikuwa kimya sijapata kuona kimya kile. Hofu yangu ilinishika kifuani, nilitembea kwa uangalifu na tahadhari huku nafsi yangu ikinionya. Kadiri nilivyokuwa nikizama ndivyo giza lilivyozidi kuongezeka hii ni kutokana na kuingia katikati ya msitu. Nilitembea mpaka nilipohisi kuchoka huku kiu ikikaba kooni, na njaa ikinililia tumboni.
Bado palikuwa kimya, sio nyuma yangu wala mbele, sio kushoto wala kulia, chini au juu kimya kilinizunguka. Huku matawi ya miti yakinitonesha nyama zangu zilizokuwa zinaning'inia mwilini mwangu. Sasa hapakuwa na ile nuru ya awali tena. Nafikiri nilikuwa nimeshafika katikati ya ule msitu wa kutisha. Mbele giza nyuma giza, juu giza chini giza, kushoto giza kulia giza. Ulikuwa msitu wa giza.

Tayari nilishamaliza mwendo wa maili kumi ndani ya ule msitu. Kwa mbali kabisa kama maili moja niliona mwanga. Hapo nikiwa nimechoka sana, miguu ikiwa haina nguvu, nikajikaza kikondoo mpaka nilipoukaribia ule mwanga. Nilishangaa, kumbe ulikuwa ni mti uwakao kama taa.
Moyoni nikasema; Nimefika kwenye mti uwakao taa.
Nikaukaribia kabisa, nao ulikuwa na matunda yawakayo taa ya njano, majani yawakayo taa ya kijani, na shina liwakalo taa nyeupe, na maua yawakayo taa nyekundu. Jamani lilikuwa linapendeza. Eneo lote lilikuwa na mwanga uliosababishwa na ule mti uwakao.
Matunda yake yalikuwa mfano wa komamanga, ua lake lilikuwa mfano waridi, majani yake yalikuwa kama majani ya mpera, na shina lake lilikuwa mfano wa mnazi. Ulikuwa ni mti mzuri sana, pengine katika miti niliyowahi kuiona huo ndio ulikuwa mti mzuri kuliko yote niliyowahi kuiona. Sio kwa sababu ya kuwa ulikuwa ukiwaka taa, bali hata maua yake yalikuwa yanapendeza na kuvutia.
Nilipousogelea kama hatua kumi iliniufikie ulibadilisha rangi zake na kuanza kumulika mulika kwa kujibadilisha rangi. Hapo nikasikia harufu nzuri ajabu, ilikuwa harufu yenye marashi yenye kufurahisha mno.

Nilipousogelea zaidi nikagundua jambo kuhusu yale matunda, Kumbe yalikuwepo matunda ya aina mbili. Aina ya kwanza yalikuwa matunda ya rangi ya njano, aina ya pili ni matunda ya rangi ya damu ya mzee. Yote yalikuwa yakiwaka, seme yale yenye rangi ya damu ya mzee yalikuwa hayana mwanga mkali kama yale yenye rangi ya njano.

Hapo nikajiuliza; Yapi yameiva kwa kuliwa na yapi ni machanga?
Hata hivyo hakuwepo wa kunijibu, nikasogelea tunda la rangi ya njano nikaligusa, Mamamaaaaaa! Nilipiga kelele na msitu wote ukarindima kwa sauti iliyojirudia huku na huku na kufanya eneo lile liwe na sauti za kutisha ambazo zilirudia sauti yangu.
Lile tunda lilikuwa la moto sana, liliniunguza mkono wangu, niliushika mkono wangu huku nikigugumia kwa uchungu. Sikuwahi kusikia maumivu ya namna ile tangu nizaliwe. Yalikuwa maumivu makali sana.
Sasa niliuchukia ule mti niliungalia kwa hasira kali, nikiuwazi mambo mabaya, kama ningekuwa na panga ningeukata walahi. Mti mzuri lakini ni katili kiasi kile. Hapo niliutazama kwa zamu huku nikishika mkono wangu ulioungua.
Akili nyingine ikanituma nijaribu kugusa moja ya yale matunda yenye rangi ya damu ya mzee. Basi nikausogelea tena huku nikiutazama ungedhani unamacho, hatua moja moja za hadhari ungedhani nataka kuupiga pigo la kigaidi.
Nikafikia tunda moja la rangi ya damu ya mzee, nikalipelekea kidole polepoke nikilitazama, nikaligusa kwa upesi tiipu! na kuondoa kidole. Halikuwa na moto, nikaona huenda sijaligusa vizuri iweje halina moto, nikapeleka tena kidole nikagusa na kuliachia. Hata mara hii halikuwa na moto. Nikagundua matunda ya rangi ya damu ya mzee ya ule mti hayaunguzi kama yaliyomatunda ya rangi ya njano.
Nikalichuma, bado lilikuwa linawaka likiwa mkononi mwangu. Nilifurahi mno. sasa tamaa ya kulila ikanishika ulimini. Je kama ni sumu, hiyo ndio ilikuwa hofu yangu. Lakini kama nisipolila tunda lile bado ningekufa na njaa. Na miti mingine haikuwa na matunda.
Basi nikiwa katika kufikiri mara ghafla nilisikia sauti za zikiongea lugha nisiyoielewa zikija kule nilipokuwa mimi. Sauti zile zilikuwa kama mita kumi tuu.
Kwa upesi nikatoka na kwenda mbali kidogo ambapo mwanga wa ule mti haufiki, kisha nikajificha. Zile sauti bado nilikuwa nazisikia zikija. Kumbe zilikuwa mbali kama kilometa tatu, ni kutokana na ukimya wa ule msitu ndio maana nilizisikia kama zipo karibu.
Bado nilikuwa nimelibeba lile tunda nikiwa bado sijalila. Kitambo kidogo kama dakika tano niliona viumbe vitatu vya ajabu vikiwa vinaufuata ule mti. Vilikuwa viumbe vyenye mbawa Mbili ambavyo niliambiwa vinaitwa Dharauwidi, na kiumbe mmoja mwenye mbawa tatu. Huyu nilimtambua kama KaaSiriel yaani pacha wa Siriel. Nilipomuona nilishtuka sana. Sikujua kilichonishtua kilikuwa ni nini.
Basi nikataka kujua nini kilichowaleta pale kwenye ule mti. Nikakaa macho nikiwatazama bila kupoteza nukta moja, huku mapigo yangu ya moyo yakidunda. Muda huo hawakujua eneo lile nilikuwepo, huenda wangejua sijui nini kingetokea.
Nikawaona wale Dharauwidi wenye mbawa mbili wakichuma yale matunda ya rangi ya damu ya mzee, huku KaaSiriel akichuma majani ya mti ule. Kumbe walikuwa wamebeba mifuko ya kuwekea matunda na maua watakayoyachuma. Walimaliza kuchuma, mimi nikiwatazama bila ya wao kujua.
Punde akaja Zeruel ndiye yule mtoa roho jamii ya Tauwidi mwenye mbawa sita. Alipokuja wale viumbe wengine walimsujudia kama ishara ya heshima, hapo nikajua kuwa Zeruel ni kiumbe mwenye cheo cha juu na mwenye kuogopwa.
Wale Dharauwidi wakaondoka wakamuacha Zeruel na Kaasiriel pale kwenye ule mti. Hapo nikawa macho zaidi huku maswali mengi yakinijia; iweje hawa wabaki wenyewe, kuna nini kinataka kufanyika. Basi nilijiuliza maswali ya kibinadamu lakini hakuwepo mtu wa kunijibu.
Ghafla bin vuu Zeruel alichuma tunda moja lenye rangi ya damu ya mzee na kuling'ata kipande kisha kipande kingine akamnyoshea Kaasiriel naye achukue ang'ate. Nilishangaa kumuona Zeruel alipong'ata lile tunda la ule mti akibadilika umbo lake na kuwa na umbo zuri la kiume la binadamu. Alikuwa mwanaume mwenye uso mzuri, kifua kipana kilichokatika katika, mrefu mwenye rangi ya shaba akiwa uchi wa mnyama, niliuona uume wake ukiwa haujatahiriwa, alikuwa na mavuzi ya rangi ya kijivu. Hayo yote yaliufanya moyo wangu upwite kwa wasiwasi sana.
Hapo Nikamuona Kaasiriel akiwa na aibu nyingi, naye akaling'ata lile tunda alilopewa na Zeruel. Naye akabadilka sura na maumbile yake. Alikuwa mwanamke mwenye sura nzuri sana, rangi yake ilikuwa nyeusi ya kung'aa, mwenye uso wenye macho makubwa yanayorembua, umbo lililopangika vizuri, sikuwahi kumuona mwanamke mzuri kama Kaasiriel. Alikuwa mzuri sana.
Basi hapo nami nikapata tamaa ya kujaribu kuling'ata lile tunda ili walau nijue ladha yake. Hofu ya kuwa ni sumu iliondoka baada ya kuwaona wale viumbe wakilila.
Wakati nataka kuling'ata nilimuona Zeruel akimsogelea kwa mahaba Kaasiriel, huku uume wake ukiwa umesimama na kukaza sana. Hapo nikasema haya nayo ni kama ndoto, lini nitaamka usingizini nisiyaone haya. Lakini nilijisemea tuu kwani ile haikuwa ndoto, lilikuwa ni tukio la kweli nililoliona kwa macho yangu mwenyewe, tena kwa akili zangu mwenyewe.
Walikumbatiana na kuanza kunyonyana ndimi zao, Zeruel aligeukia upande nilipokuwa nimejificha wakati Kaasiriel akinipa mgongo wake. Uso wa Zeruel ulizingirwa na utamu wa mapenzi aliyoyapata kutoka kwa KaaSiriel. Nami nikaona nishuhudie tukio lile huku nikila tunda la ule mti nililokuwa nimelibeba mkononi.
Nikaling'ata, na hapo hapo mwili wangu ukabadilika na kuanza kuwaka rangi hali iliyomfanya Zeruel ashtuke kuona taa ikiwaka kwa mbali kule nilikokuwako, nilikuwa ni mimi niliyekuwa nawaka taa. Hapo akaacha kumnyonya denda Kaasiriel na kuanza kuufuta ule mwanga ambao ulikuwa ni Mimi.
Nami nikanyanyuka na kuanza kukimbia, alipoona mwanga unakimbia naye akaanza kunikimbiza ili anikamate.

Itaendelea

Kama umeipenda Stori hii nakusihi U-like na Ku-komenti, kisha share wengine waisome.

Ikiwa unachakushauri, tutafanyia kazi maoni yako

Ulikuwa nami:
Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
069332300

Hadi wakati mwingine. Ahsanteni.
 
SIKU YANGU YA KUFA ILIPITA 03




Mtunzi: Robert Heriel




Ilipoishia.....

Nikaling'ata, na hapo hapo mwili wangu ukabadilika na kuanza kuwaka taa hali iliyomfanya Zeruel ashtuke kuona taa ikiwaka kwa mbali kule nilikokuwako, nilikuwa ni mimi niliyekuwa nawaka taa. Hapo akaacha kumnyonya denda Kaasiriel na kuanza kuufuta ule mwanga ambao ulikuwa ni Mimi.

Nami nikanyanyuka na kuanza kukimbia, alipoona mwanga unakimbia naye akaanza kunikimbiza ili anikamate.




Inaendelea...




MELI YA KIFO (MELI YA ZERUEL)




Nilikimbia kwa kasi, huku mwili wangu ukiwaka taa, Nilijishangaa namna nilivyokuwa nakimbia kwa kasi ile. Sikujua niliwezaje kukimbia kwa kasi kiasi kile. Nilikimbia mithili ya risasi nikichanja msitu huku nikiwa nimelishika mkononi lile tunda la ule mti unaowaka taa. Pengine kasi ile ilisababishwa na nilivyokula lile tunda, lakini sikuwa na uhakika.

Nyuma yangu nilifukuzwa na Jitu baya lenye hasira kali, ndiye huyo Zeruel mtoa roho ambaye alikuwa akinifukuza kwa kasi inayokaribia kunishinda. Zeruel alikimbia huku akicheka kwa sauti ya kutisha. hohohohohoo! Kisha msitu wote nao uliitikia Hohohohoho! sauti hiyo ilitokea pande zote, nyuma yangu Hohohoho! Mbele yangu Hohohohoho! kote hohohhohoho! Sauti hizo zilinizuzua na kunichanganya, eneo lote lilirindima kwa kicheko cha Zeruel huku vishindo vyake vikitua mithili ya mizinga ya makombora.

Sasa alikuwa amenikaribia kama hatua kumi tuu anishike, maya wee! Taikon siku yangu ya kufa ilikuwa imewadia, niligeuka nyuma kumtazama huku nikikimbia kwa kasi kubwa, hapo nikamuona Zeruel akiwa na uso wa Panzi utishao sana, Nilishtuka kumuona Zeruel katika jinsi hiyo.

Alipanua mdomo wake kisha akatoa ulimi mrefu uliogawanyika mara sita, zikawa ndimi sita. Ndimi mbili zilinifuata kwa kasi, nami nikaongeza kasi nikikimbia kwa kupiga kona huku na huku kukwepa zile ndimi za Zeruel zisije zikanikamata.

Kasi yangu ilikuwa ya mwisho kabisa, sikuweza kukimbia zaidi ya pale tena. Nilikimbia huku nyuma yangu Zeruel akija na ndimi zake zilizokuwa zikinikosa kosa kwani nilikuwa nikizikwepa kwa kukata kona na kuinama pale zinaponikaribia. Kila ziliponikosa zilipiga na kukata miti ya ule msitu, hapana shaka ndimi zake zilikuwa na makali kama jambia.

Kwa hofu kubwa nilijikuta nikitema sehemu ya tunda lililokuwa mdomoni ambalo nilikuwa limeling'ata, kitendo hicho kilisababisha mwili wangu kuzimika, mwili wangu haukuwa unawaka tena. Mwanga uliokuwa umebaki ni tunda nililokuwa limelishika mkononi.

Jambo hilo likamshangaza Zeruel, alipunguza mwendo na kurudisha ndimi zake mdomoni. Nami nguvu ya kukimbia ilipungua, nguvu zilibaki za kawaida kama binadamu tuu.

Tayari nilikuwa nimekimbia maili elfu moja kwa dakika kumi tuu, nikifukuzwa na Zeruel, kiumbe mwenye roho mbaya.

Giza nililokuwa limelifukuza kutokana na mwili wangu kuwaka taa lilinilaki kwa kiburi, hapo sikuwa na uwezo wa kukimbia kwa kasi kwani sikuweza kuona mbele vizuri.

Looh! Mara ghafla niligonga tawi la mti na kudondoka chini, hapo hapo lile tunda nililokuwa nimelishika mkononi likaniponyaka na kuanguka kwa mbali, nikiwa pale chini nililiona lile tunda likikiporomoka kwenda chini, Nikageuka nyuma, hapo nilimuona Zeruel akija kwa kasi akiwa umbali wa hatua mia moja hivi.

Nikanyanyuka nikijikongoja, jamani! nilihisi maumivu makali sehemu ya bega la kushoto, yalikuwa maumivu makali mno jamani. Lakini niliona ni heri yale maumivu kuliko kukamatwa na Zeruel, sikutaka kabisa niingie katika mikono hatari ya yule kiumbe.




Nikasonga upande lilipoporomokea lile tunda, nikakimbia kwa kuchechemea, ghalfa bila taarifa nilishangaa nimedumbukia kwenye shimo refu lenye kiza, hapo nilipiga kelele za kuomba msaada nikiwa naelea kuelekea chini kwenye lile shimo lenye kiza cha mauti. Jamani, sijawahi ona kiza kama kile, macho yangu hayakuweza kuona kitu chochote, kulikuwa na giza la kutisha.

Lile shimo lilikuwa refu mno, bado nilipiga kelele za hofu na wala sisemi zilikuwa kelele za kuomba msaada, kwani nilijua watoa msaada hawawezi ishi mahali kama pale. Watakaoweza kuishi kwenye lile shimo ni mashetani pekee tena mashetani wabaya wenye hasira kali na tamaa ya damu.

Sauti yangu iliunda viumbe kama vipepeo vyenye kichwa cha panya,ukubwa wa vile vipepeo ulilingana na ukubwa wa popo, nilipoona hivyo niliacha kupiga kelele, bado nilikuwa nikianguka kwenye lile shimo, bado nilikuwa sijafika chini. Vile vipepeo vyenye kichwa cha panya vilikuwa na mabawa yanayowaka taa hali iliyofanya shimo lile kuwa na shimo hafifu.

Vile Vipepeo vikawa vinapiga kelele ile ile niliyokuwa naipiga mimi; mamaaaaaaaaaa!

Huku vikinishukia chini kwa kasi kwani mimi nilikuwa chini nikielekea chini ya lile shimo, vyenyewe vilikuwa juu yangu kidogo kama mita ishirini juu yangu na wala sio juu kabisa ya lile shimo.

Shimo lote lilirindima sauti ya vile vipepeo vyenye kichwa cha panya, Kumbe navyo vikipaza sauti zao vikilia Mamaaa, navyo vinatoa viumbe wadogo zaidi ambavyo vilifanana na nyuki mwenye ukubwa wa komba mavi. Hayo yote niliyaona nikidondoka kwenye lile shimo la mauti.

Vile viumbe vikanifikia, punde nikasikia maumivu makali mguuni, kutazama nikaona kipepeo kimoja kikiwa kimening'ata mguuni, nilikipiga kofi kikaniachia, lakini tayari kilikuwa kimeniachia jeraha kubwa mguuni lenye maumivu yasiyoelezeka.

Baada ya lisaa limoja hivi bado nikiwa nadondoka kwa kasi kwenye lile shimo la giza, nilihisi marue rue, mbele ya uso wangu kilikuwepo kiumbe kidogo kilichofanana na nyuki na ukubwa wake kama Komba mavi, kiumbe kile kilipeperuka usoni mwangu, kwa kadiri kilivyokuwa kikipepea ndivyo akili yangu ilivyokuwa ikinikimbia. Hatimaye nikapoteza fahamu, wala sikujua nini kiliendelea.




***********************************




Fahamu zilinitekenya, nikazinduka. Nilishangaa kujikuta nikiwa nimenasa kwenye kamba laini kama utando wa buibui, mwili wangu ulikuwa umefungwa fungwa na kamba laini sana, mahali pale palikuwa na mwanga hafifu huku kukiwa na moshi wa ukungu. Nilitazama kwa chini, haah! Nilistaajabu kuona maporomoko makubwa ya maji kwa mbali sana kule chini. Nikainua macho yangu juu, hapo macho yangu yalipokelewa na giza nene la lilo shimo nilipotokea.

Nikatazama tena kule chini, palikuwa panatisha sana, niliona miamba na mawe makubwa kwenye yale maporomoko, moyoni nikasema laiti kama nisingenasa kwenye zile kamba, huenda ningeangukia kwenye ile miamba na ningekufa kifo kibaya sana.

Sasa nitatokaje pale, maana zile kamba zilikuwa zimenifunga, punde nilisikia harufu mbaya ikinikera puani mwangu, sasa nini kilikuwa kinanuka vibaya vile, sikuwahi kusikia harufu mbaya kiasi kile, awali niliwahi kufikiri harufu ya mzoga wa punda ndio harufu mbaya kuliko zote lakini kumbe sikuwa sahihi. Harufu niliyoisikia siku ile ilikuwa funika. Ilikuwa mbaya sana.

Nikawa nageuza shingo yangu huku na huku kutazama huenda kuna kitu kinakuja lakini sikuona kitu chochote. Harufu iliongezeka maradufu, mara hii pumzi ilikuwa nzito, nilishindwa kupumua, ilikuwa harufu nzito mno.

Punde si punde kamba zilizonishika zilitingishika, hapo nikapagawa nikiangaza macho huku na huko, lakini sikuona kitu. Nani anatingisha kamba, nilijiuliza kimya kimya nikiwa naangaza macho yangu. Au ni Zeruel, maya wee! Huenda ule ulikuwa mtego wa Zeruel, hapo nilihaha nilipofikiri habari hiyo.

Nilijiona windo lililonasa kwenye mtego wa adui, ninayesubiri kunasuliwa ili nigeuzwe kitoweo. Mapigo ya moyo yalienda upesi, damu ilikimbia jamani, huu ndio mwisho wangu, naingia katika mikono ya Zeruel, mtoa roho. Mawazo yangu yalinisemesha.

Bado eneo lilikuwa kimya huku zile kamba zikitingishika zaidi, harufu ikiongezeka, ghafla macho yangu hayakuamini, hayakutaka kukubali, yangeamini vipi kwa jambo kama lile. Jamani! Jamani! Niliona dudu baya, kubwa ambalo akili yangu ilishindwa kukubali kuwa yule alikuwa ni buibui, lakini alikuwa ni buibui mkubwa sana, urefu wake ulilingana na ng,ombe kwenda juu , alilinganana kwa mapana na marefu kwa ukubwa wa mita kumi. Alikuwa na sura mbaya mwenye magamba magumu yenye mapembe. Miguu yake ilikuwa na manyoya huku vidole vikiwa na makucha marefu, alikuwa na miguu nane kama buibui wa kawaida.




Kumbe kamba zile zilikuwa ni tando za yule buibui atishaye, alizozitega, na sasa windo lake nimenasa. Leo Taikon katika himaya ya Buibui wa shimo la kifo. Lile Buibui litishalo lilinikaribia likiwa na harufu mbaya sana. Nilianza kujitapikia kutokana na ile harufu, hapo likiwa limenisogelea karibu kabisa. Tulitazamana, niliyaona macho yake yakiwa meusi sana, likanyosha mkono wake wenye makucha likanikunjua kwenye zile kamba, kisha likapanua mdomo wake, Lololo! Jamani lilikuwa linanuka mdomo, niliona ndani ya mdomo wake meno ya makali yakiwa na udenda,




Nikasema; Sikubali

Maneno hayo yaliumba kiumbe kama ndege mwenye mkiwa wa samaki. Nilishangaa sana, kiumbe yule aliruka na kuingia ndani ya lile Dudu baya, hapo hapo lile buibui nikaliona likipaliwa, nafikiri yule kiumbe aliyetokana na maneno yangu "sikubali" alimpalia kooni. Yule Buibui alikohoa huku akipata shida kweli, ghalfa aliniachia baada ya kuona hali yake inazidi kuwa mbaya. Nikaanguka kuelekea kule chini kwenye maporomoko ya maji na miamba mikali.




Niliangukia kwenye yale maporomoko ya maji, yakanipeleka msobe msobe kwa zaidi ya nusu saa yakiwa yanaenda kwa kasi ya kufulia umeme. Yalikuwa maji ya baridi sana, hali iliyopelekea mwili wangu kufa ganzi, nilipoyaonja yalikuwa yanaladha ya sukari, bado kulikuwa na mwanga hafifu huku eneo lote liliwa limetawaliwa na moshi wa ukungu. Hatimaye maji yale yalinifikisha baharini. Huko kasi ilikuwa imeisha kabisa ya yale maporomoko




Baada ya kuogelea na kujiweka sawa majini, nikatazama upande huu na upande huu. Upande wa kulia niliona msitu mkubwa uliofukiwa na mawingu ya kijivu, mbele yangu niliona kisiwa kilichofunikwa na barafu nyeupe pee. Upande wa kushoto niliona Fukwe ambapo kulikuwa na Meli kubwa iliyokuwa imetia nanga.

Meli ile ilikuwa kubwa sana, iliyoundwa kwa namna ya kushangaza, niliitazama kwa kitambo nikistaajabu umbile lake, hapo nikapiga mbizi mpaka nilipoifikia kwani haikuwa mbali sana na pale nilipokuwa.

Hapo nikawa naiona vizuri, kwa mbele ilikuwa na muundo kama fuvu la mtu, yalikuwepo matobo mawili ambayo niliyafananisha na macho ya fuvu la kichwa, rangi yake ilikuwa ya kijivu.

nikaogelea mpaka nikafika ufukweni, hapo nikaona daraja iliyounganisha fukwe na ile Meli ya kutisha. Nikatembea kwenye lile daraja kuifuata ile Meli. Daraja lilikuwa urefu wa mita mia moja kuifikia ile Meli. Nilishtuka nilipogundua kuwa daraja lile limejengwa kwa mifupa ya watu. Almanusura niangukie baharini kwa hofu, nilitetemeka kutembea juu ya mifupa ya watu.

"Mambo haya yanatisha kama nini, hilo nalo ni daraja la mifupa" Niliwaza kimya kimya.

Nikafika kwenye ile meli, nikasimama nikiichunguza kwa umakini. Hakukuwa na dalili ya uwepo wa kiumbe chochote mule ndani. Hapo nikafikiri; meli hii imefikaje mahali hapa. Lakini hakuwepo wa kunijibu.

Nikausogelea ule mlango wa Ile Meli, lakini kabla sijaugusa nilisikia sauti ya viumbe ikija kwa nyuma yangu, nikageuka nyuma kwenye lile daraja kuangalia. Sikuona kitu, lakini kabla sijapuuzia masikio yangu, mara macho yangu yakamuona Kaasiriel akiwa na wale dharauwidi wakija kwenye meli wakitokea Msituni.

Mapigo yangu ya moyo yalidunda, hatari niliiona ikinijia kwa hamu. Nilifungua mlango wa ile meli na kuzama ndani, lakini kitendo cha kufungua mlango wa ile meli kuliifanya meli yote iwake taa. Nilishtuka na kuogopa. Nilijua jambo hilo lingewashtua wakina Kaasiriel, na hivyo wataanza kufanya msako wa aliyewasha taa.

Upesi upesi nilipita kwenye ukumbi wa ile meli pasipo kuikagua vizuri, nyuma yangu nilisikia ule mlango nilioingilia ukifunguliwa.




Nini kitatokea ndani ya Meli ya Kuzimu?

Usikose sehemu inayofuata.

Kama imekupendeza, like page yetu, kisha share wengine waisome.




Ulikuwa nami:

Robert Heriel

Taikon wa Fasihi

0693322300




Hadi wakati mwingine.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom