SEHEMU YA 24
“Scaila! Huyu ni Grace! Msichana anayenisaidia kazi humu ndani. Grace...sina haja ya kukutambulisha huyu ni nani! Nadhani ulimjua kabla ya yeye kukujua,” nilimwambia.
“Karibu sana wifi!” alimkaribisha Grace huku akitabasamu.
“Ahsante! Nimekwishakaribia wifi yangu!”
Baada ya yote, chakula kikaletwa, wote watatu tukakusanyika mezani na kuanza kula, tulikuwa tukizungumza mambo mengi, utani wa hapa na pale na mambo mengine mengi.
Wakati hayo yakiendelea, simu ya Scaila ikaanza kuita, akaichukua, akaangalia kioo, akapuuzia, akabonyeza kitufe cha kuzima, simu kama ikapigwa giza lakini ilikuwa ikiendelea kuita japokuwa haikutoa mlio.
“Janeth huyo! Nikiwa nakula huwa sitaki kuongea na simu...” alisema huku akitoa tabasamu kwa mbali.
“Na si vizuri kuongea na simu wakati wa kula!” nilimwambia.
“Kabisa.”
Tuliendelea kula kama kawaida, baada ya dakika moja, simu ile ikaanza kuita tena, ilikuwa mezani, macho yangu yalikuwa shapu sana, niliangalia kioo, jina nililoliona nakumbuka lilikuwa Alfred ama Albert, lakini akafanya kama alivyofanya.
“Huyu Janeth sijui ana nini...mpaka anaanza kunikera,” alisema, baada ya hapo, akaamua kuizima kabisa.
Niwe muwazi kwamba hapo ndipo nilipoanza kuwa na hofu na Scaila.
Nilikuwa na uhakika kabisa kwamba yule mtu aliyekuwa amepiga simu aliitwa Alfred ama Albert lakini kuambiwa kuwa alikuwa ni Janeth, haikuniingia akilini hata kidogo.
Sikutaka kuonyesha hofu yoyote ile, nilikuwa nikitabasamu muda wote kana kwamba sikuhisi jambo baya lolote lile. Tulikula na tulipomaliza, tukaenda chumbani.
Tulipofika, alipoiona picha yake moja humo, hakuamini, alisimama na kuanza kuiangalia, alifurahi kupita kawaida, akanifuata na kunikumbatia tena.
“Nashukuru kwa kunipenda na kunijali,” aliniambia huku akiniangalia.
“Usijali mpenzi! Nitakupenda siku zote za maisha yangu!” nilimwambia, akaanza kukiangalia kitanda, halafu akayarudisha macho usoni mwangu, akatoa tabasamu, nilijua anamaanisha nini! Nikamsukumia kitandani.
“Kiss me like you will never kiss me again, Nyemo...” (Nibusu kama hutokuja kunibusu tena, Nyemo...) aliniambia na kunivutia kwake. Ni ndani ya sekunde ishirini tu, kila mmoja akabaki mtupu kama alivyozaliwa.