Simulizi: Scaila Michael

sehemu ya 44

“Halo!” niliita, yaani kwa jinsi nilivyochanganyikiwa, nilipokea simu pasipo kujua mpigaji alikuwa nani, yaani nililiona jina lakini ubongo wangu ulishindwa kung’amua ni mtu gani alikuwa amenipigia simu muda huo.
“Halo!” niliita, sauti ilikuwa ya mwanamke.

“Hujambo mkwe!” nilisikia sauti hiyo, hapo ndipo nilipogundua alikuwa mama yake Scaila.
“Oh! Mama! Shikamoo!” nilimsalimia.
“Marahaba mwanangu!” aliitikia.

Nilizungumza naye, muda huo ulikuwa ni saa tatu kasoro, alichoniambia ni kwamba hakuwa akijisikia vizuri hivyo aliniomba sana nimruhusu Scaila aende kulala naye kwani mfanyakazi peke yake asingeweza kama tu ingetokea amezidiwa usiku.

“Pole sana mama!” nilisema kwa huruma.
“Haina shida. Haya magonjwa ya kizee yanatusumbua sana,” alisema mwanamke huyo.

“Kwa hiyo aje sasa hivi?” “Nimekuja kwa mjomba wake, nikirudi mida ya saa tatu, anaweza kuja,” aliniambia mama kwa sauti ya upole mno.

Kwa jinsi alivyokuwa akisikika, nilimuonea huruma mno, kwangu, mwanamke huyo nilimthamini kwa sababu sikuwa na wazazi, kitendo cha kuwa na Scaila, nilimchukulia kama mama yangu.

Nikakubaliana naye! Hapohapo nikatoka sebuleni na kumwambia Scaila kilichokuwa kimetokea, kwamba mama yake alinipigia simu na kuniomba aende nyumbani.

“Mbona hakuniambia?” aliniuliza.
“Labda alihitaji ruhusa kutoka kwangu! Amefanya jambo la maana sana,” nilimwambia Scaila.

Kwanza nikashukuru Mungu mno. Huyu Scaila alipanga kwenda klabu kukutana na mabwana zake, kitendo cha mama yake kuumwa na kumuhitaji kwenda nyumbani kingemfanya kuwa huko muda wote na hata ile nafasi ya kwenda klabu asingeipata kabisa japokuwa aliwaahidi wazazi wake kwamba ni lazima aende huko.

Nilikaa naye na kupiga naye stori sana, aliniambia maneno mengi kuhusu mapenzi yake kwangu, wakati mwingine nilimwamini lakini wakati mwingine moyo wangu uliniambia aliyekuwa akiongea hayo alikuwa Scaila, yuleyule msichana aliyekuwa na matukio mengi nje ya uwanja.

Maneno yake yakaniteka sana, ilipofika majira ya saa nne usiku, akajiandaa na kisha kumsindikiza. Kumbuka gari langu taili lilipata pancha hivyo nisingeweza kumpeleka, ila nilichomfanyia ni kumkodishia bodaboda aende huko.
 
sehemu ya 45

“Mpeleke Tabata. Kiasi gani?” nilimuuliza dereva.
“Elfu tano bosi!”
“Haina shida. Chukua hii! Keep change...” nilimwambia huku nikimpa shilingi elfu kumi na kumwambia abaki na chenji.

Alinishukuru sana, Scaila akanisogelea na kunikumbatia huku akinimwagia mabusu mfululizo, alipomaliza, akapanda kwenye pikipiki na kuondoka mahali hapo na mimi kurudi nyumbani.

Nilipofika, nikapitiliza mpaka chumbani, nikakaa kitandani. Kwa kuwa kompyuta niliiacha wazi, nikatamani kuangalia kulikuwa na mawasiliano ambayo aliyafanya Scaila kwenye WhatsApp kabla ya kuondoka, harakaharaka nikafungua na kuanza kuangalia.

Janeth: Nimesikia leo unakuja klabu!
Scaila: Nakuja! Yaani leo huyu kinyago humu ndani hawezi kunizuia. Ila najifikiria nitamtokaje!

Janeth: Mbona rahisi sana. Panga dili na mama! Mfanye kama anaumwa na anahitaji uende kulala naye. Ila mpange kwanza halafu mwambie yeye ndiyo ampigie simu huyu bwana wako.
Scaila: Wazo zuri.

Ngoja nimpigie, halafu nikiwa naondoka napitia mpaka klabu.
Sijui niseme nini ili unielewe, nilichanganyikiwa mno. Kuna wakati mwingine nilihisi kwamba mimi ndiye nilikuwa chanzo cha hayo yote.

Nilijua kabisa Scaila alikuwa na tabia hizo lakini nilipenda kuangalia sana mawasiliano yake ya WhatsApp na mwisho wa siku yalikuwa yakiniumiza kupita kawaida.

Huo ujumbe ulitumwa majira ya saa 3:16, saa 3:25 kukawa na meseji nyingine za mawasiliano ya hao watu ambazo zilikuwa hivi.

Scaila: Nimeongea naye. Nimempanga, ameniambia hakuna tatizo, atampigia simu sasa hivi.

Janeth: Basi sawa! Tutaonana huko klabu. Leo itakuwa funika bovu. Nakuletea bwana mpya, atakupa pesa kama yule Mkongo.

Scaila: Sawa. Ila nitataka nimuone Munir, japo anikune kidogo kwenye gari lake kabla ya kuondoka kwenda kulala na bwana.

Janeth: Wewe tu.
Nikashusha pumzi ndefu, niliyafikicha macho yangu, yalijaa machozi, mule chumbani niliona kama kulikuwa na hewa ndogo, nikatoka na kuelekea sebuleni.

Nilimuonea huruma mno mama yake Scaila kwa kuhisi kwamba kweli alikuwa akiumwa kumbe haikuwa hivyo, aliyafanya yote na mtoto wake kwa kuwa alimjua.
 
sehemu ya 46

Yaani kwa jinsi picha zilivyokuwa, mwanamke huyo alijua kwamba binti yake alikuwa akidanga, inawezekana hata pesa alizokuwa akizipata zilitoka huko.

Hakuwa mwanamke mwenye hekima, nilitegemea hata kama binti yake huyo alikuwa akidanga lakini alitakiwa kumwambia atulie kwa sababu tayari alimpata mwanaume mwenye msima, mwenye pesa ambaye angeweza kumfanyia kitu chochote kile na kumuoa.

Chumbani hakukukalika, kwani kila nilipojigeuza kitandani, ni kama nilisikia sauti ikiniambia muda huo huyo Scaila alikuwa huko klabu na mabwana zake.

Nikatoka chumbani na kuelekea sebuleni, nilitulia kwenye kochi na kuzima taa, nilihitaji kukaa kwenye giza, niyafikirie maisha yangu na Scaila na mwisho nije na uamuzi mmoja kabambe.

Baada ya dakika kadhaa nikasikia mlango wa chumba cha Grace ukifunguliwa na msichana huyo kutoka. Nikajua alikuwa akija sebuleni, haraka sana nikayafuta machozi yaliyokuwa yakinitoka, sikutaka agundue kitu chochote kile. Akawasha taa ya hapo sebuleni.

“Kaka Nyemo!” aliniita huku akiniangalia kwa mshangao, akaanza kunisogelea.
“Mbona sebuleni muda huu?” aliniuliza huku akiniangalia kwa huruma.

“Nimekuja kupumzika!”
“Mbona macho mekundu hivyo?” aliniuliza.
“Macho yanauma mno, nimekaa sana kwenye kompyuta!” nilimjibu.

“Na wifi?”
“Kaenda kwa mama yake!”
“Pole sana!” aliniambia.
“Nashukuru! Nenda kalale Grace!” nilimwambia.

Taratibu akainuka na kuanza kuelekea chumbani kwake. Nilimwangalia kwa nyuma, alivalia khanga moja huku akiwa na nguo ya ndani tu. Alinidatisha, nilitamani kumuita aje kunipa kampani kwani kwa jinsi kibaridi kilivyokuwa kikipiga, Scaila alivyokuwa hayupo nilihisi kabisa nilitakiwa kufarijiwa na Grace usiku huo.

“Ila hapana! Siwezi kutembea na mfanyakazi wangu! Halafu sitaki kumsaliti Scaila,” nilijisemea na kuendelea kubaki sebuleni hapo huku nikiendelea kusononeka kama kawaida yangu.

*** Siku hiyo nilichelewa kulala, nilipitiwa na usingizi alfajiri na kuamka majira ya saa moja asubuhi, tena ni Grace ndiye aliyekuwa akiniamsha na kunitaka niendelea kulala ndani.

Alionekana kunishangaa sana, haikuwa kawaida yangu kulala sebuleni kama ilivyokuwa, kwake, kile kitu kilionekana kuwa si cha kawaida hata kidogo.
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…