Sehemu ya 05
Asubuhi ilipofika, Razak akaamka, akayafikicha macho yake na kutoka kitandani. Akaanza kukumbuka kile kilichotokea usiku uliopita kama kilitokea kweli alikuwa alikuwa katika moja ya ndoto fulani.
Alitulia na kukumbuka vizuri, kichwa chake kikamwambia kwamba kile kilichotokea hakikuwa ndoto bali kilikuwa kitu halisi, ni kweli alikutana na msichana mrembo ambaye hakuwahi kumuona maisha yake yote.
Alijaribu kuivuta sura ya msichana yule kichwani mwake, urembo wake ukautetemesha moyo wake, hakuamini kama kweli ndani ya dunia hiihii kungekuwa na msichana mrembo kama alivyokuwa Aisha huku akiwa chokoraa.
Siku hiyo alitaka kumuona tena Aisha, alikuwa na uhitaji naye, ikiwezekana amwambie kwamba awe mpenzi wake na mwisho wa siku kumuoa.
Wakati akiyafikiria hayo, mara akasikia simu yake ikiwa imeingia ujumbe mfupi, kwa harakaharaka akaichukua simu ile na kuanza kuusoma ujumbe huo uliotoka kwa Sabrina.
“Nataka uniache na maisha yangu,” ulisema ujumbe huo kutoka kwa mpenzi wake, Sabrina.
“Poa, mimi mwenyewe ndiyo nilitaka kukwambia hivyohivyo” naye alijibu.
Muda huo haukuwa wa kumfikiria Sabrina, alimchoka msichana huyo kwa sababu katika kipindi cha karibuni katika uhusiano wao, haukuwa umetulia, kila siku ilikuwa ni kugombana tu.
Moyo wake ulikuwa kwa msichana mwingine kabisa, chokoraa ambaye alikutana naye usiku wa kuamkia siku hiyo, kwa jinsi alivyomjibu Sabrina ujumbe ule, hata yeye mwenyewe alijishangaa kwani alimpenda sana msichana huyo, cha ajabu, ujumbe ule aliujibu harakahara pasipo kujifikiria.
Alipomaliza kuoga, akatoka sebuleni, akakutana na wazazi wake, akazungumza nao kisha kuwaambia kwamba ana safari ya kueleka sehemu fulani ambapo kulikuwa na mtu muhimu alitaka kumuona.
“Nani?” aliuliza baba yake.
“Rafiki yangu! Nitarudi...” alijibu Razak.
“Usichelewe, kuna mengi nitataka kuzungumza nawe...”
“Hakuna tatizo.”
Razak akatoka nje, sehemu ya kupaki magari, kulikuwa na magari mengi ya kifahari, alibaki akiwa amesimama, macho yake yalikwenda kwenye moja baada ya jingine, alitaka kuchukua gari ambalo lingemfanya kuonekana wa kawaida huko atakapokwenda, mwisho wa siku akaishia katika Porte ya kijivu, akaifuata na kuingia, baada ya hapo, akaanza safari ya kuelekea Posta.
Siku hiyo hakutaka kufanya kitu chochote kile, alichokitaka ni kuonana na msichana Aisha tu. Alitokea kumpenda sana, alimhitaji kuliko msichana yeyote yule.
Aliendesha gari mpaka Feri ambapo aliamini kwamba angeweza kuonana na Aisha. Alipofika huko, akalipeleka gari lake katika sehemu ya maegesho, akaliacha hapo na kuanza kuzunguka huku na kule akimtafuta Aisha.
Alizunguka kila sehemu, kwenye yale mawe yaliyokuwa pembezoni mwa bahari, Feri kwenyewe lakini kote huko hakuambulia kitu.
Baada ya saa mbili, akawa amechoka mno lakini hakutaka kurudi nyumbani, alichokitaka ni kumuona msichana huyo hata kabla hajarudi nyumbani, alitaka kumwambia ukweli kwamba alikuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati, hivyo awe wake.
Ilipofika saa saba, tumbo lake likaanza kuuma, alihisi njaa kali hivyo kuondoka na kwenda kwenye mgahawa mmoja wa gharama na kula chakula huko.
Wakati akila huku akiangalia nje, macho yake yakatua kwa vijana wawili, ombaomba waliokuwa wamefanana sana.
Alipowaona, akayakumbuka maneno aliyoongea Aisha usiku uliopita kwamba wale aliokuwa akiwakimbiza walikuwa Ahmed na Mohammed, mapacha ombaomba waliokuwa wakiishi pembezoni mwa bahari.
Je nini kitaendelea....