Simulizi; Nitamlea

Simulizi; Nitamlea

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Joined
Mar 24, 2018
Posts
34,061
Reaction score
79,423
Simulizi; NITAMLEA
Mtunzi; Robert Heriel
+225693322300

Taikon Publisher Presents

Chungu 01.

“Kosa lake nini mpaka nimuue mtoto huyu asiye na hatia? Sitaki kuingia kwenye majuto ya kukitoa kiumbe hiki. Nitakubali majina yote ya dhihaka na kejeli. Lakini nitakulinda mwanangu. Mimi ni Mama, mlinzi wa daima.”
Maneno haya yaliandamana na machozi mazito yaliyomiminika usoni pa Johari, msichana mwenye umri wa miaka ishirini na moja. Alikuwa amesimama mbele ya kioo, ndani ya chumba kidogo alichopanga karibu na Chuo cha Uhasibu Dar es Salaam. Mikono yake miwili ilishika tumbo lake kwa upole na hofu, kana kwamba akiomba msamaha kwa mtoto aliye ndani yake.
Mimba ilikuwa ya miezi mitano. Alianza kuiona sura yake ikibadilika,

Sura ya binti mrembo aliyekuwa kivutio chuoni, sasa ilipotea taratibu. Alikua mnyonge, mwenye macho yaliyojaa usingizi wa mawazo, na tabasamu ambalo lilizikwa na siri nzito ya maisha.
Johari alikuwa msichana wa ndoto kubwa. Tangu akiwa shule ya sekondari alijulikana kwa bidii yake. Alikuwa na matumaini ya kumaliza chuo, kupata kazi nzuri, na kumnunulia mama yake nyumba ndogo kijijini Kisarawe. Lakini sasa… ndoto hizo zilikuwa kivuli cha jana.

Kilichomsumbua zaidi siyo mimba, bali ni woga wa baba yake—Mzee Hemed—mwanajeshi mstaafu mwenye misimamo mikali. Alimlea kwa mkono wa chuma, akisahau kuwa Johari si mwanajeshi bali ni msichana wa kawaida anayehitaji kueleweka. Johari alikua akiishi kwa uoga wa kupoteza heshima kwa familia, lakini zaidi, kuumiza moyo wa mama yake ambaye kila siku alimtumia ujumbe wa maombi na maneno ya matumaini.

Simu yake ililia. Alikuwa ni Salma, rafiki yake wa karibu chuoni. Johari hakuwa na nguvu ya kupokea. Alitaka kulala, lakini usingizi ulimkwepa kama majibu ya maswali aliyokuwa nayo moyoni.
“Baba ataniua… mama atalia… watu watanicheka… lakini mtoto wangu hana hatia. Ananipigapiga ndani kwa matumaini. Mimi ni Mama, lazima nimlinde.”
Alikaa kitandani, akaandika ujumbe kwenye daftari lake la siri:
“Najua kuna adhabu kubwa ya kuvunja heshima ya familia, lakini ninahisi pia kuna adhabu kubwa ya kumwua asiye na hatia. Iwapo nitafukuzwa, iwapo nitabaki pekee, nitakubali… lakini moyo wangu hautakubali kumuua mwanangu.”
********

Usiku ulipita kwa taabu. Johari hakulala. Aliutazama mfanano wake kwenye dari ya chumba chake, akihisi ukimya ukimzidi. Saa kumi alfajiri, aliinuka taratibu, akaswali na kuliweka daftari lake la siri chini ya mto.
Simu ililia tena. Salma.

Aliipokea kwa mara ya kwanza baada ya siku mbili.
“Hallo… Salma?” Sauti yake ilikuwa dhaifu.

“Eeh bwana wee! Umepotea! Kila mtu chuoni anakutafuta. Uko wapi? Hata kwa presentation hatukukuona jana!” Salma aliongea kwa kasi ile ile ya kawaida.
Johari alikaa kimya sekunde kadhaa.
“Salma…” aliita kwa sauti ya chini.
“Naam?”
“Nataka nikuambie siri moja. Lakini usijisikie vibaya. Usinihukumu.”
Salma alinyamaza. Kisha akauliza kwa sauti ya utulivu:
“Upo salama?”
Johari alitulia, akavuta pumzi ndefu.
“Mimi ni mjamzito.”
Kimya. Ni kama dunia iliganda.
Salma hakusema kitu kwa sekunde kadhaa.
“Mungu wangu…” alihemea.
“Mi… mimba ni ya nani Johari?”
Johari alikosa jibu. Machozi yalimtiririka kimya kimya.
“Ningependa nijue, lakini hata mimi sijui tena kama bado yuko upande wangu au alikimbia.”
Salma alinyamaza tena.
“Unamaanisha amekukimbia?”
“Siku ile nilimwambia, alinyamaza. Hakusema kitu. Aliondoka usiku uleule. Na tangu siku hiyo, simu haipatikani. Sijui hata kama yupo Tanzania tena.”
Salma alihisi moyo wake ukivunjika kwa niaba ya rafiki yake.
“Mungu wangu Johari… hivi umebeba mimba ya mwanaume aliyekuacha?”
“Ndiyo. Na bado nina masomo. Na bado sina kazi. Na bado baba yangu hajui. Salma, nina hofu, nina huzuni, lakini pia nina mapenzi makubwa kwa huyu mtoto aliyetumboni”
Salma alikata simu kwa muda mfupi. Dakika tano baadaye, alishika mlango wa chumba cha Johari.
“Fungua. Tuko pamoja.”
Johari alifungua mlango. Marafiki wawili walikumbatiana kimya, kwa muda mrefu. Kisha Salma akasema kwa sauti ya upole:
“Tutatafuta suluhisho. Lakini ahadi yangu ni moja—hutapitia haya yote peke yako.”

Lakini siku tatu baadaye, Johari alipata barua kutoka chuoni…
Barua ya kuitwa kwenye kikao cha nidhamu.
Kosa: Kutohudhuria masomo, na uvumi wa kuwa mjamzito.
Na huku akiwa hajamweleza Baba yake bado, Johari alikuwa anakabiliwa na vita kubwa zaidi…

*****"""""******
Siku ya kikao ilifika. Johari alitembea kwa miguu hadi chuoni. Hakuwa na nauli, na hata kama angekuwa nayo, moyo wake haukuwa tayari kwa starehe ya usafiri. Kila hatua aliyoipiga, alihisi kama anajipeleka mwenyewe kwenye hukumu isiyoepukika.
Alivaa gauni refu la rangi ya buluu iliyofifia, aliyolivaa mara ya mwisho kwenye maombi ya familia kijijini. Hapo chuoni, macho yote yalikuwa kwake. Vichwa vikageuka kumtazama kwa shauku, mengine kwa kejeli. Vicheko vya chinichini, na maneno makali.
Kwenye mlango wa ofisi ya nidhamu, alisimama kwa sekunde kadhaa kabla ya kugonga.
“Ingia,” sauti nzito ya mwanaume ilisikika.
Ndani ya ofisi walikuwamo watu wanne: Mshauri wa wanafunzi, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Wanafunzi, Mwanasaikolojia wa chuo, na Katibu wa kikao. Hawakumtazama kama mwanafunzi. Walimtazama kama tatizo.
“Bi Johari Saidi. Kwa mujibu wa kifungu cha 4.2.1 cha kanuni za nidhamu, umeitwa kujieleza kwa kutohudhuria masomo bila taarifa, na kusababisha vurugu kwa uvumi wa kuwa na mimba ambayo haijathibitishwa rasmi.”

Johari alinyamaza. Alijua hiyo ilikuwa tu lugha ya heshima. Hukumu tayari ilikuwa moyoni mwao.
“Una la kujieleza?” aliulizwa.
Alisimama. Akasema kwa sauti iliyojaa hisia:
“Ndiyo. Nina mimba. Miezi mitano. Sijakataa. Sijatoroka. Nimejificha kwa sababu ya hofu, siyo kiburi. Nilipitia hali ya mshtuko, usaliti, na hofu ya kufukuzwa hata kabla ya kujieleza. Lakini hata kama nikifukuzwa chuo, siwezi kumuua mwanangu ili niendelee na masomo. Siwezi. Nimechagua kuwa mama. Mtu wa kwanza atakayempenda huyu mtoto, hata kama dunia haitampenda.”

Ukimya uliingia. Mwanasaikolojia alimtazama Johari kwa macho yaliyojaa huruma. Lakini macho ya Mkuu wa Idara yalibaki makali.
“Kwa kanuni za chuo, mimba bila ndoa ni ukiukwaji wa maadili,” alisisitiza.
“Na?” Johari aliuliza kwa ujasiri wa ghafla. “Na maisha ya huyu mtoto ni kosa langu? Maadili ya nani? Maadili hayaanzi na tumbo. Yanaanzia kwenye utu.”
Mshauri wa Wanafunzi alinyamaza kwa muda. Kisha akasema:
“Tutakupa jibu wiki ijayo. Ondoka.”
Johari alitoka kwa miguu ile ile, lakini moyo wake ulikuwa na majeraha zaidi. Watu wengine walimwona akipita, lakini hakuna aliyejua kwamba alikuwa anakwenda kuaga chuo chake kimya kimya.

Usiku huo, akiwa amejifungia chumbani, simu yake ililia. Ilikuwa ni baba yake, Mzee Hemed.
Moyo ulimganda. Alishika simu kwa mkono wa baridi.
Aliikata.
Kisha akalia. Sana.

Baada ya kukata simu ya baba yake, Johari alikaa kimya kwa zaidi ya dakika ishirini. Simu ililia tena. Tena. Tena. Aliweka ‘silent’. Hakutaka kusikia chochote. Hakuwa tayari. Hakuwa na maneno ya kutosha kueleza kile anachopitia.
Lakini saa tatu usiku, ujumbe mfupi uliingia:
“Nataka nikuone kesho saa moja asubuhi. Usikose.”
—Mzee Hemed.

Moyo wa Johari ulianza kupiga haraka kama ngoma ya harusi ya huzuni. Hakuwa amewahi kumkataa baba yake. Lakini sasa, alikuwa na sababu ya kumuogopa zaidi ya kawaida. Alikumbuka maneno ya baba yake mwaka jana:
“Mwanangu, dunia hii ya leo si ya wanyonge. Ukikosea njia, usiniangalie. Nimekulea kwa nidhamu, sitaki aibu.”
Johari alijua hiyo “aibu” ndiyo ilikuwa ndani ya tumbo lake sasa. Mzigo wa maamuzi aliyoyafanya. Na sasa alipaswa kumkabili baba yake — mwanamume aliyeamini ukamilifu wa familia kuliko upendo wa kweli.

Asubuhi, Johari alivaa baibui kubwa la buluu iliyokolea. Alifunga kilemba, akaficha sura yake. Alipanda daladala hadi Tabata, alipokuwa baba yake akiishi kwenye nyumba ya jeshi. Mtaa ulikuwa kimya. Alipofika mbele ya mlango, alihema kwa sekunde kadhaa.
Kabla hajagonga, mlango ulifunguliwa. Mzee Hemed alikuwa amesimama mlangoni tayari. Sura yake ilikuwa ngumu. Macho yake yalikuwa kama shoka la hukumu.
“Ingiza miguu ndani,” alisema kwa sauti ya kawaida lakini ya baridi.
Johari aliingia kimya kimya. Alikaa kwenye sofa aliyokulia tangu akiwa mtoto. Kumbukumbu zilimvamia. Picha za utoto, harufu ya sabuni ya baba, sauti ya redio ya TBC usiku… lakini yote hayo yalichafuliwa na kitu kimoja: siri aliyobeba.
Mzee Hemed alikaa kiti cha mbele yake, akamwangalia.
“Nimekuwa nikisikia uvumi. Na sasa nimeona kwa macho yangu. Ni kweli?”
Johari alinyanyua uso wake. Kwa mara ya kwanza, macho yao yaligongana.
“Ni kweli baba. Nina mimba.”
Mzee Hemed alifunga macho yake kwa sekunde. Akavuta pumzi ndefu. Kisha akasimama.
“Hivi… ndivyo ulivyoamua kurudisha mkono wa kulelewa? Kwa aibu?”
Johari alijaribu kujieleza. “Baba, sikukusudia. Ilinitokea. Sikujua namna ya kukueleza…”
“Wewe unadhani kulea mtoto ni mchezo? Au unajua gharama za kuishi dunia hii? Unaelewa maana ya kubeba jina la familia?” Mzee Hemed alizidi kupandisha sauti.

Lakini kisha… kimya kilifuata. Johari alilia. Bila sauti. Bila maneno.
Mzee Hemed alimuangalia binti yake. Akaona binti mdogo aliyelelewa kwa mikono yake mwenyewe. Aliona uso wa mke wake aliyefariki miaka miwili iliyopita. Aliona uoga, maumivu na majuto — lakini pia aliona kitu kingine: msimamo.
Mzee Hemed alipunguza sauti. Kwa mara ya kwanza, sauti yake ilionekana dhaifu.
“Baba wa mtoto yuko wapi?”
“Aliniacha, baba. Sijui aliko.”
Mzee Hemed alikaa tena. Alishusha pumzi.
“Basi, wewe na mtoto huyo… mko mikononi mwangu. Sitakubali damu yangu itemwe njiani. Lakini pia sitakuficha: safari itakuwa ngumu.”
Johari alinyamaza. Kisha akasema:
“Baba, sitaki pesa. Sitaki huruma. Nataka nafasi ya kusimama tena. Kwa ajili yangu. Kwa ajili ya mwanangu.”
Mzee Hemed alinyosha mkono wake. Kwa mara ya kwanza tangu utotoni, alimshika Johari mkono na kusema:
“Tutaanza na kuandika barua ya rufaa chuoni. Hii familia haitajificha.”
*******

Siku mbili baada ya kukutana na baba yake, Johari alirudi chuoni kwa ajili ya kusikiliza uamuzi wa kikao cha nidhamu. Alikuwa amevaa sare ya chuo, japo ilibana kidogo tumboni. Uso wake ulikuwa wa utulivu usio wa kawaida, utulivu unaozaliwa si kwa sababu ya matumaini bali kwa sababu ya kukubali hatima.
Moyo wake haukuwa mwepesi. Lakini sasa alikuwa na mtu wa kumsindikiza babaake, -Mzee Hemed. Mwanajeshi mstaafu, ambaye aliingia kwenye ofisi ya Mkuu wa chuo kwa mguu mzito lakini uso wenye msimamo.
Walipoketi kwenye kiti cha wageni nje ya ofisi, wanafunzi walipita kwa macho ya kushangaa. Wengine walinong’onezana, wengine walijipitisha kusalimia hivyohivyo basi ilimradi. Lakini hakuna aliyejua kuwa siku hiyo Johari alikuwa anapigania haki ya kuishi kama mama, mwanafunzi, na mwanadamu.

Dakika kumi baadaye, mlango ulifunguliwa.
“Bi Johari, tafadhali ingia.”
Akaingia na baba yake nyuma yake. Waliketi. Kamati ile ile ilikuwa mezani.
Lakini kabla hawajaanza kuzungumza, Mzee Hemed alinyanyuka. Alisogea mbele, akawatazama mmoja mmoja.
“Naomba niseme kabla ya binti yangu. Nimeitikia kuwa naye hapa kama mzazi. Najua heshima ya taasisi hii. Lakini naomba muelewe kwamba Johari hakuvunja sheria ya chuo kwa kukusudia, bali alianguka kama binadamu yeyote anavyoweza kuanguka. Na sasa, kama mwanajeshi aliyepigana vita vya kweli, siwezi kuona mwanangu akipotezwa kwa kosa moja. Anahitaji nafasi ya pili. Kama mzazi, siwajibiki tu kumhukumu, bali kumpa sababu ya kusimama tena.”

Ukumbi ulitulia. Hakuna aliyesema neno kwa dakika moja.
Mkuu wa Taaluma alichukua faili, akasoma barua yao ya rufaa.
Kisha akasema:
“Kwa kuzingatia hali ya kipekee, na ushauri wa mwanasaikolojia wa chuo, tumekubaliana: Johari atapewa likizo ya masomo ya miezi sita. Atarudi baada ya kujifungua, kwa masharti ya kuhudhuria vipindi vya ushauri na msaada wa kijamii.”
Johari alishusha pumzi nzito. Machozi yalimtoka. Lakini kwa mara ya kwanza, yalikuwa ya faraja.
Baba yake alimshika bega. Hakuongea, lakini ulimwengu wote wa Johari ulijua — kwa kimya kile tu — kwamba hatakuwa peke yake tena.
Siku hiyo usiku, Johari aliliandika tena daftari lake la siri:
"Leo nimerudi kutoka kwenye kaburi la kukata tamaa. Niliamini hakuna anayeweza kunielewa. Sasa najua, hata mtu mkali anaweza kuwa kinga yako. Baba amenirudia. Dunia haijabadilika, bado kuna lawama, kejeli na macho ya mashaka. Lakini nimejifunza… si lazima dunia inipokee. Lakini mwanangu ananihitaji. Na hiyo tu, inanitosha.”
Mwezi mmoja baadaye, simu yake iliita.
Jina lisilosahaulika lilionekana kwenye skrini: “Dennis.”
Mwanaume aliyempa ujauzito. Aliyemtoroka.
Na kilichoandikwa kwenye ujumbe wake…
“Tuna haja ya kuzungumza. Kitu muhimu sana.”
Je, Dennis amerejea kwa sababu ya mtoto? Ana siri gani? Je, Johari ana sababu ya kumsikiliza tena, au ni mwanzo wa jeraha jipya?

Itaendelea!
Nitamlea Ndio habari ya Mjini.
Kaa humuhumu!

Robert Heriel
Taikon Master kwa Sasa Dar es salaam
 
Simulizi; NITAMLEA
Mtunzi: Robert Heriel
0693322300
Taikon Publishers presents

Chungu cha 02

Simu ya Johari ililia muda mfupi baada ya kutoka kliniki ya wajawazito. Alikuwa ameketi kwenye benchi la mbao jirani na kituo cha daladala, akitafakari kuhusu kesho ya mtoto wake. Alipoangalia simu, alishtuka.

“Dennis.”
Jina hilo lilikuwa limekufa ndani ya kumbukumbu zake, lakini sasa limerudi ghafla kama kaburi lililofukuliwa usiku. Mikono yake ilitetemeka. Hakujua kama aimbe, acheke au aitupie simu mbali. Akabonyeza simu yake kuandika ujumbe:
“Tuna haja ya kuzungumza. Kitu muhimu sana. Tafadhali nisikilize mara moja tu. Nitakuja popote.”
Johari alikaa kimya. Sekunde kadhaa zilipita kabla hajamjibu:
“Kama ni juu ya mimba, umechelewa. Kama ni juu yangu, mimi si yule wa zamani. Kama ni juu ya mtoto… unatakiwa uje na ukweli, si maneno.”
Dennis alijibu haraka:
“Ninakuja kesho saa kumi jioni. Pale bustani ya Mnazi Mmoja. Tafadhali usikose.”
Siku Iliyofuata
Johari alifika bustani saa tisa na nusu jioni, akiwa amevaa buibui refu lililoficha tumbo lake kwa kiasi. Akakaa chini ya mti mkubwa wa mkungu, macho yake yakimtafuta mwanaume aliyewahi kuwa ndoto yake. Mwanaume aliyemwacha wakati moyo wake ukimhitaji zaidi.

Saa kumi kamili, Dennis alifika. Alionekana tofauti. Ndevu fupi, macho mekundu kama mtu aliyeteseka kwa miezi kadhaa. Alikuwa na sura ya mtu mwenye mzigo wa lawama mgongoni.
Wakati macho yao yalipokutana, hakuna aliyesema neno. Walikaa kimya kwa dakika nzima.
“Nashukuru umekuja,” Dennis alianza.
“Ningeweza kutokuja,” Johari akajibu. “Lakini mtoto huyu ni nusu yangu na nusu yako. Anastahili kujua ukweli.”
Dennis alivuta pumzi.
“Nilitoroka si kwa sababu ya woga. Sikuogopa wala mimi sio mtu mwoga. Bali kwa sababu nilihisi sifai. Nilitoka nchini kwenda Nairobi kutafuta pesa ya haraka. Nilikuwa nimepata mchongo ambao uliteka Imani yangu na kunifanya nione itanipeleka kufikia ndoto yangu. Ambayo pia ni ndoto yako. Lakini Nilifanyiwa ulaghai, nikaporwa kila kitu. Nililala mtaani kwa wiki moja kabla ya kuokolewa na mtu wa kanisa. Sikuwa na njia ya kuwasiliana na kukujulisha haya. Leo hii, nimepata kazi. Siyo kubwa, lakini inanitosha kuanza upya. Na nimekuja kukuomba… siyo turudiane kwani nimeshakutia majeraha, bali unikubalie nitimize wajibu wangu kama baba wa mtoto huyu.”

Johari alimtazama kwa muda mrefu. Moyoni alihisi mchanganyiko wa hasira, huruma, na sintofahamu.
“Dennis, nilikuchukia. Sikutegemea uniache na siri hii nzito. Lakini pia... nimeishi na mtoto huyu tumboni kwa miezi sita. Kila siku nikimlilia usiku. Nikisubulishwa pekeangu pasipo msaada. Kila kitu, kila mtu, wore, vyote vilinigeukia na kunielemea. Sasa Siwezi kumsulubisha huyu mtoto kwa makosa yetu sisi wawili. Kama kweli unamaanisha, usiwe tu mzazi kwenye maneno yako yasiyoonekana. Nakuomba uje wakati wa kujifungua. Uushike mkono wangu.”
Dennis alikosa maneno. Akanyanyuka.
“Nitakuwapo. Sitakukimbia tena.”
Johari alimtazama akienda. Moyoni, hakujua kama imani imeanza kuchipua tena au ni maumivu yanajaribu kujigeuza kuwa matumaini. Lakini kwa mara ya kwanza, mtoto aliyekuwa tumboni alicheza ghafla, kama anayetoa jibu kwa miguu yake midogo. Johari alitabasamu kwa uchungu.
“Nimemsikia mwanangu. Anaona yote.” johari alifikiri huku akiondoka kurudi nyumbani

********
Wiki tatu zimepita tangu Dennis arejee. Alikuwa akijitahidi. Aliambatana na Johari kliniki, alilipa ada ya vipimo viwili, na hata kununua vitenge vya kwanza kwa ajili ya mtoto. Hakuwa kamili, lakini alijitahidi kuonyesha uwepo, kujali na upendo kama Baba mtarajiwa.

Johari alibaki na tahadhari. Upendo haukuwa umerejea — bado moyo wake ulikuwa na makovu. Lakini alifurahi kuona kwamba mtoto hatakua bila kujua baba ni nani.
Siku moja, Johari alipokuwa amelala mchana, aliota ndoto isiyo ya kawaida. Alikuwa amesimama juu ya daraja nyembamba, chini yake kukiwa na maji meusi yaliyochemka kama moto. Upande wa pili wa daraja alisimama mwanamke mzee aliyefunika uso kwa mtandio.
Mwanamke yule akasema:
“Maumivu yako hayataisha… lakini uhai wa mtoto huyu utakuwa mwangaza wako. Ukimtoa, unajifuta. Ukimlea, utajipa nafasi ya kupona.”
Johari alishtuka akiwa ametoka jasho. Moyo wake uligonga kwa nguvu. Alishika tumbo lake. Mtoto hakuwa amesogea wala hakuwa anacheza.
Aliwaita Salma na Dennis kwa hofu. Wakakimbizana hadi hospitali ya Amana.

Madaktari walichukua vipimo vya haraka.
Dakika chache baadaye, daktari alitoka akiwa na uso uliojaa tahadhari.
“Kuna changamoto,” alisema. “Mtoto ameanza kushuka mapema, lakini mlango wa uzazi haujajiandaa. Pia moyo wa mtoto unapiga polepole. Lazima tumtoe kwa upasuaji wa dharura — sasa hivi.”
Dennis alitetemeka. Johari akawa analia.
“Naomba msimwache afe… tafadhali,” johari aliwaambia wauguzi.
Walimchukua kwenye machela haraka kuelekea chumba cha upasuaji. Dennis alimshika mkono wake hadi mlango wa wodi maalumu ya uzazi, hapo akazuiwa na daktari.
“Johari!” Dennis alipaza sauti, macho yakiwa na machozi.
Johari alitabasamu kwa uchungu. Akasema:
“Kama nikitoka salama… nitaandika jina lake mimi. Kama nisipotoka… umpe jina lako.”
Mlango ukafungwa.
Dakika 25 zikawa kama masaa. Salma na Dennis waliketi kimya nje, wakisali, wakilia, wakiteta kwa sauti ya hofu.
Mlango wa chumba ukafunguliwa.
Daktari alitoka kisha akasema;
“Mama na mtoto wote wapo hai. Mtoto ni wa kike. Mdogo… lakini jasiri. Tumemuita ‘baby fighter’ hapa ndani kwani alipambana kama malkia mashuhuri wa vita.”
Dennis alijikuta akilia hadharani. Salma alikumbatiana naye kwa furaha.
Dakika chache baadaye, wakampeleka Dennis kumwona mtoto. Alikuwa mdogo sana, lakini macho yake yalikuwa wazi. Alipoitwa jina, alicheza vidole vyake.
“Nitamuita… Neema,” Dennis alisema. “Kwa sababu mimi siistahili, lakini nimepewa.”
Ndani ya chumba kingine, Johari alifumbua macho taratibu. Alikuwa na usingizi mwepesi. Sauti ya mashine, harufu ya dawa, na hewa ya baridi ilimtahadharisha na kurejesha kumbukumbu kuwa bado yuko hai.
Aliuliza kwa sauti dhaifu:
“Mtoto wangu… yuko hai?”
Muuguzi alimtazama na kusema:
“Yupo hai mama. Alilia vizuri sana. Akakuangalia kabla hujazimia.”
Johari akalia. Kwa sauti ya chini huku moyo wake ukifunguka polepole kwa furaha, akasema:
“Sasa najua… hakuna maumivu yasiyolipa zawadi.”
Lakini wakati huohuo, mbali na hospitali… mzee mmoja mrefu mwenye sura iliyochoka, akiwa amevaa kanzu na miwani ya zamani, aliteremka kwenye teksi akiwa na picha ya Johari mkononi.
“Nauliza, huyu binti anaishi wapi?” aliuliza mlinzi wa eneo fulani katika kituo cha teksi kilichokaribiana na kituo cha daladala cha Tabata.

Kwa sababu mtu huyo alifanana kabisa na mzee Saidi—baba wa Johari aliyedhaniwa amefariki miaka mingi iliyopita.
***********


Ni jioni ya siku ya pili baada ya upasuaji. Johari bado yuko hospitali akipata uangalizi maalum. Mtoto wake, Neema, amelazwa kwenye chumba cha watoto njiti kwa uangalizi wa karibu. Dennis amekuwa karibu muda wote, akiwa kimya, akimtazama Johari kwa heshima na hatia isiyoisha.
Lakini mahali pengine, siri iliyozikwa kwa miaka mingi ilikuwa inakaribia kufumuliwa. Kufumuka kama volcano iliyokuwa imezirai.

Mzee huyo mwenye uso wa kuchoka aliingia kwenye nyumba ya kulala wageni maeneo ya Tabata, huku akiwa na picha ya Johari aliyoiweka kwenye pochi yake ya zamani.
Baada ya muda mfupi, alimpigia mtu mmoja namba ya zamani aliyokuwa nayo kichwani miaka yote: “Hemed.”
Simu ya Mzee Hemed ililia usiku akiwa nyumbani, akijaribu kuandika jina la mjukuu wake kwenye shajara yake ya zamani.

Alipoona jina la mpigaji, simu ilimponyoka mkononi. Na neno likamponyoka mdomoni;
“Allan Saidi…” alisema kwa mshangao. Simu ilipigwa tena.
Akaipokea kwa mikono inayotetemeka. “Hallo…”
“Hemed… Ni mimi. Saidi. Nipo hai. Na nipo Dar es Salaam. Naomba nikuone.”
Moyo wa Mzee Hemed ulisimama kwa sekunde mbili. Saidi, kaka yake, aliyetoweka miaka 22 iliyopita baada ya ugomvi mkali wa kifamilia — sasa anampigia simu?
“Unafahamu Johari?” Mzee Hemed aliuliza kwa sauti ya hofu.
“Ndiyo sababu nipo hapa,” sauti ya Saidi ilijibu kwa utulivu.
“Johari… ni binti yangu.”
Kimya kilifunika kila kitu isipokuwa maskio na pumzi za Wazee hawa wawili waliokuwa wakiteta.
“Umesema nini?” Hemed akauliza;
“Nilimpachika mimba mama yake enzi hizo. Ulikuwa haujui. Nilitoroka baada ya msamaha wangu kukataliwa. Lakini nimejua kwa uhakika mwezi uliopita kwamba Johari ni damu yangu. Na najua sasa amezaa. Nataka nimuone.”
Hemed alishtuka sana, uso ukabadilika. Mvutano wa damu, familia, na siri ukamzidi nguvu.
“Huoni kama umechelewa?” aliuliza.
“Hemed… sihitaji kurudisha muda wa nyuma kwani nitakuwa nikipoteza muda mchache niliobakiwa nao Mbele. Nataka tu kujua kuwa binti yangu yupo salama. Na nipo tayari kupokea chochote—laana, dhihaka, au hata ukimya. Ilimradi tu niwe na amani ya moyo wangu kabla sijafa.”

Kesho yake, Mzee Hemed alifika hospitalini mapema.
Alimkuta Johari akiwa amelala, lakini alinyanyuka alipomwona.
“Baba… kuna nini?”
Baba yake alikaa pembeni ya kitanda. Alishika mkono wake.
“Binti yangu. Kuna jambo moja… nilificha. Nililiona kama aibu, sasa najua ni hasara.”
Johari alitulia. Akasubiri.
“Mtu mmoja anataka kukuona. Ni mzee. Na… ni baba yako wa damu.”
Johari alitabasamu kwa mshangao.
“Umesema nini?”
“Sikukuficha kwa ubaya. Nilikulea kama binti yangu. Mama yako alinitegemea. Lakini sasa, ukweli umeshindwa kujificha. Ukweli unanguvu kuliko Kifo. Ukweli umenifundisha funzo gumu. Mzee huyo anatamani kukutana na wewe.”
Johari alitulia. Hakuweza kusema neno. Kichwa chake kilizunguka kwa taarifa hiyo. Mtoto wake alikuwa hajajua chochote kuhusu dunia… naye mwenyewe hajui kabisa mzizi wa damu yake ni nani.
Saa mbili baadaye, mlango wa wodini ulifunguliwa…
Mzee mrefu mwenye ndevu za fedha akaingia polepole. Mikono mitupu. Macho yaliyojaa majuto.
“Johari…” alitamka kwa sauti iliyojawa na vumbi la miaka iliyopotea bila faida.
“Samahani. Samahani sana. Mimi ni Saidi. Mimi… ni baba yako.”
Johari alimtazama mzee huyo asiyejulikana kwa sekunde chache ambazo zilionekana kama miaka. Mikono yake iliyokuwa imeshikilia tumbo miezi yote sasa ilikuwa imeshikilia shuka la hospitali kwa nguvu. Moyo wake ulikuwa kama radi iliyojaa mshangao, hasira, na huzuni ya kina.
“Umesema… wewe ni nani?” aliuliza kwa sauti ya kutetemeka.
Mzee Saidi alisogea hatua moja mbele, macho yake yalijawa na machozi yaliyokauka kwa miaka mingi.
“Mimi ni baba yako wa damu. Nilitoweka kabla hujazaliwa. Nilikuwa kijana mdogo, mwenye hofu, asiye tayari kuwa na mtoto. Nilimwacha mama yako na majuto… na miaka mingi baadaye nikajua kuwa Mzee Hemed alikulea kama mtoto wake.”
Johari alihisi tumbo lake likihema kwa ndani. Moyo wake ulimwambia apige kelele, aondoke, amkatae, lakini akili yake ilibaki palepale ikijaribu kufungua picha mpya ndani ya albamu ya maisha yake. Macho yake yalimtazama Mzee Said kama kitu cha ajabu cha mwisho mwanadamu kukiona kabla hajafa.
“Na unakuja sasa? Baada ya miaka ishirini na moja? Baada ya mama kufa? Baada ya mateso? Baada ya mimi kukimbiwa na baba wa mtoto wangu? Baada ya kuitwa aibu chuoni? Unakuja sasa kusema ‘samahani’?”
Sauti ya Johari ilivunjika kama vipande vya vioo vya chupa iliyopasuka.

Mzee Saidi alinyamaza. Kisha akaketi pembeni ya kitanda, lakini hakukikalia vema — alikaa nusu, kana kwamba hafai kupumzika kwenye kiti cha msamaha.
“Sikuja kuomba ukaribu, wala nafasi. Sikuja kama mzazi anayetarajia heshima. Nimekuja kama mzee aliyeshindwa. Nimekuja kukupa ruhusa ya kunichukia, lakini pia kujua ukweli kwamba ulitoka kwa mtu ambaye hakukustahili kuwa Baba yako, lakini sasa anatamani kukuona ukiwa na maisha bora.”

Kimya kilitawala.
Salma aliingia taratibu wodini na kusimama nyuma ya mlango alipokuaa Denis. Dennis naye alikuwepo mlangoni, akisikiliza bila kupumua.
Johari alifuta machozi.
“Kwa miaka mingi nilijiona kama sikukamilika. Sikuwa najua kwa nini baba alinitazama kwa macho ya huruma kuliko majukumu. Nilidhani labda ni kulelewa bila mama. Kumbe hata mzizi wangu haukujua kuwa ulikuwa umetupwa?”

“Sikuwa na nguvu Johari. Nilikuwa na woga wa mwanaume dhaifu. Naomba unipe nafasi ya kuomba msamaha kila nitakapokuona. Usinisamehe leo, lakini usikatae kujua kuwa bado nakupenda kama nilivyotamani miaka yote.”
Johari hakujibu. Aliangalia picha ya mtoto wake iliyo kwenye bega la kitanda. Aliona uso wake mdogo, pua yake ndogo, macho yaliyojaa uzima.
“Huyu ndiye Neema,” alisema taratibu. “Mtoto ambaye amenifanya nijifunze kuwa si kila aliyeondoka na kukuacha anafaa kusamehewa… lakini kila aliyehai, anafaa kuonyeshwa uzito wa matendo yake.”
Mzee Saidi alitabasamu kwa uchungu. Akasema kwa sauti ya utulivu:
“Neema… jina la rehema. Ndiyo kilichonileta hapa.”
Wakati wote huo, Dennis alikuwa amesimama mlangoni, akilia kimyakimya. Alimwangalia Johari kwa macho ya mtu aliyepoteza, akatambua kuwa hakuna upendo mwepesi unaotoka kwenye maisha yaliyojaa majeraha.

Lakini wakati akigeuka akitaka kuondoka… Salma alimfuata taratibu.
“Kuna kitu unaficha, Dennis,” alisema kwa sauti ya chini.
“Unamtazama Johari kama mwenye deni kubwa… lakini pia una hofu kubwa.”
Dennis alitulia. Akasema kwa sauti ya fumbo:
“Salma… kuna kitu Johari hajui. Na kikitoka… kinaweza kumvunjia moyo zaidi ya mimba, zaidi ya mwanaume aliyemwacha, zaidi ya baba wa damu. Sina hakika kama ni wakati wa kumwambia…”
*************

Jioni ileile, Johari alihamishiwa kwenye wodi ya kawaida. Neema alihamishwa kutoka chumba cha uangalizi maalum na kuwekwa kitandani karibu na mamake. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Johari kumbeba mwanawe vizuri mikononi, kumtazama uso wake mdogo, na kumwambia:
“Karibu duniani mwanangu. Dunia hii haina huruma, lakini nitakupenda hadi pumzi yangu ya mwisho.”
Dennis aliingia dakika chache baadaye akiwa amebeba maua ya waridi na pakiti ndogo ya nepi. Uso wake ulikuwa na tabasamu, lakini macho yake yalibeba mzigo wa neno ambalo halikuwahi kutamkwa.

Johari alimkaribisha kwa tabasamu la heshima. Hakumkumbatia, hakumkaripia. Alimpa nafasi ya kuwepo, si nafasi ya kurudi moyoni.
“Asante kwa kuja,” alisema kwa upole.
Dennis alimtazama mtoto kisha akasema:
“Neema ni mrembo. Nitamlea, nitawalea… kwa uwezo wangu.”
Kabla hajamaliza, Salma aliingia. Aliwatazama kwa macho ya tafakari.
“Dennis,” alisema, “Naomba useme sasa. Kama huwezi leo, itakuwa maangamizi kesho. Sema sasa.”
Johari alishtuka.
“Sema nini? Salma, kuna nini?”
Dennis alikaa. Akashika kichwa. Akavuta pumzi ndefu. Akamtazama Johari machoni, kwa mara ya kwanza akiwa tayari kuvua Siri kubwa iliyouva moyo wake.
“Kuna jambo… ambalo nilikuficha, Johari. Si kwa sababu ya uoga tu, bali kwa sababu sikujua kama litafika mbali hivi. Sikutegemea mtoto. Sikutegemea kupona Nairobi. Na sikutegemea wewe kung’ang’ania kama mlima.”
Johari alinyamaza. Salma alihamasisha:
“Mwambie. Sasa hivi.”
Dennis alisema kwa sauti ya utulivu:
**“Mimi… mimi si Dennis unayemjua kabisa. Jina langu kamili ni Dennis Saidi.”
“Saidi?” Johari alirudia. “Saidi gani?”
“Baba yako mzazi — Saidi — ni baba yangu pia.”
Ghafla hewa ya chumba ikawa nzito. Johari alihisi moyo wake ukisimama, damu ikirudi nyuma kama maji yanayonywewa na ardhi ya jangwa.

Inaendelea;

Ikiwa umeipenda waweza kutoa maoni yako kujua tupo pamoja na mimi niendelee..

Je nini kinafuata? Kaa nami!

Robert Heriel
Taikon Master
Kwa sasa Dar es salaam
 
Eeeh, ishi humu Taikon!
Kule kwenye uchambuzi wa Geopolitics, yaani masuala ya uchambuzi wa mavita mavita ya kimataifa, yaani sijui Ayatollah kampiga ngwara Netanyahu, sijui Trump ameomba poo baada ya kipigo kutoka kwa Muajemi, yale mambo achana nayo.

Ishi humu, humu ndio kwako Taikon!!!
 
Eeeh, ishi humu Taikon!
Kule kwenye uchambuzi wa Geopolitics, yaani masuala ya uchambuzi wa mavita mavita ya kimataifa, yaani sijui Ayatollah kampiga ngwara Netanyahu, sijui Trump ameomba poo baada ya kipigo kutoka kwa Muajemi, yale mambo achana nayo.

Ishi humu, humu ndio kwako Taikon!!!

😄😄
Mkuu acha niwaachie huko wenye shughuli yenu mnyukane. Huko yamenishinda
 
NITAMLEA
Mtunzi: Robert Heriel
Chungu cha 03
———

Dakika kadhaa zilipita. Kimya kilitawala wodi nzima. Pumzi ya Johari ilikuwa nzito kama mtu aliyekaribia kuzama kwenye bahari iliyotulia kama mtego hatari. Mikono yake iliyokuwa ikimbembeleza Neema ilianza kutetemeka. Alimtazama Dennis kwa macho yaliyojaa maswali maelfu.

"Umesema… nini?" aliuliza kwa sauti ya kukata tamaa.

Dennis alitazama chini, akakuna ndevu zake chache kisha akasema: “Baba yako wa damu, Saidi, ndiye baba yangu pia. Hii ina maana kwamba… sisi ni ndugu. Tofauti ni kwamba… wewe ni mtoto wa pili kutoka kwa mke mwingine. Tulikulia sehemu tofauti. Na nilijua kuhusu hili miezi miwili tu iliyopita, baada ya kurudi Dar. Mama alinieleza kabla hajafariki, na akaniachia barua iliyoeleza kila kitu.”

Salma alilia kimya kimya, akajikalia kwenye kona ya kiti. Johari alishusha pumzi ndefu kana kwamba aliangusha mzigo mzito. Alimtazama Dennis, kisha akamwangalia Neema aliyekuwa amelala kwa utulivu kana kwamba dunia yake haijagawanyika vipande vipande.

“Kwa nini… kwa nini hujasema mapema?” aliuliza.

“Niliogopa,” Dennis alikiri. “Niliogopa nitakupoteza, niliogopa nitampoteza mtoto. Lakini baada ya kujua kuwa tumeunganishwa na damu moja, nilijua sina ruhusa ya kukudanganya tena. Nilitaka kuwa muwazi, hata kama itanigharimu kila kitu.”

Johari alinyamaza kwa muda mrefu. Kisha akasema kwa sauti ya mdundo wa moyo uliovunjika: “Kwa hiyo… Neema ni mtoto zinaa”

Dennis alifumba macho. Machozi yakamwagika taratibu. Hakuna aliyetaka hali hiyo, hakuna aliyetarajia hilo. Lakini ukweli ulisimama kama jua katikati ya mchana — huwezi kulikwepa, hata kwa kivuli.

Salma alisimama. Akamwendea Johari polepole.

“Johari… nilijua,” alisema kwa sauti ya pole. “Nilijua siku chache zilizopita. Nilipata taarifa kutoka kwa mtu aliyewahi kuwa karibu na familia ya Saidi. Niliwahifadhi, nikisubiri wakati sahihi. Na wakati huo ndio huu.”

Johari alimwangalia rafiki yake kipenzi kwa mshituko wa kina.

“Ulinificha?” aliuliza kwa uchungu. “Salma, wewe pia?”

“Nilikupenda,” Salma alijibu. “Nilitaka kukuokoa na mshtuko huu ukiwa tayari umeyashikilia maisha ya mtoto wako. Lakini hakuna wakati unaotosha kujiandaa kwa ukweli wa namna hii.”

Johari alijifunika uso wake. Alilia. Alilia sana.

Kisha akasema kwa sauti dhaifu: “Kwa hiyo… kila kitu kimevunjika. Sasa Neema… Neema si tu mtoto wa maumivu, ni zao la damu iliyoingia kwenye kitovu Cha zinaa. Nifanye nini sasa? Nimkatae?”

Dennis aligeuka, akamwangalia Johari kwa macho ya kujuta yaliyojaa maombi ya msamaha. Kisha akasema:

“Neema si kosa. Ni zawadi kutoka kwa Mungu. Damu yetu haiwezi kubadili thamani yake mbele za Mungu. Nilikuja kwa nia safi, sikujua ukweli huu mpaka baadaye. Na bado… bado najua nina wajibu kwa mtoto huyu.”

Johari alimwangalia kwa macho meusi, yasiyo na taa. Alimkumbatia Neema kwa nguvu zaidi, kana kwamba alikuwa akijilinda kutokana na ulimwengu mzima.

Kisha akasema taratibu: “Nitamlea mtoto huyu. Kwa jina la upendo. Lakini nitahitaji muda. Muda wa kusamehe, muda wa kupona, muda wa kuelewa kilichotokea. Na Dennis… sitaki kukuchukia. Lakini sitaki kukurudisha ndani ya moyo wangu kwa sasa. Hii siyo hadithi ya mapenzi tena. Hii ni hadithi ya majuto, maamuzi, na majira.”

Dennis alitikisa kichwa kwa heshima. Akaweka maua mezani, akasogea kumtazama Neema kwa mara ya mwisho kabla hajageuka.

“Sawa,” alisema. “Nikihitajika, nipo. Lakini sitavunja tena milango ya maisha yako. Wewe na Neema… mmekuwa mwanga wangu, hata kwenye giza la makosa yangu.”

Aliondoka kimyakimya.

Salma alimbusu Johari kichwani. “Tuko pamoja. Mpaka mwisho.”

Johari akamwangalia rafiki yake. Kisha akasema: “Salma… tafuta jina la binti aliye na nguvu ya kubeba dunia nzima mgongoni. Maana nadhani hilo ndilo jina la Neema halisi.”

***********

Siku tatu zimepita tangu Dennis aondoke hospitalini bila kurudi tena. Hakupiga simu, wala kutuma ujumbe. Alitoweka kama alivyotokea, lakini tofauti na mwanzo — sasa aliondoka akiwa na ukweli kamili, mzigo wa damu, na nafsi iliyofungwa ndani ya moyo wa Johari.
Johari aliruhusiwa kurudi nyumbani. Alikaa chumba cha kulala kilichojaa vitenge alivyovikata mwenyewe kwa ajili ya mtoto. Kwenye kona ya kabati kulikuwa na pakiti ya nepi iliyoandikwa jina la Neema kwa peni nyekundu. Kila kitu kilimkumbusha Dennis. Lakini pia kila kitu kilimwambia: “Simama.”

Neema alikuwa akicheka kila mara alipoguswa kidevu. Alikua haraka kama maua yanayokua katikati ya jangwa. Na kila macho ya Johari yalipotazama uso wa binti yake, aliwaza: “Huyu ndiye aliyebeba historia ya uhai wangu. Huyu ndiye ushahidi wa kila tone la damu inayotiririka kimya ndani yangu.”

Siku ya Kumi Tangu Kurudi Nyumbani

Salma alimtembelea Johari akiwa na zawadi ya khanga yenye maandishi yaliyosema: “Ukweli huponya, lakini kwanza huuma.”
“Anaonekana kama wewe,” Salma alisema, akimbembeleza Neema.
Johari alitabasamu. Kisha akasema:“Salma… usiku uliopita nilimwota mama.”
“Mama?” Salma aliuliza kwa hofu ya kimya.
“Ndio. Alikuwa amevaa gauni jeupe la harusi. Alinikumbatia, akanitazama usoni kisha akasema, ‘Usiogope jina lake, Johari. Jina si kosa. jina ni kumbukumbu. Neema ni zawadi. Usiikatae kwa sababu ya kifurushi ilichokuja nacho.’”
Salma alinyamaza. Kisha akasema:“Labda ni ishara kwamba upo sahihi kumlea. Na pengine Dennis naye ana nafasi.
Johari alinyamaza. Lakini kabla hajajibu, mlango uligongwa.
Aliposogea kuufungua, alikuta mtu aliyevaa koti la beige, miwani, na alikuwa na bahasha mkononi.
“Johari binti Saidi?” aliuliza.
“Ndio. Wewe ni nani?”
“Mimi ni mwanasheria. Nimeletwa na mzee Saidi. Kuna barua hii kwa ajili yako. Amelazwa kwenye hospitali ya Rufaa Muhimbili — hali yake si nzuri.”
Johari alichukua bahasha kwa hofu. Aliifungua na kukuta karatasi yenye maandishi ya mkono wa uzee. Ilikuwa imeandikwa kwa mwandiko wa mtu anayejua anakaribia mwisho.

Binti yangu Johari,
Nakuandikia nikiwa kitandani, uso wangu umezeeka kuliko umri wangu. Maisha yangu ni mkusanyiko wa makosa, majuto, na sasa matumaini madogo.
Nilikimbia majukumu muda ukiwa upo mbali NAMI. niliikimbia familia, nikakukimbia wewe.
Sikuja katika maisha yako mapema, lakini naondoka nikiwa na imani moja: Uliumbwa kwa sababu ya rehema, si kwa sababu ya ajali.
Neema ni zawadi, lakini pia ni urithi. Nimekuandikia jina langu kwenye hati ndogo ya usuluhisho wa kifamilia. Huu ni uthibitisho kwamba ninakutambua. Na ninataka ujue kuwa damu yako ni yangu , siyo kwa fahari, bali kwa ukweli.

Na kama nitakufa kabla hujaniona tena… basi kumbuka: Mtu anaweza kuwa na kosa, lakini isiwe sababu ya kutengwa na damu yake.

Mimi ni mzazi asiye kamili. Lakini ningetamani kurudi nyuma hata kwa siku moja, nikushike mkono ule wa kwanza ulipozaliwa.
Samahani, Johari.Samahani kwa kila kitu.Baba yako, Saidi.

Barua hiyo ilidondoka mikononi mwa Johari. Alikaa sakafuni, akalia kwa sauti ya bubu anayejaribu kulalama. Salma alinyamaza, akakaa pembeni yake. Neema alilala kwa utulivu kana kwamba sauti ya mama yake ni kelele ya utulivu aliouzoea tumboni.
“Salma…” Johari aliita. “Nahitaji kumwona.”
“Asubuhi twende. Usiku huu tulie, tufunge barua hii kwa moyo, si macho.”

Lakini wakati huo, mbali na hapo…

Dennis alikuwa ameketi kwenye kona ya dirisha la hoteli ya bei rahisi, akiangalia barua aliyoiandika kwa Johari. Hakuipeleka. Alikuwa anaiangalia kama mtu anayepima uzito wa neno moja kabla hajalisema.
Kwenye barua aliandika:

Johari,
Kama nilikuwa mkosaji, samahani. Kama nilikuwa zawadi kwa muda mfupi, nashukuru. Lakini Neema ni zaidi ya sisi wawili. Naamini siku moja atajua kwamba hata kama hakuwa matokeo ya mpango wa binadamu — alikuwa mpango wa Mungu.
Kama hutaki niwepo, sitalazimisha. Lakini nitakaa mbali nikiwa na macho, moyo, na mkono wa kusaidia siku yoyote utakaposema: “Sasa.”
Kwa sasa… nitaondoka mji huu. Lakini si kwa sababu ya woga. Ni kwa sababu ya heshima. Nitakupenda daima — I love you.
Dennis.

Barua hiyo aliikunja, akaweka kwenye bahasha. Aliandika jina la Johari juu. Kisha akaifunga ndani ya kitabu cha hadithi cha mtoto, akaacha mezani kwa mama mlezi wa hiyari aliyemkaribisha tangu afike Dar.
Kisha akaondoka.
———

Saa mbili baadaye, hospitali ya Muhimbili.
Johari aliingia taratibu kwenye wodi ya wazee. Kitanda cha mwisho kilikuwa kimefungwa pazia jeupe. Alipofungua, alimwona mzee Saidi — amedhoofu, lakini alipomtazama binti yake, macho yake yalipata mwangaza wa ghafla.


“Johari…” alitamka kwa sauti iliyobeba uchovu na ushindi.


Johari alimtazama, hakusema chochote. Kisha alipiga hatua mbili mbele, akasogea kando ya kitanda.
Kisha akasema kwa sauti ya pole:
“Nimekuja. Si kwa sababu umekuwa mzazi mzuri. Bali kwa sababu bado naamini kuwa kila mtu ana nafasi ya pili. Baba, nakusamehe. Lakini samahani… siwezi kurudisha muda uliopotea.”
Mzee Saidi alilia. Kwa mara ya kwanza, bila aibu. Akasema:
“Umenipa zaidi ya nilichostahili.”
Kisha akanyosha mkono wake. Johari aliushika.
“Neema yuko hai?”
Johari alitabasamu. “Yuko hai. Jasiri kuliko wote niliowahi kukutana nao.”
Machozi yalidondoka kutoka kwa wote wawili.
Na kwa mara ya kwanza, Johari alihisi kuwa yuko tayari kuanza ukurasa mpya.
********"

Siku tatu baada ya kuonana na Johari, mzee Saidi alifunga safari yake ya mwisho. Alikufa alfajiri akiwa na utulivu usioelezeka, mikono yake ikiwa imefungwa kwa rozari aliyopenda kuitumia kusali tangu alipougua.

Johari alipokea taarifa hiyo akiwa bado amelala, Neema akiwa kifuani kwake. Machozi hayakutoka mara moja moyo wake uliingia kwenye ganzi ya huzuni.
Salma alimshika mkono.

“Pole Johari… lakini umefanya jambo kubwa. Ulimpa msamaha kabla hajaondoka.”

Mazishi yalifanyika Kisutu, katika makaburi ya familia. Johari hakualikwa rasmi, lakini alifika akiwa amevaa buibui jeusi, akisimama mbali na hema kuu la waombolezaji.

Aliwaona wanaume wawili wakiongoza shughuli: Mzee Majaliwa, kaka mkubwa wa Saidi, na Bi Jamila, dada yao pekee. Walimkazia macho mara aliposogea macho yaliyojaa baridi ya uhasama.

Baada ya mazishi, Johari alijaribu kuzungumza na ndugu wa marehemu. Alijitambulisha kwa heshima, lakini kilichofuata kilimvunja moyo zaidi.

Mzee Majaliwa alimtazama juu-chini, kisha akasema:

“Unajiita nani tena?”

“Johari. Binti wa Saidi,” alisema kwa sauti ya adabu.

Majaliwa alicheka kwa dharau. “Saidi hakuwa na binti. Alikuwa peke yake. Huyo mzazi wenu alikuwa na matatizo ya akili kabla hajafa, na sasa unakuja kutaka mali?”

Bi Jamila alingilia: “Tuna ushahidi wote. Hatujawahi kumuona mama yako. Hatukujua hata kama uliwahi kuwepo. Na hata kama ulizaliwa naye, mali ya mzee wetu haiwezi kutolewa kwa watu wa mtaani waliokuja dakika za mwisho.”

Johari aliumia. Lakini kabla hajaondoka, mwanasheria wa familia aliwasilisha wosia.

Mbele ya mashahidi, alisoma:

“Mimi, Saidi Salim, nikiwa na akili timamu, natamka kuwa mali zangu zote — kiwanja kilichopo Tabata, nyumba yangu ya Mbagala, na akaunti ya benki namba XXXX — vitakwenda kwa binti yangu wa damu, JOHARI SAIDI. Namtambua rasmi kama mrithi wangu mkuu. Nimeacha ushahidi wa DNA, barua, na picha ya pamoja kama vielelezo. Kaka yangu Majaliwa na dada yangu Jamila wasiwe na mamlaka ya kugawa mali hizo.”

Ukumbi mzima ulitawaliwa na kimya kizito. Kisha, kelele za ghadhabu zikalipuka kutoka kwa ndugu wa marehemu.

“Huu ni utapeli!” Jamila alipiga kelele.
“Huyo mwanasheria kashirikiana na huyo binti wa mtaani!” Majaliwa alitishia kumtoa nje kwa nguvu.
Lakini wosia ulikuwa halali , ulithibitishwa kisheria. Hata hivyo, damu ya chuki haikutulia.

Usiku huo huo…

Ndani ya nyumba ya Mzee Majaliwa, walikaa kikao cha haraka, kimya na kizito.

“Hatutaruhusu mali ya kaka yetu ichukuliwe na mtoto wa kahaba. Hatujui hata mama yake alikuwa nani,” alisema Majaliwa kwa sauti ya hasira.
“Huyu mtoto… ana nguvu zisizo za kawaida. Ameweza kuteka hata roho ya kaka yetu aliyekufa na taabu,” Jamila aliongeza kwa chuki.

Ndipo mzee mmoja mrefu mwenye ngozi ya kijivu aliingia sebuleni. Alikuwa mganga na mtabiri wa ukoo wao, mtu ambaye jina lake halikutajwa hadharani, bali alijulikana tu kama “Bwana Mshale.”

Majaliwa alimweleza kila kitu.

“Tunataka mtoto huyu aondoke. Akose amani. Akose urithi. Tumrudishe alikotoka — hata kwa njia ya kiroho.”

Bwana Mshale alitikisa kichwa. “Mnachotaka ni kizito. Lakini kinawezekana. Lakini lazima Johari avunjike. Asiwe na nguvu hata ya kuinua macho mbele ya jua.”

Jamila akasema: “Tutafanya chochote. Tutatoa sadaka, hata damu. Ilimradi mali irudi mikononi mwa damu ya kweli.”

Bwana Mshale alifungua kitabu cha zamani. Ndani yake kulikuwa na jina moja kubwa, lililoandikwa kwa mkaa:

“NEEMA.”

“Tutaanza na mtoto. Kwa sababu mama akiwa dhaifu — atasalimisha kila kitu.”


---

ITAENDELEA...

Pole Kwa kuisubiria. Mambo ni mengi ndugu zangu. Maoni yenu hasi au Chanya ni muhimu.
Tukutane chungu Cha 4.
 
Shusha vitu:

UKWELI HUPONYA LAKINI KWANZA HUUMA
 
NITAMLEA
Mtunzi: Robert Heriel
Chungu cha 04

———

Usiku uliotangulia ulionekana kama wa kawaida kwa Johari. Neema alilala mapema, akitabasamu kana kwamba alikuwa ameota ndoto ya peponi. Salma alikuwa amesalia nyumbani kwa Johari kwa ajili ya kumpa msaada kwa wiki mbili za kwanza. Yote yalionekana shwari.
Lakini saa nane usiku, upepo mkali ulianza kuvuma nje ya dirisha. Mbwa wa jirani wakaanza kubweka mfululizo. Miti ilianza kugugumia kana kwamba ilikuwa inalia.

Ndani ya nyumba, Neema alilia ghafla kwa nguvu isiyo ya kawaida. Sauti yake ilikuwa kama kilio cha maumivu, si cha kawaida ya mtoto mchanga.
Johari aliruka kitandani. Akambeba haraka.
“Neema! Eeh Mungu wangu! Mbona unatetemeka hivi?”

Salma naye aliamka, akaja mbio na maji ya uvuguvugu.
“Anatetemeka kama mtu aliyeingiwa na baridi ya ghafla,” alisema. “Na hahisi hata joto la mwili wako. Johari… kuna kitu hakiko sawa.”

Walimpeleka haraka hospitali. Vipimo havikuonyesha ugonjwa wowote. Lakini daktari mmoja wa zamu, mzee mwenye macho ya kipekee, alimsogelea Johari na kuangalia kichwa cha Neema.
Akatamka kwa sauti ya fumbo:“Hii si homa ya kawaida. Msaidie mtoto wako kwa joto la roho, si tu joto la mwili.”
Johari alishtuka. Salma akamvuta pembeni
“Huyu daktari… ni Mwislamu mzuri sana. Lakini watu wa karibu wanasema ana karama ya kuona roho. Anaweza kuona vitu vinavyojificha.”
Johari alimtazama kwa macho ya kuchanganyikiwa.
“Mimi sipendi mambo ya kishirikina, Salma. Lakini… kama kuna kitu kinamnyemelea mwanangu, sitakaa kimya.”

Siku ya Pili:

Siku iliyofuata, Johari alipata simu kutoka kwa mwanamke mmoja mzee, aliyejitambulisha kama Mama Kisu, rafiki wa marehemu mama yake. Waliwahi kukaa pamoja wakati mama ya Johari akiwa na mimba. Mama kisu alifika Kwa Johari baada ya kuelekezwa.
“Nimemuota mama yako usiku. Alilia. Alisema kuna mkono wa giza unainuka juu ya nyumba yako,” alisema kwa sauti ya kupasua moyo.
“Ninachokuambia… si cha uongo. Wewe na mtoto wenu mpo kwenye shabaha ya familia ya mume aliyekupenda, lakini aliyeacha majeraha mengi nyuma.”
“Mimi…?” Johari alishindwa hata kuuliza swali kamili.
“Hakuna mtoto anayeweza kulia ghafla saa nane usiku kwa siku tatu mfululizo — bila sababu ya kimwili,” mama Kisu aliongeza. “Kuna kufuli la kiroho limefungwa juu ya mtoto. Ni kazi ya wale waliokosa haki kisheria sasa wanataka kuitafuta kwa njia ya mapepo.”
Johari alitetemeka. Akamshika Neema kifuani.
“Hili halitatokea. Nitapambana.”
Mama Kisu alimtazama, kisha akatoa kutoka kwenye mkoba wake kitenge cheupe chenye maandishi ya Kiarabu. Akampa Johari, akasema:

“Funika kitanda cha mtoto kila usiku kwa siku saba. Na kabla hapajapambazuka, mwangalie usoni, taja jina lake kwa sauti ya mapenzi, si ya hofu.”

Wakati Huohuo:

Kule Tabata, ndani ya chumba kilichojawa na mafuvu ya ndege, ngozi ya fisi, na mawe ya ajabu, Bwana Mshale aliketi akiwa na Jamila na Majaliwa.
“Jaribio la kwanza limetingisha imani yao,” alisema. “Lakini Johari ni binti wa msimamo. Hatayumba kirahisi.”
Majaliwa akainua sauti: “Tumia nguvu zote. Tumtese hadi ajute kuzaliwa!”
Bwana Mshale alichukua chupa ndogo nyeusi

“Tutamfunga kwa ndoto. Tutamuingiza Neema kwenye giza lisilopatikana. Akilia, hata sauti yake haitasikika.”
Jamila akacheka kwa sauti ya kikatili.
“Tutafanya akili ya Johari ichanganyikiwe. Atadhani anazungumza na mama yake, kumbe ni kivuli cha roho iliyoharibiwa!”
Bwana Mshale alichukua picha ya Neema na ya Johari aliiunganisha kwa sindano moja, kisha akaiviringisha kwenye kitambaa cha uganga, na kusema:
“Kwa jina la uchawi wa wachawi, kwa jina la damu iliyokatwa, fungua milango ya ndoto za giza…!”

Usiku wa Tatu:

Johari alilala akiwa amemfunika Neema kwa kitambaa alichopewa na Mama Kisu. Saa nane kasorobo, ghafla alijikuta kwenye mto mrefu wa damu. Kando ya mto, alisimama mwanamke aliyevalia joho jeupe lenye michirizi ya kijivu.
“Mimi ni mama yako,” alisema mwanamke huyo.
Johari alikimbia kumkumbatia, lakini mama huyo akamsimamisha.
“Wameshaingilia usingizi wa mtoto wako. Ndani ya siku saba, ataacha kupumua akiwa usingizini, kama hutatimiza agano la ulinzi.”
“Agano gani mama?” Johari aliuliza kwa hofu.
“Simama kwenye ardhi ya asili, utaje jina la mtoto wako mbele ya jua linapochomoza. Semeni Kwa pamoja. Vunja vizuizi vya damu.”
“Mama… siwezi pekee yangu.”
“hauko pekee. Angalia upande wako wa kushoto.”
Johari aligeuka. Akamwona mwanamume aliyevaa joho la kijani na ndevu fupi.
Dennis.
“Dennis?” aliuliza kwa mshangao.
Lakini kabla hajamsogelea, ndoto ikavunjika ghafla.


Alifumbua macho yake kwa haraka. Alimtazama Neema alikuwa analia tena, lakini si kwa sauti — kwa sauti ya kimya. Midomo inatikisika lakini sauti haitoki.
Johari akapiga kelele:
“SALMA! SALMA! Haraka! Mtoto hawezi kulia tena!”
Salma aliingia kwa haraka.
Wote walimtazama Neema kwa hofu. Na kwa mara ya kwanza, Johari alitamka:
“Sitakubali. Hii siyo ndoto. Hii ni vita. Na Neema… ni sababu yangu ya kuishi.”
********

Tangu kuzaliwa kwa Neema moyo wa Johari ulikuwa wa baridi isiyo ya kawaida. Ndani ya nyumba ya Johari, kila nuru ilionekana kuzimika mapema, hata taa za balbu ziliwaka kwa mwanga hafifu. Salma alikuwa ametoka kwenda kwao kwa dharura, akimuacha Johari na mtoto.

Mara kadhaa, Johari alihisi hewa nzito. Joto la mwili wake lilipanda ghafla, na sauti ya Neema ilipotea kabisa. Alilia kwa machozi kimya kimya bila kutoa sauti, na midomo yake ilikuwa ikitetemeka
“Nitapigana,” Johari alijisemea, akiwa amembeba Neema kwa nguvu.

Saa kumi alfajiri, Johari alimuita Mama Kisu kwa haraka. Mwanamke huyo mzee alifika akiwa amevaa leso nyeusi, shanga za mbao shingoni, na kikapu kidogo kilichojaa unga mweupe na vifuniko vya miti ya miiba.

“Mtoto wako yupo kati ya dunia mbili. Lakini bado hajakata pumzi. Tunahitaji sadaka ya damu ya mweupe, moto wa mkaa wa mkaratusi, na dua ya ukoo wako wa mama. Leo ndio siku ya vita.”
Johari hakusita. Alitayarisha kila kilichohitajika. Walikaa chini ya kivuli cha mti wa mparachichi, pembeni ya nyumba. Mama Kisu alianza kufanya tambiko lake kwa maneno ya kijadi.

Lakini walipofika hatua ya tatu ya tambiko — upepo mkali ulivuma. Ardhi ilitetemeka kama kuna kitu kinainuka kutoka chini. Maji ndani ya sufuria ya tambiko yaligeuka kuwa meusi. Moto ukazimika ghafla. Na kelele ya ajabu ikasikika kutoka hewani:

“ACHENI! SIO YENU!”
Mama Kisu alisimama kwa haraka. Mikono yake ilitetemeka. Alishika moyo.

“Majaliwa… Jamila… wameleta pepo wa kichawi Wamechimbua kaburi la enzi za mababu... na wamevuta roho ya malkia wa laana.” Aligeuka kwa Johari kwa macho ya hofu. “Naona kivuli cha kifo juu ya nyumba yako.”
“Mama Kisu… usiniache!” Johari alilia.

Lakini kabla hajamfikia, Mama Kisu aliinama ghafla, akatema damu nyingi puani na mdomoni. Alipiga kelele ya mwisho:
“mLinde mtoto… mimi naondoka… mlango wa kuzimu umefunguliwa…”

Akaanguka , akafa papo hapo.

Johari alilia kwa kilio kisicho na mwisho. Akambeba Neema na kukimbilia ndani, akifunga kila dirisha, kila mlango, kila mshono wa pazia. Lakini hewa ya kichawi iliendelea kupenya. Maji kwenye jagi yakaanza kuchafuka bila kuguswa. Kioo cha ukutani kikapasuka chenyewe.

Ndani ya dakika ishirini, Johari alikuwa amepoteza fahamu, akiwa amelala sakafuni, Neema akiwa juu yake akitetemeka bila sauti.
********

Mahali Pengine: Nairobi

Dennis alikuwa kazini kwenye duka la vifaa vya ujenzi. Ghafla, alisimama katikati ya kazi, mapigo ya moyo wake yakimwambia jambo lisiloeleweka.
Akaanguka chini. Akiwa hajitambui, aliona ndoto ya sekunde chache:

'Johari akiwa ameanguka sakafuni, damu ikitiririka puani. Neema akiwa kimya. Nyuma yao, kivuli cha mwanamke mzee kilikuwa kikipiga kelele, lakini bila sauti.
Aliposhtuka, Dennis hakusema neno. Aliomba ruhusa na kuaga bila maelezo ya kueleweka. Aliingia Kwenye Basi kurejea Dar es Salaam.


***
Siku ya 5
Mchana wa siku iliyofuata, Johari alikuwa bado hajazinduka. Neema alikuwa amelala pembeni yake, lakini uso wake ulikuwa kama wa mtoto aliyekata tamaa ya kuishi.

Wakati huohuo, nje ya nyumba, majirani walianza kusema:

“Eeh! Kuna harufu ya vumbi la kaburi!”
“Kulikuwa na kelele usiku… kuna jambo haliko sawa pale ndani.”
Ndipo Dennis alifika. Alikuwa amechoka, macho yamevimba, akiwa mikono mitupu. Alipoingia ndani, alikuta mwili wa Mama Kisu ukiwa umefunikwa kwa leso. Na kelele ya upepo wa mauti ikiwa imesimama juu ya dari.
Alimkuta Johari chini chumbani amekauka. Neema naye alikuwa hapumui sawasawa.
Dennis alifunga mlango. Akaenda kusimama katikati ya chumba.

Alifunga macho. Kisha akasema:
“Baba wa Neema ni mimi. Nitamlinda. Hii roho ya nyeusi ya kichawi haiwezi kushinda damu yangu.”
Alichukua maji kwenye bakuli. Akayasoma sala aliyojifunza kutoka kwa babu yake mzaa mama aliyekuwa mlinzi wa ukoo wa upande wa mama.

“Kwa jina la muumba wa mwanga, kwa jina la damu safi ya toba, ninasimama hapa kama ngao ya mwanangu.”

Ghafla! Sakafu ilitingishika. Kivuli kikaanza kutoka kwenye kuta , sura ya mwanamke mwenye macho ya giza ikatokea. Ilitaka kumvaa Neema.
Dennis alifungua kiganja chake na kutamka:

“Huyu si wa ukoo wenu. Na mimi ni mlango mpya wa kizazi hiki. Rudini kuzimu ambako mliachwa!”
Mwanga mweupe ukamulika kutoka dirishani. Kivuli kililipuka kwa kelele ya kuchana hewa:

“TUUUTAKUJAAA… TUTARUUUU…!!!”
Ghafla, vyombo vyote vilitulia. Harufu ya mauti ilipotea. Neema alipumua kwa nguvu, akalia kwa sauti ya kwanza baada ya siku mbili.
Johari alifumbua macho. Macho yake yalimtazama Dennis. Kwa mara ya kwanza, hakuona tu mwanaume aliyemuumiza… aliona msalaba wake wa tumaini.
---

Dakika Baadaye
Dennis alimwosha mtoto, akamtayarisha, akamuweka kwenye blanketi. Alimnywesha maziwa kwa chupa.
“Neema yuko salama,” alisema kwa upole. “Na nimerudi si kwa sababu ya huruma… bali kwa sababu sasa najua — mimi ndiye ngao ya familia hii.”

Johari alilia. Alimkumbatia. Hakusema neno. Lakini mioyo yao ilizungumza kwa sauti ambayo uchawi hauwezi kuisikia.
***"


Uchawi umeanza kuondoka, lakini si salama bado. Ingawa sauti ya uchawi imetulia, familia kubwa ya damu yenye maagano sasa imeanza kusonga kwa visasi vya kurithi na chuki za ukoo.
---

Kikao cha Siri: Ndugu wa Mzee Saidi

Katika kijumba cha urithi huko Magomeni, ndugu wa Mzee Saidi walikuwa wamekusanyika. Meza kubwa ya mninga ilikuwa imejaa nyuso zenye hasira, ukimya na ukatili wa maneno yaliyokandamizwa kwa muda mrefu.

Jamila — dada mkubwa wa Saidi — alisimama na kusema kwa ukali:

“Huyu Johari si sehemu ya ukoo huu. Alizaliwa nje ya ndoa. Alifichwa. Na baba yetu alimkana hadi kifo. Sasa anakuja kurithi ardhi yetu? Hapana. Hatufanyi ujinga huo.”
“Lakini yuko kwenye wosia wa marehemu,” mmoja wa wazee alijaribu kusema kwa tahadhari.

Jamila akagonga meza:
“Wosia unaweza kubadilishwa kama ulifanywa kwa udanganyifu wa kihemko! Tutapeleka kesi mahakamani. Na kabla ya hapo… tutaondoa uhai wake wa kiroho.”
Majaliwa akanyoosha mkono.

“Nina mtu wa kazi hiyo. Bwana Mshale yupo tayari kupeleka shetani mfu hadi nyumbani kwa Johari.”
Jamila alikubali kwa kichwa.
“Anataka urithi? Tumpe vita ya ukoo.

"***
Wakati Huo: Nyumbani kwa Johari
Johari alikuwa amekaa sebuleni, macho yake yakiwa kwenye picha ya mtoto wake wa siku sita. Neema alikuwa amelala kwa utulivu. Dennis alikuwepo, akipanga orodha ya vitu vya kliniki.

Lakini Johari alikuwa kimya.

Dennis alimsogelea:

“Unaota?”
Johari akatabasamu kwa huzuni.
“La. Lakini ninaona. Ninaona mbele kuliko macho. Mama yangu alikuwa na ndoto za kweli. Na sasa… nahisi kipawa kile kinarudi kwangu.
Dennis alimshika mkono.
“Tutapambana pamoja.”
Johari alitulia.
“Mzee wako… Saidi… aliacha nini kwenye wosia?”
Dennis alitoa bahasha ya zamani. Ndani kulikuwa na barua fupi iliyoandikwa kwa mkono wa mtu aliyechoka lakini mwenye hekima:

“Kwa jina la damu yangu, napenda kusema wazi kuwa Johari — aliye binti yangu wa damu — anastahili sehemu ya urithi wangu. Shamba la Kigamboni, nyumba ya Kariakoo, na sanduku la kumbukumbu ya ukoo. Nimekosea sana. Lakini napenda dunia ijue kuwa nilijaribu kurekebisha. Johari ndiye mlango wa rehema wa ukoo huu.

Johari alisoma barua hiyo huku machozi yakimtiririka.
“Lakini watakataa,” alisema. “Sijawahi kuitwa binti hadharani. Sasa wanataka kuniua kimya kimya.”
---

Usiku wa Sita:
Saa nane usiku, upepo wa ajabu ulivuma ndani ya nyumba. Dirisha la chumba cha Johari lilifunguka ghafla. Sauti ya kichaa ikasikika kutoka hewani:

“Toka kwenye nyumba ya ukoo! Urithi si wako! Toka au upotee!”
Johari alishtuka. Dennis alikuwa usingizini chumba kingine. Neema alianza kulia kwa sauti ya ajabu — kama mtu mzima.
Johari alikimbia kumchukua. Lakini ghafla… taa zilizimika. Vyombo vikaanza kuanguka sakafuni. Nguo zikaanza kuruka hewani. Kivuli cha mtu kikasimama kwenye kona ya chumba:

“Mimi ni mlinzi wa ukoo huu. Umeingia pasipo idhini. Utapotea.”
Johari alilia:
“Hapana! Siwezi kuondoka! Hii ni haki yangu — damu yangu!”
Kivuli kilimfuata kama ukungu wa baridi Kumkaba koo. Akashindwa kupumua.
---

Dennis alishtuka. Aliona ndoto ya Johari akinyongwa na kivuli chenye mikono kama mizizi ya miti. Alikimbia hadi chumbani akafungua mlango kwa nguvu.

“ACHIA MKE WANGU!”
Mwanga mkali ukatoka kwenye kiganja chake. Haukutoka kwa umeme, wala jua. Ilikuwa nuru kutoka ndani ya damu ya ukoo — nuru ya msamaha na agano la toba alilowahi kulitoa kwa Mungu alipokuwa mtoto mdogo.
Kivuli kikapiga kelele:
“Unayo damu ya waliokombolewa…!”
Kikayeyuka.

Johari alianguka sakafuni akiwa hai lakini amedhoofika.
Dennis alimkumbatia. Akamuweka kitandani. Akamfunika Neema.
“Hii vita si ya kawaida,” alisema. “Na siwezi kuruhusu upotee.
---

Siku ya Saba:

Asubuhi, Johari aliamka akiwa na nguvu mpya.

“Naenda kwa mwanasheria wa Saidi,” alisema. “Kama wameanza vita ya urithi, basi na mimi nina silaha — ukweli na damu ya haki.”
Dennis alimuangalia kwa heshima. Aliona ndani yake sio mwanamke tu, bali askari jasiri.
“Nitakuwa upande wako. Mpaka mMwisho.

ITAENDELEA...

Maoni Yako yawe Hasi au chanya ni muhimu.

Tukutane chungu Cha 05
 
Hili ni tatizo labda mwandishi anataka tension kuona kuna wafwatiliaji?wengi ni wasomi wa kimyakimya shaka ondoa mwaga wino ndg!kazi iko vzr🤝
 
NITAMLEA
Mtunzi: Robert Heriel
Taikon Publishers

Chungu Cha 05

Johari aliamka asubuhi hiyo akiwa mwepesi kimwili lakini moyo wake ulikuwa mzito kama mwamba. Usiku uliopita ulikuwa na ndoto ya ajabu, ndoto iliyomrudisha enzi za utoto, akiwa anatembea kwenye shamba la mihogo na mwanamke mmoja mzee ambaye sauti yake haikuonekana lakini maneno yake yaligonga ndani ya moyo wake:
“Haki ya mtu haichukuliwi bila damu, lakini damu isiyo ya vita ni laana.”

Akashtuka ghafla, akamkuta Neema kando yake, alikuwa kanacheka tu huku akicheza vidole vyake vya miguu. Dennis alikuwa jikoni, anaandaa chai na mkate wa siagi, macho yake yakiwa yamepotea kwenye mawazo. Mawazo ya hatma.

“Wewe siyo baba wa kawaida,” Johari alimuambia kwa sauti ya chini, bila hata kumwangalia.
Dennis akamwangalia, akatabasamu kwa shida. “Na wewe siyo mama wa kawaida.”
“Leo nitaenda kwa wakili wa baba yako,” Johari akasema, “nataka kujua kila kitu kuhusu wosia. Siyo stori tena, Dennis. Nataka karatasi. Sahihi. Na kila alichosema kabla hajafa.”
Dennis akanyamaza, akamsogezea kikombe cha chai. “Ukihitaji niandamane nawe…”
“Leo, naenda peke yangu. Kuna vita zingine mtu huingia pekee,” Johari akamkatisha akasema na kuondoka taratibu, mkono mmoja umemshika Neema kifuani kama kinga ya moyo.

Aliingia kwenye pikipiki ya mtaani, akamwambia boda ampeleke ofisi za wakili Luwunga maeneo ya Posta. Njiani hakusema neno. Macho yake yalikuwa yamekaza kuangalia mbele kana kwamba anapigana kwa macho.

Alipofika kwa wakili, mlinzi alimfungulia, akamwelekeza moja kwa moja hadi kwa Bw. Luwunga. Mzee huyo alimpokea kwa heshima kubwa, kama mtu aliyemngojea kwa miaka mingi. “Karibu binti wa marehemu,” alisema kwa sauti ya ukale. “Habari zako ni nzito, lakini haziogopeshi watu waliopo upande wa ukweli.”

Johari aliketi, akavua ushungi wake na kumwangalia wakili huyo moja kwa moja machoni. “Mzee wangu, usinizungushie maneno kama wazee wa familia. Mimi si msichana wa kurembesha maneno. Nipe nakala ya wosia, kila kilichoandikwa, kila alichoacha, na nafasi yangu ndani yake.”

Luwunga akachomoa faili nene, akalifungua. “Kuna wosia mmoja ambao wengi wanaujua. Lakini kuna barua nyingine, ya mkono wake, ambayo aliandika kwa ajili yako pekee. Alisema nikikupatia mapema, unaweza kudhoofika. Alisema: ‘mpatie Johari barua hii akishaonyesha hana tuu huzuni, bali msimamo.’”

Johari akanyamaza. Luwunga akamkabidhi karatasi moja ya zamani lakini yenye mwandiko wa hivi juzi, imeandikwa kwa mkono wa mtu mwenye uchovu wa miaka. Alianza kusoma, moyo ukipiga mapigo yasiyoeleweka.

“Kwa Johari wangu wa damu… Najua umelia, umekosa, umepigwa na kuangushwa. Lakini ukisoma barua hii, jua kuwa damu yako ina mzizi wa tofauti. Uko kwenye ukoo wa akina Saidi — ukoo wenye baraka lakini pia laana iliyozikwa ndani ya historia. Utamlea mtoto aliyezaliwa na roho ya kuona, Neema. Yeye ni daraja. Daraja la kupita kutoka historia ya damu hadi baraka za kizazi kipya.
Shamba la Kigamboni, nyumba ya Kariakoo, na sanduku la ukoo , vyote ni vyako. Lakini utapigana. Na ukilegea, watachukua hadi roho ya mwanao.”

Johari alimaliza kusoma akiwa anatetemeka. “Hii… hii si barua ya kawaida....”

Luwunga akamwangalia kwa huruma. “Wote waliotangulia walishindwa kuhimili mzigo huu. Baba yako alikuwa wa kwanza kuikimbia historia yake. Lakini kwa kukuandika wewe hapa… alikuwa anakutambua kama askari wa mwisho katika ukoo wenu.”

Johari akachukua faili na karatasi zote. Akamshukuru wakili kwa sauti ya chini, kisha akatoka nje akiwa kama aliyechomwa na jua la utosi. Hakurudi nyumbani. Alielekea Kariakoo, kwenye ile nyumba ya marehemu. Mlinzi alipomwona, alimtambua na kumfungulia bila kuuliza.

Aliingia moja kwa moja kwenye kabati la nyuma ya chumba cha kulala. Ndani yake alikuta sanduku la mbao, limefungwa kwa kufuli la chuma. Kando ya kabati, kulikuwa na maandishi madogo:
“Weka damu ya mrithi hapa.”

Bila hata kufikiria, Johari alichoma sindano kwenye kidole, akaweka tone la damu. Sanduku likafunguka polepole. Ndani yake kulikuwa na kitabu kikubwa cha ngozi, picha ya mama yake akiwa mjamzito, ramani ya nyumba ya ukoo kule Bagamoyo, na mkufu wa shaba wenye jina la Neema.

Johari aliketi sakafuni, akaanza kusoma ukurasa wa kwanza wa kitabu cha ukoo. Ndani yake, kulikuwa na majina ya mababu zake, baadhi wakiwa walimu wa dini, wengine waganga, wengine wachawi waliogeuka watakatifu.

Kisha akaona jina lake: Johari binti Saidi, limeandikwa kwa kalamu ya dhahabu, kando yake kukiwa na maneno: “Aliyetoka kwenye giza kuleta nuru.”

Ghafla, simu yake ikaita. Dennis. “Upo salama?” aliuliza kwa hofu. “Salma kaniambia kuna kesi imefunguliwa dhidi yako kuhusu urithi. Kina Jamila wamekufungulia mashitaka.”
Johari akatabasamu kwa uchungu. “Sawa. Vita sasa imewekwa mezani.”

Usiku huo alirudi nyumbani akiwa mchovu wa mwili lakini mwenye moto thabiti. Dennis alimwandalia maji ya moto na chakula. Neema alikuwa amelala lakini alikuwa anaota. Aliamka ghafla, akamwangalia mama yake na kusema kwa sauti nyororo:
“Mama… yule uliyemuita mama yako… siye aliyekuzaa.”

Johari alitetemeka. Dennis aliamka na kuketi karibu. “Umesema nini?”
Neema alitulia. Halafu akarudia tena, kwa sauti ya utulivu usio wa mtoto:
"Yule alikuwa mama mlezi. Mama yako wa damu aliuawa siku tatu baada ya kukuzaa.”
Johari alishika kifua. Moyo wake ulikuwa kama bomu linalosubiri kulipuka. “Hapana… usinieleze hivi…”

Dennis akamshika mkono. “Mtoto wetu anaona zaidi ya sisi. Na kama kweli haya ni kweli… basi urithi sio wa mali tu, ni wa maumivu ya damu. Damu ya ukoo na vizazi”

Johari akainuka taratibu. Akamchukua Neema mikononi. Akasema kwa sauti ya kujiamini:
“Watakata urithi. Watachoma nyumba. Watafanya kila hila. Lakini mimi ni mama wa kizazi kipya. Sina muda wa kulilia damu ya jana wakati nina damu ya kesho kifuani mwangu.”

Neema alitabasamu. Dennis alimtazama Johari kwa heshima mpya.
Kwa mara ya kwanza, hakuona mwanamke aliyepitia mengi. Alimwona kama shujaa aliyezaliwa na aliyetumwa kuzibadilisha nasaba zilizochafuka.

Na usiku huo… Johari aliandika barua ya kwanza rasmi kwa jaji wa mahakama ya wilaya:
“Mimi ni Johari binti wa Saidi. Sina hofu ya haki yangu. Nipo tayari kukutana nao uso kwa uso. Kwa ajili ya mtoto wangu. Kwa ajili ya jina langu. Na kwa ajili ya kizazi kinachokuja.”
------

Kulikuwa na ukimya mzito mahakamani, ukimya wa roho zaidi ya miili. Ukimya wa majira yanayosubiri kishindo.

Jaji aligonga mezani mara tatu kwa nyundo ya mbao. Sauti hiyo iligonga mioyo ya watu kama radi kabla ya mvua ya ukweli kunyesha.

“Mahakama hii ya Wilaya ya Kinondoni inafungua kikao cha kusikiliza kesi ya urithi kati ya mlalamikaji Johari binti Saidi dhidi ya walalamikiwa, yaani ndugu wa marehemu Saidi, akiwemo Jamila Saidi na Majaliwa Saidi.”

Watu walikuwa wamejaa ndani ya mahakama hiyo. Viti vya mbele waliketi ndugu wa familia ya Saidi, upande wa kulia akiwa Johari akiwa amevaa vazi la heshima, lakini sura yake ilikuwa kama ya mtu aliyekula sumu. Pembeni yake alikaa Dennis, akiwa kimya kama kivuli, lakini tayari kwa lolote.

Majaliwa aliketi upande wa walalamikiwa, akiwa amepiga suti ya bei ghali, lakini macho yake yalikuwa kama ya fisi anayekodolea maiti. Jamila alipaka midomo rangi nyekundu, lakini ndani yake kulikuwa na woga uliojificha kwenye tabasamu la kishetani.

Wakili wa Johari, Bw, Luwunga, akasimama. Alipumua taratibu, akatulia kwa sekunde chache kama anasikiliza sauti ya ndani ikimwambia nini aseme.

“Mheshimiwa Jaji,” akaanza, “leo si hoja za maneno tu, bali ni hoja ya damu. Leo tunawasilisha ushahidi kamili kwamba Johari si tu mtoto wa marehemu Saidi kwa damu, bali pia kwa dhamira na desturi. Na kama kuna haki duniani, basi hakika haitamtelekeza.”

Jaji alimtazama. “Endelea na ushahidi.”

Wakili Luwunga alitoa faili nene. Akaweka mezani nakala ya cheti cha kuzaliwa cha Johari, barua ya mkono wa marehemu Saidi aliyomwandikia Johari siku chache kabla ya kifo chake, na ramani ya mali zake zilizogawiwa likiwemo shamba la Kigamboni, nyumba ya Kariakoo, na akaunti ya benki yenye milioni 92.

“Kila alichoandika marehemu kinaonyesha kuwa alimtambua Johari kama mtoto wake wa damu. Hii hapa barua iliyo na sahihi yake, na hii hapa DNA test iliyofanywa siku tano kabla ya kifo chake, ambayo inathibitisha kwa asilimia 99.998 kuwa Johari ni binti yake wa halali.”

Jamila aliruka kama mtu aliyekalia mkaa. “Hapana! Tunapinga! Barua hiyo ni bandia. Tumeletewa picha tu, siyo original!”

Majaliwa akaongezea: “Na hiyo DNA? Iliandaliwa na wao wenyewe. Tusiingize sayansi ya mitaani kwenye mambo ya kifamilia.”

Wakili Luwunga aligeuka taratibu, akawatazama, kisha akamtazama jaji. “Mheshimiwa, tutaleta mtaalamu kutoka maabara ya serikali kuthibitisha uhalali wa nyaraka hizo. Lakini kabla ya hapo, tunaomba ruhusa kusoma sehemu ya barua ya marehemu Saidi mbele ya mahakama.”

Jaji akasema kwa sauti nzito: “Ruhusa imetolewa. Soma.”

Wakili alisoma:
“Kwa Johari wangu… Kama utasoma barua hii, basi ni wazi kuwa nimeondoka duniani. Nilipotea kwa muda mrefu, lakini damu haiwezi kujificha. Wewe ni binti yangu. Nimekosa nafasi ya kukuona ukikua, lakini naomba nikae nawe katika maisha yako yajayo kupitia urithi huu. Nao si urithi wa mali tu, bali wa jina langu, damu yangu, na baraka zangu. Wote waliopinga hili wanajua ukweli, ila wameamua kuficha.”

Baada ya kusoma, ukimya uligubika ukumbi wa mahakama. Hata upepo uliokuwa ukiingia dirishani ulisitisha safari yake. Muda huo, Johari alimtazama Majaliwa machoni, macho yake yakisema maneno ambayo midomo haikuyasema:
“Ulitaka kuniua kwa uchawi, lakini sasa mimi ndio nipo mezani mbele yako, na haki iko upande wangu.”

Majaliwa alipiga kelele: “Huyo mzee hakuwa na akili timamu kabla hajafa! Tulikuwa naye, alisahau hata jina lake la mwisho. Kila siku alikuwa akitaja majina yasiyojulikana. Alisema atawagawia wake zake wote nyumba wakati alikuwa na wake wawili tu. Huyu msichana anatunga!”

Jamila naye akajitutumua. “Na hata kama ni mtoto wa damu, hakujulikana kwa familia. Hakufanyiwa tambiko. Hakutambuliwa rasmi. Huu urithi ni kwa watoto wa ndoa tu!”

Wakili wa upande wa Johari alijibu kwa busara: “Basi mahakama itumie sheria ya mtoto halali wa damu, sio mila zinazobagua watoto wasiotokea kwenye ndoa.”

Jaji aliandika vitu kadhaa kwenye daftari lake. Halafu akasema: “Mahakama itapokea ushahidi wote na kuendelea kusikiliza hoja za pande zote. Kikao kinaahirishwa hadi kesho saa tatu asubuhi kwa ajili ya ushahidi wa mtaalamu wa DNA na mashahidi wawili waliokuwa karibu na marehemu.”

Wakati kila mtu akinyanyuka kutoka kwenye viti, Neema aliyekuwa amebebwa na Dennis alilia ghafla, kisha akasema maneno kwa sauti ya ajabu:
“Babu alisema: urithi wangu ni damu ya amani, sio pesa ya chuki. Msigawane makaburi ya ndugu yenu!”
Kila mtu aligeuka. Mahakama ilitulia. Jaji alimtazama mtoto huyo kisha akasema polepole:

“Ninahitaji kukutana na mtoto huyo binafsi. Mahakama inapaswa kujua kama huyu ni mtoto wa kawaida au la."
Neema alitulia. Johari alimkumbatia. Dennis alimtazama kwa mashaka, lakini moyoni alijua, nguvu ya kizazi kipya imeanza kufanya kazi.

Nje ya mahakama, Jamila alimtupa Majaliwa macho ya sumu. “Huyu msichana si mtu wa kawaida. Tuna kazi ya kufanya usiku wa leo.”
Majaliwa akamjibu kwa sauti ya chuki: “Tutampeleka kwa Bwana Mshale. Ikiwa sheria haitufai, uchawi utamaliza kazi.”

Na usiku huo, tambiko jipya lilianza…

Inaendelea

Maoni Yako ni muhimu.
 
NITAMLEA
Mtunzi: Robert Heriel
Chungu cha 06

Usiku ulitanda kama giza la kiyama. Mtaa wa Manzese kulikuwa kimya, lakini ndani ya nyumba moja ya ghorofa ya pili, ndimi za mshumaa zilikuwa zinacheza kama mapepo. Kwenye chumba kidogo kilichojaa moshi wa ubani, walikuwepo Jamila, Majaliwa, na mzee mmoja aliyefunga kichwa kwa leso ya manjano, miguu yake ikiwa kwenye damu ya jogoo mweusi.

“Hamuwezi kushinda kesi ya urithi kama haki ipo upande wa mtoto wa damu,” aliongea kwa sauti ya kukoroma, “isipokuwa haki hiyo iogope kuonekana.”

Majaliwa alikunja uso, macho yake yakiwa na hasira kama mtu aliyekosa shabaha ya mwisho. “Tunaomba njia ya kuhakikisha jaji haoni tena ukweli. Na yule Luwunga, huyo wakili mshenzi, anasumbua sana.”

Mganga alitabasamu. Akachukua kifuko kidogo cha ngozi, akatoa jini mdogo aliyekuwa amefungwa kwa nyuzi za shaba. Jini huyo alitupwa kwenye sakafu, ukawa moshi mweusi, ukajizungusha kama kimbunga ukajaza chumba chote.
“Leo… Ndotoni mwa jaji na Luwunga, kitanda chao hawatalala,” mganga alikoroma. “Wataona moto hata kwenye maji ya baridi. Kesi yenu mtaishinda si kwa ushahidi, bali kwa woga wao.”

Usiku huohuo, jaji aliyekuwa amemaliza kuandika maelezo ya mashahidi, alishtuka kutoka usingizini akajikuta akiwa analia. Alijikuta amelala juu ya moto, jicho moja la jini likimkodolea. Jini yule mdogo alifanana na mnyama komodo dragon mwenye jicho moja. Wakili Luwunga naye alikurupuka usingizini, kalamu yake ya kazi ikiwa imechomoka ndani ya mfuko na kupinda kama nyoka. Ndani ya nyumba yao, harufu ya mzoga ilizagaa, bila asili, wala chanzo.

Siku iliyofuata mahakamani, jaji aliketi akiwa na sura ya mtu aliyepoteza fahamu. Alitazama barua za ushahidi kama karatasi tupu. Luwunga hakuweza kusimama vizuri, alipata degedege ya ajabu kabla ya kuingia ukumbi wa mahakama.

Majaliwa akacheka chini ya kope zake. Jamila akavuta rosary ya wachawi walioweka kwenye shingo, akasema kwa sauti ya moyoni:
“Leo tunavuna. Leo, haki itaogopa kutazamwa.”

Na kweli, dakika thelathini baada ya kikao kuanza, jaji aligonga nyundo mara tatu.
“Kwa ushahidi usio thabiti, na kutokana na kutokuwepo kwa uthibitisho wa wazi wa uhalali wa mlalamikaji, Mahakama hii inaamua urithi wote wa marehemu Saidi Saidi kubaki kwa ndugu zake waliobakia, yaani walalamikiwa Jamila na Majaliwa.”

Ukumbi ulilipuka. Majaliwa akapiga kofi moja la taratibu. Jamila alitupa kitambaa chake, akacheka kwa kejeli.
Johari aliketi, machozi yakimdondoka bila nguvu. Neema alikuwa usingizini pembeni yake, hajui kuwa dunia ilikuwa imemkataa kwa mara nyingine.

Nje ya mahakama, mvua ndogo ilinyesha. Dennis hakusema neno. Walisafiri kimya mpaka nyumbani, nyumba ya kupanga iliyokuwa Tabata. Siku kadhaa baadaye, Dennis alifungasha begi lake. Alimwangalia Johari na kusema:
“Naenda Morogoro, kuna kazi ya muda imetokea. Nikifanikiwa, nitawatafuta.”
“Kama hutarudi, niambie mapema,” Johari alimwambia, kwa macho ya mtu aliyeshajifunza kuachwa.
Dennis alinyamaza. Akapiga hatua tatu, akarudi, akambusu Neema kwa upole, kisha akaondoka.

Maisha yakabadilika. Johari hakuwa tena yule aliyekuwa anatembea na matumaini. Alianza kuuza uji wa moto kwenye chupa ya chai, kila alfajiri akipiga hatua mitaani kwa sauti ya kuvutia wateja:
“Uji motooo! Wa lisheee! Usiache mamaaaa!”
Lakini wengi walimcheka, wengine wakamnong’onea:
“Yule ni binti wa Saidi, si alishindwa kesi?”
“Mwenzenu amefulia. Hata chakula hana.”

Siku moja, mwenye nyumba aliibuka kwa hasira. “Sikiliza mama Neema, miezi miwili hujalipa kodi. Na sitaki maneno! Nikipata mtu wa kupanga, nakuondoa.”
Johari alijaribu kusema, “Naomba wiki moja, mzee wangu...”
“Wiki ya nini? We si ulishindwa kesi? Ulikuwa unajiona wa maana sana! Hebu toka nje,” mzee huyo alifoka kwa hasira, akifungua na kufunga mlango kwa nguvu.

Bahati sana, siku hiyo hiyo, mzee Hemed alikuwa amerejea kutoka mkoani, safari ya miezi miwili ya kwenda kuuguza dada yake Mwanza. Alipita kwa Johari kumjulia hali. Alipokaribia nyumba hiyo ya kupanga, alisikia makelele.

“Eti mtoto wa mzee Saidi!” mwenye nyumba alipiga kelele, “Hapa siyo kwa maneno, hapa ni kwa hela! Hebu toka nje, mama!”

Johari alikuwa amenyeshewa na mvua ya aibu. Majirani wote walikuwa wamekusanyana wakishuhudia. Alikuwa amesimama nje ya mlango akiwa na Neema mikononi, mkononi amebeba chupa yake ya chai iliyopoa.

“Mwenye nyumba, acha hizo!” sauti ya Mzee Hemed ilikatisha makelele. Wote wakamwangalia.
Johari aliduwaa. “Baba…” alitamka kwa mshangao.
“Binti yangu,nimerudi! Dennis yupo wapi?"
“Ameondoka,” Johari alijibu kwa sauti ya chini.
Mwenye nyumba alimtazama mzee huyo, “We nani tena?”
“Mimi ni mtu niliyemlea na kumuangalia mtoto huyu. Huyu unayemsimanga. Na sasa nimerudi. Leo, leo hii, namchukua binti yangu. Johari, vaa viatu, tunakwenda nyumbani.”

Johari alilia kama mtoto mdogo. Neema akamkumbatia kwa nguvu.
Mzee Hemed alimtazama mwenye nyumba na kusema:
“Kodi yenu ntakulipa, lakini kumbuka, kumtoa mtu ndani ya nyumba, lakini huwezi kumtoa kwenye historia yake. Wala kubadili hatma yake. Johari atarudi. Siku moja. Kwa kishindo.”

Na safari ya pili ya matumaini ikaanza, kwa machozi, kwa aibu, lakini pia kwa mshindo wa roho iliyokataa kufa.
------

Maisha kwa Johari yalianza tena lakini si kwa mtindo wa sinema. Hapana. Yalianza kwa upole wa maumivu. Polepole kwa majaribu. Kwa hatua za kutembea juu ya barafu bila viatu.

Mzee Hemed alimkaribisha kwa moyo mkunjufu. Alimwekea chumba chake cha zamani kilichokuwa bado kinabeba harufu ya vitabu vya kale na kumbukumbu za utoto na mama yake mlezi, Johari. Neema aliingia kwa mikono iliyojaa maswali, lakini alikumbatia kila kona ya nyumba hiyo kwa upendo. Ilikuwa ndogo, ya bati na mbao, lakini ilitoa hifadhi ya moyo wenye upendo.

Siku kadhaa baadaye, Johari alipika chai kwa uangalifu. Alimuita Mzee Hemed mezani. Wakiwa wanakunywa kwa ukimya, mzee huyo alimtazama, akamshika mkono.
“Binti yangu... unajua nini?” aliuliza kwa sauti ya kupumua.
“Nini baba?”
“Haki haifi. Inachelewa. Ila ikifika, haina huruma.”
Johari alitabasamu kwa uchungu.
“Lakini babu, si tulishapoteza hiyo haki?”
“Usidanganyike. Haki ni kama mbegu. Inakua kimya kimya, hadi ikuweke kivulini.”

Siku ya pili, waliketi sebuleni. Neema alikuwa anatengeneza michoro yake, akichora nyumba kubwa yenye bustani, Johari akashangaa kuona alama za moyo kila kona.
“Neema, hiyo nyumba ni ya nani?”
“Ya kwetu, mama. Tutakuja kuishi humu siku moja.”

Johari alicheka, kisha akamtazama mzee Hemed. Lakini kabla hajazungumza, mzee huyo alishika upande wa shavu lake kushoto, akainama, macho yakikodoa, midomo ikishindwa kusema.
“Babu!” Johari alipiga kelele. “Babu kuna nini?”
Mzee Hemed aliinama taratibu, akashindwa kuzungumza. Johari aliita bajaji akampeleka hospitali. Walikuja haraka. Kisha...
Baada ya vipimo, daktari alikuja kwa sura ya mashaka.
“Mzee amepatwa na kiharusi. Tumemweka ICU. Anaweza kuamka, lakini atakuwa na ulemavu upande mmoja wa mwili.”

Johari alikaa kwenye benchi ya hospitali usiku kucha. Alimshika Neema mikononi, akamwangalia huku machozi yakimdondoka.
“Hata wewe baba... hata wewe?” aliuliza kimoyomoyo.

Wiki ilipita. Mzee Hemed alitoka ICU, lakini hakuweza tena kusimama. Hakuweza tena kuzungumza kama zamani. Alikuwa kitandani, akimtazama Johari kama mtu anayetaka kusema kitu, lakini maneno yamehama kinywani.

Kila kitu kilibadilika. Johari akawa mlezi wa mzee. Akawa mama wa Neema. Akawa mama wa nyumbanj. Akawa kila kitu, lakini hakukuwa na mtu hata mmoja wa kumsaidia.

Pesa ilikata. Chakula kikaanza kuadimika. Mahitaji ya Neema shuleni yalikuwa mzigo usiobebeka. Johari akaanza kuamka alfajiri kuuza uji tena, safari hii kwa mapipa madogo ya plastiki. Mtaa ukamgeuka pia.

“Mama mmoja tu na mimba kubwa kama barabara ya lami. Leo kaja na mtoto anayeitwa Neema. Neema ya nani?”
“Si yule alishindwa kesi? Sasa anauza uji. Hahaha!”

Wanaume wa mtaa nao waliishia kumtupia maneno:
“binti mzuri hivi, lakini huna mtu? Au ulipoteza kitu huko nyuma?”
“Single mother wanapenda kutoa lawama. Si mlikuwa na wanaume, mkawadharau.”

Maneno hayo yalimgonga Johari kama mwamba unavyogonga samahani ya mfinyanzi. Alijikuta akilia, jioni wakati Neema amelala, alisema:
“Labda nilikosea. Labda mimba hii ilinifungia maisha mazuri. Labda Neema alikuja mapema mno. Labda... labda natakiwa kukubali tu maisha haya. Bila faraja. Bila mtu.”

Siku moja alipokuwa anapanga sabuni kwenye rafu ya duka dogo alipata kazi ya muda, mwanaume mmoja alifika. Alivaa suti, lakini sura yake ilikuwa laini. Mikono yake ilikuwa kama mtu aliyewahi kupitia kazi ngumu.
“Samahani dada... naitwa Gervas. Nimepotea njia. Naweza kuuliza barabara ya Msimbazi?”
Johari alimtazama, akamsaidia. Gervas alitabasamu.
“Naona! biashara ni yako?”
“Ndiyo,” alijibu. “Ya uji. Na hivi vidogo vidogo tu.” si hili duka"
“Wewe ni mwanamke mzuri. Si mtu wa aina hii ya maisha,” Gervas alisema kwa sauti ya chini.

Siku zilizofuata, Gervas alianza kuja mara kwa mara. Alileta chai, akaleta sabuni, wakati mwingine akaweka pesa kwa siri. Neema akamzoea. Johari akaanza kuona mwanga mweupe wa matumaini.
“Unajua,” Gervas alisema siku moja, “wewe ni aina ya mwanamke niliyetamani kumpa jina langu.”
Johari alicheka. “Gervas... mimi ni mzigo. Nina mtoto. Nina baba mlemavu. Nina historia ya kesi. Sina cha kujivunia.”

Lakini Gervas alimtazama machoni. “Hakuna mwanamke mwenye mzigo, kama mwanaume mwenye roho ya kweli yupo.”

Johari alianza kuamini kuwa huenda hii ndiyo faraja aliyokuwa anaisubiri.
Lakini siku moja alipokuwa jikoni, alimsikia Gervas akimwambia Neema:
“Baba yako yuko wapi? Unajua nilimwambia mama yako kuwa nitataka mtoto mmoja tu wa kwangu.”

Neema alinyamaza. Baadaye alimwambia mama yake usiku:
“Mama, Gervas hapendi watoto wasio wake. Mbona baba Dennis hakusema hivyo?”
Johari alichanganyikiwa. Kwa mara nyingine, alijiona anatumbukia shimoni. Je, apoteze nafasi ya mwanamume mwenye kazi, mwenye pesa, lakini asiyeweza kumpenda Neema kwa dhati?

Siku mbili baadaye, Gervas alikuja na pete. Akapiga goti. “Johari, nipe nafasi ya kukupenda maisha yako yote. Uwe wangu. Tufanye maisha pamoja.”

Johari akaishika pete. Akamtazama Gervas, kisha akamtazama Neema aliyekuwa mlangoni, macho yake yakiwa na swali moja:
“Na mimi je, mama?”

Kimya kilitanda. Moyo wa Johari ukawa kwenye vita kali kati ya upendo na uaminifu kwa damu ya tumbo lake na Ugumu na unafuu wa Maisha.

ITAENDELEA...

Unafikiri johari atafanya Nini?
Ungekuwa wewe ungefanya Nini?

Chungu cha 07 kipo njiani
 
NITAMLEA
Mtunzi: Robert Heriel
Chungu cha 07

Johari alikaa kimya mbele ya Gervas, uso wake ukikosa mwelekeo. Pete ya uchumba iling’aa kama mtego wa dhahabu mbele ya bundi anayesubiri kufa kwa njaa. Neema alikuwa amesimama mlangoni, macho yake hayakucheka wala kuuliza, yanasema yote bila maneno.

Gervas alinyanyuka taratibu, akashusha mkono wake wenye pete.
“Si lazima unijibu sasa, Johari. Chukua muda wako. Lakini nataka ujue… nataka maisha na wewe, siyo maigizo. Ila pia… najiandaa kuwa na familia yangu. Siyo kuishi na kivuli cha mwanaume mwingine.”

Kauli hiyo ilimchoma Johari kama sindano yenye sumu ya mamba. Kwa muda mrefu, alikuwa na kiu ya kupendwa lakini sasa hakujua kama hii ni faraja au ni njia nyingine ya kuumizwa polepole.

Usiku huo, akiwa kitandani huku Neema kalala kifuani mwake, Johari alijikuta akisema kimoyomoyo:
“Mapenzi ya dunia hii yamejaa masharti. Watu hawapendi mtu vile alivyo… wanapenda sehemu zao wanazozipenda tu.”

Asubuhi ilipofika, alimwandikia Gervas ujumbe mfupi:
“Ahsante kwa kila kitu. Lakini siwezi kuishi na mtu asiyeweza kumpenda binti yangu kama sehemu ya maisha yangu. Na Neema si kivuli cha mtu… ni mwanga wa maisha yangu.”

Alimtuma kwa whatsapp, akafuta namba mara moja. Jioni ile ile, Gervas hakupatikana tena. Hakujibu wala kuuliza. Alikuwa kama kivuli kilichopitia sakafuni na kupotelea chini ya meza.

Maisha yakazidi kuwa mabaya. Johari alianza kuuza maandazi ya shilingi mia kwenye ndoo ya plastiki. Neema naye alijifunza kuamka mapema, kumwaga majivu ya jiko, na kusafisha vyombo bila kulia. Alikuwa mtoto mwenye akili sana lakini macho yake yalikuwa yameanza kubeba uchungu wa maisha bila kusema.

Mtaani, kashfa ziliongezeka.
“Yule single mother hajui kudeka. Ndiyo maana wanaume wanamkimbia.”
“Eti binti yake anaitwa Neema, lakini hawana hata sabuni ya kufua!”
“Mama balaa yule. Ana roho kama simba lakini mifuko yake ni kama vichekesho.”
" Single mother ni wanawake hatari sana. Ona alivyo. Mzuri wa sura lakini roho yake sasa"

Johari alianza kukonda. Ngozi yake ikaanza kupoteza mng’ao. Mzee Hemed alikuwa amelala kwenye godoro lililozeeka, akihitaji msaada wa kila siku. Johari hakulala vizuri hata usiku mmoja kwa wiki nzima. Wakati mwingine angeamka usiku kumtazama Neema, akiwa amelala kwenye kitanda cha plastiki bila godoro, na machozi yalimtoka kimyakimya.

Alijaribu kuuza mitumba. Alienda hadi Manzese sokoni kuokota nguo zilizouzwa Kwa bei ya kutupa, na kuziuza Buguruni kwa akina mama wa mitaa. Lakini faida haikufika hata shilingi elfu tano kwa siku. Ilikuwa kama kusukuma gari bila mafuta.

Siku moja, akiwa amechoka kabisa, alienda kwa jirani kumuomba unga wa sembe. Jirani alimwangalia kutoka kichwani hadi miguuni, kisha akatoa mfuko wa sembe wa robo na kusema:
“Chukua… lakini usizoee. Sisi pia hatuna.”

Johari alirudi nyumbani na mfuko huo kama mwanafunzi aliyepewa mtihani wa kuchagua kati ya njaa na aibu. Alipika kwa upole. Alimlisha Neema. Akamvalisha nguo. Kisha alikaa mlangoni kwa muda mrefu, akiwa hana jibu la maisha.
“Kwanini Mungu ananiangalia tu?” aliuliza. “Kwa nini kila nikijaribu kuinuka, mguu mwingine unavutwa chini?”

Siku hiyo hiyo jioni, alikaa na Neema pembeni ya kitanda.
“Neema…”
“Ndiyo mama.”
“Unajua mama anakupenda sana, siyo?”
“Najua mama.”
“Ukikua… usije ukasema mama alikukosea.”
Neema alimgusa Mamake usoni, kwa mkono wake mdogo. “Mama, mimi na wewe ni timu. Hakuna anayeweza kutugawa.”

Maneno yale yalimchoma Johari kwa uchungu
“Wewe ni zawadi… lakini dunia haijui jinsi ya kuhifadhi zawadi kama wewe.”

Usiku huo huo, mvua ilianza kunyesha. Ukuta wa nyuma wa nyumba yao ulikuwa umeanza kupasuka. Maji yalianza kuingia kwa kasi. Johari alishika ndoo, akaanza kuyamwaga nje. Lakini yalizidi. Umeme ukakatika. Giza likatanda. Mzee Hemed alikohoa kwa nguvu. Neema anaye alikuwa analia.

Johari aliketi sakafuni, miguu ndani ya maji, macho yake yakitazama dari kwa chuki.
“Mungu… kama unaniona… basi niondoe kabisa. Au nionyeshe sababu ya kuendelea kuvuta pumzi. Maana nimechoka!”

Siku ya pili asubuhi, Johari aliamka akiwa amefunga begi lake moja. Alimvika Neema sweta la zamani, akambeba kwenye mgongo. Akamwambia Mzee Hemed:
“Baba… samahani. Siwezi tena. Naenda kutafuta namna nyingine ya kuishi. Nitamlea huyu mtoto hata nikifa. Acha nisafiri nisipopajua, maana hapa hapa ninapopajua pananiadhibu, mwanga umegeuka adui yangu.”

Akatoka nje. Mtaa ulikuwa kimya. Lakini miguu ya Johari ilikuwa ikipiga kelele na haraka ya mtu anayefukuzwa na maisha. Hakujua anaenda wapi. Hakujua atakula nini. Lakini alijua anaondoka — na hatarudi nyuma.
-------------

Barabara za Dar es Salaam zilitazama miguu ya Johari kwa mshangao. Miguu ile ilikuwa imezoea maumivu, lakini sasa ilikuwa inabeba uzito wa dunia nzima, uzito wa mtoto, uzito wa njaa, uzito wa majuto, na uzito wa ndoto zilizoshindikana.

Alitembea hadi Ubungo kwa mguu. Alijua pale pana watu wengi, na kwa watu wengi, huenda angekuta mkono mmoja wa msaada. Alikaa kwenye kivuli cha duka moja, akamweka Neema mapajani, akachomoa chupa ya maji ya dafu iliyojazwa uji. Alianza kuuza kama kawaida.

“Sista, njoo uonje uji bora,” alijaribu kutabasamu, lakini sura yake ilikuwa imeparara na jua, macho yake yalikuwa yamevimba kwa kukosa usingizi, na sauti yake ilikuwa nyembamba kama mtu aliyelazimika kuongea.

Watu walikuwa wakimkwepa. Siku hiyo aliuza chupa mbili tu. Neema alikuwa ameketi chini ya gazeti lililokunjwa, akichora kwenye vumbi kwa kidole chake.
“Mama, tunaenda nyumbani leo?” aliuliza.
“Nyumbani ni wapi Neema?” Johari alijibu kwa sauti ya chini. “Nyumbani ni penye mtu anayekupenda. Anayekujali. Sehemu tulivu yenyw amani. Huko hakuna kurudi Tena.”

Alimshika mkono, wakatembea mpaka Kimara mwisho. Alikuwa ameambiwa na mama mmoja kuwa kuna kazi za kufua kisha kulala hapohapo. Alifika kwenye nyumba ya mama Nuru, mjane mnene mwenye sura ya mashaka na macho ya kupepesa kila dakika.

“Unataka kazi?”
“Ndiyo mama.”
“Una mtoto?”
“Ndiyo, huyu hapa.”
Mama Nuru alimwangalia Neema kwa jicho la juu.
“Huyu mtoto hatakaa hapa. Hakuna nafasi. Kama unataka kazi, muache kwa mtu halafu urudi.”
Johari aliinamisha kichwa. “Samahani, siwezi.”

Mama Nuru alikenua meno. “Basi fanya hivi… kila siku njoo saa kumi na moja asubuhi, fanya kazi hadi jioni. Utaondoka na elfu mbili. Ukiweza, sawa. Ukishindwa, sikulazimishi.”

Johari alikubali. Akaanza maisha mapya ya kufua nguo kwa mikono hadi kucha zake zikaisha ukali. Kila jioni Neema alikaa nje ya nyumba hiyo kwenye kivuli cha mti, akicheza na mawe, akingoja mama yake arudi, akiwa na kanga moja ya kufunika mabega.

Usiku wa kwanza, walilala kwenye ofisi ya shule ya msingi iliyokuwa imefungwa. Mlango ulikuwa umeharibika. Johari alisukuma benchi pembeni, akamvalisha Neema nguo zote alizokuwa nazo, kisha akajifunika yeye na nguo ya ndani yenye matundu.

Mvua ilinyesha usiku huo. Sakafu ilikuwa ya saruji. Maji yaliingia kama mgeni asiyealikwa. Johari alimkumbatia Neema kwa nguvu, akimwambia:
“Lala tu mwanangu. Siku moja tutalala kwenye godoro la springi. Huko mbele… kuna kitu.”

Asubuhi yake, Johari alitokwa na damu puani. Alijua mwili wake umechoka. Lakini aliendelea. Akapika uji, akaenda kuuza kwenye daladala. Watu wengine walimlipa mia mbili. Wengine hawakulipa kabisa.

Siku moja alizidiwa. Akiwa amesimama kwenye kona ya Morocco, miguu ikamkataa. Alianguka. Neema alikuwa naye, akapiga kelele:
“Mama! Mama!”

Watu walikusanyika. Mama mmoja alichomoa leso, akamfuta jasho.
“Dada una presha?”
“Sijui… sijala.”

Alichukuliwa hadi duka la dawa. Daktari wa mitaani alimpima, akasema:
“Damu yako iko chini. Pia una upungufu mkubwa wa damu. Hutakiwi kufanya kazi ngumu. Unahitaji chakula bora.”

Johari alicheka kwa uchungu.
“Chakula bora… hata sembe sijui inanunuliwa wapi kwa bei nzuri.”

Usiku huo, walilala nje ya kanisa dogo la KKKT. Askari wa doria aliwafukuza saa tisa usiku. Wakakimbilia uani mwa shule ya sekondari, wakajificha nyuma ya jiko la walimu.

Neema alianza kukohoa.
“Mama, baridi…”
Johari alijivua blauzi yake, akamfunika Neema. Akabaki na kitenge kifupi, mwili wake ukitetemeka. Lakini moyoni alikuwa anajiambia:
“Nitamlea. Atakua! Ataishi. Hata kama nitakufa mimi.”

Kesho yake, akiwa bado mgonjwa, alijitokeza kazini kwa mama Nuru. Alifua nguo hadi mikono ikachubuka. Jioni, akapewa elfu mbili. Alimnunulia Neema maandazi mawili na juisi ya kopo.

“Neema…”
“Ndiyo mama.”
“Leo nakuletea soda. Unastahili furaha.”

Neema alimkumbatia kwa nguvu. “Mama, wewe ni hodari kuliko watu wote.”
Johari alibaki kimya. Aliona machozi yakimjia. Aliyazuia kwa nguvu. Lakini moyoni, kulikuwa na kilio kisichosikika.

Aliendelea hivyo kwa wiki mbili. Mwili wake ukazidi kudhoofika. Siku moja akakuta Neema ana homa. Hakukuwa na pesa ya hospitali. Akampeleka kwa mtaalamu wa mitishamba. Akaandikiwa majani.

“Loweka haya majani, mpe mtoto anywe. Atapona.”

Johari alifanya hivyo. Neema akapona kidogo. Siku chache baadaye, homa ikarudi. Alijikuta akililia kimya kimya.
“Mungu, nichukue mimi… lakini Neema aendelee kuishi. Ataishije, wewe unajua"

Siku hiyo hiyo, akiwa kwenye kona ya barabara, aliona tangazo la kazi ukutani.
“Kazi ya ndani. Inahitaji msichana mwenye nidhamu. Malipo: elfu kumi kwa siku.”

Alipiga namba.
Sauti ikajibu:
“Tafadhali njoo ghorofa ya tatu, nyumba namba 12, Kinondoni B.”
Alifika pale jioni. Akaambiwa kazi ni kupika, kufua, na kupangilia nyumba.

“Tutakupa chumba chako. Ila mtoto hataishi hapa.”
Johari alibaki kimya. Akaondoka bila kusema neno.

Usiku huo walilala katika kitalu cha matofali. Chini ya mti mkubwa. Mbwa walikuwa wanabweka. Neema alilala usingizi wa haraka. Johari alitazama mbinguni. Hakukuwa na mwezi. Hakukuwa na nyota. Kulikuwa giza tupu.

“Mungu… niambie. Niendelee au nijitupe barabarani. Ni nani wa kuniona?”

Hakukuwa na jibu. Ila kesho yake, aliamka tena. Akiwa na nguvu za mwili zilizotengenezwa na mapenzi kwa mtoto wake, si chakula. Si usingizi. Si pumziko.

ITAENDELEA...

Unamaoni Gani?
Unatamani nini kitokee?

Twende chungu Cha 08
 
NITAMLEA
Mtunzi: Robert Heriel
Chungu cha 08
---

Ilikuwa ni ijumaa ya jua kali, jua la Dar es Salaam lilikuwa linapiga bila huruma kama mkono wa deni lisilolipwa. Johari alikuwa ameketi kando ya stendi ya Magomeni Mapipa, akiwa amemshikilia Neema mapajani. Uji mwingi ulibaki, haukununuliwa, tumbo halikuwa na kitu, moyo haukuwa na matumaini.

Pale pembeni, kulikuwa na wahubiri wawili wakihubiri kwa sauti kali, mmoja akiwa na biblia iliyochoka na mwingine kipaza sauti cha redio ya mchina.

“Watu wa Mungu! Msikate tamaa! Tumaini bado lipo! Mungu anakujua, anakusikia, na hajakuacha! Mungu si mwanadamu aseme uongo! Hata ukiwa kwenye tope la mwisho, mkono wake unaweza kukutoa!”

Johari alimtazama yule mhubiri kwa jicho la kushangaa. Maneno yake yaliingia rohoni kama maji kwenye ardhi kavu. Alihisi kama ile sauti ilikuwa inamwambia moja kwa moja, “Wewe Johari… naam, wewe. Hujafika mwisho.”

Aliachia tabasamu la ndani, akachomoa shilingi mia mbili pekee aliyokuwa nayo ndani ya pochi. Akasogea kwenye kisanduku cha sadaka kilichotengenezwa kwa mbao na kuandikwa kwa peni: “Tumaini lipo.”

“Mama, tunatoa hii hela kweli? Hatujanunua hata maandazi” Neema alimnong’oneza kwa sauti ya kusita.
Johari akamsogelea bintiye na kusema kwa sauti ya taratibu, machozi yakianza kumlengalenga:
“Mwanangu, Mungu hajatuacha. Hii mia mbili inaenda kununua tumaini… si mkate Wala maandazi. Mkate utakuja.”

Neema alimwangalia mama yake, akasita, kisha akacheka kimoyomoyo.
“Basi mimi namwamini Mungu kama wewe.”

Baada ya sadaka, waliendelea kutembea hadi maeneo ya Mwembechai. Kule walikuta msikiti mdogo. Johari alikuwa na msukumo wa rohoni. Akamwambia Neema,
“Leo ni ijumaa. Tutaenda kuswali.”

Lakini walikuwa wachafu, mavazi yao yamechakaa, na hakuna sehemu ya kuoga. Akachota maji ya barabarani, maji ya mvua yaliyobaki kwenye mashimo ya lami iliyoharibika. Akachukua chupa yake ya uji, akaisafisha, akaweka maji, akamwogesha Neema nyuma ya kibanda kilichokuwa kimefungwa.

“Baridi mama,” Neema alilalamika.
“Subiri kidogo, tuwe wasafi kwa Mungu.”
Baada ya hapo, Johari naye akaoga haraka haraka, akavua blauzi yake na kuigeuza, akafunga khanga kama hijabu. Walipoingia msikitini, baadhi ya wanawake walimkodolea macho, wengine wakimbeza wengine wakiteta kimyakimya.

Lakini Johari alitulia kwenye safu ya nyuma kabisa. Alimsujudia Mungu kwa mara ya kwanza akiwa na huzuni ya kutosha kujaza bahari.

“Ewe Mungu, sikutafuti kwa sababu nina raha. Nakutafuta kwa sababu sina pa kutegemea. Kama uko, tafadhali nitazame leo.”

Baada ya swala, hakukaa hata dakika. Alitoka nje, akamshika mkono Neema, wakaenda hadi kwenye uwanja wa wazi kusubiri muujiza wa maisha.

Saa mbili jioni, akiwa ameketi kwenye kingo za barabara ya Kawawa, kijana mmoja mrefu mwenye uniform ya kampuni ya ulinzi alimkaribia. Alikuwa na kipaza sauti kikubwa.

“Dada! Samahani. Samahani sana. Naona unakaa hapa kila siku. Unatafuta kazi?”

Johari alinyanyuka kwa tahadhari. “Ndiyo. Kazi yoyote ya halali, niko tayari.”
Yule kijana akamwangalia chini juu. “Tuna nafasi ya ulinzi kwa wanawake. Kituo kiko Tegeta. Ni kazi ya kulinda banda la bidhaa za ujenzi. Malipo ni elfu saba kwa siku. Unaweza?”
“Naweza!” Johari alijibu haraka. “Nitafanya usiku au mchana?”
“Kuna zamu mbili. Usiku au mchana. Wewe unataka ipi?”
“Niwe usiku. Mchana nitauza uji wangu.”
“Keshokutwa uje ofisi ya kampuni yetu pale Mwenge. Uje na nakala ya kitambulisho. Ukikubaliwa, kazi inaanza siku hiyohiyo.”

Johari alirudi kulala na Neema kwenye uchochoro ule ule wa shule ya zamani, lakini roho yake ilikuwa na mwanga mpya.

Siku ya kuanza kazi ilipofika, alienda Mwenge mapema. Akapewa sare, suruali ya kaki, fulana yenye nembo ya kampuni, na buti nzito za ulinzi. Neema alibaki kwa mama mmoja jirani aliyekubali kumuangalia kwa elfu mbili kwa siku.

Zamu ya kwanza ya Johari ilikuwa usiku. Banda la mbao lilikuwa limejaa saruji, mbao, nondo, na kokoto. Hakukuwa na taa, hakukuwa na choo, hakukuwa na jiko. Kazi ilikuwa kulinda na kukaa macho.
Usiku wake wa kwanza, mbu walimla kama mkate wa asubuhi. Buti zilimvimbisha vidole. Lakini alikumbuka maneno ya yule mhubiri:
“Tumaini bado lipo!”

Alipokuwa akizunguka banda hilo, alisikia kelele kutoka vichakani. Alichukua tochi yake na fimbo aliyopewa, akasogea polepole. Lilikuwa paka tu. Lakini hofu haikuondoka.

Mara nyingine, vijana wa mtaani walipita wakamtolea macho. Wengine walimwambia:
“Dada, kazi gani hii? Wewe mzuri hivyo, huna haja ya kulinda nondo.”

Alijifanya hasikii. Lakini usiku wa pili, alikumbana na vijana waliokuwa wamelewa. Walimfuata kwa sauti ya kejeli.
“Mrembo… uko peke yako?”
“sisi tukupe pesa, tujivinjari usiku wa leo?”

Johari alibana fimbo yake kwa nguvu. Akasema kwa sauti ya ujasiri:
“Niacheni. Siko hapa kutafuta wanaume. Niko hapa kutafuta riziki ya mtoto wangu.”

Wale vijana walicheka, wakamtupia chupa za pombe na kuondoka. Lakini Johari alijua, kazi ya ulinzi haikuwa lelemama. Ilihitaji moyo wa simba aliyejeruhiwa.
Asubuhi alirudi kwa Neema, akimkuta kalala mlangoni kwa yule mama aliyemuahidi kumwangalia. Mama huyo alimwambia:
“Mtoto wako analia sana usiku. Halali. Wakati mwingine anasema, ‘nataka mama yangu.’”

Johari alimkumbatia Neema. “Pole mwanangu… mama bado yupo. Hajaondoka.”

Hiyo ndiyo ikawa ratiba yao mpya. Mchana Johari anauza uji, usiku analinda banda. Mapato si mengi, lakini sasa walikula kila siku, hata kama ni ugali na chumvi.

Siku moja akiwa lindoni, Johari alisali kimya kimya:
“Baba wa mbinguni… sitaki mamilioni. Nataka tu mahali pa kulala, chakula cha kila siku, na afya ya binti yangu. Kama hayo unaweza kunipa… nitakushukuru hadi mwisho.”
_________

Johari alianza kuona dalili za mwanga wa matumaini. Mwezi mmoja na nusu tangu aingie kwenye kazi ya ulinzi, maisha yake yalianza kujikusanya kama vipande vya kioo kilichokuwa kimevunjika na sasa vinarudi kuunda sura mpya ya matumaini. Si kwamba kila kitu kilikuwa kimekaa sawa, lakini angalau sasa alikuwa na pa kushika.

Kila alfajiri alirudi kwa Neema, akambembeleza, akamlisha, kisha akalala masaa matatu au manne kabla ya kuamka na kuandaa uji wa kuuza. Alikuwa ameweka ndoo yake ya uji stendi ya magari eneo la Sinza Kijiweni, karibu kabisa na stand ya bodaboda. Akiwa amevalia kitenge, na tabasamu la mtu anayekaribisha wateja kwa moyo mkunjufu, alianza kuvutia watu.

“Dada uji wako unakaa kama umeweka limbwata. Kama dawa ya homa ya mapenzi!” mmoja wa wateja wake, dereva wa bodaboda alicheka huku akipiga funda la uji.
“Acha masihara. Nipe mia tano, japo hiyo kashfa yako nimeisamehe,” Johari alimjibu kwa kicheko kilichobeba faraja.

Hicho kicheko hakikuwa cha kawaida. Kilikuwa cha mtu anayefufuka kutoka kwenye huzuni ya siku nyingi. Kilikuwa na sauti ya mtu aliyekubali kwamba maisha hayatabiriki, lakini bado yanaweza kuwa na utamu kidogo japo kwa muda usiodumu.

Neema naye alianza kubadilika. Mwili wake ulicheka na tabasamu likaota tena kwenye midomo yake midogo. Alipoanza kuchezea mchanga mbele ya nyumba ya mama mlinzi aliyekuwa akimlea mchana, alitengeneza sura ya mama yake na kusema:
“Huyu ndiye mama. Anauza uji na analinda nondo.”

Wakati mwingine Johari alipoona binti yake akifanya hivyo, macho yake yalijaa machozi kimyakimya. Lakini kwa mara ya kwanza, machozi yale hayakuwa ya maumivu, yalikuwa ya shukrani.

Usiku kazini kwake, alipokaa ndani ya kibanda cha mbao, alianza kuandika kwenye daftari lake la zamani alilokuwa amelihifadhi tangu chuo. Aliandika maneno ya shukrani:
“Ee Mungu… sijui kama niko sahihi kukuamini, lakini sijui pa kuamini pengine. Sina pesa nyingi. Sina nyumba. Sina hakika ya kesho. Lakini nina sababu ya kuamka kila siku. Hiyo imenitosha.”

Kwenye siku ya jumatatu ya pili ya mwezi wa pili, boss wake alimwita kwenye ofisi ndogo pale Mwenge.

“Johari, nimeona rekodi zako. Hujawahi kuchelewa, hujalala kazini, na umekuwa ukiripoti kila tukio. Tuna mpango wa kukuongeza mshahara kidogo. Kutoka elfu saba Hadi elfu kumi kwa siku.”

Johari alishika kichwa kwa mikono yote miwili, machozi yakimtiririka. “Asante sana. Sijawahi pata barua nzuri kama hii.”
Lakini kama ilivyo kawaida ya dunia, furaha ya maskini huwa haidumu. Kuna wakati mtu anapoanza kuona barabara ikiwa safi mbele yake, ndipo huja mlima mkali. Na kwa Johari, mteremko wake ulianza usiku mmoja wa zamu alipokuwa kazini.

Alikuwa ametulia ndani ya kibanda, amevalia koti la ulinzi, akisoma kurasa za kale za kitabu cha “Maisha si Vita, Ni Kunyamaza.” Ghafla, alisikia makelele ya magari na mihemko isiyo ya kawaida nje ya banda.

Alipotoka nje, alikuta kundi la vijana waliovaa kiraia wakikata nondo na kujaribu kufungua magunia ya saruji. Johari alikimbilia kwao, akapiga kelele:
“Heee! Mnatafuta nini hapa?! Hii ni mali ya watu!”

Vijana wale hawakujali. Mmoja alimgeukia kwa hasira:
“Una roho ya paka wewe! We ni nani uje kutuambia cha kufanya?”
"Unataka kufa? Eeh! Unataka kufa?"
Johari alijikaza, akipiga kelele huku akipuliza filimbi ya onyo. Lakini vijana wale hawakuogopa. Badala yake, mmoja alimsukuma chini, na mwingine akamrushia tochi aliyoishikilia.

Kwa bahati, kulikuwa na dereva wa bajaji aliyekuwa akipita jirani. Aliposikia makelele, alikuja kumsaidia Johari na kuwafukuza wale vibaka.

Siku iliyofuata, boss alimwita tena. Safari hii, uso wake ulikuwa umejaa majonzi.

“Johari… umekuwa mlinzi mzuri. Lakini wateja wetu wamelalamika kwamba hauko salama. Wanasema kuna wezi walijaribu kuiba usiku wa jana. Tunalazimika kukuondoa kwenye kazi kwa muda… hadi tuchunguze.”

Johari alihisi dunia inazunguka. “Una maana naondolewa kazini?”
“Sio rasmi… ila kaa nyumbani kwa wiki mbili kwanza. Tutakujulisha baadaye.”

Alipotoka pale ofisini, alijua haina haja ya kungoja barua. Hii ilikuwa ni barua ya kutimuliwa. Na mshahara wa mwisho ulikuwa bado hawajamlipa, na Bado anadaiwa na mama aliyemlea Neema.

Wakati anarudi nyumbani, Neema alimkimbilia na kumwambia kwa furaha:
“Mama leo sijalia mchana! Mama mkubwa alinipa uji tuu!"
Johari alitabasamu kwa tabu. Hakuwa na uji wa kuuza kesho. Hakujua kesho inaanza vipi.

Siku mbili baadaye, alienda tena kwenye sehemu yake kuuza uji. Hakupata wateja wengi. Uji uliharibika. Walirudi na chupa nyumbani ikiwa bado imejaa nusu.
Ndani ya wiki moja, mambo yalirudi kama zamani. Kodi ya nyumba haijalipwa. Umeme umezimwa. Mama anayemwangalia Neema mchana akasema wazi:
“Dada, kama huwezi kunilipa japo elfu mbili kwa siku, siwezi tena kumwangalia mtoto wako. Samahani sana.”

Johari alilia usiku huo, akimkumbatia Neema. Ndoto ya kuwa salama iliisha kwa haraka kama moshi wa sigara kwenye upepo wa bahari.

Siku ya tatu asubuhi, akakuta karatasi ya onyo langoni:
“UNADAiwa kodi Miezi Miwili. Tafadhali lipa ndani ya siku TATU au uondoke.”

Na kama filamu mbaya inavyoanza, jioni hiyo, Johari akiwa amekaa nje, aliona mtu akimfikia kwa haraka. Alikuwa ni Dennis. Hakuwa na mzigo wowote, hakuwa na tabasamu. Alikuwa amechoka vibaya.

“Johari,” alijikuna kichwa. “Nimepata kazi Mwanza. Sina uhakika wa lini nitarudi. Nimekuja kukuaga.”

Johari alimtazama kwa muda mrefu. Hakuwa na nguvu ya kuhoji, kulalamika, wala kumlaumu. Alimjibu kwa sauti iliyokufa ndani:
“Safari njema. Siye Tupo.”

Neema alimuuliza, “Mama, baba anatuacha tena?”
Johari alimshika mkono bintiye. “Hatutegemei watu tena. Tumebaki sisi wawili.”

Usiku huo, Johari alilala akiwa amemkumbatia Neema. Moyo wake ulikuwa umevunjika kwa vipande vipya tena. Nuru aliyokuwa ameanza kuona… ilizimika kama mshumaa uliopigwa na upepo.

ITAENDELEA...

Chungu Cha 09 kinakuja
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom