Simulizi: Namchukia Mama Yangu

Simulizi: Namchukia Mama Yangu

Sehemu ya 28

Japokuwa mabadiliko yale yalikuwa mazuri, lakini hali ya mama ya kokosa raha kushinda chumbani peke yake hata sisi wanae tulikosa raha.

Wasiwasi wangu ulikuwa labda mama anateseka na aliyotufanyia. Niliingiwa wasiwasi wa kumpoteza mama kufa kwa kihoro.

Mama aligeuka kama mgonjwa na kupungua kila siku mpaka kupelekea kuugua vidonda vya tumbo. Hali ile ilifanya tukutane kutaka kujua kipi kimemsibu mama yetu japokuwa niliamini aliyoyafanya ni sehemu ya maumivu ya majuto.

Kila tulipomuuliza mama ana tatizo gani aliishia kulia, nilikuwa na wasiwasi wa kuwaeleza dada zangu tatizo la mama linaweza kusababishwa na nini.

Niliamini mtu wa kutusaidia kipindi kile ni mama Amina. Niliamua kwenda kwa mama Amina kuomba ushauri kuhusu tatizo la mama.

Alinieleza tatizo la mama yetu linatokana na kuumizwa na vitendo alivyotufanyia wanaye.
“Mama yenu anashindwe kuwaeleza ukweli tatizo hilo kwa kuhofia mnaweza kumtenga na kufa kwa kihoro . Nilimuhakikishia hakuna tatizo litakalotokea bila kumueleza wewe unajua kila kitu.”

“Sasa tufanyeje, mama hali ni mbaya. Mimi nimemsamehe leo na kesho kiama, nina imani hata dada zangu pia watamsamehe.”

“Mwaija najua sasa hivi moyo wako umetulia mfuate mama yako na kumueleze unayoyajua kuhusu yeye na kuonesha amemsamehe ili kuondoa donge moyoni mwake.”

“Mmh! Nitaweza, nina wasiwasi mama yangu kulia mbele yangu. Nampenda sana mama yangu naumia na hali yake pia nitaumia zaidi akilia,” nilishindwa kuzuia hisia zangu.

“Sasa tutafanya nini?”
“Mama Amina kaa na mama na kumweleza yote kisha tukutanishe wote nina imani una nafasi ya kurejesha furaha ndani ya familia yetu. Sio siri sisi wote kwa sasa hatuna raha.”
“Nitafanya hivyo, wewe nenda kesho nitakuja.”

“Mama Amina wewe ndiye tegemeo langu la mwisho kwa mama yetu.”
“Shaka ondoa mdogo wangu, mama yetu atarudi katika hali ya kawaida maadamu mmeamua kulimaliza.”

Niliachana na mama Amina na kurudi nyumbani. Sikuwa na furaha mpaka nipate simu ya mama Amina kuhusu mama amepokeaje alichomueleza.

Siku iliyofuata nilikuwepo nyumbani lakini mawazo yangu yalikuwa mbali sana. Nilisubiri simu ya mama Amina kwa shauku kubwa. Nikiwa namalizia kumuosha mtoto simu iliita, mapigo ya moyo yalinibadilika ghafla, nilimuacha mtoto kwenye beseni na kuikimbilia simu sikutaka kumtuma msichana wa kazi aifuate niliona angechelewa.

Lakini haikuwa ya mama Amina, nilijikuta nikichukia. Baada ya kuzungumza nilirudi kummalizia kumuosha mtoto. Kabla sijaanza kumuosha iliita tena. Nilimtuma msichana wa kazi.

“Niletee,” hamu yote iliniisha.
Alipokuwa ameishika nilimuuliza nani, akaniambia mama Amina. Nilimwacha mtoto na kuwahi kama itakatika na salio sikuwa nalo.

“Haloo,” nilipokea huku mapigo ya moyo yakiwa juu.
“Vipi mbona unahema?”
“Mwenzangu, hata sijielewi mama kanichanganya sana, vipi umeisha fika nyumbani?”

“Ndipo ninapoongelea.”
“Umeisha zungumza na mama?”
“Ndiyo.”
“Amesemaje?”
“We upo wapi?”
‘Nyumbani.”

“Njoo basi mara moja.”
Nilishindwa kuendelea kumuosha mtoto nilimfuta na mimi kubadili nguo bila kuoga na kuondoka. Nilipofika barabarani nilikodi teksi kwenda Tandika kwa mama.

Bahati nzuri kipindi kile hakukuwa na foleni kubwa barabarani kama sasa. Gari lilikwenda mpaka njia panda ya Mandera na Tazara Vetenari ilikata kulia.

Nilifuata barabara ya Vetenari kabla sijafika maghorofa ya Tazara nilishangaa dereva kusimamisha gari pembeni karibu na kituo kidogo cha polisi.

“Vipi mbona unasimama?”nilimuuliza dereva.
Kuna gari nyuma limeonesha ishara ya taa tusimame sijui ana shida gani.
“Sawa,” nilitulia sikushughulika naye nilijua ni watu wake.

Baada ya muda nililiona gari la mzee Sambi likisimama mbele yetu. Nilishtuka mpaka mapigo ya moyo yalinienda mbio. Baada ya gari kusimama alishuka mzee Sambi na kuja kwenye gari letu.

Alipofika alitoa miwani yake na kusema kwa kushtuka:
“Ni wewe Mwaija?” alishtuka.
“Ndiye mimi, ulijua nitakufa?”
“Sivyo Mwaija ni historia ndefu.”
“Ya kunitaka kuniua na kunidhulumu mali yangu?”

“Mwaija naomba tukae pembeni tuzungumze.”
“Katu sitazungumza na wewe muuaji,” nilimjibu kwa hasira.

“Usiniite hivyo Mwaija nipe nafasi unisikilize.”
“Ili?”
“Utajua sababu ya mimi kuondoka ghafla.”
“Nikijua itanisaidia nini, nilikufuata kukuuliza?”

“Ha! Mwaija umeolewa?” mzee Sambi alishtuka baada ya kuona pete ya ndoa kutokana na kurusha mikono wakati wa kusema.

“Ulifikiri siolewi?” nilimjibu kwa nyodo.
“Na huyo mtoto wako?” alizidi kushtuka kila dakika.
“Ndiyo, uliambiwa mi mgumba?” nilimjibu kwa nyodo.

“Mwaija angekuwa wangu huyo, mama yako anahusika kwa kiasi kikubwa kuvuruga uhusiano wetu.”

“Aliyetaka kuniua ni mama au mkeo?”
Muda wote dereva wa teksi alikuwa akitushangaa jinsi tulivyokuwa tukirumbana.
“Huwezi kunielewa naomba basi uje kwenye gari langu tuzungumze.”

“Mlinikosa kuniua hamtanipata tena, ilimtuma mkeo aniue ili mchukue nyumba. Sawa, mmechukua vyote hivyo, lakini sijawafuata kukuulizia kitu chochote.”

“Mwaija nyumba bado yako.”
“Usinichefue, kukusikiliza usinifanye mjinga, uliniambia nini kuhusu mkeo na matokeo yake kimetokea nini. Kwa taarifa yako najua kila kitu katika ile nyumba.”

Nilimweleza yote siku nilipokwenda na kumkuta na mkewe wakiwaonesha wapangaji nyumba. Nilimuona akishangaa kama kaona meli barabarani.

“Basi naomba tuzungumze Mwaija ili unielewe nipo radhi kukupa chochote ili tuondoe tofauti zetu.”

“Naomba hayo tuachane nayo, endelea na maisha yako na mkeo mchawi. Achana na watoto wa watu kuwaumiza kwa kuwaroga na mkeo.”
“Mwaija maneno gani hayo?”
“Tuachane na hayo naomba uendelee na safari yako.”

“Sasa?”
“Kuhusu nini?”
“Nipe hata dakika tano.”
“Nimeitwa nyumbani mama anaumwa naomba uniache niwahi.”
“Naomba namba yako ya simu.”
“Siwezi kukupa, mume wangu ana wivu sana.”
“Sasa ita..”

“Dereva hebu tuwahi safari yetu.”
Dereva aliondoa gari na kumuacha mzee Sambi amesimama barabarani. Dereva hakuniuliza mpaka tulipofika kwenye kona ya Maguruwe.

“Dada vipi?”
“Achana naye,” nilimjibu kwa mkato.
Nilijikuta nikiwa mtu mwenye hasira baada ya kuachana na mzee Sambi mpaka machozi yalinitoka huku kifua kikinijaa. Nilifika nyumbani na kumlipa dereva kisha niliingia ndani.

Nilipokelewa na mama na ndugu zangu pamoja na mama Amina.
“Karibu mama yangu,” mama Amina alinitania kutokana na kumwita mwanangu jina lake
Nililompa mwanangu kama shukurani kwake kwa kuwa sehemu ya kupatikana kwa mwanangu.

“Asante, shikamoo.”
“Marahaba mama yangu.”
“Shikamoo mama,” nilimgeukia mama.
“Marahaba, za nyumbani?”
Mama yangu aliitikia kinyonge, hali ile ilizidi kuumiza moyo wangu.

“Nzuri mama, shikamoo kina dada.”
“Marahaba mama Husna,” waliitika wote.
Nilikwenda kukaa pembeni ya mama na kumpa mjukuu wake, alipokea na kugundua mama alikuwa akitokwa na machozi.
Baada ya kuketi mama Amina alifungua kikao kile cha kifamilia.
 
Oyah wewe usirudie kuqoute hadithi nzima
Ndugu mwandishi riwaya yako ipo vizuri Sana Ila sidhani km ni busara kuweka bandiko hapa mpk usujudiwe au ulambwe miguu...

Unaweka kiepisode kimoja mpk pale ujisikie ndo uweke nyingine....km ulidhamiria kushare na Sisi basi usitupe manyanyaso hvyo...weka mzigo wa kutosha angalau tukate kiu...

Sent using Jamii Forums mobile app

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Sehemu ya 29

Nilikwenda kukaa pembeni ya mama na kumpa mjukuu wake, alipokea na kugundua mama alikuwa akitokwa na machozi.
Baada ya kuketi mama Amina alifungua kikao kile cha kifamilia.

“Jamani nina imani mtashangaa uwepo hapa kwenu muda huu,” alianza kuzungumza mama Amina.

“Walaa,” tulijikuta tukijibu kwa pamoja.
“Basi leo sikuja kama mlivyonizoea, kuna jambo zito limenileta ambalo nina imani hamlijui lakini mama yenu anataka mlijue kabla mauti hayajachukua uhai wake.
“Nina imani hivi karibuni mmeona mabadiliko ya hali ya mama yenu?”

“Ni kweli,” tulijibu kwa pamoja.
“Nina imani hali hii imewashtua sana na kukosa jibu, ni kweli?”
“Kweli,” dada alijibu.

“Nina imani mi si msemaji ila mzungumzaji mkubwa ni mama yenu ataeleza kinachomtesa moyoni mwake.”
“Hakuna tatizo,” dada mkubwa alijibu.
“Kabla sijamkaribisha mama yenu naomba kuwauliza.”

“Uliza tu,” tulimkubalia.
“Je, mnampenda mama yenu?”
“Zaidi ya sana.”
“Kama amewakosea mpo tayari kumsamehe?”

“Leo mpaka kesho kiama,” tulijibu wote kwa vile tulikuwa tukimpenda mama yetu.
“Haya mama Zamda hebu toa dukuduku lako wanao wamesema wamekusamehe leo na kesho kiama.”

Wote tulihamisha macho yetu kwa mama aliyekuwa ameshikilia mkono shavuni. Mama alitoa mkono shavuni na kufuta machozi kwa mtandio kisha alikohoa kidogo na kupenga makasi na kujifuta kwa kitambaa kidogo cha mkononi kisha alisema kwa sauti ya kujilazimisha.

“Nikuwa na mtihani mzito baada ya kugundua nilichokifanya si sahihi hasa kwa mzazi kama mimi. Lakini nimekuwa na wakati mgumu kuyasema haya kwenu.

“Kwangu ni sawa na kutembea bila ya nguo mbele ya kadamnasi, lakini sina jinsi lazima niseme. Namuomba Mungu anipe nguvu ya kuweza kuyasema haya.

“Nina imani huenda wanangu mnasema mtanisamehe mama yenu kwa vile hamjui kipi kibaya nimewafanyia ambacho kinaweza kuwafanya wanangu mkanichukia na kutaka hata tusizikane kitu ambacho nina imani kitaniweka katika wakati mgumu sana hata kusababisha nife kwa kihoro.”

“Mama kwa lolote baya hata kama ulitaja kutuua, mimi nakutoa wasiwasi kwa upande wangu nichosema sitabadili kauli yangu. Kama nitafanya hivyo basi Mungu anifufue nguruwe siku ya kiama.”

Nilijikuta nikisema kwa uchungu mpaka machozi yakanitoka huku moyo ukiniuma. Niliamini mama yetu alikuwa na mzigo mkubwa moyoni mwake kuyaanika mabaya yake kwa mdomo wake.

Niliamini kuyasema yale ilikuwa njia ya kumpa nafuu mama kwa kile alichotaka kukitoa mbele yetu. Dada zangu nao waliungana nami kumuhakikishia mama hakuna atakaye badili kauli ya kumsamehe.
Baada ya kauli yangu mama alishusha pumzi ndefu na kusema:

“Kwanza napenda kumshukuru Mungu kunipa watoto wenye mapenzi makubwa kwangu japokuwa mama yenu nilikosa mapenzi ya dhati kwenu japo niliamini nawapenda sana lakini mapenzi yangu kwenu yaligeuka sumu.”
“Pia namshukuru mama Amina Mungu amzidishie, kwa umri namzidi sana lakini amekuwa mwanamke shupavu mwenye moyo wa kipekee kuipigania familia yangu Mungu atakulipa.”

“Amina,” aliitikia mama Amina.
Mama alianza kumwaga siri zake kwa kujilazimisha kama mtu aliyekuwa akinyweshwa shubiri. Kuanzia siri mzito ambayo hatukuijua ya kifo cha baba kuwa yeye ndiye alichangia.

“Wanangu kifo cha baba yenu naweza kusema mimi ndiye chanzo. Kilitokana na mateso mazito yaliyofanya mimi mama yenu niingie kwenye mchezo mbaya.

“Baba yenu aliondoka nyumbani nikiwa na ujauzito wa miezi miwili wa Mwaija na kuhamia kwa mwanamke wa nje.

“Mwanzo sikushtuka kwa vile mahitaji yote ya muhimu nilikuwa nayo nilijua atarudi. Lakini adha ya mateso ilipoanza baada ya kuishiwa kila kitu ndani. Kwa kweli nilitesema kufikia hatua ya kushinda na njaa mimi na ninyi wanangu, kibaya nilikuwa mjamzito.

“Yeye baba yenu alikuwa ameshikwa na mwanamke wa nje ambaye alimfanyia madawa na kumfanya aisahau familia yake.
“Kila kukicha hali ilizidi kuwa mbaya nikawa napita kwa majirani kuwaombea chakula. Kuomba kila siku nilishindwa na kuamua siku nyingine kuwakorogea uji bila sukari.

“Nilianza kuuona mzigo ma maisha hali yangu ya ujauzito niliyokuwa nayo njaa mawazo. Nilikuwa nakonda kila siku na kushinda nalia kutokana na mateso mliyokuwa mkipata wanangu.

“Kuna siku mlishindwa kunyanyuka kitandani kutokana njaa, Nilijikutana naingia nyumba ya jirani na kuiba unga. Nilishindwa na kuwa aibu mtaani.

“Nilijikuta nikipata mawazo mengi kufikia kuwaza kunywa sumu, lakini moyo ulinisuta kufanya hivyo kwa vile ningetoa uhai wa kiumbe kisicho na hatia pia kuwaacha wanangu kwenye mateso mazito.

“Siku moja nilipata wazo baada ya kumuona mwanamke mmoja akiuza mboga za majani huku akiwa na tumbo kubwa. Sikusita kumuuliza na kunieleza ana watoto wanne mumewe kamkimbia na kuamua kufanya biashara ile ambayo ilimsaidia kupunguza ukali wa maisha.

“Wazo lile nililiafikia na kumuomba msaada wa mimi kupata zile mboga. Alininielekeza jinsi ya kupata hizo mboga nami nikaingia kwenye biashara ya kuuza mbogamboga.

“Mwanzo niliona aibu, lakini aibu ilinitoka baada ya kumaliza mapema na kununua mahitaji muhimu ya siku ile japo hayakulingana na aliyokuwa akinipa baba yenu.

“Siku za kujifungua nazo zilikaribia nikawa nachoka sana. Ilibidi niapumzike na biashara ile kutokana kuelemewa na tumbo.

Ugumu wa maisha ulianza kujirudia, lakini nilipata bahati kuna dada mmoja alihamia jirani ambaye kwa kweli tulikuwa tumezoeana.

“Nilipomueleza matatizo yangu hakutaka kuniacha alinisaidia mahitaji madogomadogo. Namshukuru Mungu nilijifungua mtoto salama mwenye afya nje.
“Kwa vile tulikuwa na vitu ndani alinishauri niuze baadhi ili nipate kupata fedha ya kujikimu na maisha.

“Nilifanya vile kwa kuuza kabati kubwa la nguo na tivii na deki kwa bei ya kutupa. Baada ya kufanikiwa zoezi lile alinishauri nihangaike kwa vile baba yenu kuikimbia familia yake, lazima kutakuwa na mkono wa mtu. Bila hivyo nitaiua familia yangu.

“Siwezi kumlaumu kwa kunipa wazo la kumuhangaikia baba yenu. Baada ya kuyafanyia kazi mawazo yake ambayo baadaye yalikuwa majuto ya milele.
“Alinipeleka kwa mtaalamu mmoja ambaye alinieleza kila kitu juu ya baba yenu kushikwa kishirikina na mwanamke wa nje.

“Aliniahidi kunisaidia basi alinipatia tiba ya kusafisha mwili wangu na dawa nyingine.
Niliamini uchawi upo na dawa zipo, ndani ya siku wiki moja ya kutumia zile dawa baba yenu alirudi na kuonekana kama mtu ambaye hakuelewa alikuwa wapi.

“Kwa vile nilikuwa nimepewa dawa na kumtuliza, nilimwekea kwenye chakula na kwenye maji na kuchukua nguo alizorudi nazo na kuzipeleka kwa mtaalamu ambazo alizifanyia dawa.

“Baada hapo baba yenu alitulia nyumbani na hali ya maisha ilirudi kama zamani kwa kurudisha vyote nilivyoviuza. Pia alionionesha na nyumba aliyokuwa akijenga ambayo baadaye aliiandika jina la Mwaija kama zawadi ya kuzaliwa kwake bila ya wewe kuwepo.

“Niliendelea kutumia dawa nilizopewa. Kila nilipokwenda kwa mtaalamu alinieleza vita iliyokuwa nje ni kubwa kwa yule mwanamke aliyekata kumchukua tena baba yenu.
Lakini mganga alinihakikishia hawezi kufanya kitu. Nilimshukuru shoga yangu kuweza kuikoa familia.

“Wakati nikiamini mambo yametulia kumbe yule mwanamke alikuwa halali kwa ajili ya baba yenu, alizozunguka pande zote za dunia. Mwaija alipofikisha miaka miwili mambo yalibadilika.

“Ya mwanzo ilikuwa cha mtoto, kwanza tulianza kukosana ndani jambo si jambo linakuwa ugomvi mkubwa. Nilirudi haraka kwa mtaalamu na kunipatia dawa. Lakini ndiyo kwanza zikamfukuza ndani baba yenu.
“Baba yenu alitoweka sikujua yule mwanamke kamficha wapi. Nilihangaika kutumia dawa za yule mtaalamu bila mafanikio. Taratibu maisha yakaanza kuwa magumu tena.

“Niliapa kuuza hata nguo ya ndani ili kumshikisha adabu yule mwanamke. Nilihangaika kila mganga niliyeelezwa nilifika niliuza vito vyangu vyote ili kuhahakikisha namrudisha baba yenu, lakini nilidunda na kujikuta nimeuza nguo zangu zote za maana ili kuhakikisha naendelea kumhangaikia baba yenu.

“Hamuwezi kuamini wanangu kipindi cha kuhangaika mama yenu sikujua malezi yenu. Nilikonda nilikuwa sijijali kuoga na kubadili nguo ikikuwa kitu muhimu kwangu kwa wakati ule kwa ajili ya kumuhaingaikia baba yenu. Mpaka nakufa yule mwanamke siwezi kumsahau.

“ Kuna mtu alinieleza kuna sehemu nikienda baba yenu atarudi na asingetoka tena. Kwa vile kulikuwa mbali nilikuchukueni na kuwapelekenia kijijini kwa mama na mimi kuondoka kwenda kuangaika.

“Nilikwenda mpaka Ufipa ambako nilikaa zaidi ya miezi mitatu na kubahatika kumpata mganga ambaye alinihakikishia baba yenu hatarudi tena kwa yule mwanamke na kama angerudi basi ningekwenda kuchoma mikoba yake.

Pia alinihakikishia kama yule mwanamke atatia tena mkono basi atabakia jina.
“Baada ya kupata tiba nilirudi nyumbani na dawa kibao, za kuoga, kunywa, kuchoma na kuchanganya kwenye chakula. Niliandikiwa dawa zote na matumizi yake.

“Baada ya kupewa dawa nilirudi nyumbani nikiwa nipo hoi.Nilikonda mama yenu na kusawajika kwa ajili ya kuhangaika kumrudisha mume wangu nyumbani.

“Nilifika nyumbani majira ya saa moja usiku, siku ileile sikutaka kulala. Nilichukua dawa zangu, nilianza kwa kuoga dawa na nyingine kuwagia kila kona kuondoa uchawi. Kisha nilianza kufanya kama nilivyoelekezwa jinsi ya kumvuta baba yenu
 
Sehemu ya 30

“Baada ya kupewa dawa nilirudi nyumbani nikiwa nipo hoi.Nilikonda mama yenu na kusawajika kwa ajili ya kuhangaika kumrudisha mume wangu nyumbani.

“Nilifika nyumbani majira ya saa moja usiku, siku ileile sikutaka kulala. Nilichukua dawa zangu, nilianza kwa kuoga dawa na nyingine kuwagia kila kona kuondoa uchawi. Kisha nilianza kufanya kama nilivyoelekezwa jinsi ya kumvuta baba yenu.

“Kwa vile nilikuwa nimefika jioni sana, usiku ulipofika nilichoma dawa huku nikimwita baba yenu kwa jina arudi nyumbani. Nilifanya bila bila kupumzika kama nilivyoelezwa mpaka nitakaposikia hodi.

“Narudia tena kusema uchawi upo na dawa zipo. Nikiwa katikati ya zoezi ambalo lilikuwa linachukua zaidi ya saa moja na nusu. Nilisikia mlango ukigongwa, niliacha kunuiza na kwenda kufungua mlango.

“ Sikujua nani anayegonga, nilipofungua mlango kidogo nianguke kwa mshtuko baada ya kumuona baba yenu mbele yenu.”
Kauli ya mama alifanya mwili wangu usisimke, nilimuangalia mama aliyekuwa akizungumza taratibu huku akifuta machozi, moyo uliendelea kunifukuta.

“Nilimuona baba yenu kama msukule aliyerudishwa baada ya kuchukuliwa kichawi. Alikuwa kama mtu asiyejifahamu. Kama mmeisha wahi kuona mtu akirudishwa baada ya kuchukuliwa kichawi ndivyo baba yenu alivyokuwa.

“Ile hali nilielezwa na mganga itajitokeza, lakini alinieleza nimshtue kwa kumpiga na maji ya dawa usoni kisha nimuoshe kwa dawa aliyonipa na nyingine nimpe anywe, siku ya pili angeamka akiwa mzima kabisa.

“Baada ya baba yenu kuingia ndani moyo uliniuma sana kutokana na hali aliyokuwa nayo. Kumbe alikuwa yupo na yule mwanamke aligeuzwa msukule kwa kufanyishwa mambo bila kujua.

“Nilifanya kama nilivyoelekezwa nimpige usoni na maji ya dawa ili kumzindua kwenye kifungo cha kichawi. Baada ya kuchanganya dawa kwenye maji nilimpiga nayo usoni na kumfanya ashtuke kama anatoka usingizini.
“Cha kwanza kilikuwa kuwauliza wanawe, nilimueleza mmekwenda kumtembelea bibi yenu kijijini. Alijinyoosha kama mtu aliyekuwa amechoka sana na kupiga miayo.

Nilimpelekea bafuni maji niliyochanganya na dawa kuoga. Baada ya kuoga nilimpa dawa ya kunywa na kumuacha alale.

“ Mmh! Yaani baba yenu alipolala ha..ha..ku..amka tena.”
Mama alianza kulia kilio cha kwikwi kitu kilichofanya wote tulie kilio cha kimya kwa kutokwa machozi huku nikizidi kumuonea huruma mama yetu.

Ilibidi mama Amina aingie kazi ya kumbembeleza mama aliyekuwa akilia kilio cha kwikwi. Nilipowangalia dada zangu kila mmoja alikuwa akilia.

Kwa kweli ilikuwa simulizi yenye kuumiza na kuupasua moiyo bila ganzi. Baada ya mama kunyamaza aliendelea kuzungumza kwa sauti ya kilio na kuzidi kuniumiza.

“Kwa kweli sikuelewa sababu ya kifo cha baba yenu, nilijiuliza labda dawa niliyompa kunywa na kama ni ile nilikosea sehemu gani. Niliulimia mara mbili baada ya kuhaingaika kote kumbe natafuta kumuua mume wangu.”
Kufikia hapo tena mama akaanza kulia tena.
Nilishindwa kujizuia nilijikuta nikisema kwa sauti bila kujielewa:

“Mama hujamuua baba, ulifanya kwa ajili yetu lakini bahati mbaya ikatokea iliyotokea.”
“Hapana wanangu bila mimi msingekuwa yatima.”
“Si kweli, wangapi yatima si kwa tukio kama lako?”nilihoji.

“Lakini bila mimi baba yenu asingekufa.”
“Angekufa kwa kitu kingine, mama toka ulipoanza kuzungumza sijaona sehemu uliyochangia kifo cha baba. Mama tunakuomba uondoe wazo hilo,” dada mkubwa alisema.

“Basi wanangu baada ya msiba tulifanya kila kitu na kumuhifadhi baba yenu. Nilikonda kwa mawazo, lakini ninyi wanangu ndiyo nilionifanya nisimame imara ili kuhakikisha nawasomesha na hamtetereki kimaisha.
“Sijui niseme nini, lakini baada ya kifo cha baba yenu vitu vingi vilijulikana. Alikuwa na gari na nyumba pia malipo yote ya kazini kwake nilipata.

Baada ya kupata vitu vyote hivyo nilimalizia nyumba ya Mwaija na kupangisha. Naweza kusema nilifanya kosa kukueleza Mwaija baba yako alikuachia nyumba kubwa.

“Hilo naomba nikiri nilifanya kosa, nimekula fedha yako bila kukushirikisha kwa miaka yote hiyo. Lakini leo nitakukabidhi kila kitu.
“Kupitia mali alizoacha baba yenu niliweza kuwasomesha wote ila sikutaka msome sana kwa vile mngeondoka na kuniacha peke yangu. Hapo ndipo nilipoanza kufanya makosa makubwa.

“Baada ya Zamdana na Rehema kuolewa niliona nyumba inapwaya na kujikuta nikipata wazo la kuwarudisha nyumbani hapo ndipo nilipo kwenda kwa mtaalamu na kuzisambaratisha ndoa zenu na ninyi kurudi nyumbani bila kujua mimi ndiye mbaya wenu. Niliweza kuwafanya kuzichukua ndoa kitu kilichokuwa furaha yangu.

“Nilifanya hivyo kwa Mwaija ambaye nilikuwa nampenda sana, wewe ndiye sikutaka kabisa aondoke nyumbani. Yote yaliyokutokea nilifanya mimi mama yako.

“Wanangu nachukua nafasi hii kuwaombeni radhi kwa yote niliyowafanyia pia namuomba mwenyezi Mungu asisamehe kwa kila baya niliyowafanyia wanangu. Sijui bila mama Amina, wanangu wangeendelea kuishi maisha gani.
“Mwanangu najua nimewaumiza bila ya ninyi kujua, naomba mnisamehe nipo chini ya miguu yenu.”

Mama alisema huku akinyanyuka kitini ili apige magoti. Tulinyanyuka wote na kumwahi kabla hajapiga magoti nakumwambia tumemsamehe mama yetu.
Baada ya zoezi lile mama Amina alizungumza:

“Nina imani mmemsikia vizuri mama yenu, siku zote mtu akigundua kosa lake na kutubu hata Mungu umsamehe. Mama yenu kagundua makosa yake na leo kayasema yote bila kuacha kitu.

“Kwa vile mmemsaheme nawaomba muishi kama zamani mpendeni mama yenu. Alifanya vile kwa mapenzi mazito kwa wanaye lakini akawa anaharibu.

“Namshukuru Mungu kwa upande wangu nimemaliza kazi yangu nina imani kila mmoja ameona mabadiliko?” mama Amina aliuliza.
“Ni kweli,” tulijibu kwa pamoja.
“Mimi nafikiri sina cha zaidi nakushuku tumelimaza salama wacha nikimbie,”mama Amina alitaka kutuaga.

“Mama Amina tunashukuru kwa kila ulilotufanyia, nina imani si kwa uwezo wetu bali ni Mungu ndiye aliyetuongoza kukujua wewe na kututoa kwenye kiza kizito.
“Kwa upande wa mama bado tunampenda sana tena sana. Alichotueleza hakitapunguza upendo wetu kwake.

Tunampenda mama leo kesho kwa vile kilichofanyika ni funzo si kwake hata sisi tutazaa na kutorudia kosa.
“Mama ondoa unyonge lililopita limepita, tumshukuru Mungu kwa kulifungua mapema kabla hujafa. Inawezekana tukio hili lilikuwa kutukumbusha kumrudia Mungu wetu.

“Namalizia kumshukuru tena mama Amina wewe si mganga tu bali ni sehemu ya familia yetu. Sisi hatuna cha kukulipa bali Mungu ndiye mwenye uwezo huo.

Wadogo zangu hatuna budi kumtunza mama yetu kwa vile amebakia kama jicho letu. Tusimuwekee kinyogo bali tumpende na kumtunza,” dada mkubwa alisema kwa hisia kali mpaka machozi yakamtoka.

“Mama nakupenda nitaendelea kukupenda,” dada Rehema alisema maneno mafupi.
“Mama nataka kukuambia mapenzi yangu kwako ni makubwa sana, nataka kukueleza chanzo cha matatizo yangu niliyajua muda mrefu toka nikiwa na Beka.

Lakini bado sikuwa tayari kukuchukia mama yangu, niliamini unatupenda japokuwa sikupenda maisha tuliyokuwa tukiishi. “Nilijitahidi niwe tofauti na dada zangu.
Nilikuwa na bahati iliyoishia na matatizo, hata baada ya kugundua sababu ya matatizo yangu bado moyo haukukubali mama unaweza kuwa adui yetu.

“Nimehangaika kuupata ukweli bila mafanikio, na nilipoupata bado niliendelea kumpenda sana mama yangu. Nilitamani kukueleza lakini niliogopa.

“Inawezekana wote hamjui kikao hiki kimeitishwaje, nataka kuwaeleza, mimi ndiye niliyemfuata mama Amina na kumuomba aitishe kikao hiki ili kuufungua moyo wa mama aliokuwa na mzigo mzito pia kwa sitojua kwa dada zangu kwa vile mimi nilijua haya mapema.

“Mama inawezekana ukaona nimekuvunjia heshima kwa kukulazimisha kuyasema mambo mazito kwetu. Mama naomba unisamehe nilifanya hivyo kwa ajili ya kukuweka huru.
“Nilijua unaumia na kuendelea kuteketea kama mshumaa, huwezi kujua hali iliyokuwa nayo ilitutesa sana wanao kiasi gani. Lakini leo nataka kukuambia toka moyoni kuwa tumezaliwa upya,” nami nilimalizia.

“Asanteni wanangu, narudia kusema namshukuru Mungu kunipa watoto yenye mapenzi ya dhati na mama yenu. Nimejifunza kitu nina imani kila kitu ni uweza wa Mungu.
“Mama Amina nashukuru sana mdogo wangu, Mungu atakulipia, narudia wanangu mnisamehe sana.”
“Tumekusamehe mama,” tulisema kwa pamoja.
***
Kikao kilisha salama kwa watoto wote kuiswafi mioyo yetu kwa mama. Kwa upande wangu niliutua mzigo mzito ulionielemea moyoni mwangu na kuwa huru huku nikiendelea kumshukuru Mungu.

Furaha ilirudi katika nyumba yetu, dada yangu aliolewa harusi kubwa na mwingine anaendelea na kazi huku akiwa na bwana ambaye alimuahidi kumuoa.

Namalizia kuwa kumshukuru mama Amina kwa msaada wake wa hali na mali kuhakikisha anapigania afya yangu mpaka leo hii ninayotoa ushuhuda huu nina afya njema na watoto watatu wawili wa kike na mmoja wa kiume.

Dada zangu wote wana mtoto mmojammoja.
Pia namshukuru sana mwandishi wa mkasa huu kwa kukubali kupoteza muda wake kuandika mkasa mzito kama huu. Mungu atamlipia kwa kazi yake ya kujituma bila kuchoka.

Mwisho kabisa nawashuku wasomaji wote kwa kupoteza muda wao kufuatilia simulizi yangu mpaka leo ambapo nahitimisha mkasa huu, Mungu atawalipa pia nina imani kuna kitu mmejifunza hasa wazazi nina imani mmeona madhara ya ushirikina.

Wapeni uhuru watoto wenu waishi maisha yao hata kama mnawapenda sana.

MWISHO.
 
Mwisho kabisa lakini ndio mwanzo wa kitushushia kitu kingine hadithi nzuri inafundisha sana
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom