Simulizi: Mtoto wa Baba Paroko

Mtoto wa Baba Paroko : SEHEMU YA SITA

Cc. Shunie lovelovelove Smart911 hearly Luno G moneytalk sweet pie kisukari instanbul havanna kuku mweus Lubebenamawe Uncle Yoso TsotsiKwesta ichumu lya

Damu Nzito Kuliko Maji

Mwaka 1986, Boniface Mapunda akiwa shemasi tayari akisubiri kula kiapo cha upadri alichagua kwenda kufanya kazi Jimbo Katoliki Sengerema katika kilichokuwa kigango cha Nyagawa.


Katika maeneo ya kiutawala ya Kanisa Katoliki, basi eneo dogo kabisa huitwa Jumuiya, jumuiya kuanzia mbili na kuendelea huzaa kile kiitwacho Kigango, vigango viwili na kuendelea huzaa Parokia kisha Parokia mbili na kuendelea huzaa Jimbo. Jimbo ndio eneo la mwisho kiutawala ambalo huongozwa na Askofu ambaye ndiye kiongozi wa juu wa kanisa katika ngazi ya jimbo.


Boniface Mapunda alichagua kwenda Sengerema kwani ndipo chimbuko la mama yake mzazi. Baba yake akiwa Mngoni wa Songea mama yake alikuwa Msukuma wa Sengerema. Alipenda kutumia muda ule kwenda kuhudumu kule kwanza kama sehemu ya shukrani kwa mama yake lakini pia alitaka kubadili mazingira kwani muda mwingi wa likizo zake akiwa seminari kuu Peramiho alitumia akiwa kwao Songea.


Boniface Mapunda ndiye leo ni Padri Mapunda, Mkuu wa Seminari ya Kipalapala Tabora.

**************************************

MariaClara, binti wa mzee Alphonce Mabula alikuwa na umri wa miaka 19 mwaka 1986. Hakuwa tu msichana mzuri kwa kumtazama kwa macho lakini pia sauti yake na haiba aliyokuwa nayo hakika ilimuhakikishia mzee Alphonce Mabula ng’ombe za kutosha kama mahari pindi binti yake atakapotaka kuolewa.


MariaClara alikuwa binti wa kanisani, siku hizi tungemwita, kwa ‘swaga’ za kizazi kipya ‘church girl’ na pengine kwenye ukurasa wake wa Instagram kwenye ‘bio’ angekuwa ameandika ‘God Fearing’ au ‘Born again’, lakini hayo hayatuhusu sana, tuyaache.


Kama alivyokuwa baba yake yaani mzee Mabula, MariaClara nae alikuwa hivyo hivyo. Usafi wa kanisa, kuhudumia maua na kujitolea kufua mavazi yaliyotumika madhabahuni ndiyo hasa ilikuwa kazi MariaClara akizifanya tena kwa kujitolea na bila kulazimishwa.


Ni katika mazingira hayo Padri Mapunda, aliyekuwa akiitwa Shemasi Mapunda wakati ule, alipokutana na MariaClara. Shemasi Mapunda akiwa nae kijana wa miaka kama 33 hivi alivutiwa sana na MariaClara. Uzuri wa MariaClara haukumuacha salama.


Shemasi Mapunda damu ilikuwa ikimchemka sana wakati ule na ukweli ni kuwa si mara moja wala mbili alishawahi kuvunja amri ya sita tena akiwa katika masomo ya kuhitimu upadri. Alijikaza sana lakini alishindwa na aliamua kusema na MariaClara.


MariaClara alikataa katakata kwani mpaka wakati ule bado alikuwa hamjui mwanaume na isitoshe alijua ukali wa baba yake. Kukataa kwa MariaClara hakukuzuia harakati za shemasi Mapunda kuhakikisha anampata binti Maria.


Hatimaye shemasi Mapunda alifanikiwa, MariaClara kwa mara ya kwanza alimjua mtu mume kwa kulala na shemasi Mapunda. Ni katika mahusiano yale MariaClara alitambua kuwa jina lingine la Boniface Mapunda aliitwa Kapalata na kwasababu yeye ni msukuma, aliamua awe anatumia jina hilo pindi awapo faragha na shemasi Mapunda. Hivyo jina Kapalata ni moja kwa moja linahusiana na mahusiano ya padri Mapunda na MariaClara na si vinginevyo.


Mahusiano haramu kati ya shemasi Mapunda na MariaClara yaliendelea kwa siri kubwa na Mapunda alimsihi sana MariaClara afanye siri kati yao tu kwani ingejulikana basi asingeweza kupata tena kutimiza ndoto yake ya kuwa padri. MariaClara, kwanza kwa kujua ukali wa baba yake na imani na dini aliyokuwa nayo, hakika kama ni siri ilifika pahala pake kwani hakuna hata rafiki yake mmoja aliewahi kujua kuwa MariaClara ana mahusiano na shemasi Mapunda.


Baada ya kumaliza muda wake wa mapumziko shemasi Mapunda aliondoka Sengerema na kumwacha MariaClara. MariaClara alikuja kugundua ana uja uzito miezi miwili baada ya shemasi Mapunda kuondoka. Alijiapiza na kwa kuogopa kutomtaja muhusika wa ule ujauzito. Kwanza alihisi atatengwa kwa kukubali kulala na Shemasi, alijionea dhambi kubwa mbele ya jamii. Kitimtimu cha kipigo cha baba yake kilimkimbiza kijijini na kwenda Dar es Salaam.


Alipofika Dar es Salaam, MariaClara akiwa amefikia kwa mjomba wake aliyejulikana kwa Majina ya Jibril Mgeni. Aliendeleza jitihada za kumtafuta shemasi Mapunda ili angalau aweze kumsaidia katika changamoto alizokuwa anapitia. Njia aliyotumia ni kuuliza kwa mapadri mbalimbali aliokuwa akiwasiliana nao kwenye parokia alizowahi kusali, kwani MariaClara hakuacha kujitolea kazi za kanisa hivyo alifahamiana na kuzoeana na mapadri wengi wa Parokia mbalimbali za Jimbo la Dar es Salaam hasa maeneo aliyowahi kuishi.


Siku moja alifanikiwa kuwasiliana na Padri Mapunda baada ya miezi minne tokea afike mjini, wakati ule mimba ya Eric ikiwa na miezi sita. Alimweleza jinsi alivyopata tabu na ujauzito ule na kumuasa aangalie namna ya kumsaidia. Wakati ule, Padri Mapunda ndiyo kwanza ametoka kula kiapo cha wito wake na kuwa padri kamili alimsihi sana Maria kuwa aitoe ile mimba kwani haiwezekani wala haitawezekana yeye kuwa na mtoto katika wito wake ule.


Majibu ya Padri Mapunda yalimtia simanzi sana MariaClara, alilia na kujutia ila akakumbuka kuwa kwa hali ilivyo ni kweli Padri Mapunda hana namna. Maria alikumbuka nyakati walivyokuwa wakiwa pamoja kule Sengerema na alisikitika hali ile kutokea.


Kupata mawasiliano na padri Mapunda ilikuwa tabu sana hivyo kuanzia siku ile MariaClara aliamua kuachana na suala la kumtafuta juu ya mtoto. Alipojifungua aliamua kumwita mwanae Eric Nyagabona.


Japo MariaClara hakuwasiliana tena na padri Mapunda kwa miaka 32 sasa, lakini hakuacha kujua nini kinaendelea kwa Padri Mapunda. Kutumia mapadri mbalimbali MariaClara alikuwa akijua kila mwenendo wa padri Mapunda. Mapenzi na padri Mapunda hayakuwahi kwisha, labda kwasababu alijua Eric ni damu yake.


Siku Eric alipomwambia kuwa amepangiwa Seminari ya Kipalapala MariaClara ilitoa machozi. Eric alipomuuliza alimwambia ni machozi ya furaha na kuwa sasa ana uhakika mwanawe anakwenda kuwa padri. Eric hakuelewa.


Leo Askofu Kengele anataka kufanya nini? MariaClara uvumilivu ulimfika kikomo. Ukimya wa miaka zaidi ya 30 unaishia hapa.

***********************************

“Padri kuna nini?”, Eric alimuuliza Padri Mapunda baada ya kumuona haeleweki baada ya kuongea na simu na kisha kuikata ghafla na kubadilika sura.


“Eric wewe asili ya kwa mama yako ni wapi? Najua hatujafikia hatua hii ya kuwachunguza ila nikuulize leo”, Padri Mapunda aliuliza.


“Mimi kwa mama ni Nyagawa, Sengerema kwa baba ni jirani kulekule”, Eric alijibu kama alivyofundishwa na mama yake. Aliambiwa kuwa babake ni Msukuma pia japo alifariki.


“Babu yako mzaa mama aliitwa nani?” Padri Mapunda aliuliza tena.


“Alphonce Mabula” Eric alijibu.


Jibu lile lilimtia ganzi Padri Mapunda, alijua aliyepo mbele yake ni kijana wake, hakuamini.


Wakati akiwa anatafakari aseme neno gani tena, simu ya Eric aliyokuwa ameishikilia yeye ilianza kuita tena na aliyekuwa akipiga alikuwa ni mama yake Eric, yaani MariaClara.


“Maria”, Padri Mapunda wakati huu aliita huku machozi yakianza kumtiririka mashavuni. Ni miaka 32 imepita sasa hakuwahi kusikia sauti ya MariaClara, achilia mbali kusumbuliwa nae hata kwa nukta moja. Sasa, Padri Mapunda alikuwa ni mzee wa miaka 65, hakuamini.


“Kapalata”, MariaClara alimwita Padri Mapunda kwa jina lile alilozoea siku zote.


“Eric ni mwanao. Nimefanya yote uliyoniambia, sikuharibu wito wako tena hata kukutaka shilingi moja ya kumtunza Eric, leo nakuomba jambo moja tu hakikisha Eric anapata upadri. Ni hilo tu baba”, MariaClara aliongea kwa uchungu sana uliomfanya Padri Mapunda awe analia kama mtoto. Mzee wa miaka 65 alilia machozi mengi.


Padri Mapunda kwa wakati ule uchungu mwingi ulimwingia. Hali ya ubaba ilimwingia kabisa, alijisikia usaliti usio kifani. Hali ya kuwa yeye ni Padri ilimtoka kabisa na hakika moyo na macho yake vyote vilishuhudia kuwa aliepo mbele yake ni kijana wake na yeye kama baba halali wa Eric anao wajibu wa kuhakikisha ndoto za kijana wake zinafikiwa.


“Maria, nawezaje kukiuka maagizo ya askofu? Nami nitakuwa nimetenda kosa lilelile alilotenda Eric la utovu wa utii. Na uzee huu unataka niende wapi?”, Padri Mapunda alimjibu MariaClara aliyekuwa akitoa kwikwi ya kilio.


“Kapalata, maisha yangu yaliharibikia mikononi mwako leo unataka maisha ya damu yako mwenyewe nayo yaharibikie mikononi mwako?” MariaClara alimuuliza Padri Mapunda kwa uchungu mkubwa.


Alimkumbusha mstari katika biblia wa kitabu cha Esta 4:14 pale ambapo mjomba wa Esta yaani Modekai alipoona wayahudi wanauawa kwa amri ya mfalme Ahusero iliyochagizwa na jemedari wake Hamani na kumwambia Estayeye akiwa kama malkia anayependwa sana na mfalme aingilie kati kutetea wayahudi na kumwambia, “Wajuaje kuwa umekuwa malkia kwa ajili ya wakati kama huu?”


“Kapalata, huwezi kujua ilitokea vile mimi kubeba ujauzito wako tena na mwanao kuja kusoma seminari ambayo wewe ndiyo mkuu wake kwa ajili ya wakati kama huu. Usipomtetea wewe nani atamtetea mwanangu?” MariaClara aliendelea kuongea mfululizo.


“Maria, nafahamu lakini sioni jinsi naweza kumsaidia zaidi ya kumtii askofu kwanza” Padri Mapunda au kama afahamikavyo Kapalata kwa Maria alijibu tena.


“Kapalata, do something. He is your son for God’s sake!”(Kapalata fanya jambo. Huyo ni mwanao ati!). MariaClara aliongea kwa kiingereza cha kuibia alichojifunza kwenye shirika la misaada la tajiri Jaques Lorento alikokuwa akifanya kazi za usafi.

Alimaliza kusema hivyo na kukata siku kwasababu kilio kilimzidi na hakutaka kuamini kuwa mtu wa mwisho aliyedhani anaweza kumsaidia mwanae Eric anadai hawezi.


Sentensi ya mwisho ya MariaClara ilimuingia sana padri Mapunda, aligeuka na kumwangalia Eric tena. Alisogea na kumkumbatia.


“Mama yako ni mjomba wangu” Padri Mapunda alimwambia Eric ili kumtoa kwenye lengo.

Eric alimkumbatia padri Mapunda kwa hisia kubwa kuliko kawaida.


“Mjomba nisaidie, bado napenda kumtumikia Mungu kwa wito wa Upadri” Eric akiwa amemkumbatia Padri Mapunda alimsihi.


“Deum nemo vidit umquam unigenitus Filius autem sacrificium quod paratus eram ut ego sum”, Padri Mapunda alimwambia Eric kwa kilatini huku akiwa amemkumbatia kwa nguvu kabisa na akibubujikwa machozi. Eric alishangaa kusikia maneno hayo lakini hakuelewa ni kwanini padre Mapunda aliyatamka, alibaki kimya.


Maneno hayo yalimaanisha kuwa ‘Mungu alikuwa tayari kumwacha mwanae wa pekee (yaani Yesu Kristu) ateseke kwa ajili ya ulimwengu lakini yeye hataweza na kuwa ni lazima afanye jambo kuokoa jahazi na kuhakikisha Eric anaupata upadri.’

**************************************

Je, Padri Mapunda Anataka Amsaidieje kijana Wake Eric? Ataweza Kuruka Vizingiti Vya Uchunguzi Vya Kanisa katoliki Lenye Ujasusi Usiomithilika Katika Taasisi Zake? Usiache Kufuatilia Simulizi Hii Itakayokusisimua siku ya Jumamosi

the Legend☆
 
Mapigo ya moyo yakiongezeka kama Pikipiki ya msafara wa Rais,,, ,ahaaaaa
Sent using Jamii Forums mobile app
 
Mbona wengi wanapingana nadhani hatakuwa wa kwanza wala wa mwisho

Sent using Jamii Forums mobile app
Uko sahihi mkuu. Damu ni nzito kuliko maji. Katika hali ya kibinadamu sio rahisi kwake kuona ndoto za mwanae zinapotea ikiwa anaeza kufanya jambo kumsaidia

the Legend☆
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…