Sehemu ya 44
Deborah akabaki akimwangalia John, hakuelewa alichokuwa amekizungumza, wakati mwingine alihisi kama mwanaume huyo alikuwa akimtania.
Alimwangalia usoni, alionekana kumaanisha kile alichomwamia. Haikumuingia akilini mwake, ilikuwaje amwambie alikuwa akimpenda? Alimchukulia kama mfanyakazi mwenzake lakini pia kwa muonekano wa mwanaume huyo, hakustahili hata nusu kuwa naye.
“John!” aliita Deborah huku akimwangalia usoni, kwa kiasi fulani John akaonyesha kutokujiamini.
“Naam!” akaitikia.
“Umesemaje?” aliuliza.
John akabaki kimya, si kwamba Deborah hakusikia alichoambiwa, alikisikia sana ila alihitaji kuona ni kwa jinsi gani mwanaume huyo alikuwa akijiamini kumwambia neno lile lile tena na tena.
John akavuta pumzi, alimwangalia Deborah, uzuri wa msichana huyo uliendelea kumchanganya zaidi. Kubaki kimya pasipo kurudia neno lile ungeonekana kuwa udhaifu mkubwa, kama kweli alikuwa akijiamini ilikuwa ni lazima amwambie tena.
“Ninakupenda!” alisema.
“Unamaanisha ama?” aliuliza.
“Deborah! Najua unahisi ni utani kwa sababu tu muonekano wangu na wako ni vitu viwili tofauti. Nimetamani nikwambie hiili kwa kipindi kirefu mno, nimetokea kukupenda tangu siku ya kwanza nilipokutia machoni mwangu, hicho ni kitu ambacho siwezi kukaa kimya huku kikinifurukuta moyoni mwangu,” alisema John huku akimkazia macho msichana huyo.
“Hapana!”
“Unamaanisha nini? Kwamba hunitaki?”
“Simaanishi hivyo!”
“Unamaanisha nini?”
“Natakiwa kupata muda wa kufikiria sana kuhusu hilo, si unajua mambo ya uhusiano si ya kukurupuka,” alisema Deborah.
John akashusha pumzi, siku zote aliamini kwa mwanamke yeyote ambaye alimpa muda mwanaume wa kujifikiria, asilimia tisini na tisa walikuwa wakikubaliana na kilichosemwa ila hawakutaka kuwajibu haohapo.
Moyo wa John ukaburudika, akajisikia amani moyoni mwake, mapenzi aliyokuwanayo kwa msichana huyo yalizidi kuongezeka hivyo baada ya kumaliza wakaendelea na safari.
Wakafika nyumbani kwao, akateremka na kuagana naye kisha kuingia ndani.
Akajilaza kwenye godoro lake, moyo wake ulikuwa na furaha kupita kawaida, kila kitu kilichotokea kilionekana kama ndoto fulani ambapo baada ya muda angeamka na kujikuta akiwa kitandani.