Abdallahking
JF-Expert Member
- Mar 19, 2018
- 3,983
- 10,804
Simulizi: JAMANI MCHUNGAJI !!
Mwandishi: GEORGE IRON MOSENYA
Imeletwa kwenu na: BURE SERIES
SEHEMU YA 1
Masikio yake hayakuamini anachokisikia lakini ubongo wake uliamini kuwa mkewe alikuwa kwenye ndoto nzito sana, jasho lilikuwa linamtoka na alikuwa anajiviringisha pale kitandani kwa staili za ajabu ajabu
"Mchungaji.,ah! mchungaji...mchungaji" ndizo sauti alizokuwa anatoa mwanamke huyu
"Mh! ndoto gani tena hizi jamani au ndio....," alisita kumalizia neno hilo kwani kwa misingi yake ya dini ilikuwa haipaswi kumuhukumu mwanadamu mwenzako bila kumshrikisha Mungu muumba wa vyote. Miguno hiyo ilikuwa inashabihiana kabisa na ile ambayo huwa inasikika katika filamu za ngono.
Alitua ‘briefcase’ yake chini na kulegeza tai yake kabla ya kuondoa koti lake la suti, tayari ilikuwa saa nne usiku akiwa ametoka kwenye kikao cha kampuni. miguno iliyoendelea pale kitandani ilimtia hasira kiasi fulani lakini jina lililotajwa ndio lilimkera zaidi
"Honey! honey, iam back" taratibu akamwamsha na kuikatisha ndoto yake.
"Mh! mchungaji ah! mume wangu, umerudi karibu, saa ngapi hivi" kwa sauti ya ulevi wa usingizi alianza kuzungumza yule mwanamke huku akiyapikicha macho yake kwa kutumia kiganja kimoja na mkono mwingine ukiishikilia kanga iliyokuwa inataka kudondoka kutoka kifuani, mwanga wa taa iliyokuwa imewashwa ilimsumbua kuizoea hali.
Hasira ilimkaba kooni kijana huyu, alijaribu kutabasamu lakini sura yake ilifanana na mtu aliyepokea barua ya kufukuzwa kazi huku nyumbani akiwa na familia kubwa pamoja na wakwe waliokuja kuchukua mahari yao ambayo ilikuwa haijamaliziwa bado. Alichukizwa sana na suala la mke wake kukosea jina lake na kumuita mchungaji, mwanzoni alilisikia hilo jina katika ndoto lakini sasa alikuwa anamsikia mkewe akilitaja jina hilo wakati ameyafumbua macho yake.
* * * *
Lilikuwa suala gumu sana kumshawishi kijana Timoth aweze kukuelewa kuhusu umuhimu wa kuwa na mwenza ndani ya nyumba. Shughuli za kufua, kuosha vyombo na kufanya usafi ndani ya nyumba yake zilimchosha sana lakini hakutaka mke.
Aliyaogopa mapenzi sana kupindukia visa vya mafumanizi alivyovisoma kwenye magazeti na kusikia redioni vilimtikisa sana kaka huyu aliyekuwa na miaka takribani ishirini na tisa (29) na tayari akiwa na mafanikio yake kama kijana kwa mshahara alioupata kutokana na kazi yake ya afisa masoko wa kampuni ya usafirishaji ya Lookman ya jijini Dar-es-salaam.
Kwa ushauri wa mama yake mzazi na pia mchungaji wa kanisa lake bwana Marko, Timoth alianza kufikiria kuhusu suala hilo na hatimaye hisia za mapenzi alizokuwa amezifungia gerezani akazipa msamaha zikawa huru na uhuru huo zikautumia kumwangukia binti mrembo mwimba kwaya hapo kanisani aliyeitwa Noela, halikuwa suala gumu sana kwani wachungaji walikuwa kati yake hvyo Noela hakuleta longolongo uhusiano ukaanza rasmi hadi walipofunga ndoa takatifu kanisani hapo. Japo alikuwa anahofu ya kutendwa lakini aliifunga akili yake na kusema maneno haya.
“Nipo tayari kumuoa binti Noela Philemon, na nitaishi naye katika shida na raha hadi hapo kifo kitakapotutenganisha” makofi, nderemo na vifijo vilifuatia.
Timoth Getafe na Noela Philemon wakawa mke na mume rasmi!!
Timoth aliamini alikuwa amekosa mengi kwa kuwa katika maisha ya ukapera muda wote ule, kwani raha alizozipata kwa kuwa na Noela kama mke wake alijihisi yupo nchi ya kufikirika ambayo ni zaidi ya jengo la kifalme huko uingereza, zaidi ya Tanzania na amani yake, zaidi ya raha anazopata mtoto kwa kunyonya ziwa la mama huku joto la asili lillojaa upendo wa kweli wa mama likipenya katika ngozi yake.