HILIKI YA CHUMBAGENI – 15
NA JOSEPH SHALUWA
ILIPOISHIA...
“Hapana siwezi kuzichukua, naomba zikusaidie tafadhali mpenzi,” akasema Bravo.
“Hapana Bravo. Mimi sijiuzi, nikichukua hiyo pesa ni kama umeninunua. Hii 30 yenyewe nachukua kukuridhisha tu. Wewe ni wangu, isitoshe una familia, hutakiwi kutumia fedha hovyo.
“Nikiwa na shida na pesa nitakuambia, lakini kwa sasa kwa kweli sina kazi nazo. Naomba tu uzichukue!” akasema Tunu.
“Mh! Hata Viola hayupo hivi... mwanamke anakurudishia pesa? Mwanamke wa nje anajali familia yangu? Basi kama ni hivyo ni afadhali ingewakuwa huyu ndiyo mke, halafu Viola ndiyo awe nyumba ndogo.... haya mambo ni mageni kabisa kwangu,” akawaza Bravo akichukua zile noti.
Tunu akamvuta Bravo kifuani mwake, akamkumbatia kwa nguvu!
Alijuta kumfahamu Tunu!
SASA ENDELEA...
WALIGANDANA kwa dakika tatu nzima, hakuna aliyechoka kati yao. Muda ulizidi kwenda, hapakuwa na dalili za kuachiana. Lakini Bravo akakumbuka kwamba alitakiwa kuwasiliana na Viola.
Hata kama alikutana na mambo tofauti kwa Tunu, lakini bado nafasi ya mkewe ilikuwa palepale. Alimuachia Tunu, kisha akamwambia: “Nakupenda sana mama, naomba uniruhusu niondoke mpenzi.”
“Sawa baba, nakutakia usiku mwema, uote ndoto njema, niutawale usiku wako kipenzi changu!”
“Asante sana mama.”
Bravo akawasha simu yake, kisha akampigia dereva aliyemfikisha pale kwa Tunu. Akamsubiri kwa dakika tano tu akawa amefika, maana hakuwa mbali sana na eneo la Chuda. Alikuwa Mabanda ya Papa.
Bravo akaondoka!
***
Alipofika hotelini, alijitupa kitandani kwa uchovu mwingi. Bado alikuwa akimtafakari Tunu, mtoto wa Kitanga na mambo yake ya Pwani ambayo yalikaribia kuutibua ubongo wake.
“Kweli sasa nimeamini kuna watu wameumbwa kwa ajili ya mapenzi... Tunu ameumbwa kwa ajili hiyo. Ameumbwa kwa ajili ya kumfurahisha mwanaume... tena mwanaume mwenyewe naamini ni mimi.
“Kwa umri wake, najua atakuwa hajachezewa sana na manyang’au ya mjini. Bado atakuwa na mengi mazuri ya kuufurahisha moyo wangu. Lazima Tunu aingie kwenye maisha yangu,” akawaza Bravo akiwa kitandani ametulia.
Hakuwa na haja ya kuoga, kila kitu kilifanywa na Tunu chumbani kwake. Akiwa bado anaendelea kuwaza, simu ikaita.
Alipoangalia kwenye kioo, akakutana na jina la Tunu.
“Waoooo! Raha ya moyo wangu ananipigia...” akawaza Bravo akikaa vema kitandani ili aweze kuzungumza na daktari wa moyo wake...
“Halooo baby.”
“Haloooo honey, naamini umefika salama kipenzi changu!” ilikuwa sauti laini, tamu, isiyochosha ya Tunu.
“Ndiyo mpenzi, nipo kitandani hapa.”
“Nimekupigia kwanza kujua kama umefika salama, pili kukushukuru kwa kunipa raha na tatu kunipa hela. Asante sana mpenzi wangu. Wewe ni mwanaume wa tofauti sana. Unajua kila kitu. Unajali, unanipenda kwa dhati na unajua mapenzi, utafikiri ulikwenda jando la Kisambaa!” akasema Tunu kwa sauti yake ileile.
Bravo akadata!
Sifa zote hizo! Kiukweli Bravo hakuwahi kufisiwa na mwanamke kwa kiwango hicho. Akakumbuka hata anavyompatia fedha mkewe, hakuwa akimshukuru kwa kiwango hicho. Sasa akakiri kweli alikutana na mwanamke wa kumfanya awe mwanaume kamili!
“Asante mpenzi, umenifanya nijihisi kidume cha nguvu!”
“Siyo kukufanya, wewe ni kidume cha nguvu Bravo... bahati mbaya umeoa, lakini siyo neno, nitatumia nafasi hiyohiyo ndogo uliyoniachia mpenzi wangu!” akasema Tunu.
“Kuoa? Sahau kabisa mambo ya mke Tunu. Wewe una nafasi yako. Tena nataka kukuhakikishia kuwa, wewe una nafasi kubwa zaidi ya mke wangu Viola, nafasi yako ni kubwa sana. Tofauti ni kwamba, Viola naishi naye, wewe hautuishi pamoja.
“Lakini pia siyo neno, nitajua cha kufanya. Napanga mikakati rasmi ya kukufanya uwe na nafasi kubwa kwa vitendo siyo maneno maneno, mimi sitaki kuwa mtu wa maneno maneno,” akasema Bravo.
“Unamaanisha nini?”
“Subiri vitendo, hebu nitajie majina yako kamili,” akasema Bravo.
Tunu alishindwa kuelewa sababu ya kuambiwa vile na Bravo, lakini hakuwa na pingamizi zaidi ya kujibu: “Baby kwani mara hii umesahau kuwa naitwa Tunu?”
“Najua ni Tunu, lakini nahitaji majina yako kamili.”
“Tunu Abdallah.”
“La ukoo?... mama majina huwa ni matatu, la kwanza, ubini na ukoo.”
“Hapo sawa, ngoja sasa nikutajie kikamilifu. Naitwa Tunu Abdallah Mdoe.”
“Basi subiri utekelezaji wangu,” akasema Bravo.
“Mpenzi najua umechoka, sasa nakutakia usiku mwema. Ulale salama baba, uniote kipenzi cha miye!” akasema Tunu.
“Nawe pia Tunu.”
Wakakata simu zao.
Ile amekata tu, simu ikaita tena. Alipoangalia, akakutana na mkewe Viola....
“Ah! Limeshaanza! Kwani linataka nini? Linataka kunivurugia furaha yangu hili limwanamke,” akawaza Bravo akiangalia ile simu.
Iliita mpaka ikakatika, wakati akijishauri kupokea. Kwake ilikuwa ahueni, simu ilivyokatika. Baada ya muda, simu ikaanza kuita tena... akaamua kupokea.
“Haloo!”
“Mume wangu jamani Bravo, ndiyo nini kunifanyia hivyo?” akauliza Viola.
“Nimekufanyia nini kwani?”
“Mbona hupatikani kwa muda mrefu, isitoshe nilikuambia ningekupigia.”
“Kazi nyingi Viola.”
“Na kwa nini ukazima simu?”
“Nimekuambia kazi nyingi, nini usichoelewa?” Bravo akajibu kwa ukali.
“Sasa huo ukali wote unatokea wapi Bravo? Nimekuuliza jambo la kawaida tu, tena linalotuhusu wote, iweje sasa unanijia juu?”
“Kama huna cha kuongea, usiwe unanipigia simu, sawa? Mimi nimechoka na kazi, nahitaji kupumzika sasa,” akasema Bravo kisha akakata simu.
Akaizima kabisa!
ITANDELEA....